Tuhuma za wabunge kuchukua au kuomba rushwa kutoka katika mashirika na taasisi wanazozisimamia, zimechukua sura mpya baada ya kubainika mkakati unaosukwa na wabunge wafanyabiashara ya mafuta kuiangamiza Mamlaka ya Nishati na Maji (EWURA), waweze kurejesha uchakachuaji wa mafuta.
Mbali na hilo, kuna mbunge aliyeomba kiasi cha Sh milioni 100 kutoka taasisi inayosimamiwa na kamati yake, huku mwingine akiomba walipe posho badala ya kupewa chai na chakula, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.
“Spika hakufanya uamuzi wa kuvunja Kamati kutokana na habari zilizochapishwa magazetini, bali kwa muda mrefu vyombo vya dola vimekuwa vikifuatilia mienendo ya wabunge hawa na wengi wameonekana kukiuka mienendo na taratibu za kibunge.
“Upo ushahidi wa sauti kabisa, ambapo mbunge huyu anaomba posho, mwingine anaomba milioni 100. Watumishi wa hilo shirika wakamuuliza, ‘hivi tukikupa hizo milioni 100 sisi tutazitoleaje taarifa katika mizania ya hesabu?’ Akawaambia atawapa njia jinsi ya kufanya. Ndipo wakaripoti kwenye vyombo vya dola, likaanza kufanyiwa kazi… watu wameona matokeo tu, wabunge wanafuatiliwa nyendo zao,” kilisema chanzo cha habari kwa JAMHURI.
Dk. Kashilillah awaasa wabunge
Kwa upande wake, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah, ameiambia JAMHURI kuwa Spika amechukua hatua si kwa sababu ya magazeti kuchapisha taarifa hizo juu ya wabunge, bali kutokana na uchunguzi ulioanza muda mrefu kufuatilia nyendo za wabunge. Aliwataka wabunge kuweka maslahi ya aifa kwanza, na kwamba taarifa za kutuhumiwa kupokea au kuomba rushwa zimepatikana kutoka miongoni mwa wabunge wenyewe na vyombo vya dola vikazifanyia kazi. Anasema uchunguzi unaoendelea unaweza usiwe na matokeo mazuri kwa baadhi ya wabunge.
“Sheria iko wazi. Hawa ikithibitika, wengi wanaweza kuishia gerezani na kupoteza ubunge,” anaonya. Kifungu cha 28 cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge ya Mwaka 1988 kinasema Mbunge akipatikana na kosa la kuomba rushwa, anaweza kutozwa faini ya Sh 20,000 au kifungo cha miaka mitatu jela.
Ibara ya 67 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inasema bayana kuwa Mbunge anaweza kupoteza sifa ya kuendelea kuwa mbunge iwapo atafungwa jela kwa kipindi kinachozidi miezi sita kutokana na kosa lolote.
Spika wa Bunge, Job Ndugai, baada ya tuhuma hizo kutokea amevunja Kamati za tano za Bunge na kuhamisha wajumbe 27, na akaelekeza uchaguzi ufanyike upya kwa Kamati zilizopoteza Mwenyekiti na Makamu wake au mmoja wa viongozi hao.
Zipo taarifa kuwa wabunge katika kamati walikopelekwa wabunge wanaotuhumiwa kwa rushwa, wajumbe wake wameanza kuwakataa kwa maelezo kuwa kamati zao si ‘kijiwe’ cha wala rushwa.