SoC04 Changamoto ya utapeli uliokithiri nchini itaweza kushughulikiwa kupitia tume ya kupambana na utapeli

Tanzania Tuitakayo competition threads

usikivu

New Member
Aug 19, 2022
1
0
Matukio ya utapeli nchini yamezidi na yanazidi kushika kasi nchini. Matapeli wamekua wakibuni mbinu mpya kadiri siku zinavyosonga. Utapeli wa mitandaoni na usio wa mitandaoni umekuwa mwiba mkali kwa wananchi wengi huku ukiwaachia maumivu ya kupoteza pesa walizotegemea zingewanufaisha kwa namna moja au nyingine.

Utapeli hutokea mtu anapojipatia mali au fedha kwa njia ya udanganyifu. Jambo la kusikitisha na kukatisha tamaa ni aliyetapeliwa kuonekana mzembe bila kufahamu ya kua utapeli unaweza kumkumba yeyote (wapo watu wakubwa na maarufu waliotapeliwa). Kwa maana hiyo badala ya watu kushiriki ili kusaidia tapeli kupatikana na kuchukuliwa hatua za kisheria hujikuta kumkejeli na kumdhihaki mtapeliwa. Jambo hili ni baya sana, hupelekea watu wengi wanaotapeliwa kuogopa kusema kwa watu wengine au kufuatilia haki yake mahakamani na kuona kwamba wataonekana wazembe.

Mbaya zaidi utapeli umezidi kujikita mizizi na kuchanua mpaka kwenye taasisi na kampuni zilizosajiliwa na serikali. Utapeli umeonekana ni njia rahisi ya kujipatia fedha bila kuvuja jasho wala kutumia mtaji mkubwa. Hatua sahihi zisipotumika kukomesha utapeli itapelekea kuzidi kuchanja mbuga na hata kusababisha wanaofanya kazi kwa uaminifu kutoaminiwa.

Hii hapa ni baadhi ya mifano ya utapeli zilizowahi kufanyika na zinazoendelea kufanyika,
Utapeli kupitia utoaji wa mikopo,
Njia hii hutumika na baadhi ya watoaji wa mikopo (makampuni, taasisi au watu binafsi). Humtapeli mkopaji kwa kuficha au kutokuweka sawa baadhi ya masharti yaliyopo kwenye mkopo. Wakati wa marejesho ndipo mkopaji hujikuta akirudisha kiasi kikubwa baada ya mkopo kuongezeka maradufu. Hii hupelekea kusuasua kwenye marejesho ya mkopo na hata kutaifishiwa mali alizoweka rehani.

Utapeli kupitia uwekezaji,
Matapeli wengine huja kwa njia ya uwekezaji na hujifanya kutafuta washirika watakaonunua hisa kwa kuwalaghai watapata gawio kutokana na faida itakayopatikana. Hata hivyo baada ya kupata washirika wengi waliotoa michango hutokomea na kuwaacha washirika hao wakihaha bila msaada wowote.

Pia wapo baadhi hujitokeza kwenye kilimo na ufugaji, huku huwaaminisha watu soko la mazao watakayolima au kufuga ni la uhakika na faida kubwa. Lakini masharti yaliyopo ni kununua mbegu kutoka kwao na kwa bei kubwa. Kitakachotokea ni baada ya mauzo ya mbegu kua kubwa hutokomea na mwisho wa siku ikifika kipindi cha mavuno mazao hayo hukosa soko na kua hasara.

Utapeli kupitia biashara ya ‘network marketing’
Hii ni biashara inayohusisha muunganiko wa watu, kiingilio kwenye biashara hii ni kiasi fulani cha pesa ambacho hupelekea kupewa aina fulani ya bidhaa kwa ajili ya kuuza. Lakini pia kwa kuaminishwa ukitaka kutengeza pesa zaidi itabidi kumleta mtu atakapotoa kiingilio nawe utapata faida naye akileta mtu bado utapata kiasi fulani cha pesa. Hali hii hupelekea watu kuacha shughuli zao muhimu na kuingia mtaani kwaajili ya kutafuta watu wa kuwaunganisha ili hata kurejesha pesa yao waliyotumia kama kiingilio.

Hizo ni baadhi ya utapeli unaofanyika mitaani, lakini zipo nyinginezo kama
  • Utapeli kupitia wachezesha kamaria mitaani
  • Udalali wa vitu kama ardhi
  • Utapeli wa mitandaoni.
  • Utapeli kupitia usaili wa nafasi za kazi (utoaji wa ajira)
  • Utapeli wa kutumia vilevi (dawa za kulevya)
  • Kughushi matangazo ya taasisi za umma
Kwa njia hizo chache inaonyesha jinsi gani utapeli umeshamiri mitaani lakini hatua zinazochukuliwa hazirizishi na wala haziwezeshi waliotapeliwa kurudishiwa pesa zao. Ni vyema kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa ili utapeli unakomeshwa nchini.

Iundwe tume/taasisi ya kupambana na utapeli ili kutatua changamoto hii.
Tume/taasisi hii itakua na kazi zifuatazo;
  1. Kuhakikisha inachunguza mapema taarifa zote zenye viashiria vya utapeli.
Hii itasaidia kubaini utapeli mapema na kutoa taarifa kwa raia ili kuepusha watu wengi zaidi kutapeliwa

2. Kushirikiana bega kwa bega na vyombo vya usalama kuwasaka wahalifu wa utapeli.

Tume/taasisi hii itabidi kuundwa na baadhi ya askari na wataalamu wa teknolojia. Hii itasaidia na kurahisisha kuwakamata wahalifu wa utapeli hata wale wanaotapeli kwa njia ya mtandao.

3. Kutoa elimu kwa raia kuhusiana na masuala ya utapeli
Hii itasaidia raia kua makini na kuhakiki vizuri taarifa zote zinausiana na jambo fulani ili kuepuka mitego wanayotumia matapeli.

4. Kuhakikisha mali/fedha zote zilizopatikana kwa njia ya utapeli zinarejeshwa kwa wahusika.
Hivi sasa tapeli anapotiwa hatiani hutozwa faini na kuachiwa bila kurejesha kwa wahusika mali/au fedha walizotapeli. Hii ni kutokana wahusika kutofungua kesi za madai, kwa hivyo ikiwepo tume hii itakua ni rahisi kukusanya taarifa za waliotapeliwa na kuzifikisha mahakamani ili kuhakikisha wanarudishiwa mali/fedha zao.

5. Kuhakikisha madalali wote wanasajiliwa kupitia kampuni au vyama vya kidalali,
Hii itasaidia dalali anapotapeli kukamatwa kwa urahisi kutokana na taarifa zao za msingi kuwepo kwenye kampuni au chama husika.

Kama rushwa imechukuliwa kwa ukubwa kutokana na madhara inayosababisha basi ni vyema pia utapeli kuchukuliwa kwa ukubwa huohuo. Wapo wanaopoteza ajira zao kutokana na utapeli, wapo wanafilisika kutokana na utapeli, wapo wanaochanganyikiwa kutokana na utapeli pia wapo wanaodiriki hadi kujitoa uhai kutokana na utapeli.

Utapeli unapelekea wanapojitokeza wawekezaji waaminifu kukosa washirika kutokana na watu kua na wasiwaasi wa kutapeliwa.

Kwa hali hii ni vizuri serikali ikautambua utapeli kama janga la kitaifa. Hii itawezesha kuweka mikakati imara ya kuhakikisha ya kupambana na kutokomeza utapeli nchini. Haya yote yatasaidia kuikoa jamii ya mtanzania inayopoteza fedha na mali kutokana na matendo ya utapeli yanayotokea nchini.
 
Back
Top Bottom