Hadithi: Mikataba ya kishetani

JIPATIE NAKALA YAKO MKONONI UPATE KUBURUDIKA NA STORY NZURI ZA LT.BEN MTOBWA

HARAKATI ZA JORAM KIANGO

1/ MTAMBO WA MAUTI

2/ MIKONONI MWA NUNDA

3/ TUTARUDI NA ROHO ZETU

4/ ROHO YA PAKA

5/ NAJISIKIA KUUA TENA

6/ MIKATABA YA KISHETANI

Hivo hapo mkuu
Ahsante....
 
***

Nyumba ya Dkt. Twalib Khalfan ilimlaki kwa vilio vya kwikwi vya kina mama waliokuwa wamekaa ndani wakiomboleza, huku nyimbo za dini zikiimba kwa mbali. Afande Chaku alipitiliza moja kwa moja mpaka chini ya muembe alipokuwa amekaa mfiwa akiomboleza pamoja na wanaume wachache.

Chaku hakusumbuliwa na macho ya waombolezaji, walimchukulia kama mmoja wao kutokana na nguo za kiraia alizokuwa amevaa. Aliwasalimu wote na kuwapa pole. Kisha alijikaribisha katika kiti kimojawapo kilichokuwa kitupu. Akaomba kuongea na Dkt. Khalfan faragha. Khalfan hakuwa na hiyana, alinyanyuka toka alipokuwa amekaa na kumuelekeza mgeni kuingia ndani ya nyumba yake ambapo walikaa kwenye ukumbi wa chumba kikubwa kilichokuwa na utulivu ambao Afande Chaku aliufurahia kimoyomoyo.

Wakakaa kwenye viti vilivyokuwa ndani humo.

“Dkt. Khalfan Twalib, pole sana kwa msiba uliokupata.”

“Asante sana.” Twalib aliitikia kwa sauti ndogo lakini iliyomfikia vema Afande Chaku.

“Mimi ni afisa wa Polisi,” Chaku aliongea akitoa kitambulisho chake na kumkabidhi Dkt. Twalib ambaye alikitazama kwa muda kabla ya kukirudisha kwa Afande Chaku.

“Nimebeba jukumu hili la kumpata muuaji, hivyo ningeomba ushirikiano wako.” Afande Chaku alisema. Dkt. Twalib Khalfan aliitikia kwa kichwa bila kusema lolote.

“Dokta, kuna lolote ambalo umeliona si la kawaida hapa msibani?” Chaku alianza kuuliza.

Dkt. Twalib Khalfan alisita kabla ya kujibu, pengine alikuwa akijaribu kuvuta picha. “Ndiyo,” alijibu huku amemkazia Afande Chaku macho.

“Lipi?” Chaku aliuliza kwa shahuku kubwa iliyojionyesha dhairi machoni mwake.

“Mwandishi wa habari mwenye baibui jipya.”

“Baibui?” Afande Chaku alishangaa, akatoa daftari na kalamu, tayari kwa kunukuu chochote alichoona kinafaa.

“Ndiyo, alikuja mwanana mama akidai ni mwandishi wa habari akiwa amevalia baibui lililoficha sehemu kubwa ya mwili na sura yake.”

Afande Chaku alinukuu kitu fulani. Kisha akamtazama tena mwenyeji wake, “Alisema anaandika gazeti gani?”

This Day.”

Afande Chaku alinukuu tena.

“Kwanini unamuhisi kuwa si wa kawaida?” Afande Chaku aliuliza.

“Kwasababu mhariri wa This Day, ni rafiki yangu. Alinipigia jana kunipa pole. Nikamdokeza juu ya mwandishi wake huyo. Mhariri alishangaa, kwani kwa mujibu wa maelezo yake hajapata kumtuma mwandishi kwangu na hana jina hilo katika orodha ya waandishi wake,” Khalfan alifafanua.

Kalamu ya Afande Chaku ilicheza katika kurasa za daftari lake. “Hakuna kitu kingine ambacho si cha kawaida kwa mwandishi huyu?” aliuliza.

“Kipo”

“Kitu gani?”

“Ni kitu kidogo tu. Lafudhi yake. Pamoja na ukweli kuwa anazungumza Kiswahili, si lugha yake ya kwanza. Ama ni mgeni ama amekulia ugenini.”

Afande Chaku alitafakari hilo kabla ya kuendelea na swali lake la pili. “Dkt. Khalfan kitu fulani kimekua kikisumbua sana akili yangu na ya kila mtu anayehusika kwa namna moja ama nyingine na swala hili. Ni namna ya jinsi marehemu alivyokutwa na maafa. Alikuwa kati ya Rais ambaye kwa kawaida anakuwa na maadui wengi kama alivyo na marafiki. Upande wa pili alikuwepo tajiri mkubwa ambaye pia ana maadui lukuki kama alivyo na marafiki. Tunahitaji maoni yako. Unadhani muuaji alimkusudia yeyote kati ya hao wawili akakosea shabaha na kumuua yeye?”

Lilikuwa swali ambalo tayari lilikuwa limemsumbua sana Khalfan. Hakuweza kuamini kama kuna mtu duniani aliyepata kumchukia Cleopatra kiasi cha kumuua, tena hadharani. Hata hivyo, kwa yale aliyoyasoma gazetini na kutazama eneo la maafa katika televisheni alishindwa kujizuia kushuku kuwa muuaji alikuwa mtu anayeijua kazi yake, hivyo asingekuwa na namna yoyote ya kupoteza shabaha kwa kiwango kile.

Alimweleza hayo Afande Chaku.

“Nakumbuka kusoma mahala kwamba marehemu alikutwa na kifo wakati mkiwa mmetengana?” Afande Chaku aliongeza swali lingine.

“Ni kweli.”

“Mlitengana kwa muda gani?”

“Kama miezi sita hivi.”

“Kitu gani kiliwatenganisha?”

“Sijui.”

Afande Chaku aliinua uso na kumtazama Khalfan kwa mshangao. “Sikuelewi. Mkeo wa ndoa, mliyeishi naye miaka nenda rudi atakuachaje na usijue sababu?”

“Hata mimi nimekuwa nikijiuliza swali hilo hilo kila siku,” lilikuwa jibu la Khalfan, ambalo lilizidi kumchanganya Chaku.

“Mligombana?”

“Hatujapata kugombana”

Chaku alitafakari kwa muda. Akakumbuka kile kijikaratasi alichokipata kwa daktari wa Muhimbili. I love you King Suleiman. Penzi lao liliingiliwa kati. Ama mume hajui ama anajisikia kiburi kukiri hilo hadharani. Akaamua kubadili mkondo wa maswali yake.

“Mna watoto?”

“Mmoja tu.”

“Yuko wapi?”

“Yuko masomoni Arusha, kidato cha tano. Kesho atakua hapa. Nimemtumia tiketi ya ndege.”

“Unaweza kukumbuka siku za mwisho kabla ya marehemu kuondoka alikuwa na mwenendo gani?”

Khalfan alitafakari swali hilo kwa muda kabla hajajibu kwa neno moja tu, “Alibadilika.”

“Kwa vipi?”

“Hakuwa Cleopatra yuleyule ambaye nilimfahamu. Alikuwa mtu mwingine. Alikuwa mkimya mara kwa mara, huku akionekana kutafakari jambo kwa muda mrefu. Simu yake ya mkononi ilipoita, aliipokea bila uhuru huku akihakikisha siyasikii maongezi yake. Halafu akaanza tabia ya kuchelewa nyumbani. Nilipomuuliza alidai shughuli nyingi. Siku moja alipata kulala nje, mwenyewe akidai kuwa anakesha kazini.” Khalfan alieleza.

King Suleiman huyo! Chaku aliwaza akichekea tumboni, wazo ambalo alijikuta akilitilia mashaka pale Khalfan alipoongeza, “Kama angekuwa mtu mwingine ningeweza kumshuku kuwa amerubuniwa huko makazini. Nadhani unajua ofisi kubwa zilivyo na mambo ya kishenzi. Lakini si Cleopatra. Nilimwamini, aliniamini. Nilimkuta bikira, alinikuta bikira.

Wanaume tunavopenda kudanganywa! Chaku aliwaza tena huku akibadili mkondo wa maswali yake. Aliuliza hili na lile, hata yale ambayo hakuyahitaji mradi Khalfan aendelee kuzungumza. Baada ya muda aliitazama saa yake. Muda ulikuwa umekwenda. Akainuka na kuaga kwa kumshukuru Khalfan kwa ukarimu na ushirikiano wake.

“Wewe pia nakushukuru sana, afisa. Umenitoa upweke.”

Khalfan alimjibu, akainuka na kumfungulia mgeni wake mlango.

Ghafla, kama aliyekumbuka jambo, Chaku aligeuka na kuutia mkono wake mfukoni. Aliutoa ukiwa na kile kipande cha karatasi alichopatiwa na Daktari. “Samahani,” alimwambia Khalfan. “Kuna karatasi hii imekutwa katika mfukon wa marehemu. Unaweza kumfahamu mtu huyu aliyeachiiwa ujumbe huu?”

Khalfan aliusoma, kwanza harakaharaka, kisha taratibu. Mara akainua macho yake kumtazama Chaku. Alikuwa amebadilika sura na sauti.

“Unasema mliupata wapi?” aliuliza.

“Marehemu alikuwa nao mfukoni,” Chaku alimjibu.

Khalfan alizidi kubadilika. Alitetemeka mikono na midomo. Akashindwa kuhimili machozi ambayo yalimtoka bila kutarajia.

“Unamfahamu huyu King Suleiman?”

“Namfahamu sana.”

Moyo wa Chaku ukajawa na shahuku.

“Ni nani?”

“King Suleiman ni mimi.”

“Wewe! Yakoje mambo haya?”

Khalfan alimtazama Chaku. Kwa namna fulani alimhurumia, kwani asingeweza kuelewa. King Suleiman lilikuwa jina ambalo mwanzo wa penzi lao lilitumiwa kama siri miongoni mwao. Baadaye, baada ya ndoa, liligeuka kuwa jina pekee lililotumika kuthibitishha penzi na kukoleza mahaba yao. Lilianza kama mzaha, wakiwa shule ya msingi.

“Mwalimu: Cleopatra!”

“Cleopatra: Abee!”

“Mwalimu: Simama mbele ya darasa uniambie nani hapa anafaa kuwa mfalme Suleiman.”

“Cleopatra: Yule pale!”

Darasa zima lilipiga makofi.

“Mwalimu: Darasa hili litaongozwa na Mfalme Suleiman kama kiranja na Cleopatra msaidizi wake. Sawa?”

Ndivyo ilivyokuwa. Miaka ya shule ya msingi ilipoteketea walipotezana kwa muda. Walionana wakiwa sekondari. Ni Cleopatra aliyemwona kwanza Khalfan, “King Suleiman!” aliita. Dkt. Khalfan aligeuka na kushangazwa na msichana anayevutia kwa sura na umbile, kasimama pale akitabasamu. Alikuwa malaika!

“Malaika!” Khalfan aliita akimkimbilia na kumkumbatia.

“Malaika wangu! Ulipotelea wapi?” alimuuliza akimkumbatia kwa nguvu zaidi. Walipotengana kimwili, kiroho hawakupata kutengana tena. Kila mmoja aliishi kwaajili ya mwingine, alisoma kwaajili ya mwingine. Moyoni mwa Khalfan, Cleopatra alikuwa malkia halisi wa ‘Mfalme Suleiman.’
 
7

Hakuna mtu aliyefahamu kikamilifu kazi ya Tenga Mfaume pale hotelini, pengine hata yeye mwenyewe hakuifahamu. Alikuwa kila mahali. Mara alijihusisha na ununuzi wa bidhaa, mara kudai madeni na mara nyingine kuhudumia wateja vyumbani na kumbini. Wakati wafanyakazi wenzake wengi hawakumpenda sana kwa kumchukulia kuwa anapendelewa, alikuwa swahiba mkubwa wa viongozi wa juu. Mara kwa mara alionekana akiranda na Meneja mkuu mitaani huku wakizungumza kama mtu na rafiki yake. Wenzake walipotaka kujua anatoka wapi na wakubwa hao au nini anazungumza nao jibu lake lilikuwa lilelile, ‘mambo ya kikazi.’ Baadhi walianza kumwogopa kwa kumchukulia kuwa ama alikuwa mpelelezi wa hoteli ama aliyepandikizwa na Serikali hotelini hapo, wazo ambalo mwenyewe alilifurahia sana kimoyomoyo ingawa kwa sauti alilikanusha mara kwa mara.

Tenga hakuwa akishibana na viongozi pekee. Pia, alikuwa kipenzi cha wageni wengi hotelini hapo. Haikumchukua muda kujenga urafiki na mgeni yeyote aliyemtaka, hasa wanawake. Siku zake nyingi za mapumziko alizitumia kwa kuwaongoza wageni kuitembelea miji ya kale kama Bagamoyo, Zanzibar au Kilwa. Mara mbili tatu alipata kwenda mbuga za Mikumi na Manyara kwa gharama za wageni hao.

Licha ya uchangamfu na utanashati wake, Tenga alikuwa na sifa nyingine ya pekee, jicho. Wenzake walimtania kuwa alikuwa na macho matatu, moja la kuonea kile ambacho wengine hawaoni. Kwa mfano, kwa jicho lake hilo la ziada aliweza kubaini mara moja mteja aliyeingia ana fedha za kutosha kumweka katika hoteli hiyo au angekuwa mtu wa kusumbua kimalipo baadaye. Kwa jicho hilohilo, aliweza kubaini mgeni anayehitaji Company ama ya mwanamke ama ya mwanaume, huduma ambayo aliitoa katika muda wake wa ziada.

Ni katika mfumo huo wa maisha Tenga alipovutiwa na Mrs. Macbain, msichana mrembo ambaye alikuwa akimsubiri mume wake, atakayemfuata siku mbili tatu zijazo, kwa uzoefu wake aliamini kuwa wake wengi wa wakubwa huchoshwa na wanaume zao ambao wana shughuli na pilikapilika nyingi kiasi cha kusahau wajibu wao kwa wake zao. Hivyo, wanawake wa aina hiyo wanapopata mwanya huwa na tabia ya kujiachia mradi taarifa hazimfikii mumewe.

Kwa matumaini hayo, macho ya Tenga yalimfuata Monalisa Macbain kila alipopita, rohoni akiwa na matumaini kuwa wakati ungefika akalivua joho lililofunika uso wake na kuvaa uanamke walao kwa jioni moja. Haikutokea. Ilikuwa kama tamaa za fisi kumfuata binadamu usiku kucha kwa matarajo kuwa mkono wake mmoja ungedodoka, hali iliyopelekea Tenga azidishe udadisi wake kwa mwanamke huyu.

Alishangazwa kwa jinsi alivyokuwa akipenda upweke. Hakupata kujishughulisha na mtu yeyote hotelini humo, ama wageni ama watumishi. Muda wake mwingi aliutumia chumbani kwake, tena akiwa amejifungia. Tenga alishangaa zaidi jioni ile alipolazimisha kumpelekea mlo wake wa usiku huku akiwa amevaa sura yake ya ukunjufu kwa matarajio ya kusisimua. Alipogonga aliitikiwa “Karibu.” kwa Kiswahili fasaha kabisa. Alipojaribu kuongea hiki na kile kwa lengo la kufungua milango alibaini kuwa msichana huyo hakuhitaji mazungumzo. Aliagwa kwa neno jingine moja tu, “Asante.” Awali hakupata kuhisi kuwa msichana huyo alikuwa Mswahili.

“Mume wake atakuja lini?” Tenga alimuuliza msichana mmoja wa mapokezi mara alipopata nafasi.

“Mume wa nani?”

“Huyu msichana anayekaa namba 405, Mrs Macbain”.

Msichana huyo alicheka kabla ya kumjibu kwa kebehi, “Unamtakia nini mume wake? Umeshaanza mambo yako. Angalia utachomwa moto!”

Jibu hilo halikumridhisha Tenga. Akaendelea kumfuatilia mgeni yule kwa macho yake na hila za ziada. Ilimshangaza hata Tenga mwenyewe alipopata hisia za kuanza kumchukia binti yule, kwasababu ambazo hakupata kuzifahamu, hali iliyopelekea pale ofisa mmoja wa polisi aliyevaa kiraia alipofika hotelini hapo na kuuliza juu ya wageni waliomo hotelini na mienendo yao asisite kumtaja Monalisa Macbain.

Polisi alichukua amelezo yake akaondoka zake.

Tenga hakuridhika na alichokiona machoni mwa polisi yule. Aliweza kusoma hali ya kupuuza kile ambacho yeye alieleza kama tuhuma kwa msichana huyo. Binafsi hakukata tamaa. Ari yake ya kumfahamu zaidi na zaidi haikuishia hapo.

Ni hilo lililosababisha jana afanye jambo ambalo hakulitegemea. Alikuwa akitoka kazini wakati alipomwona mgeni huyo akitoka nje ya hoteli na kutembea kwa miguu kuifuata barabara. Tenga aliamua kumfuata. Alitumia kila hadhari kuhakikisha mgeni huyo hamtilii mashaka kwa kuwa mbali ilivyowezekana. Safari ya mama huyo iliishia mataa wa pili ambako aliingia dukani na baadaye kutoka na kitu kwenye mfuko. Nje ya duka alikodi teksi na kumpa dereva maelekezo. Gari likatiwa moto. Tenga alitamani kukodi gari pia ili amfuate lakini alisita kufanya hivyo. Badala yake aliingia dukani na kuuliza mwanamke aliyetoka hapo kanunua nini.

“Yule aliyetoka sasa hivi sio? Kanunua baibui. Ni ajabu na kweli maana hafanani na wavaaji wa baibui,” alisema dada mmoja wa wauzaji dukani humo.

Tenga pia alishangaa.

Wakati akitoka dukani humo aliiona teksi iliyomchukua mwanamama yule ikirejea na kusimama katika maegesho yake. Akaifuata na kuingia ndani ya gari.

“Wapi afisa?” dereva alimuuliza

“Tafadhali, nipeleke ulipompeleka abiria wako wa muda mfupi uliopita,” alimsihi dereva.

“Yupi? Yule mwanamke?”

“Naam”.

“Ni mkeo?”

“Hapana”.

Dereva akashangaa, “Kwanini basi nimfuate? Maadili yetu hayaturuhusu kufanya mambo ya aina hiyo.” dereva alijitetea.

“Usijali, yule ni binamu yangu. Hatujaonana miaka mingi. Nataka kumshangaza kidogo”. Tenga alisisitiza.

Dereva alikubali shingo upande. Akatia gari moto na kuielekeza Mikocheni. Njia haikuwa na magari mengi, hivyo, iliwachukua dakika zipatazo kumi kufika mahala ambapo dereva alimshusha abiria wake.

“Alishukia hapa?” Tenga alihoji kwa mshangao.

“Ndiyo. Binamu yako ni mtu wa ajabu sana. Hapa ni wapi na wapi!”

Lilikuwa eneo moja kati ya machache ambayo majengo yake yalikuwa hayajakamilika. Nyumba bora za kitajiri zilikuwa mbele na nyuma ya mtaa. Kwanini ashukie hapa? Jibu halikumtatiza Tenga. Bila shaka hakutaka dereva ajue wapi hasa alikuwa akienda.

Kiu ya udadisi ikazidi kumshika. Kiu hiyo ikamfanya ashawishike kumlipa dereva ujira wake.

“Na wewe unashuka hapa?”

Tenga alikubali kwa kutikisa kichwa.

“Ama kweli wewe na binamu yako ni watu wa ajabu. Hapa wapi hapa?” Dereva huyo alisema akipokea ujira wake na kuutia mfukoni.

Tenga alishuka. Akatazama huko na huko kabla ya kuona baa moja kwa mbali kidogo iliyokuwa na wateja wachache wanaopata vinywaji vyao. Hakuwa na haraka, akaiendea na kupata kiti kilichojificha kidogo lakini kikimwezesha kuona eneo ambalo mama Macbain alishukia.

Akaagiza kinywaji chake. Bia aina ya safari ikaletwa. Alikuwa katika kumalizia bia ya pili alipomwona mtu wake akitembea kurejea eneo aliloshukia. Kama asingeambiwa Monalisa alinunua baibui, kamwe asingemfahamu. Alikuwa peke yake, akitembea harakaharaka kuliko ilivyokuwa kawaida yake.

“Baibui saa hizi?” mnywaji mmoja alisema akimtazama mama yule.

“Atakuwa ametoka kilioni, hapo nyumba ya tatu,” mnywaji mwenzake alimjibu.

Tenga hakuweza kujizuia, “Kilio cha nani?” akauliza.

“Hujasikia kuwa Cleopatra, mkewe Khalfan ameuawa kwa risasi mbele ya Rais? Khalfan si mtu mdogo. Vigogo wanamiminika kwake kama nzige kumpa pole.” Msemaji alimfafanulia Tenga.

Tenga aliwasikiliza huku macho yake yakiwa kazini kumtazama Monalisa. Alishangaa kumwona akichepuka toka barabarani na kufuata uchochoro mmoja wa jengo ambalo lilikuwa halijaisha. Hata kabla hajajua hatua gani zaidi achukue,alimwona Monalisa akitoka tena. Safari hii akiwa hana baibui. Yeyote ambaye hakupata kumwona kabla hajajitanda baibui lile asingekuwa na namna yoyote ya kuhisi kuwa mwanamama aliyeingia uchochoroni hapo muda mfupi uliopita ndiye huyu anayetoka. Ndivyo ilivyokuwa kwa wanywaji wenzake. Hakuna kati yao aliyewahusisha watu hawa wawili, aliyeingia na aliyetoka uchochoroni.

Monalisa alitembea harakaharaka na kutokomea. Tenga pia alimaliza bia yake upesiupesi na kufuata alipoelekea. Hakuweza kumwona. Na hata angemwona ingesaidia nini? Alijiuliza. Mara alikumbuka namba ya yule mpelelezi. Aliyekuja hotelini kufuatilia wageni. Akatoa simu yake ya mkononi na kumpigia.

“Kitu gani hasa kinakufanya umshuku?” askari alimhoji mara bada ya kumsikiliza.

“Baibui.”

“Baibui?”

“Kununua, kuvaa na baada ya muda mfupi kulitupa,” alijibu Tenga.

“Kitu kingine?”
 
***

Baibui! Afande Chaku alishituka. Alikuwa kaketi katika meza yake, mikono yake ikiwa imeshikilia kichwa chake ambacho alikiona kizito kuliko ilivyokuwa kawaida yake. Alihisi hata akili yake kwamba ilikuwa kama iliyodata kutokana na uzito wa mambo.

Alikuwa amerejea hapa muda mrefu uliopita akitokea kwa bosi wake Matata ambaye alimlaki kwa kila aina ya vitisho, “Tulikupa siku tatu ambazo zinayoyoma. Leo mwisho. Hadi kesho usipokuwa na jambo la maana la kuripoti, nitatarajia barua yako ya kujiuzulu. Vinginevyo, utatoka kwa aibu.”

Kauli hiyo ilifuatia maelezo yake kwamba alikuwa hajapata jambo jipya la kumwarifu. Angemwarifu lipi? Taarifa za kujiona kuwa amefika mwisho wa njia katika jitihada zake za kupata walao chanzo cha mauaji yale. Pale alipobahatika kupata jina la King Suleiman katika mfuko wa marehemu, alipata hisia kuwa mtu huyo angekuwa mpenzi wa marehemu ambaye angekuwa na chochote cha kuwasaidia kupata kiini au chanzo cha kifo chake. Hivyo, mume wa marehemu alipothibitisha kwamba King Suleiman ni yeye kwa Chaku, ilikuwa kufika mwisho wa mkondo wa mwanzo wa kitendawili kipya.

Kama walikuwa wametengana na huku bado Cleopatra akiwa na ujumbe kama ule, ambao unathibitisha mapenzi yake ya dhati kwa mumewe, kitu gani basi kiliwatenganisha? Na ilikuwaje akawa na ujumbe ule wakati wa kifo chake? Swali juu ya swali. Yote yakimrejea Chaku kulekule kwenye swali zito zaidi; muuaji alimkusudia Rais au yule bepari?

Mtuhumiwa wa pili katika swala hilo, Dkt. Khalfan machoni mwa Chaku, hakuona haja ya kuendelea kumshuku. Mahojiano aliyoyafanya naye muda mfupi uliopita, mapenzi ambayo hayakuweza kufichika katika macho na sauti yake kwa marehemu na uwazi wake katika kujibu maswali ulimfanya Chaku amfute mara moja katika orodha ya watuhumiwa wake.

Mtu mwingine, ambaye angeweza kusaidia swala hili tayari alikuwa katika chumba cha maiti Muhimbili, mwandishi Frank Mwaipula. Kifo chake kilikuwa pigo jingine kwa Chaku na kiliacha maswali mengi kuliko majibu. Kwa tabia yake ya kupenda hafla mbalimbali na kwa maelezo toka kwa wataalamu waliochunguza picha za kamera za tukio hilo, haikuelekea kuwa alikuwa amepanga au kujiandaa kuupora ule mkoba.

Kuuawa kwake kinyama ndiko kulikoibua maswali mengi zaidi. Hakukuwa na shaka kuwa wauaji walilipora begi. Ya nini basi wafanye unyama mkubwa kama ule wa kumuua kikatili kana kwamba hawakuridhika na walichokifuata? Swali kubwa zaidi ambalo lilimsumbua ni iwapo mauaji haya yalikuwa na uhusiano wowote na yale ya Cleopatra. Binafsi, alihisi tofauti kubwa ya utekelezaji wa mauaji hayo. Kazi ya kumuua Cleopatra ilikuwa ya kitaalamu ambayo mtu anaweza kuiita kazi safi. Hata silaha iliyotumika haikuwa ya kubahatisha kama bastola ya kawaida iliyommaliza Mwaipula.

Chaku hakuona vipi angeweza kuyaeleza kwa ufasaha kwa bosi wake na yakaelezeka. Kwanza haikuwa tabia yake kujieleza kwa maneno zaidi ya vitendo, pia bosi wake, Inspekta Matata, hakuwa mtu mwenye sikio la kusikiliza blabla ndefu kama hizo.

“Inspekta, nitakapokuwa tayari, nitakueleza nilipofikia.” Chaku alimwambia.

“Hapo ndipo tunapotofautiana,” bosi wake alirukia. “Nilisema na ninarudia kusema kuwa nataka taarifa yako kwa kila hatua unayopiga. Kila hatua unayotarajia kupiga, sawa afisa?”

Chaku alimtazama kwa muda kabla hajakubali kwa sauti ya unyonge,”Sawa mkuu.”

Chaku aliporejea ofisini kwake, macho yake yalipokelewa na gazeti la mchana, Za moto moto, ambalo nakala yake ya siku hiyo iliwekwa mezani, mbele ya kiti chake ili asikose kuiona habari iliyopewa uzito wa juu, ilivyopambwa na gezeti hilo nusura imtie wazimu, MWANDISHI AUAWA KINYAMA, ilisomeka. Kwa mikono inayotetemeka kidogo Chaku aliinua gazeti hilo na kulisoma harakaharaka.

Kila kitu kilikuwa pale. Kitu ambacho kilitarajiwa kufichwa hadi wakati utapojiri, kilianikwa kwa mapana na marefu. Mwandishi alikiunganisha kifo hicho na kile kilichotokea mbele ya Rais, hoteli ya Sheraton, hasa pale alipoeleza kuwa inaaminika mwandishi huyo alipora begi la marehemu na kutoweka nalo. Kuna mashaka kuwa Ikulu inahusika na kifo hicho, kwamba aliweza kusoma siri ambazo hazikustahili kusomwa na mtu asiyekusudiwa, aya moja ya habari hizo ilisema.

Mhariri wa gazeti hilo hakuishia hapo. Aliandikia habari hiyo tahariri ndefu ambayo ilishutumu vikali jeshi la polisi na vyombo vingine vyote vya usalama kwa kushindwa kudhibiti usalama nchini. “Iweje raia mwema asiye na hatia auwawe mbele ya kadamnasi, mbele ya Rais, huku vyombo vya usalama vimelala usingizi? Kama angependa muuaji huyo angeshindwa nini kummaliza hata Rais wetu mpendwa huku wanaojiita wana usalama wakinywa bia zao katika mabaa? Tunadhani wakati umefika wa vyombo hivi kuvunjiliwa mbali… iliendelea tahariri hiyo ambayo Chaku hakuisoma hadi mwisho.

Alilitupa gazeti hilo chini na kuitisha kikao cha dharura.

“Nani kapeleka taarifa hii kwa waandishi?” aliuliza kwa sauti ndogo lakini iliyojaa hasira. Kama alivyotegemea hakuna aliyejitokeza kukubali. “Mnajua hili ni swala la kitaifa? Ni swala la kufa mtu au kupona? Na vichwa ambavyo vitaanza kukatwa viko humu humu. Changu kitaanza, vingine vitafuatia.”

Kila mtu alikuwa kimya.

“Namtaka mtu aliyefanya hujuma hii.” Chaku aliendelea. ‘Namtaka haraka.” Aliongeza, “Kila mtu afanye uchunguzi wake, kwa kujua taarifa hizi zilikuwa mikononi mwa nani na zilipelekwa kwa nani na nani. Sitojali wadhifa wala cheo cha yeyote anayehusika.”

Wakati kikao hicho kinaendelea ndipo askari mmoja alipopokea simu ambayo upande wa pili ulitaja kitu kama ‘baibui’ Afande Chaku alipata kumsikia Dkt. Khalfan akimzungumzia mwandishi wa kike aliyemfuata msibani kutafuta habari akiwa amevalia baibui jipya.

Chaku alisikiliza maongezi yao kwa muda kisha alimtaka afisa wake kuuliza baibui hili limeokotwa wapi.

“Anasema ni Mikocheni.”

“Muulize mtaa gani, na tukiohili limetokea lini?”

Mzungumzaji aliuliza na kisha kueleza, “Anasema ni mtaa wa Daima, hatua chache toka klabu ya Oasis, karibu na nyumba ya Hayati Cleopatra. Ni tukio la jana…”

“Nini?” Afande Chaku alishtuka. Alikumbuka kuwa klabu hiyo iko jirani na nyumba ya Dkt. Khalfan. “Nipe namba yake halafu mwambie akusubiri popotealipo. Tunalitaka baibui hilo haraka kabla halijashikwa na watu wengi. Pata kila kitu toka kwake.”

Afisa alikubali, aliandika namba hiyo na kuituma kwa Afande Chaku kwa njia ya meseji.

“Anaitwa nani?” Afande Chaku aliuliza akinukuu.

“Tenga Mfaume,” alijibu. “Ni mtumishi wa hoteli pale Hollyday Inn.” Afande Chaku alinukuu jina hilo kwenye simu yake na baadaye kuandika mawili matatu katika daftari lake dogo la mfukoni. Simu yake ya mkononi iliita wakati hajamaliza nukuu zake kikamilifu. Alikuwa Inspekta Matata.

“Umefanya nini?” alinguruma.

Afande Chaku hakuhitaji kuambiwa kuwa alikuwa tayari ameliona gazeti la mchana huo.

“Nimefanya nini?”

“Hujui ulichokifanya sio? Hujui kama unaiweka nchi rehani kwa kuvujisha habari nyeti kama hizi?”

Afande Chaku ahakujua amjibu nini. Aliamua kunyamaza akisikiliza kila aina ya vitisho, shutuma na laana kwa sauti iliyojaa pilipili. Alimaliza kwa kumpa Afande Chaku saa ishirini nan ne awe amempelekea jina na taarifa za uvujaji huo. Alikata simu kabla ya kusubiri hoja za upande wa pili.

Afande Chaku akakata simu yake pia na kujiinamia kwa muda. Alipoitazama saa yake alishangaa kuona ikimwashiria kuwa ilitimia kumi na robo. Kwa jinsi alivyochoka mwili na akili, hakukumbuka kula wala hakusikia njaa. Hata hivyo, ili kuilinda afya yake aliamua kuuendea mgahawa wa karibu ili apate walao glasi ya maziwa.

Wakati akijipatia kinywaji hicho kwa mishikaki miwili ya ng’ombe mara alimkumbuka Joram Kiango. Simba akizidiwa hula majani. Aliwaza wakati akitoa simu yake na kuitafuta namba yake. Aliipata.

Simu iliita mara mbili tatu kabla haijapokelewa. Kisha sauti ya kiume iliitika kwa kuuliza swali, “Nani mwenzangu?”
 
8

Taarifa ya kifo cha mwandishi wa habari, Mwaipula, ambacho kilihusishwa moja kwa moja na kifo cha Cleopatra kilizaa upya hamasa ya wananchi ya kutaka kujua kulikoni. Awali, kwa tabia ya Watanzania, baada ya siku mbili tatu za kuzungumza hili na lile, tukio lile lilianza kusahaulika na kuachiwa ‘wahusika.’ Maswali mengi na udadisi uliokuwa ukisumbua vichwa, kwa taarifa hii mpya, ulizaliwa upya miongoni mwa wanajamii walio wengi.

Mmoja kati ya watu hao alikuwa Joram Kiango. Alikuwa amejitahidi vilivyo kutohusisha fikra zake na tukio la mauaji ya Cleopatra, licha ya jitihada tele za Nuru kumshawishi. Habari za gazeti lile la jioni ambalo alikuwa na nakala yake mkononi, zilianza kumsisimua. Kama watu wengine alijikuta akianza kubanwa na shahuku ya kufahamu undani wa kinachoendelea. Hata hivyo, alijikumbusha tena na tena kuwa hakuwa na haja wala sababu ya kuingia katikati ya dimba hili. ‘Sio kazi yako.’ Alijikumbusha.

Hata hivyo, hakuweza kujizuia, pale alipopokea simu ya Afande Chaku akimtaka wakutane jionihiyo kwa ‘maongezi’ kidogo.

Joram Kiango alimfahamu Chaku katika sura zote mbili. Moja ilikuwa ile sura yake ya kitaaluma, iliyoainisha jinsi alivyokuwa mpelelezi shujaa, makini, mwenye akili za ziada. Sura yake ya pili ni ile ya mlevi, ambaye alikunywa kama samaki, kana kwamba alikusudia kujiua. Sura iliyomfanya mara nyingi ‘ajiachie’ kwa kusahau kula, kuoga, kubadili nguo na hata kupiga mswaki.

Joram Kiango hakupenda sana kukutana ana kwa ana na Chaku. Harufu ya jasho la mwili wake na ile ya pumzi yake toka mdomoni ilikuwa ikimsumbua sana, hasa kwa kuzingatia kwamba mengi kati ya maongezi yao yalikuwa ya kunong’ona ili yasifikie sikio la mtu mwingine. Lakini hakuwa na jinsi. Chaku alikuwa mmoja kati ya ‘sosi’ wake wakubwa waliommegea mambo ya ndani kabisa kila alipokuwa mhitaji. Si hilo tu hata uchambuzi na upembuzi wake wa mambo ulikuwa wa kiwango ambacho mara nyingi kiliamsha kitu katika ubongo wake mwenyewe.

Hayo, na kwa hili la kifo kingine cha kutatanisha, yalifanya Joram aafiki kukutana naye usiku huo. Mara nyingi safari kama hizi Joram alizoea kufuatana na Nuru, kufanya kila anayewaona awachukulie kama wapenzi walioamua kutoka. Leo alikuwa peke yake. Nuru alikuwa ameruka mara moja kwenda Nairobi ambako shirika moja la kimataifa liliwaalika kwa kazi maalumu. Joram hakujisikia kwenda Nairobi. Nuru angekutana nao kuona uzito na uhalali wa kazi yao kabla ya kuingia mkataba.

Afande Chaku alichagua meza ya mbali kidogo na jengo la hoteli. Aliketi pwani, juu ya mchanga, karibu kabisa na mawimbi ya bahari, akifaidi upepo mwanana ambao ulikuwa ukimpuliza mwilini. Juu ya meza yake palikuwa na chupa kubwa ya maji ya baridi ambayo tayari aliyanywa nusu. Mara kwa mara akiitazama saa yake ya mkononi na kubaini kuwa alikuwa na dakika kumi zaidi za kumsubiri Joram Kiango.

Chaku alifahamu fika kuwa alikuwa akivunja kiapo na maadili yote ya kazi yake kukutana na mtu kama Joram kwa nia ya kujadili swala nyeti kama hili. Kwa bahati mbaya, hakuwa na jinsi. Kifo cha mwandishi yule ambacho kwa kila namna kilihusiana na kifo cha Cleopatra kilifanya kazi ya uchunguzi iwe ngumu na ya hatari zaidi kila dakika iliyopita. Hivyo, alijikuta mhitaji wa kichwa kinachofikiri kwa upeo mpana zaidi katika masuala ya aina hii. Kichwa cha Joram Kiango kilikuwa muafaka zaidi.

Kitu kingine kilichomshawishi Chaku kuchua hatua hii ni ushirikiano wa ajabu aliokuwa akiupata toka kwa bosi wake, Inspekta Matata. Ushirikiano wake ulikuwa wa vitisho na unyanyasaji kwa kiwango ambacho Chaku alijisikia kumtia ngumi au risasi ya kichwa.

Kwa ujumla, ni hulka hii ya Matata iliyomfanya achukue tabia hii na ya kukutana na watu kama Joram na kuuza habari. Toka Matata alipomnyima fursa ya kuendelea na kesi zake nyeti, na toka alipoamua kumfanya hayawani kwa kutompa kazi yoyote muhimu Chaku alibadilika. Taarifa zote nyeti ambazo alihisi bosi wake alikusudia kuzikali, alizivujisha ama kwa akina Joram Kiango ama kwa wahariri walioaminika, jukumu ambalo alilifanya bila malipo zaidi ya kinywaji na alifarijika kwa hatua zilizofuatia.

Aliitazama tena saa yake. Bado alisaliwa na dakika tano kabla ya muda waliopeana na Joram. Akamimina maji katika glasi na kuyanywa taratibu huku akiyasafirisha macho yake kwenda baharini ambako taa za meli zilizokuwa zikisubiri kuingia bandarini na zile za vyombo vya wavuvi zilimulika kwa nuru za rangi mbalimbali. Alizitazama meli hizo kwa muda kabla hajapata hisia fulani ambazo zilimfanya ayarejeshe macho yaketoka baharini. Mtu mmoja aliyevaa koti na kofia pana za wachunga ng’ombe wa Texas alikuwa akijikaribisha kwenye kiti cha pili mezani hapo. Uso wake uliofichwa nusu ulikuwa na kitu kama tabasamu, ambalo halikuonekana kuwa mahala pake.

“Wewe nani?” Afande Chaku aliuliza.

Mgeni huyo alicheka kidogo kabla ya kusema, “Huitaji kunifahamu. Wewe sio Afande Chaku?”

“Kama ndiye?”

“Chukua hiyo!”

“Na hiyo!”

Joram Kiango alifika dakika tano zaidi ya muda walioafikiana. Mlolongo wa magari barabarani ulichangia kumchelewesha. Alitupa macheo eneo ambalo alimtarajia mwenyeji wake kuketi, akamwona akiwa amelalia meza. Hakushangaa. Hakupata kukutana na Afande Chaku akiwa hayuko taabani kwa ulevi. Kwa bahati, mar azote alilewa mwili tu, akili zke zilikuwa timamu sana kila walipoweka mezani kile kilichowakutanisha. Akamwita mhudumu mmoja na kumwagiza wiski toti nne na maji ya soda. Akamwelekeza wapi alete vinywaji hivyo, mwenyewe akitangulia.

Joram Kiango aliketi kwenye kiti kilichomwelekea Afande Chaku. “Wewe mlevi,” aliita. “Utakunywa kama samaki hadi lini?” Hakuitikiwa. Kisha akapata hisia nyingine. Afande Chaku alikuwa hanuki pombe wala sigara kama ilivyokuwa kawaida yake. Zaidi alikuwa msafi, ndani ya suti yake nzuri nyeusi. Nywele zake pia zilichanwa vizuri.

“Vipi? Umekesha wiki nzima hadi ulale baa?” alihoji tena. Afande Chaku hakujibu. Joram akamtazama kwa makini. Mara akabaini kitu. Afande Chaku alikuwa hapumui!Joram akanyoosha mkono wake na kumgusa kwa mgongo wa kiganja chake. Afande Chaku alikuwa amepoa! Si hilo tu, kwa nuru hafifu iliyokuwa eneo hilo Joram Kiango aliweza kuona michirizi miwili ya ujiuji mweusi uliokuwa ukichomoza chini ya kifua chake na kuelekea katika uso wake uliolala juu ya meza.

Ilikuwa damu.

Kiasi Joram Kiango alishtuka. Kati ya yote aliyotegema katika ujio wake hilo halikuwemo. Huku akiwa bado amekaa, kana kwamba hakuna kilichotokea Joram Kiango aligeuka na kutazama huko na huko. Watu wa karibu zaidi walikuwa meza ya tano kutoka hapo; vijana wawili wa kiume walikuwa katika harakati za kuvinjari mwili wa msichana wao kwa zamu. Joram Kiango akageuka na kumtazama tena Chaku ambaye sasa alikuwa marehemu. Akamsogelea taratibu na kumkagua mfuko baada ya mfuko. Katika mfuko wa koti alitoa daftari dogo la kumbukumbu, kalamu na kadi mbili tatu za biashara. Akavichukua vitu hivyo na kuvitia mfukoni mwake. Katika mfuko wa ndani wa koti Joram alikuta bastola na pochi. Akaiacha bastola na kuchukua pochi. Mifuko ya suruali haikuwa na chochote cha muhimu zaidi ya noti mbili tatu za elfu kumi kumi. Joram aliziacha. Alitazama huko na huko kabla ya kuanza kuondoka kwa mwendo wa utulivu.

Hatua tatu nne baadaye alikutana na muhudumu ambaye alikuwa akimletea vinywaji vyake.

“Vipi mzee? Nimechelewa?” Mhudumu huyo alimwuliza.

“Hapana, hujachelewa. Niwekee pale, nakuja.”

Joram Kiango aliongeza mwendo hadi alipofikia gari lake. Alilitia moto, akaligeuza na kuondoka kwa mwendo wa kasi.
 
Mchana huo Tenga alijisikiafaraja kuliko kulikoilivyopata kumtokea maisha yakeyote. Alihisi milango na madirisha yote yaliyofunga maisha yake ikifunguka na kuruhusu nuru mpya ambayo iliahidi maisha mapya na neema mpya.

Faraja hiyoilikiteka kichwa cha Mfaume Tenga tangu pale alipopokea simu toka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa anaitwa Afande Chaku. Mtu huyu, awali alitaka kumsimulia kwa tuo juu ya kile alichopata kumweleza yule mpelelezi aliyefika hotelini. Alikuwa msikilizaji mzuri na alimtupia maswali ambayo yalimfanya Mfaume afikiri kwa upeo mpana zaidi juu ya suala la mrembo huyo. Aidha sauti yake ilikuwa na kila dalili ya madaraka bila chembe zozote za ukingaufu, sauti ambayo ilimfanya Mfaume aitii pale msemaji huyo alipomtaka kumfuatilia mama yule kwa makini zaidi na kwa uangalifu zaidi.

“Angalia, fanya kila jitihada asishuku kuwa unamchunguza. Tumia kipaji chako cha kuzaliwa.” Ilisema sauti toka upande wa pili wa simu. Ni hiyo iliyomtia uhai mpya Mfaume. Na alianza kazi mara moja.

Kwa tabia ya mgeni yule, Mfaume aliamini kuwa alikuwa chumbani kwake ambako alitoka kwa nadra sana. Hakuna sababu ya kuendelea kusubiri hadi atakapotoka ili amfuatilie. Aliamua kumtembelea. Akamfuata msichana wa mapokezi nakumshawishi hadi akatoa kadi ya akiba ya kufungulia mlango wa chumba hicho. Kisha, alichukua dawa ya mbu ya kupuliza na kuelekea chumbani humo. Alikandamiza kadi mlangoni na mara ukafunguka. Aliusukuma na kuingia ghafla.

Mfaume alitegemea kumshtua mgeni huyo, kisha ajitetee kwamba hakujua kama chumbani humo kuna mtu. Ikaondokea kuwa kinyume chake. Ni Mfaume aliyeshtuka na kupigwa bumbuazi kubwa kwa kile alichokiona.

Aliduwaa macho yakiwa yamemtoka pima.

“Ingia!” Sauti ya mwanamama huyo ilimwamuru. Aliposita, mkono wake wenye nguvu ambazo Mfaume hakuzitegemea ulimvuta ndani na kumbwaga kwenye kochi huku mlango ukijifunga nyuma yake.

Tangu nilipotoka katika nyumba ya marehemu kengele za kuashiria hatari zilisumbua ubongo wangu. Niliweza kupumua kidogo mara baada ya kuvua lile baibui na kulitupa katika pipa la taka. Nilipumua zaidi baada ya kufika hotelini na kujifungia chumbani kwangu ambako sikuwa na muda wa kupoteza. Niliingia katika kazi ngumu ya kuuvua usichana na kuvaa uvulana. Nilianza kwa kuyabandua matiti yangu ya bandia yaliyogharimu zaidi ya dola elfu ishirini kuyaunda. Nikayahifadhi katika mfukowake ulioandikwa free style pad na kisha kuyahifadhi katika begi. Nikalibandua wigi langu lenye thamani ya juu vile vile na kulihifadhi. Baadaye nilianza kazi ngumu ya kubandua ile ngozi ya bandia iliyoficha mwili wangu wa asili,kazi ambayo ilihitaji uangalifu mkubwa na utulivu wa hali ya juu,hasa ikizingatiwa kuwa gundi niliyotumia ilikuwa imara sana.

Nilikuwa tayari nusu msichana nusu mvulana pale mlango ulipofunguka bila kugongwa na uso wa mtumishi mmoja wa hotelini hapo kuchungulia. Niliduwaa, lakini si kwa kiwango alichoduwaa yeye. Alitokwa na macho, mwili wake ukiwa kama ulioshikwa ganzi na kuishiwa nguvu. Kwa upande wangu niliwaza harakaharaka. “Ingia,” Nilimwamuru. Alipochelewa kidogo kutii amri yangu nilimsaidia kwa kumkwida shati na kumvuta ndani kwa kono langu, kono la Jibril. Aliangukia kwenye kochi. Nikafunga tena mlango, nikiongeza na komeo za mkono. Kisha, nikamwendea mgeni huyo na kumtazama kwa makini. Sura yake haikuwa ngeni machoni mwangu. Mara mbili tatu nilipata kumfumania akinitazama kwa namna ya kuhitaji kitu cha ziada toka kwangu. Hata maneno yake, kila alipopata fursa ya kuzungumza nami alionyesha kunitaka sana.

Sasa alikuwa akinitazama kwa namna tofauti kabisa. Mwili wake ulilowa jasho huku ukitetemeka mithili ya kinda la ndege. Macho yalimtoka pima kana kwamba yanatazamana ana kwa ana na Zirael mtoa roho za watu.

Haikuwa uongo. Alikuwa amekitafuta kifo kwa nguvu zake mwenyewe na amekipata. Hofu iliyogubika macho yake ilifanya nitamani kucheka. Lakini kicheko kilikuwa mbali na nafsi yangu kwa siku na wakati huo. Nilitamani kumhurumia, lakini huruma pia ilipaa kitambo na kutoweka tangu alipofungua mlango na kunikuta katika hali ile.

“Ulijua unatafuta nini kwangu?” Nilimuuliza nikimsogelea taratibu.

Alifungua mdomo, akashindwa kutoa sauti.

Hali yake ilifanya nikumbuke mhanga wangu wa kwanza tangu nilipoingia katika shughuli hizi, mara baada ya kuhitimu. Nadhani lilikuwa sehemu ya jaribio lililoandaliwa rasmi na wakufunzi wangu ili kuona ukamilifu wangu.

Mhanga alikuwa mwanamume wa umri wa kati, mwenye asili ya Kiarabu. Wakati nakabidhiwa jukumu hilomhanga huyo, Abdul Karim Shahibu, alikuwa mjini Paris, katika hoteli moja ya kifahari iliyoitwa Le Monde. Nilipewa jina lake, namba ya chumba chake na changu ambacho kilielekeana naye. Nilipewa jina langu pia la hotelini hapo; Beauty Masondo, mtoto wa tajiiri mmoja wa madininchini Malawi. Nilipewa wiki moja tu, kumaliza kazi hiyo, mimi nilitumia siku mbili tu.

Nilijibadili kuwa msichana mrembo mwenye miguu mirefu, mipaja ya haja na mwendo wa kinyonga. Aidha, nilivaa nguo fupi, viatu vya mchuchumio na blauzi ambayo iliruhusu sehemu ndogo ya matiti yangu ya bandia kuonekana.

Mwarabu aliniona toka siku ya kwanza tu nilipoingia hotelini humo. Nilichokiona katika macho yake wakati akinitzama toka unyayo hadi utosi kilinifanya nifahamu mapema kuwa sikuwa na kazi kubwa. Jioni hiyo hiyo tulikutana tena mlangoni, yeye akitoka mie nikiingia chumbani kwangu. Alinisalimu kwa Kiingereza, nikamjibu kwa Kiarabu. Hakuamini masikio yake. Alipozungumza maneno mengine mawili matatu na mie kumjibu kwa ufasaha, alichangamka zaidi. Alinikaribisha kwenye mlo wa jioni hiyo.

Inshallah, nilimjibu.

Kesho yake siku nzima hakuisha kunipigia simu. Ya kwanza nilipokea na kumshauri tusubiri jioni. Hadi jioni inafika alikwisha nipigia mara tatu zaidi. Mara hoo nakusalimu, mara nakukumbusha na kadhalika. Nilienda chumbani kwake saa moja kasoro za jioni hiyo. Nilimkuta akinisubiri, kavaa joho la kulalia, ndani akiwa hana vazi jingine. Alinitia kichefuchefu, palepale nikawa nimemchukia.

“Taratibu!” nilimwambia nikijitia kucheka huku nikiukwanyua mkono wangu ambao aliunasa na kuuelekeza mahala fulani katikati ya miguu yake.

Chumba chake kilikuwa kama baa. Niliweza kuona kila aina ya vinywaji toka pombe kali, mvinyo hadi vinywaji laini. Juu ya meza yake ndogo kulikuwa na chupa mbili tupu za John Walker. Macho na sauti yake pia ilionyesha kuwa vinywaji hivyo vilikuwa vikifanya kazi yake vyema kichwani mwake.

Alinitaka tufahamiane, mwenyewe akijieleza kwa ufupi tu kwamba ni mfanyabiashara wa mafuta aliyekuja mapumzikoni. Mie pia nilimweleza kwa ufupi kwamba nipo likizo nikitokea Ugiriki ambako nachukuwa shahada yangu ya pili.

“Good.” Alisema akinikumbatia na kunibusu kwa domo lake lililojaa harufu ya pombe. Alianza kupeleka mikono yake katika sehemu zangu za hatari. Sikuwa tayari kuendelea kustahimili. Niliinuka na kujifanya navua nguo. Nikamwona akitabasamu, tabasamu ambalo lilitoweka ghafla pale alipoanguka sakafuni, kifudifudi. Hakujua nini kilimpiga.

Nilimgeuza chali na kumwagia wiski nyingine juu ya shati lake, nikichanganya na unga wa kokeni niliokuwa nao. Baada ya kuhakikisha kuwa hakukuwepo na dalili yoyote ya uwepo wangu chumbani humo, nilitoka nikiufunga mlango wake taratibu na kuufungua wangu. Saa mbili baadaye tayari nilikuwa angani nikipaa kuelekea London ambako ningesubiri maelekezo mengine.

Siku mbili baadaye niliiona picha ya mhanga huyo katika kurasa za mbele za magazeti mbalimbali. Alielezewa kama mrithi pekee wa mmoja wa wafalme wa falme za kiarabu, aliyekuwa safarini Ulaya kwa nia ya kuvunja mikataba yao na makampuni ya Kimarekani yanayochimba mafuta katika visima tisini vya baba yake, ili apate wabia wapya. Kifo chake kilielezwa kuwa kilitokana na ulevi wa kupindukia na matumizi makubwa ya dawa za kulevya.

Nilichekea tumboni.
 
Huku hujatenda haki na wala sijaielewa vizuri
Hii ni double story. Muuaji anaelezea safari yake ya kuua mpk alipofika hapo at the same tym anaendelea na kisa chake cha upelelezi wa mauaji yake mwenyewe.
 
***

Msichana aliyekuwa mapokezi Hollyday Inn alishangaa kidogo alipomwona kijana mrefu wa kiume akivuta begi lake kutoka nje ya hoteli. Hakukumbuka aliingia lini wala hakujua alitokea chumba kipi. Alimtazama toka aliposhuka kutoka katika lifti na kisha kutembea taratibu kuelekea lango kuu.

Mgeni huyo alipomfikia alimsalimu na kumuaga kwa alama ya dole huku akitabasamu. Alipita hadi nje ambako alionekana akiita gari mojawapo la teksi za hotelini hapo, akaingia. Gari ikatiwa moto na kutokomea.

Mara msichana huyo akamkumbuka Mfaume. Alitazama eneo la kadi wanayoita ‘malaya’ ambayo aliichukua. Ilikuwa haijarudishwa. Hilo lilimtia wasiwasi. Kwa kawaida, kadi hiyo hutumika kwa amri ya Meneja wa hoteli tu, pale mgeni anaposahau na kuifungia yake chumbani au kuondoka nayo. Alikuwa amemwamini Mfaume kwa kujua kuwa ingemchukua dakika chache tu kuirejesha.

Kisha, msichana huyo akabaini kitu gani kilimfanya amkumbuke Tenga Mfaume. Ni shati alilovaa yule mgeni aliyetoka punde. Lilifanana sana na shati alilovaa Tenga Mfaume siku hiyo, shati ambalo siku zote amekuwa akijitapa hotelini hapo kwamba ni yeye pekee aliyekuwa nalo nchini. Lilikuwa moja ya zawadi zake nyingi ambazo alizipokea toka kwa rafiki zake mbalimbali wa ughaibuni waliopata kulala hotelini humo.

“Shati la milionea.” Mara kwa mara Tenga Mfaume alitamka.
















9

Moto ulilipuka upya kufuatia kifo cha Afande Chaku. Vigogo wa kamati maalumu iliyokuwa ikitafuta ufumbuzi wa kifo cha kutatanisha cha Bi. Cleopatra walikuwa bado hawajajinasua katika jinamizi la mwandishi wa habari ambaye walimtegemea kuwa ufunguo la sakata zima kwa kiwango fulani. Wakiwa bado wanalitafakari hilo mara yameibuka mengine. Mpelelezi mahiri, aliyetwishwa mzigo wa kuongoza timu mahususi ya kutafuta ufumbuzi naye ameuawa kinyama muda mfupi uliopita!

Taarifa za kifo chake ziliwasilishwa na Inspekta Matata katika kikao cha dharura kilichoitishwa usiku huo. Kwa mujibu wa maelezo yake kikaoni hapo maiti ya Chaku iligunduliwa katika hoteli ya Sunlight ya ufukwe wa bahari maeneo ya Msasani. Mmoja wa wahudumu wa hotelini hapo, ambaye alimuhudumia marehemu aliuarifu uongozi wa hoteli mara alipobaini kuwa alikuwa akizungumza na maiti wakati akijaribu kumwamsha ili amlipe pesa za vinywaji alivyotumia. Alihisi mteja wake huyo alikuwa marehemu pale alipomgusa kifuani na kushangazwa na jinsi alivyopoa. Baadae aliona damu iliyoganda kwenye kifua chake, ambayo marehemu aliilalia. Kijana huyo alikuwa jasiri wa kutozungumza hadharani tukio hilo hadi alipompeleka chemba meneja wake ambaye baada ya kuthibitisha aliitarifu polisi.

“Maiti amechukuliwa bila ya wateja wala wafanyakazi wengine kujua.kwao walidhani ni mlevi mmoja aliyezidiwa anabebwa kupelekwa nyumbani kwake.” Matata alikitaarifu kikao.

Wenzake, waliopigwa butwaa walimtazama kwa macho yaliyojaa maelfu ya maswali. Mkuu wa majeshi alikuwa wa kwanza kuyaweka maswali yake hadharani. “Kwasasa kinachoendelea ni kipi?” Alimuuliza.

“Kwanza tulichokifanya ni kumuhifadhi meneja wa hoteli na msaidizi wake. Tunaamini watatusaidia sana.” Alijibu.

“Kuwahifadhi kwa maana ya kuwatia ndani, sio?” Mkuu huyo wa majeshi aliuliza.

Inspekta Matata alikubali kwa kichwa kabla hajaongeza, “Wako ndani, lakini katika mazingira tofauti. Wako chumba cha peke yao, wanakula na kunywa wanachotaka.”

“Kwanini umewaweka ndani?” Kigogo mwingine aliingilia kati.

“Kwa usalama wao na wetu pia.” Matata alimjibu kwa sauti ambayo ilimwonyesha kila mtu katika meza hiyo ya mviringo ahisi anavyojisikia; mtaalamu anayezungumza na makinda katika taaluma hiyo.

“Fafanua…” Kigogo yule alisisitiza.

“Nini?”

“Hayo madai ya usalama wao na wetu. Sijakuelewa.

Matata alitabasamu kidogo kabla hajaeleza, “Hakuna anayejua Afande ameuawa na nani. Ni wao peke yao pamoja na muuaji wanaojua kuwa afisa muhimu kama yule ameuawa. Hivyo, tuliona ni hatari kuwaacha mitaani kabla upepo haujatulia.” Alikohoa kidogo. Akaendelea, “Hali kadhalika, wanao mwelekeo wa kutusaidia sana. Yule mhudumu anadhani kuwa alimuona muuaji na kuzungumza naye na kuwa anaweza kumtambua wakati wowote. Kwamba ni mtu mrefu na mtulivu aliyekwenda hotelini humo na kumuomba huduma ya kinywaji ambayo aliitaka ipelekwe ufukweni ambako marehemu aliketi peke yake. Kisha, alienda akaketi meza moja na merehemu. Wakati anampelekea oda yake mhudumu anadai alipishana na mteja huyo akiwa na haraka. Awali, alidhani kuwa anaelekea maliwatoni lakini alipoona kimya ndipo alipoiendea meza ile na kutoa vinywaji ambavyo havikutumika na kumdai Afande Chaku.”

Wenzake walimkazia macho. Alikuwa akisema ukweli lakini ukweli huo haukuweza kuwaridhisha. Mjumbe mmoja alishindwa kustahimili, “Nikuambie kitu Inspekta?” hata kabla ya kusubiri jibu la Matata aliendelea. “Maelezo yako ni matamu sana lakini vitendo hatuvioni. Sidhani kama kuna yeyote kati yetu aliyekutarajia kuwa mtoa habari za matukio badala ya ufumbuzi. Mtu kauawa mbele ya Rais, tunataka kujua kama muuaji alimkusudia Rais au la. Aidha, tunamtaka muuaji huyo akamatwe. Tulichoambulia kwako ni taarifa ya kifo kingine, ambacho kinahusiana sana na cha Cleopatra. Haya, hata kabla hilo pia kupatiwa ufumbuzi leo unatuletea taarifa nyingine ya kutisha zaidi; kuuawa kwa mpelelezi wako mkuu katika sakata hili. Mimi binafsi nasikitika kuwa naanza kupoteza imani na uwezo wako.”

Matata alijaribu kutabasamu kuficha hasira kali iliyompanda ghafla na kumpanda kooni. Tabasamu lilikataa. Akaishia kumkazia macho mjumbe huyo. Alikasirika zaidi alipowatazama wajumbe wengine na kuona wakitikisa vichwa kumuunga mwenzao mkono.

“Nadhani huu ni wakati wa kufikiria kung’atuka,” alinong’ona kwa sauti dhaifu.

***

Masudi Kipanya, Patrick Mgata, David Chikoko na wengineo walikuwa miongoni mwa wachoraji mashuhuri sita walioshangazwa na kitendo cha polisi kuwataka msaada. Kwa utamaduni wa Tanzania kuwasaidia polisi kuna maana moja tu, kukamatwa, kuwekwa rumande na kuanza kumiminiwa maswali na vitisho. Hivyo ilimshangaza kila mmoja wao, alfajiri hiyo walipotembelewa na polisi waliovaa kiraia.

“Kipanya?”

“Masoud Kipanya anaishi kwenye kurasa za magazeti.” Aliwajibu.

Polisi walicheka. Mmoja wao alitoa kitambulisho chake.

“Tunahitaji msaada wako. Unaweza kuvaa mara moja tutoke?” alieleza.

Moyo wake ulipoteza mapigo. Hata hivyo, sauti yake haikupotezan usanii pale alipowauliza, “Mbona hamna pingu?”

“Za nini”

Alioga upesiupesi, akabadili nguo toka katika mavazi ya kulalia na kisha kuongozwa kwenye gari lililokuwa na namba za kiraia. Ni humo alimowakuta wakina Chikoko na Mgatta. Tofauti na alivyotegemea, badala ya kupelekwa Kituo cha Kati, gari ilielekezwa nje ya mji likifuata njia ya Bagamoyo. Lilichepuka na kuelekea kulia hadi katika Hoteli ya Kunduchi ambako lilisimama. Walielekezwa katika moja wapo ya vyumba vya mikutano ambako waliombwa kujisikia huru.

“Tunahitaji msaada wenu katika suala nyeti la kitaifa.” Mmoja wa maafisa waliowaleta alieleza. “Jana kama saa kumi hivi zilizopita mtu mmoja muhimu sana ameuawa.Hapa tunaye mtu mmoja ambaye anaamini alimwona muuaji. Tumempa mamia ya picha za watuhumiwa sugu wa mauaji, ndani na nje ya nchi, hakuweza kumtambua. Hivyo, nyie kama wachoraji, tunadhani mkikaa naye na kumsikiliza huku mkifanya uchawi wenu kwenye makaratasi au kompyuta bila shaka tutaipata sura yake halisi.”

Kwa mara ya kwanza wachoraji hao walitabasamu kwa dhati. Kwa gharama za jeshi la polisi walipatiwa kifungua kinywa cha haja. “Ambaye hachori bila kutia vitu vikali tumboni anaruhusiwa kunywa chochote anachotaka.” Mwenyeji wao alizidi kuwakarimu.

Saa moja baadaye, mhudumu ambaye alikuwa akiwasaidia polisi kumpata mtuhumiwa alitambulishwa kwao. Kwa kila hali alikuwa taabani, kukesha, maswali elfu moja na moja aliyoulizwa na tukio la kuona maiti ya mtu bila kutegemea vilikuwa vimemmaliza. Hata hivyo, baada ya nusu saa ya mizaha ya wachoraji hao, chai ya nguvu na kushushia bia mbili baridi, alichangamka.

Aina nyingine ya maswali ikaanza.

“Pua pana kama hii?”

“Hapana, imechongoka kidogo.”

“Miwani?”

“Hakuwa nayo.”

“Nywele?”

“Fupi tu za kawaida.”

Na kadhalika na kadhalika. Ilitayarishwa michoro aina aina. Mhudumu huyo, ambaye baadaye alifahamika kuwa aliitwa Mwanakatwe, alitoa ushirikiano kwa kila mchoraji. Alitazama kila mchoro wa awali na kukanusha hapa na kuelekeza pale.

Siku ilipita bila mafanikio.

Siku ya pili matumaini yalianza kuonekana. Mwanakatwe alianza kutoa maelezo madogomadogo. “Urefu huu una tofauti kidogo… viatu vilikuwa vyeusi… na kadhalika. Wachoraji wawili walimtia matumaini zaidi. Alitazama picha zao kwa makini, nuru ya utambuzi ikizidi kuchanua katika macho yake.

Michoro hiyo ilipowekwa katika kompyuta na utaalamu wa Coral drawing na graphic designing kutumika baada ya marekebisho mawili matatu, Mwanakatwe aliangua kicheko.

“Ni huyu hapa,” alisema

Kipanya na Mgatta walitazamana kwa mshangao.

Maafisa wa upelelezi walipoitwa kutazama michoro hiyo miwili ambayo Mwanakatwe aliafikiana nao, wao pia walitazamana kwa mshangao. Walichukuana chemba ambapo mmoja alimuuliza mwenzake, “Nadhani unamfahamu mtuhumiwa wetu.”

“Bila shaka. Si mwingine zaidi ya Joram Kiango.”

“Inawezekana?”

“Nani anajua?” alimjibu.

***

“Joram Kiango!” ilinguruma sauti ya kigogo mwingine. “Ni Joram Kiango! Na bado mmekubali kumwacha hai katika swala nyeti kama hili! Mnajua mmefanya kosa ambalo tutalijutia maisha yetu yote?”

Inspekta Matata alimjua fika Joram Kiango. Kwa kiasi fulani, alimchukia kama ilivyokuwa kwa vigogo wenzake wengi wenye mengi ya kuficha. Ushoga wa siri ulioanza baina ya Inspekta mstaafu, Kombora ni moja ya mambo yaliyofanya mzee yule ajikute akistaafishwa mapema wakati alikuwa bado na nguvu na akili zake timamu. Moja ya ajenda alizopewa Matata ni kufuta kabisa Ujoram Kiango katika Jhamuhuri ya Tanzania. Hivyo yeye pia angeshusha pumzi kama bastola iliyomwondoa Chaku ingefanya hivyo kwa Joram Kiango pia. Kwa bahati mbaya, haikufahamika mapema kuwa mgeni ambaye alikuwa akitarajiwa na Afande Chaku angekuwa Joram Kiango. Kamwe asingeondoka akiwa hai.

Kwa sauti, Matata alisema, “Haikufahamika mapema. Lakini maadamu hili limetokea, tayari amejiweka katika mstari wa shabaha. Toka kesho soma magazeti, tazama televisheni uone. Hata kama atajifanya panya ajichimbie ardhini kama Saddam Hussein tutamchoropoa na kumfunga mdomo kabla hajaufungua.

Msikilizaji wake alimtazama kwa macho yenye mashaka. Akasema, “Inspekta, nadhani unamfahamu Joram Kiango. Kamwe si mtu wa kubeza na wala hatabiriki.”

“Namjua sana,” Matata alisema akitabasamu. “Ni play boy tu mwenye bahati. Naona bahati yake imefika ukingoni. Tulia uone.”

Kimya kifupi kilitawala kati yao. Mmoja akaitazama saa yake, wa pili akiwa amejiinamia. Aliyeinama aliinuka na kutazama huko na huko. Yeye pia aliitazama saa yake kabla hajasema, “Nadhani sina budi kuondoka.” Kisha, kama aliyekumbuka jambo aliketi tena na kumkazia macho Inspekta Matata. “Sidhani kama nina haki ya kukufundisha wajibu wako. Lakini kuna swala hili la huyu mtu ambaye tayari tumemtumia mara mbili, kumwondoa yule mwandishi na sasa afisa wa upelelezi. Unadhani tuko salama kuwa na mtu anayefahamu yote hayo miongoni mwetu?”

Matata aliangua kicheko, “Yule niachie mimi. Tutampa ujira wake wa mwisho kati ya leo na kesho. Ataupokea lakini hatautumia. Tayari amejichimbia kaburi lake mwenyewe.

“Nani ataifanya kazi hiyo?”

“Niachie mimi.”

Mgeni aliinuka tena, kisha akakumbuka jambo jingine na kumkazia macho Matata, “Hili ni kati ya mimi na wewe. Niambie tafadhali. Nani aliyemuua Cleopatra?

Inspekta Matata alicheka kidogo kabla ya kumjibu, “Sijui.”

“Una uhakika?” Kigogo alisisitiza.

“Kwanini nikudanganye?” alimjibu kwa swali jingine.

Kigogo alimtazama kwa macho ya kumsoma rohoni. Chochote alichokitafuta katika uso huo hakukipata. Akageuka na kuanza kuondoka. Matata akabonyeza tufe chini ya meza yake, sehemu ya ukuta ikafunguka na kuruhusu mlango wa lifti kufunguka, mgeni akaingia na kupaa toka katika chumba hicho cha siri hadi ghorofa ya pili ambako ilifunguka naye kutoka. Akatumia ngazi kushuka hadi chini ambako mlango wa kioo ulifunguka wenyewe mara alipoukaribia. Alipita ndani ya bustani kubwa yenye miti na maua mbalimbali hadi alipoliacha gari lake. Akalitia moto. Geti la lango kuu lilifunguka lenyewe vilevile kwa harufu au uzito wa gari lake, ingawa mlinzi mwenye sare za kampuni moja ya ulinzi aliketi pale akisoma gazeti.

Kigogo aliingia mitaani na kutokomea.

Matata alimtazama mgeni wake katika screen maalumu hadi alipotokomea mitaani. Screen hiyo ni moja ya vitu ambavyo vilikuwa siri hata kwa mkewe katika jumba hilo. Siri nyingine ilikuwa chumba hicho cha chini ya ardhi. Ni watu wachache sana waliofahamu uwepo wake. Na wachache zaidi walioweza kukifungua. Mhandisi aliyeongoza ujenzi huo alikufa kitambo kwa ajali ya gari. Msaidizi wake aliuawa na majambazi nyumbani kwake.

Machoni mwa wapiti njia, nyumba hii ilikuwa ya kawaida tu, yenye ghorofa mbili, ambayo kama nyumba nyingine nyingi jijini Dar es Salaam iliota na kupaa kama uyoga. Hakuna aliyefahamu fika jinsi ilivyokuwa ndani.

Kama ilivyokuwa kwa mwenye nyumba, machoni mwa watu wengi alikuwa Afisa wa juu wa ama jeshi la polisi ama usalama aliyekuwa akiongoza kitengo nyeti ambacho haakikutofautiana sana na kile cha polisi wa kimataifa INTERPOL. Kwa sura alikuwa mtu makini, mzalendo halisi, aliyekuwa tayari kupoteza maisha yake kulinda maslahi ya nchi yake. Lakini, kwa sura yake ya pili, ambayo daima ilifichwa katika kinyago cha umakini na uzito wa majukumu, alikuwa mtu wa kuogopwa. Toka miaka ya themanini, fisadi alipogeuka shujaa, uongozi ulipoanza kununuliwa kwa pesa, huku aibu ya kufanya madhambi ikizidi kuyoyoma; Matata alijikuta katikati ya dimba hilo. Alifanya chochote kilichomwongezea chochote, mradi mfuko wake wa mafichoni ulizidi kutuna. Wakorofi wengi waliokwenda kinyume cha matakwa ya watu wake ama walifutika duniani ama waliozea gerezani; wawili watatu walipata kuponyoka na kukimbilia nje ya nchi ambako hawakupata hali ya kutia tena miguu yao katika ardhi ya nchi yao. Mmoja kati yao tayari amefia huko ugenini kwa ajali yenye utata.

Zamani kidogo tatizo la Matata lilikuwa fedha, namna ya kuzipata. Sasa tatizo lake halikuwa fedha isipokuwa namna ya kuzitumia. Ingawa siku hizi haikuwa tena aibu kutangaza utajiri wake japo mchafu kiasi gani, bado kwa nafasi yake fursa hiyo hakuwa nayo. Kwa majina ya ndugu zake na watoto wake tayari alijenga hoteli nne za kitalii. Alikuwa na hisa nzito katika kampuni mbili za uwindaji, ikiwa ni pamoja na kumiliki hekta elfu kumi za ardhi ya kitalii. Nchini Kenya na Afrika Kusini alikuwa na majengo ya ghorofa kumi na tano yaliyotumika kibiashara. Pamoja na miradi yote hiyo kutumia fedha bado lilikuwa tatizo. Swala la mfuko wa madeni ya nje, EPA, swala la Richmond, mikataba tata ya madini na uwindaji kharamu ni miongoni mwa maswala ambayo yalikuwa yamemmwagia neema zaidi na zaidi. Dola za marekani bilioni mbili alizopokea katika harakati za kuziba na kuzibua mambo zilikuwa na miezi tele chumbani humu zikisumbua kichwa chake.

Katikakati ya fanaka zote hizo yule mwanamke wa Ikulu akafumuliwa kichwa. Halafu, toka kusikojulikana anaibuka huyu mtu anayejiita Joram Kiango.

“Atanitambua,” Inspekta Matata aliapa kimyakimya.

***

Mara nyingi Joram Kiango aliwapuuza polisi,lakini kamwe hakupata kuwadharau, hasa pale inapotokea mmoja wao kuuawa kinyama huku akiwa katikati ya suala nyeti, polisi, kama nzige au nyuki waliolala, huamka na kuanza mashambulizi makali kushoto na kulia.

Joram Kiango alilitegemea sana hilokwa kifo cha Afande Chaku. Ni kwa kuamini hivyo ndipo mara tu alipoiacha maiti ya Chaku alifanya haraka kurudi nyumbani kwake ambako alitumia dakika zisizozidi ishirini tu kuchukua vifaa alivyovihitaji; kompyuta yake ya mapajani, bastola, mabomu mawili ya machozi, suitcase yenye mavazi yake ya kazi ainaaina na nyaraka zake nyeti. Kisha alitegesha alarm yake ambayo humwarifu mara chumba chake kinapotembelewa na mtu ambaye hakumtegemea. Muda mfupi baadaye alifungia gari yake katika gereji na kwa kupitia mlango wa uani aliingia mitaani.

Dar es Salaam ina hoteli bubu nyingi sana. Baadhi zikiwa katika maeneo duni ambayo hayafikiki kwa gari isipokuwa vichochoro vya njia ya miguu. Moja ya hoteli hizo iliitwa Darajani Inn. Iko katika mtaa wa Manda, Magomeni, katikati ya uchochoro maarufu unaoiunganisha Magomeni na Kigogo, Mburahati hadi Luanga. Akiwa amefunika kichwa chake kwa kofia pana ya wachunga ng’ombe na sehemu kubwa ya uso wake kwa miwani mieusi, hakuna aliyeweza kumtambua mara moja. Alipatiwa chumba cha uani ambamo alishangaa kubaini kuwa kulikuwa na bafu na choo cha kujitegemea huku maji yakitoka katika mabomba kama kawaida. Aidha, kulikuwa na televisheni ndogo ambayo mwenyeji wake aliiwasha kumtia matumaini zaidi.

“Tukuletee nini, mzee?” tuna bia kila aina na kuku wa kukaanga.” Mhudumu huyo, mvulana wa miaka ishirini na mitano, aliuliza.

Joram Kiango alikuwa na njaa. Alikuwa na kiu vilevile. Lakini njaa na kiu yake kubwa zaidi ilikua kuijua hatma yake katika mkasa huu. Hivyo, alimruhusu kijana huyo kwa kumwambia kuwa pindi atakapohitaji chochote atamwarifu.

Mara kijana huyo alipotoka, Joram Kiango aliufunga mlango wake kwa komeo na kisha kuketi kwenye kiti pekee chumbani humo, daftari dogo la Afande Chaku likiwa mikononi mwake. Akijua kuwa atake asitake tayari amelazimishwa kuingia katika sakata la Cleopatra alijikuta akilazimika kulisoma daftari hilo kwa makini na utulivu mkubwa, kwani lilikuwa kiungo pekee baina yake na marehemu.

Afande Chaku alikuwa mwandishi wa aina yake. Kuna maeneo ambayo aliyaandika mambo mengi kwa ufupi sana, mara nyingine neno moja tu kama, ‘vurumai.’ Maeneo mengine, hasa pale alipohojiana na wahusika ana kwa ana alinukuu kila kauli kwa uzito wake. Jina la bosi wake Afande Chaku, Inspekta Matata, lilitajwa mara mbili tatu huku mara kwa mara likifuatiwa na alama ya kuuliza (?) au ya mshangao (!) ambazo Afande Chaku aliziandika kila baada ya nukuu mbili tatu. Haikumchukua muda Joram Kiango kushuku kuwa Afande Chaku alikuwa katika shinikizo zito ambalo halikutoka popote isipokuwa kwa Matata.

Tathmini ya Afande Chaku juu ya mauaji ya Cleopatra pia yalimfumbua macho Joram Kiangon kwa kiwango fulani. Maelezo hayo mafupi yalimthibitishia kile alichokuwa akikifikiria muda mrefu kwamba ili kumuua ama Rais ama mtu karibu na Rais, mbele ya halaiki kama ile na muuaji atoke salama salimini, kwa vyovyote alikuwa mbali na alitumia silaha kubwa. Afande Chaku alimtajia aina ya silaha, jumba na chumba ambacho aliamini muuaji alikitumia. Joram aliafikiana naye mara moja.

Mazingira ya kifo cha yule mwandishi koko pia yalimsisimua Joram. Mateso ya kishetani aliyoyapata na purukushani za chumbanihumo,vitu vyote hadi magodoro yakiwa yametupwa ovyo ilifanya Joram akubaliane na hisia za Afande Chaku kuwa chochote ambacho wauaji walikuwa wakitafuta ama walikipata kwa shida ama hawakukipata kabisa.

Mtu anayeitwa ‘King Suleiman’ katika kimemo alichokuwa nacho Afande Chaku ndani ya daftari lake nalokilimvutia Joram, hasa baada ya maelezo mafupi kuwa kilikuwa katika mfuko wa nguo alizovaa wakati mauti yanamkuta. Hata hivyo, yeye pia kama Afande Chaku, alivunjika nguvu baada ya kukuta nukuu za Afande Chaku katika mahojianao yake na mume wa marehemu zikifafanua kuwa ‘King Suleiman’ alikuwa yeye.

Nukuu ndogo ya Afande Chaku juu ya mtumishi wa hoteli, ‘anayehitajika kuzungumza naye,’ ikiwa pamoja na namba yake ya simu ilimvuta Joram. Baaada ya kuona alama ya nyota ambayo Afande Chaku aliichora juu kwa namna ya msisitizo. Joram Kiango alinukuu katika simu yake na kuamua kumuona yeye kwa niaba ya merehemu.

Baada ya kusoma nukuu zake kwa makini, ikiwa pamoja na zile ambazo hazikuhusiana na suala hilo, Joram Kiango alijikuta katika hali ile ile aliyomshuku Afande Chaku kuwa nayo; maswali mengi pasipo majibu. Swali la msingi likiwa lile lile ambalo lilimsumbua kila mtu; nani alimuua Cleopatra na kwasababu gani? Maswali mengine kama uhusiano uliopo baina ya kifo cha Cleopatra na yule mwandishi au kifo cha Afande Chaku na Cleopatra yalimsumbua pia. Hata hivyo, aliamini jibu la swali moja likimwelekeza kwa jingine. Alilihitaji jibu hilo, kwa udi na uvumba,akizingatia ukweli kuwa upatikanaji wake kwa namna moja hadi nyingine ulikuwa wake. Hakujisikia kama alikuwa na mtu mwenye uwezo wa kuishi hai mapangoni kama Osama walau kwa wiki mbili tu.

Tatizo lilikuwa aanzie wapi naswali lipi.

Alifikiri kwa muda wa dakika mbili tatu kabla hajakumbuka jambo. Akalichukua tena daftari la hayati Chaku na kulifunua taratibu hadi alipofikia ukurasa uliotaja aina ya silaha inayoshukiwa kumuua Cleopatra. AK 47 bunduki maarufu duniani hasa kwa wapigania uhuru wa misituni na wadunguaji katika nchi mbalimbali duniani. Bunduki hiyo,iliyogunduliwa na Mrusi, Avtmat Kalashnikova mwaka 1947 na baadaye kuboreshwa tena na tena na wataalamu mbalimbali, ilikuwa kipenzi cha wadunguaji wengi duniani. Ikiwa nyepesi, inayokubali mabadiliko katika maumbile yake ilikuwa imetumiwa mara nyingi katika shughuli hizo. Hivyo Joram hakusita kuafikiana na Afande Chaku katika hisia zake, kwamba ilitumika kumuua Cleopatra.

Baada ya kulitafakari hilo, Joram aliifungua suitcase yake na kuichomoa kompyuta yake. Akachomeka nyaya kwenye umeme kisha kuiwasha. Alifungua mtandao pepe na kutafuta mtandao wa Google ambako alipata kurasa zilizomweleza mengi zaidi kuhusu AK 47, majeshi ya nchi, ya waasi, vikundi na matukio mbalimbali yaliyoihusisha silaha hiyo. Alipotosheka na mtandao huo alihamia katika mitandao mingine, kama Yahoo, Gmail, Hotmail na mengineyo, na kupokea majibu ambayo aliyachambua kwa makini. Kwa mfano, alitaka kujua mauaji ya kigaidi ambayo AK 47 ilitumika toka miaka kumi iliyopita. Majibu yalikuwa lukuki, ya kusisimua.

Akiwa mdau katika ufuatiliaji wa maswala ya aina hii alitumia namba yake ya siri kuingia katika mitandao nyeti zaidi iliyoelezea matukio ya silaha hiyo kwa undani zaidi. Matukio yapatayo arobaini na nne yaliripotiwa kwa uwazi, majina au aina ya watuhumiwa yakitajwa au kupendekezwa na wahanga waliopata kupoteza maisha yao kwa silaha hiyo.

Carlos Ramirez, yule mtuhumiwa mashuhuri anayetumikia kifungo, alitajwa mara mbili tatu kuhusika na matukio yapatayo matatu ya udunguaji kwa AK 47. Katika tukio moja, mwanasiasa mmoja wa Amerika Kusini aliuawa. Tukio la pili, Marekani, Washington DC Gavana wa jimbo alijeruhiwa vibaya na kuponea chupuchupu. Tukio la tatu lililomhusu Carlos na kufanya ashukiwe lilitokea katika nchi za Kiarabu dhidi ya Rais mmoja ambaye alionekana kibaraka kwa utawala wa Israel. Huyu, alifia hospitalini, lakiniilikuwa baada ya kueleza jinsi mtu anayejiita mkono wa Zibril alivyomtumia ujumbe wa vitisho mara tatu kabla ya jaribio hilo.

Joram hakuona kama huyu alikuwa mtu wake, kwani tayari alikuwa gerezani, pia mara nyingi alitoa onyo kabla ya kutekeleza kusudio lake. Aidha Carlos alikuwa mwanasiasa zaidi.

Joram aliendelea kuchimbua. Watuhumiwa wengine kadhaa hawakumvutia kabisa. Matukio yao hayakuonyesha kuwa na uwiano wala malengo maalumu isipokuwa ama wazimu wa mtu aliyekuwa nyuma ya silaha hiyo ama uroho wa pesa.

Wakati akikaribia kuvunjika moyo Joram alikutana na tukio moja lililomfanya asite kuzima kompyuta na kutafuta usingizi. Ilikuwa baada ya kukutana tena na taarifa ya mauaji ambayo yamekuwa yakiwasisismua sana wanahabari na wachunguzi wa masuala ya ugaidi wa kimataifa, mauaji ambayo mtafiti mmoja alipata kuyaita ‘Mkono wa Jibril,’ jina ambalo liliwavutia wana habari hata wakaanza kulitumia kulitumia katika taarifa zao kila yalipotokea mauaji ya aina ile. Mauaji ambayo muuaji hakupata kuonekana wala kutuhumiwa kwa vigezo vya dhati na mpelelezi yeyote yule duniani. Ilikuwa kama mkono wa Jibril ulipita mahala kama upepo, akaua kwa namna ile ile na silaha ile ile, kabla ya kuibuka upya, miaka kadhaa baadaye katika nchi tofauti, kwa kazi tofauti.

Joram Kiango, kama tu yeyote yule aliyevutwa na habari yoyote iliyohusishwa na ‘Mkono wa Jibril’ alizisoma habari hizo kwa makini na tafakuri. Katika miaka mitano iliyopita zaidi ya matukio tisa yalihusishwa na mkono wa Jibril. Aina ya silaha iliyotumiwa, uhakika wa shabaha na kutoweka kwa muuaji bila kuacha chembe chembe yoyote ya kasoro ambayo ingeweza kumfanya apatikane. Hata hivyo mauaji matano kati ya hayo yalitibuliwa toka mikononi mwa ‘Mkono wa Jibril’ baada ya watuhumiwa kadhaa kupatikana na ushahidi kudhihirisha kuwa waliyafanya au kushiriki.

Mauaji matatu kati ya hayo yaliendelea kuwa kitendawili, moja likiwa kifo cha yule mrithi wa tajiri wa kiarabu, Abdul Karim. Kifo cha pili kilikuwa cha yule kadinali aliyetarajiwa kuwa papa kufuatia muda wa papa aliyekuwa madarakani kukaribia ukingoni. Cha tatu kilikuwa kifo cha Rais mmoja aliyefunguliwa. Vifo hivi vilikuwa vikimshawishi Joram Kiango kuwa vilitokea kwa mkono wa mtu mmoja, mkono wa Jibril.Joram aliamini kuwa matukio hayohayo yalifanyika kwa mkono mmoja hasa ikizingatiwa kuwa risasi ilikuwa ileile, ilifumua paji la uso vilevile na muuaji kutoweka kama tone la maji katika bahari.

Hivyo, aliposoma tena habari zilizokusanywa na watayarishaji wa mtandao huo juu ya ‘Mkono wa Jibril’ akili yake ilizinduka ghafla alipoyalinganisha na tukio la kifo cha Cleopatra. Kwa kusoma daftari la Chaku na aina ya risasi iliyotumika,ukamilifu wa shabaha na kutoweka kwa muuaji, hakuwa na shaka kuwa mkono uliotumika ulikuwa ‘Mkono wa Jibril,’

Kwa namna fulani, Joram alijisikia faraja kwa kulibaini hilo. Aliamini kuwa ilikua hatua moja mbele. Hata aliichukulia kuwa ilikuwa hatua fupi sana, kwani bado ilizua maswali mengi zaidi ya majibu. Mkono wa Jibril ni moja ya makusudi ya watu? Kwa uzoefu wake Joram alishuku kwa kuwepo kundi la magaidi kuliko mmoja mmoja kwani ndani ya kundi, kuna mmoja, siku moja atatapika ukweli, ama katika ulevi ama kwa matumizi ya fujo ama hata usaliti tu. Gaidi mmoja mmoja ni yeye na roho yake. Hatatoa siri zake kwa gharama zozote hata kwa kumwuza mama yake mzazi.
 
Back
Top Bottom