JanguKamaJangu
JF-Expert Member
- Feb 7, 2022
- 2,628
- 6,294
Waziri Bashungwa akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Deo Ndejembi ameshuhudia urejeshwaji wa barabara ya Liwale - Nangurukuru iliyosombwa na maji ikisimamiwa na Mtaalam mwenye taaluma ya Falsafa kwa kusaidiwa na Wananchi wakati Mkandarasi akiwa hayupo eneo la Kazi.
“Haiwezekani sisi tutoke Dodoma hadi huku Liwale kutokana na changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara iliyopo, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amelazimika kutoa Helikopta yake tufike huku, lakini hapa site hakuna Mkandarasi, mnaweka mtu aliyesoma falsafa kusimamia kazi ya ujenzi wa barabara”, ameeleza Bashungwa.
Kadhalika, Waziri Bashungwa amesema Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa fedha ya kumtafuta Mkandarasi wa kujenga barabara ya Masasi - Nachingwea - Liwale km 175 kwa kiwango cha lami ili kumaliza changamoto inayoendelea kujitokeza ya kufungwa kwa barabara.
Bashungwa ameeleza kuwa Serikali itaanza kujenga kwa awamu barabara ya Nangurukuru - Liwale yenye urefu wa kilometa 230 kwa kiwango cha lami ambapo amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi kutenga fedha na kumtafuta Mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi kipande cha kilometa 10 kwa kiwango cha lami.
Kwa Upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amesema ataendelea kufuatilia kwa ukaribu kazi zote ikiwemo urejeshwaji wa miundombinu katika Mkoa huo hasa Wilaya ya Liwale, Nachingwea na Ruangwa na hatasita kumchukulia hatua Mkandarasi na Mtaalam yoyote anayeshindwa kutekeleza majukumu yake ilasavyo
Naye, Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka ameishukuru Serikali kwa kuanza kuchukua hatua za kurejesha mawasiliano ya barabara kutokana na changamoto kubwa ya barabara na madaraja yanayounganisha wilaya ya Liwale na maeneo mengine kujaa maji na kupelekea kufungwa hadi sasa.