Historia ya "Muasisi" na Muasisi wa TANU Mikindani Msham Awadh 1955

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
21,898
31,969
Msikilize "muasisi" wa TANU Mikindani kisha soma historia ya Msham Awadh kutoka kitabu cha Abdul Sykes (1998)



SIKILIZA HISTORIA HII YA ''MUASISI'' WA TANU NA SOMA HISTORIA YA MSHAM AWADH

Tukio dogo la kiburi cha askari mpumbavu wa mkoloni ndiko kulisababisha watu wa Mikindani wafungue tawi la TANU.

Askari mmoja mpita njia aliingia katika ubishi na kijana mmoja wa pale mjini, akiitwa Hassan Masudi Vuni.

Akitumia mamlaka yake ya kukamata mhalifu, askari huyo alimpiga Vuni kwa kumuonea.

Miongoni mwa watazamaji wa tukio hilo alikuwa Rashid Ali.

Rashid Ali alikwenda kusimulia tukio hili kwa Mohamed Ali Abdallah.

Alipokuwa akisimulia mkasa ule, pamoja naye alikuwa Suleiman Hassan Msepele.

Walipokuwa wakijadiliana Msepele alitamka kwamba tukio kama hilo kamwe lisingeweza kutokea Dar es Salaam kwa sababu Mwafrika mmoja kwa jina lake Julius Nyerere alikuwa ameanzisha chama cha siasa kupigania uhuru.

Rashid Ali na Mohamed Ali Abdallah walitamani kujua mengi zaidi kuhusu Mwafrika huyu aliyekuwa akijulikana kwa jina la Nyerere na chama chake cha siasa, lakini Msepele hakuwa na mengi ya kueleza kuhusu Nyerere na chama chake.

Kwa hiyo basi, hawa watu watatu waliamua kumtuma mtu Dar es Salaam kupata habari zaidi kuhusu chama hicho. Mohamed Ali aliandika barua na kumpa Msham Awadh na Ali Muhidin kumpelekea Nyerere.

Ndani ya barua hiyo Mohamed Ali alimweleza Nyerere kwamba ukoloni ulikuwa bughudha kubwa katika Jimbo la Kusini, na wangependa kufungua tawi la TANU mjini Mikindani ili kupigania uhuru.

Mwaka 1955 Mohamed Ali alikuwa na umri wa miaka 45.

Alikuwa hana elimu kama elimu inavyojulikana kwa kuwa hakusoma shule yoyote.

Alipokuwa kijana mdogo baba yake alimpeleka Zanzibar kusoma elimu ya dini. Wakati huo Zanzibar ilikuwa ndiyo kituvu cha elimu ya Kiislamu.

Huko Zanzibar kijana Mohamed Ali alisoma kwa Sheikh Mohamed LíKhamus.

Kisha aliendelea na masomo yake mjini Dar es Salaam kwa Sheikh Wazir bin Said, mwanafunzi wa Sheikh maarufu sana na aliyekuwa khalifa wa Tariqa ya Askariyya, Sheikh Idrissa bin Saad.

Baada ya kumaliza masomo yake mjini Dar es Salaam alisafiri hadi Belgian Congo na halafu alirudi Ujiji nchini Tanganyika kufanya biashara ndogo ndogo.

Katika mwaka 1947 alirudi Lindi na kutoka hapo alikwenda Mikindani na kuwa fundi cherahani.

Msham Awadh alikuwa akijulikana Lindi nzima na Mikindani kwa sababu ya biashara yake.

Mshama Awadh alikuwa alikuwa muuza uzuri, yaani vitu vya urembo kama vile uturi, dalia, marashi, rangi na manukato mengine kwa wanawake wa hii miji miwili.

Alikuwa akiuza bidhaa zake kikapuni akipita nyumba hadi nyumba.

Hawa walikuwa ndiyo aina ya watu walioanzisha na kuongoza harakati za kumaliza utawala wa kikoloni.

Hawakuwa wajuzi wa lugha ya Kiingereza wala hawakuwa na ujuzi wa maisha ya ulimwengu wa kimagharibi kama walivyokuwa baadhi ya Waafrika wengine waliyopata elimu ya kimagharibi.

Msham Awadh na Ali Muhidin walikwenda hadi Dar es Salaam kukutana na Nyerere, Rupia, Chamwenye, Kambona na Dossa katika makao makuu ya TANU, New Street.

Msham Awadh na Ali Muhidin walipewa kadi za TANU na wakaambiwa wafungue tawi Mikindani.

Wakati Msham Awadh na Ali Muhidin wakiwa njiani kwenda Dar es Salaam kukutana na Nyerere, Mohamed Ali alisafiri kwenda Lindi kukutana na Mnonji na kumweleza kuwa Mikindani walikuwa wamekusudia kufungua tawi la TANU.

Mnonji alimpa kadi Mohamed Ali na akawa mwanachama na akamwambia arudi Mikindani na kuanza kufanya kampeni kwa nguvu kwa ajili ya TANU na awafahamishe watu kuwa Nyerere yupo njiani kuja Jimbo la Kusini.

Julius Nyerere, Ali Mwinyi Tambwe na Rajabu Diwani waliwasili Mikindani kutoka Lindi siku ya Jumamosi.

Kabla ya kuwasili ujumbe huo, kazi kubwa kuliko zote waliyokuwanayo uongozi wa TANU Mikindani ilikuwa kutafuta mahali pa kumlaza Nyerere.

Walimwendea Ahmed Adam, Mnubi mmoja tajiri na mtu wa makamo, aliyemiliki nyumba moja ya fahari.

Nyumba hii ilikuwa ya ghorofa moja na ilijengwa kwa mawe na chokaa.

Ahmed Adam aliombwa awe mwenyeji wa Nyerere na ujumbe wake.

Nyumba hii tayari lilikuwa na kisa chake.

Ilijengwa na hayati kaka yake Ahmed Adam baada ya Vita Kuu ya Kwanza.

Kaka yake alikuwa askari wa Kinubi aliyekuwa katika jeshi la Wajerumani.

Huenda alichukuliwa Misri mwishoni mwa mwa karne ya kumi na tisa na Wajerumani kuja Tanganyika kama mamluki katika jeshi la Wajerumani wakati wa vita vya Maji Maji.

Baada ya vita alilipwa kiinua mgongo na serikali ya Ujerumani na kwa kutumia fedha hizo alijenga nyumba hiyo.

Katika Vita Kuu ya Kwanza yeye alipigana katika jeshi la Wajerumani dhidi ya Waingereza.

Baada ya vita Wajerumani wakiwa wameshindwa vita, Waingereza waliitikadi nyumba hiyo kama mali ya adui wa himaya ya Kiingereza na kwa hiyo ilibidi itaifishwe.

Hii ilikuwa ndiyo nyumba pekee iliyokuwa nzuri yenye kumilikiwa na Mwafrika na kwa ajili hii haikuweza kukosa kuhusudika.

Utawala wa Waingereza ulikuwa katika taratibu ya kuitaifisha nyumba hiyo wakati ilipofahamika kwamba serikali isingeweza kufanya hivyo kwa sababu ya kifungu cha sheria ambacho kilisema kuwa mali ya Waafrika waliokuwa wakitumika katika majeshi ya watawala wao haiwezi kutaifishwa.

Hii ilinusuru nyumba hiyo na hivyo ilibakia mikononi mwa mwenyewe mpaka alipofariki na nyumba hiyo ikaja kuwa katika miliki ya mdogo wake, Ahmed Adam.

Ahmed Adam alikubali kumpokea Nyerere na ugeni wake nyumbani kwake.

Nyumba hiyo ilikuja kuwa tawi la kwanza la TANU Mikindani. Siku hiyo hiyo ya Jumamosi, usiku Nyerere aliitisha mkutano na wanachama kama thelathini hivi walihudhuria.

Nyerere aliwaeleza kwa ufupi juu ya ile safari yake ya Umoja wa Mataifa na hali ya siasa kwa ujumla mjini Dar es Salaam.

Nyerere aliwahakikishia waskilizaji wake kuwa kulikuwa na uwezekano mkubwa sana kuwa Tanganyika itakuwa huru katika uhai wao.

Siku iliyofuatia mkutano wa hadhara ulifanyika mjini Mikindani mahali palipojulikana kama Jangwani, karibu na ufuko wa Bahari ya Hindi.

Mkutano huu uliohudhuriwa na watu wengi na uliendelea bila mushkeli wowote ukitoa kitendo kidogo kilichofanywa na mwalimu mmoja wa shule, Abdulrahman Muhibu aliyekuwa amelewa.

Muhibu alikuwa ametoka kunywa pombe na alipita karibu na uwanja wa mkutano ambapo Nyerere alikuwa akihutubia. Katika hali yake ya ulevi alimpigia kelele Nyerere akamwita muongo.

Huenda Muhibu alikuwa akifahamu vyema ujumbe wa Nyerere, na akiwa vile alivyokuwa, mtumishi wa serikali na mlevi, aliona wazo la mwalimu wa shule Mwafrika kama yeye kuwaongoza watu hadi uhuru upatikane ni jambo lisilowezekana. Kwa haraka Muhibu alikamatwa na watu na ilikuwa karibu wamtie adabu ndipo Nyerere alipoingilia na hivyo kumnusuru.
 
Mzee Mohamed ninakusudia kufanya jambo fulani litakaloninufaisha mimi lakinu pia litakujengea heshima wewe. Nitakutafuta
 
Back
Top Bottom