Jinsi unavyowaruhusu wengine wakutumie kwa mafanikio yao

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,915
3,411
Rafiki yangu mpendwa,

Kwenye haya maisha ni labda utajipanga ili uweze kupata kile unachotaka au utapagwa na wengine uwasaidie kupata kile wanachotaka.

Ni uchague kupambana kufikia kusudi na ndoto zako, au wengine wakutumie wewe kufikia kusudi na ndoto walizonazo.

Hivyo ndivyo maisha yalivyo rafiki, hayajawahi kuwa na huruma kwa mtu ambaye anakataa kujitambua yeye mwenyewe.

Simba anapokuwa anamkimbiza swala, simba anakimbia kupata chakula ili aendelee kuwa hai, wakati swala anakimbia kuepuka kifo ili aendelee kuwa hai. Simba akimla swala ni sawa na swala akiweza kukwepa asiliwe na swala pia ni sawa.

Hakuna swala la kwamba ni hai au siyo haki, sawa au siyo sawa nyikani, anayepona ni aliye imara.


Hali hii ya nyikani bado ipo ndani yetu sisi binadamu, hasa inapokuja kwenye mafanikio makubwa. Wanaofanikiwa ni wale wanaotumia kila fursa kuweza kujijengea mafanikio makubwa. Wanafanya yale yaliyo sahihi ili waweze kupata kile wanachotaka, bila ya kujali wengine wanawachukuliaje.

Wengi wasiofanikiwa huwa hawawaelewi wale wanaofanikiwa sana. Wanavyowaona wakiendelea kupambana licha ya kuwa tayari wana mafanikio makubwa wanawashangaa. Wanajiambia wao wakifika ngazi za mafanikio kama walizofika wale waliofanikiwa, hawatajisumbua tena.

Na hapo unakuwa na majibu kwa nini watu hao wanakuwa hawajafanikiwa mpaka hapo, kwa sababu hawana msukumo mkubwa wa mafanikio. Kwa sababu hawana mpango wao wa mafanikio. Matokeo yake wanakuwa wameishia kwenye mipango ya watu wengine.

Rafiki, ninaposema uwe na mpango wako ili usitumike kwenye mipango ya wengine simaanishi usiingie kwenye mipango ya wengine kabisa. Hili haliwezekani, kila mmoja wetu kwenye vipindi mbalimbali vya maisha huwa tunaingia kwenye mipango ya watu wengine. Yaani tunatumika kuwatimizia wengine ndoto zao.

Tatizo linakuja pale ambapo kwa maisha yako yote unapambana kuwatimizia watu wengine ndoto zao, wakati wewe umezisahau kabisa ndoto zako.

SOMA; Kama hujavurugwa, huwezi kufanikiwa.

Tuchukue mfano wa ajira, kwa sehemu kubwa, kwenye ajira unakuwa unatimiza ndoto za wale ambao wamekuajiri, iwe ni mtu au taasisi. Lakini wewe binafsi unakuwa na ndoto zako. Kama kazi unayokuwa unaifanya kwenye ajira haiendani na ndoto zako, hupaswi kudumu kwenye ajira hiyo kwa kipindi cha maisha yako yote. Badala yake unapaswa kupita kwa muda tu na kujipanga ili ukapambanie ndoto zako.

Hata wale waliopo kwenye biashara, wengi hudhani wapo huru na wanapambania ndoto zao. Ila wengi sana wapo kwenye vifungo vya faida kubwa na kutaka kuonekana. Wengi waliopo kwenye biashara waliingia kwa sababu ya kutafuta faida kubwa au kufuata mkumbo.

Hakuna ubaya wowote kuingia kwenye biashara kwa sababu ya faida, kwa sababu fedha unazihitaji sana. Lakini pale unapozisahau kabisa ndoto zako kwa sababu ya hiyo faida, unayafanya maisha yako kukosa kukamilika kwa namna fulani.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimekuonyesha jinsi kukosa mipango ya maisha yako kunavyowapa wengine fursa ya kukutumia kwenye mipango yao. Na nimekupa mwongozo wa jinsi ya kushika hatamu ya maisha yako ili uweze kujenga mafanikio makubwa. Karibu ujifunze na kufanyia kazi ili uwe na maisha yenye maana kubwa kwako.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.
 
Back
Top Bottom