SERIKALI imedaiwa kuwalinda wamiliki wa makampuni yaliyokwapua pesa kutoka kwenye mfuko wa uwezeshaji Commodity Import Support (CIS), zaidi ya sh bilioni 200, imefahamika.
Habari ambazo Tanzania Daima imezipata, zinasema zaidi ya makampuni 70 ambayo baadhi yanamilikiwa na wabunge na wakurugenzi wa mashirika ya umma, wamekingiwa kifua na serikali wasifikishwe mahakamani baada ya kugoma kulipa madeni yao.
Vyanzo vya habari kutoka Wizara ya Fedha na Uchumi pamoja na ofisi ya wakala aliyepewa jukumu la kukusanya madeni hayo, Kampuni ya Msolopa Investment Ltd, vimedai kuwa Jeshi la Polisi, limeombwa kushiriki kuwakamata wadaiwa hao.
Hapa katika Wizara ya Fedha, baada ya kuona wadaiwa wanapiga chenga kulipa, tulimwandikia Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, tukimtaka atoe askari wake washirikiane na wakala wa kukusanya madeni hayo ili wadaiwa sugu watiwe mbaroni, lakini ameshindwa kutoa askari, alisema ofisa mmoja Mwandamizi Wizara ya Fedha.
Imedaiwa kuwa baada ya barua hiyo ambayo iliandikwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha kushindwa kufanyiwa kazi, Kampuni ya Msolopa nayo iliandika barua kwa jeshi hilo ili litoe askari wake, lakini IGP Mwema alisema jeshi lake linakamata watu wenye makosa ya jinai tu na si wa madai.
Msemaji wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Ingiahed Mduma, alipoulizwa kuhusiana na wizara yake kuomba msaada Jeshi la Polisi, alisema mpango huo unaweza kuwa ni maandalizi tu ya kuwakamata baada ya kipindi cha miezi sita walichowapa wadaiwa hao kurejesha fedha zao, kutimia juzi.
Kama kuna barua hiyo kwenda Jeshi la Polisi, inaweza kuwa ni maandalizi tu ya kuwakamata, lakini wewe hutakiwi kujua, kwasababu haya ni mambo ya ndani, tulikuwa tumewapa miezi sita ambayo imemalizika juzi na kama unataka habari zaidi, njoo ofisini, alisema Mduma.
Tanzania Daima ilipowasiliana na Ibrahim Msolopa kuhusiana na madai hayo, alikiri kuomba msaada wa polisi lakini ameshindwa kupewa baada ya serikali na jeshi kushindwa kutoa ushirikiano.
Ni kweli tuliomba msaada kwa IGP Mwema ili atusaidie kuwafikisha wadaiwa hao mahakamani kutokana na wengine kuonyesha uhuni, lakini alisema hadi serikali imwambie, alisema.
Alisema kazi ya kukusanya madeni hayo, imekuwa ngumu na hali hiyo imechangiwa na serikali kuwalinda baadhi ya watuhumiwa ambao wamekuwa wakionyesha kukaidi kulipa madeni yao.
Kwa mujibu wa Msolopa, kampuni yake imefanikiwa kukamata nyumba tano za wadaiwa walioziweka dhamana wakati wa kukopa, lakini hata nyumba hizo zikiuzwa, haziwezi kulipa deni husika kwani yameongezeka.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa, aliwahi kusema kuwa wakala huyo hatafanikiwa kukusanya madeni hayo hadi pale suala hilo litakapofanywa kuwa la jinai.
Akizungumza na Tanzania Daima hivi karibuni, Dk. Slaa alisema suala hilo litafanikiwa pale ambapo serikali itaamua kuwatafuta wahusika walioandikisha makampuni hayo ambayo mengi ni hewa.
Dk. Slaa ambaye ndiye aliyekuwa akilia na serikali juu ya ufisadi huo kupitia mfuko wa CIS, alisema hatua ambazo serikali imezichukua haziwezi kubaini ufisadi huo kwani zaidi ya sh bilioni 800 zimefujwa na makampuni hewa.
Kati ya makampuni 916 yanayodaiwa kukopa fedha hizo serikalini kwa lengo la kuagiza bidhaa nje ya nchi mara baada ya kutokea matatizo ya kifedha nchini, ndani ya kipindi cha miezi saba sasa, Msolopa Investments imeweza kuyafikia makampuni 450 tu, huku mengine yakiwa taabani na hayafanyi kazi na hayana uwezo wa kurejesha madeni hayo.
Mfuko wa CIS ulianzishwa miaka ya 1978 na 1980 baada ya nchi kukabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha za kigeni. Uhaba huo ulisababisha wafanyabiashara waliokuwa wakiagiza bidhaa kutoka nje kushindwa kulipia bidhaa hizo.
Katika kulinda heshima ya nchi, serikali iliomba mkopo kutoka kwa wafadhili wa nje ili zipatikane fedha za kigeni kulipia mrundikano wa madeni.
Baada ya kupata msaada serikali ilianzisha mfuko uitwao Commodity Import Support (CIS), ambapo wafanya biashara waliokuwa wanadaiwa bidhaa walizoagiza kutoka nje walikopeshwa na kulipia deni kwa fedha za kigeni.
Ili kusimamia vizuri fedha hizo za CIS na kwa kuwa wafanyabiashara wengi walikuwa wateja wa National Bank of Commerce (NBC), Benki Kuu (BoT) iliagiza NBC ifungue akaunti iitwayo External Payment Arrears (EPA) kwa ajili ya kukusanya marejesho yaliyokuwa yakifanywa na waliokopa kwenye mfuko wa CIS.
Marejesho hayo yalikuwa yakitumwa Benki Kuu kila mwezi ili kwenda kufidia kwenye mfuko waliokopa. NBC ilisimamia akaunti hiyo ya EPA kwa muda, lakini baadaye ilifungwa na kuhamishiwa BoT.
Source: Tanzania Daima