Elias Msuya
Member
- Dec 23, 2011
- 15
- 37
Hatimaye Serikali imekiri kwamba madai ya kuwa na uchaguzi ulio huru na wa haki hayawezekani kutokana na muda uliopo kufikia tarehe ya uchaguzi yaani Oktoba 25, 2025.
Mbali na wadau wengine, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimekuwa na madai ya kuwepo kwa mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi maarufu No Reforms, No Election' ili kuwa na uchaguzi ulio huru na wa haki.
Chama hicho kimeapa kuwa hakutakuwa na uchaguzi mwaka huu kama mabadiliko hayo hayatafanyika.
Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 17, 2025 jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Waziri wa wizara hiyo, George Simbachawene alisema madai ya chama hicho kutaka katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu, hayatekelezeki kwa kipindi kilichobaki kuelekea Oktoba mwaka huu.
“Lakini msingi na jambo la maana hapa ni je, mawazo yao hayo yanatekelezeka kwa kipindi hiki na kama yanatekelezeka yana gharama kiasi gani kwa kuangalia muda, kuwashirikisha wananchi ili kuwapatia haki ya kuwashirikisha kwa sababu jambo linalogusa katiba haliwezi kuwa ajenda ya kikundi cha watu, haliwezi kuwa ajenda ya CCM peke yake au ajenda ya chama fulani peke yake ni lazima liwe ajenda ya Watanzania wote.
“Je, katika kipindi hiki ambacho katiba yetu inasema uchaguzi ni Oktoba tunaweza tukayafanya hayo yote ya kuwashirikisha wananchi wote kwa sababu ule mchakato wa katiba mpya ile ya wakati ule tulichukua mwaka mzima sasa tunaweza tukafanya hayo? Ni dhahiri mtu anapodai kitu ambacho hakiwezekani unajiuliza dhamira yake ni nini?” amesema Simbachawene.
>>>>>>>Msikilize Waziri Simbachawene hapa
Ni madai ya muda mrefu
Chadema imekuwa kufanyika kwa mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi ikiwa pamoja na kufanya marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Katika maboresho hayo wanataka iundwe Tume Huru ya uchaguzi tofauti na hii ya sasa (INEC) ambayo viongozi wake akiwamo Mwenyekiti na makamu wake wanateuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM na ndiye mgombea wa chama hicho.
Hata uteuzi wa makashina wa tume hiyo pamoja na upatikanaji wa wafanyakazi wa tume hiyo wote ni watumishi wa umma wanaofanya kazi chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye ni mwenyekiti wa CCM. Hali hiyo hiyo haiifanyi tume hiyo kuwa huru.
Soma pia: Uchaguzi ukiwa huru na wa haki
Madai haya yamekuwepo kwa zaidi ya miaka 30 tangu mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa nchini mwaka 1992 na uchaguzi mkuu wa kwanza kufanyika mwaka 1995. Kumekuwa na madai ya kuwa na Tume huru ya uchaguzi, lakini yanapigwa danadana tu.
Kimsingi kulipaswa kuwa na mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ili kuweka uwanja sawa wa uchaguzi kwa vyama vyote kwa kuondoa nguvu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano kuingilia mfumo wa uchaguzi. Hilo CCM wamekuwa wakilikwepa miaka yote.
Ni Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete aliyeanzisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba mwaka 2012 uliotarajiwa kutoa majibu ya muda mrefu ya kupatikana uwanja sawa katika uchaguzi, pamoja na mengine.
Lakini mchakato ule haukufika mwisho, kwani mwaka 2014 baada ya Bunge Maalum la Katiba kutoa Katiba inayopendekezwa kwa ajili ya kupigiwa kura, mambo ndio yaliishia pale.
Baada ya Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli kuingia madarakani, alifutilia mbali mchakato huo, akijikita zaidi kwenye miradi ya maendeleo. Lakini baada ya kifo chake, Rais Samia Suluhu Hassan, alirejesha matumaini ya utawala wa kidemokrasia kwa kuanza kufanya mikutano ya maridhiano na makundi mbalimbali vikiwamo vyama vya siasa, huku sera yake ya 4R (Reconciliation, Resilience, Reform and Rebuild).
Mbali na kikosi kazi alichokiunda kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Chadema pia walifanya mazungumzo na timu ya CCM kusaka maridhiano. Hata hivyo, mazungumzo hayo yalikwama, huku Chadema wakidai kuwa CCM walikataa mapendekezo mengi waliyopeleka.
Badala yake Serikali ilipeleka muswada wa Sheria za uchaguzi ikiwamo Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya 2023, Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (2023) na Sheria ya Vyama vya Siasa (2023), ambazo zilipitishwa.
Sheria hizo zimekuwa zikilalamikiwa kutojibu maswali ya kupatikana mfumo huru wa uchaguzi, kwani ili kupata mfumo huru wa uchaguzi ni lazima kwanza kufanya mabadiliko ya Katiba. CCM haikukubaliana tena hoja hiyo.
Leo, Waziri Simbachawene anaposema madai ya Chadema hayatekelezeki, maana yake ni kwamba: kwanza anakubaliana na hoja zao lakini tatizo muda wa kuzifanyia kazi hautoshi. Pili, huenda anamaanisha kuwa uchaguzi ujao ujao hautakuwa huru wala wa haki, ila inabidi upelekwe hivyo hivyo kwa kuwa muda hautoshi?
Kwa maana nyingine, kauli hii inaashiria kuwa Serikali inajua wazi kwamba uchaguzi hautakuwa huru wala wa haki, lakini inabidi upelekwe hivyo hivyo ilimradi CCM ishinde, kisha mambo mengine yaendelee.
Kama ni muda, Rais Samia alikuwanao wa kutosha kufanya mabadiliko tangu alipoingia madarakani Machi 2021. Isitoshe, hata kama angetaka kufanya hayo mabadiliko mwaka huu 2025 yangefanyika tu, suala ni nia.
Kutofanyika kwa mabadiliko hayo ni makusudi kwa lengo la kuilinda CCM. Ni mwendelezo wa danadana za Serikali kwa madai ya kupatikana kwa mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano yatakayoleta mfumo huru wa uchaguzi pamoja na mengine.
Leo Simbachawene atasema hivi, uchaguzi utafanyika, kesho atakuja mwingine atasema lake, ilimradi mfumo wa uchaguzi unazidi kuchakachuliwa kila unapowadia uchaguzi.
Soma pia Wanaopinga mabadiliko wanavyosema