IWE CHUNGU AMA TAMU
Kwetu ulimi maneno, mengine ni ya ziada,
Siye twatoa misemo, na nyimbo kwenye ibada,
Ladha kwetu siyo somo, ladha kwetu siyo shida,
Iwe chungu iwe tamu, cha msingi ni kushiba.
Vya maana twaviona, twanusa na kusikia,
Hizo suti za kushona, na vingi vya kuvutia,
Tulivitamani sana, tumeshindwa kufikia,
Iwe chungu iwe tamu, cha msingi ni kushiba.
Iwe biringanya mbichi, ama pilipili manga,
Karoti ama kabichi, ama dagaa mchanga,
Sie milo haichoshi, tunatamani kusonga,
Iwe chungu iwe tamu, cha msingi ni kushiba.
Sie hatuna ratiba, tupatacho tunakula,
Tunachopenda kushiba, hatuchagui vyakula,
Bila soda tunashiba, tunakula kisha sala,
Iwe chungu iwe tamu, cha msingi ni kushiba.
Kwetu hatuna jokofu, hatuchachishi viporo,
'Tabaki na yako hofu, utumbo hauna kasoro,
Kunenepa hatuhofu, leo twala kesho doro,
Iwe chungu iwe tamu, cha msingi ni kushiba.
Si kwamba hatutamani,tamaa twaweka ndani,
Twapiga kazi jamani, siku tuwe na vyetu ndani,
Maisha hatulingani, tajiri na masikini,
Iwe chungu iwe tamu, cha msingi ni kushiba.
Shughuli na matukio, twajua chungu na tamu,
Jaani ndo kimbilio, kama vile si timamu,
Njaa huleta kilio, hatujui neno hamu,
Iwe chungu iwe tamu, cha msingi ni kushiba.