BARD AI
JF-Expert Member
- Jul 24, 2018
- 3,591
- 8,817
Kina cha maji cha Bwawa la Mtera, Mkoani Iringa kimepungua na hivyo kupunguza Uzalishaji wa umeme kutoka megawati 80 mpaka 72.
Hayo yamebainika leo Septemba 9, 2023 baada ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kutembelea bwawa hilo ili kuona uzalishaji wa umeme.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ussi Salum amesema uvumi kuwa baadhi ya watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kufungulia maji bila utaratibu na hivyo kusababisha upuugufu wa maji ya kuzalisha umeme sio wa kweli.
"Tumeridhika na uzalishaji wa umeme, kwa sasa kina cha maji kimepungua kwa sababu ni kipindi cha kiangazi, mvua ndio ambazo zinajaza Bwawa la Mtera na hivyo kusaidia uzalishaji Kidatu," amesema Salum.
Amesema lengo la ziara hiyo ni kujionea hali halisi ya uzalishaji umeme kwenye vyanzo vya maji vya Mtera, Kidatu, na Kihansi na kujipanga iwapo mvua za kiwango cha juu zitanyesha kama ilivyotangazwa na mamlaka ya hali ya hewa hivi karibuni.
Katika bwawa hilo, mashine zote mbili zina uwezo wa kuzalisha megawati 72 huku kila moja ikizalisha megawati 38.
Mkurugenzi wa Uzalishaji Umeme kutoka Tanesco, Pakaya Mtamakaya amesema mashine hizo zinauwezo wa kuzalisha mpaka megawati 80 kina cha maji kinapojaa.
Amesema watahakikisha umeme unaendelea kupatikana licha ya bwawa hilo kupungua kiwango chake cha maji kutokana na uhaba wa mvua.
"Kawaida huwa tunapata mvua mara mbili kwa msimu na iwapo msimu ukichelewa husababisha uhaba wa maji, lakini hauathiri upatikanaji wa umeme kwani kuna vyanzo mbadala vya uzalishaji," amesema.