Kanuni (principles) na masharti (conditions) ya kutumia ushahidi wa mazingira (circumstantial evidence) Mahakamani

Apr 26, 2022
82
121
Ushahidi wa mazingira (circumstantial evidence) - huu ni ushahidi ambao hautoi uthibitisho wa moja kwa moja wa ukweli wa jambo fulani, bali unategemea mazingira yanayozunguka tukio husika ili kutoa hitimisho.

Ushahidi wa kimazingira mara nyingi hutegemea matendo ya mtuhumiwa na mazingira ya tukio yanayoashiria uwezekano wa kuwepo kwa uhusiano kati yake na tukio fulani lililotokea.

Kwa Mfano, ikiwa mtu alionekana karibu na eneo la tukio wakati lilipotokea, kuwa mtu wa mwisho kuonekana na marehemu, kupatikana karibu na eneo la tukio la wizi ukiwa na vitu vilivyoibwa bila maelezo ya msingi umevipataje, kukimbia baada ya tukio n.k, hata kama hakuna ushahidi wa moja kwa moja kwamba mtu huyo alihusika, lakini mazingira yanaweza kufanya aweze kutiliwa mashaka au kushukiwa kuhusika (kuwa suspected).

Je ushahidi wa mazingira unaweza kukubaliwa Mahakamani?

Ndiyo
, hata kama hakuna shahidi aliyeona au kusikia tukio wakati linafanyika, bado mtuhumiwa anaweza kutiwa hatiani na kufungwa kwa kutumia ushahidi wa mazingira (circumstantial evidence).

Hata hivyo kuna kanuni (principles) na masharti (conditions) ya kisheria, ili ushahidi wa kimazingira uweze kuzingatiwa na kutumika Mahakamani, hizi ni baadhi ya kanuni na masharti ya kuzingatia:

1: Ushahidi huo lazima uwe unamuunganisha kabisa mshtakiwa husika na tukio au kosa husika bila kuacha tafsiri nyingine yoyote tofauti vichwani mwa watu.

2: Maelezo yanayosemekana kumuunganisha mshtakiwa na tukio husika lazima yathibitishwe pasipo shaka yoyote (beyond reasonable doubt).

3: Ikiwa ni kesi ya mauaji ushahidi wa mazingira unatakiwa kuwa wa kusadikika (cogent) kiasi cha kumshawishi Jaji au Mahakama. N.k.

Kanuni hizi tatu ziliainishwa na Mahakama ya Rufani kwenye kesi ya Godlizen Daud Mweta na Solomoni Joel Soloo dhidi ya Jamhuri, rufaa ya Jinai namba 259 ya mwaka 2014, Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Dar es Salaam.

Zipo kesi nyingi sana zinazoelezea kanuni na masharti ya kutumia ushahidi wa mazingira Mahakamani kama vile:

1: Kesi ya Manoja Masalu na Malugu Buponi dhidi ya Jamhuri, Rufaa ya Jinai Namba 143 ya mwaka 2020, Mahakama ya Rufani ya Tanzania, kikao cha Mwanza.

2: Kesi ya Safari Anthony Mtelemko na Safari Kija Elkana dhidi ya Jamhuri, Rufaa ya Jinai Namba 404 ya mwaka 2021, Mahakama ya Rufani ya Tanzania, iliyoketi Tabora.

3: James Msumule @ Jembe na wenzake wanne (4) dhidi ya Jamhuri, Rufaa ya Jinai Namba 284 ya mwaka 2021, Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Iringa. N.k.

4: Lucas Daud Wage Vs Jamhuri, Rufaa ya Jinai Namba 555 ya Mwaka 2021, Mahakama ya Rufani ya Tanzania iliyoketi Mtwara.

Kesi zote hizi zinapatikana mtandaoni kwenye tovuti (website) inayoitwa TANZLII.

Kwa ufupi ushahidi wa kimazingira ni ushahidi ambao sio wa moja kwa moja ambao unatumika kumuunganisha mtuhumiwa au mshtakiwa na tukio au kosa husika kwa kuangalia muunganiko wa vipande vya matukio (chain of events).

Ushahidi huu unaweza kuthibitisha kesi peke yake kama unajitosheleza au kwa kuungwa mkono na ushahidi mwingine wa ziada.

Mwandishi: Zakaria Maseke
(0754575246 - WhatsApp)
 
Back
Top Bottom