The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 746
- 2,103
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka wakati wa Hafla ya kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Kituo cha Polisi Chang’ombe kinachojengwa katika eneo la Chang’ombe, jijini Dodoma.
Adhma hiyo ya kujenga kituo imekuja baada ya matendo ya uhalifu ikiwemo uporaji, ubakaji, udhalilishaji, matumizi ya dawa za kulevya kushamiri katika maeneo ya Chang’ombe hali inayopelekea wananchi wa maeneo hayo kuishi kwa wasiwasi wakihofia matendo hayo ya uhalifu.
“Maeneo mengi ya jiji la Dodoma tutafunga kamera za usalama barabarani, hatuwezi kuwa na jiji ambalo polisi wetu wanakimbizana na wahalifu muda wote, tutatumia teknolojia hiyo kudhibiti uhalifu wa aina mbalimbali, Dodoma ni Makao Makuu ya nchi lazima pawe salama nawashauri wahalifu watafute shughuli nyingine ya kufanya hapa si salama tena kwa kazi zao” Mtaka
Akizungumzia Ujenzi wa Kituo hicho cha Polisi, Mkuu wa Mkoa huyo aliwataka wananchi kushirikiana na serikali kuhakikisha kituo hicho ujenzi wake unakamilika mapema ili kianze kutoa huduma za kiusalama katika maeneo hayo.
“Chang’ombe inakua inahitaji kituo kikubwa kitakachofanya kazi saa ishirini na nne ili wafanyabiashara na wananchi wafanye shughuli zao kwa muda wote na sio biashara zifungwe kwa kuhofia uhalifu, sasa kazi ya serikali sio kukwambia ufunge biashara yako muda gani kazi ya serikali ni kukulinda ili kuwepo na uhuru wa kutoa huduma, kwahiyo wananchi tushirikiane ili kituo kimalizike haraka” Mtaka
Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Naibu Katibu Mkuu Ramadhani Kailima alisema wizara imetoa kiasi cha shilingi milioni 10/= kama mchango wake katika ujenzi wa kituo hicho na kikikamilika kitaweza kutoa huduma mbalimbali ikiwemo upelelezi wa matukio, upelekaji wa majarada ya kesi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ambayo yatapelekwa mahakamani kwa hatua za kisheria.
Katika hafla hiyo Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde alichangia papo hapo mifuko hamsini ya sementi kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho na kumkabidhi Mkuu wa Mkoa Anthony Mtaka.