Habari wanaJamiiForums, habari watanzania wenzangu.
Naitwa suzana, kama mwandishi wa habari wa kujitegemea nimepata Fursa ya kuonana na kuzungumza na binti mmoja, muhanga wa mila potofu (nyumba ntobhu) ambaye amenisimulia mkasa wake. Hivyo nami nauleta kwenu kwani kuna mambo ya kujifunza.
Picha na Freepik
Mwanzo wa mkasa;
Kwa majina naitwa Bhoke Nyamuhanga (jina halisi limehifadhiwa), bila shaka kwa jina langu tu tayari umekwisha fahamu kabila langu. Mimi ni mkurya. Baba yangu aliyemuoa mama yangu ni mwanamke na ni mkurya lakini Baba yangu mzazi sio mkurya. Hivyo nina Baba wawili.
Kwetu ukuryani tunazo mila nyingi ambazo kiuhalisia mpaka hivi leo zinapingwa kwa kuwa zina matokeo hasi moja kwa moja na moja ya mila hizo ni nyumba ntobhu.
Sisemi haya kwa ubaya maana najua kila kabila lina mila na desturi zake ambazo kwa upande mmoja ni sahihi na upande mwingine si sahihi, lakini nasema haya kama muhanga wa mila hii ya nyumba ntobhu.
Kwa wasio fahamu, nyumba ntobhu ni kitendo cha mwanamke ambaye hakubahatika kuolewa au mume wake alifariki bila wao kupata mtoto hivyo kwa kutaka kuendeleza ukoo wake huamua kuoa mwanamke (kwa kulipa mahari waliyokubaliana baina ya pande mbili ) na kumchukua mwanamke huyo na kumfanya mkewe.
Mwanamke aliyeolewa na mwanamke huyo hana neno juu ya mumewe, na atapaswa kumuheshimu kama mume wake.
Kama mke ana jukumu la kuitunza familia na kutenda majukumu yote yampasayo isipokuwa tendo la ndoa tu.
Kwenye tendo la ndoa, mume (yule mwanamke) atapaswa kumtafutia mkewe mwanaume wa kufanya nae tendo hilo na mtoto atakaye patikana ni mali ya mume (yule mwanamke) na sio mwanaume aliyetafutwa wala mwanamke aliyeolewa.
Mimi ni binti niliyepatikana kwa njia hiyo, mama yangu alitafutiwa mwanaume wa kushiriki nae tendo na baada ya mimi kupatikana baba yangu mzazi (mwanaume) akapotelea pasipo julikana maana kazi yake ilikwisha hivyo nikalelewa na mama yangu pamoja na baba yangu (yule mwanamke).
Tangu utoto wangu mpaka kujitambua kwangu, baba yangu (yule mwanamke) alikuwa akinitimizia majukumu yote kama mtoto, kuanzia kula, kusoma, kuvaa na mahitaji yote ya muhimu.
Nilipofika sekondari maisha yale ya kuchaguliwa wanaume yakamshinda mama yangu hivyo, akaamua kutoroka nyumbani.
Maisha hayakuwa mabaya bila mama maana baba alitimiza majukumu yote na ukizingatia ni mwanamke hivyo alijua vyema kucheza nafasi zote mbili, yaani, kama baba na kama mama.
Tatizo lilikuwa kwangu, mbali na kwamba alijitahidi kucheza nafasi ya baba lakini nilimuhitaji sana baba yangu mzazi, jambo ambalo nikimueleza mara kwa mara alikuwa akikasirika mno na kuniambia kuwa yeye ndiye baba yangu mzazi na ana haki zote juu yangu.
Kiu ya kumtafuta baba yangu mzazi (mwanaume) ilipozidi akaamua kupanga mpango wa kuniozesha kusudi arudishe mahari alizotumia kumuoa mama yangu. Kwa Kuwa maji yalimzidi unga, angalau akataka kurudisha mali zake alizohisi amepoteza.
Ukizingatia nami tulifundishwa vyema shuleni kuhusu mila potofu ikiwemo hiyo, hivyo nilichachamaa kumjua baba yangu mzazi naye alipoona hilo, akataka kuniozesha ili nitoke mbele ya uso wake.
Nami nikalijua hilo mapema hivyo nikafunga safari kutoka Mara mpaka Dar es salaam aishipo Baba mdogo ( Anamuita yule baba yangu Shangazi) maana afadhali yeye hakuwa akiendekeza mila hizo, upepo wa Dar ulijua kumstaarabisha.
Mpaka leo hii nipo kwake, kwakuwa nina kipaji cha kusuka nimejiajiri.
Baba yangu (yule mwanamke) ametokea kumchukia sana Baba mdogo kwanini amenipokea na kuishi nami ilhali anahitaji kuniozesha kulipa mahari.
Chuki yake juu yangu imedhihirika sana kiasi kwamba hataki kuongea nami na nimesikia za juu juu kwamba endapo nikijiroga tu kurudi Mara, basi ataniozesha. Nami sipo tayari kabisa katika hilo kwani ndio kwanza napambana kutimiza ndoto yangu ya ususi na kumtafuta baba yangu mzazi.
Ndugu Mtanzania mwenzangu;
Changamoto kama hizi huwapata wasichana wengi sana japo ni ngumu kupata ujasiri wa kuongea. Kwa upande wangu, nashukuru elimu niliyoipata shuleni ilinipa ujasiri wa kutaka kumtafuta baba yangu mzazi.
Kwa miaka na miaka tumekuwa tukipambana kuua mila zenye matokeo mabaya kwa wanawake japo ni ngumu kumaliza tatizo hili.
Kwa tukio kama hili, wanawake wote ni wahanga tukianzia na baba yangu (yule mwanamke) anaishi maisha ya hasira na manung’uniko kwa kupoteza mahari yake ambayo kama asingali fanya tukio lile asingali pata hasara. Kwa mama yangu mzazi kushiriki tendo la ndoa na wanaume asiowapenda kwa sababu tu yupo chini ya aliyemuoa na kwangu pia, nimeingia kwenye uadui na mtu ambaye kiuhalisia sina makosa pia mpaka sasa sijapata kumuona baba yangu mzazi.
Ni rahisi sana kuchunga wanyama lakini si binadamu mwenzako. Baba yangu (yule mwanamke) hakuweza kunichunga mimi wala mama yangu kwa kuwa binadamu tumepewa upeo na akili ya kupambanua mema na mabaya.
Mila potofu zinawafanya watu wengi kuwa wakimbizi kwao wenyewe. Unashangaa kwanini mtu huyu anakaa miaka mingi bila kwenda kwao kumbe ni mila potofu zilizopo kwao zinamfanya asiende kwao.
HITIMISHO
Serikali yetu inajitahidi sana kuhamasisha baadhi ya makabila kuacha kujihusisha na tamaduni zisizo rafiki kwa maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla ingawa uhamasishaji unapaswa kuongezwa zaidi na zaidi kuwafikia wahanga.
Wazazi na walezi, ni jukumu lenu pia kuwalinda watoto wanaoandamwa na mila hizo kama alivyofanya Baba yangu mdogo.
Binti, serikali inafanya sehemu yake, walezi watafanya sehemu yao lakini nawe pia unapaswa kufanya sehemu yako kama nami nilivyojitahidi kucheza nafasi yangu.
Mila potofu bado zipo kwani matokeo yake yanaonekana mpaka leo hii, ewe mtanzania mwenzangu tusaidiane kumaliza tamaduni mbovu katika nchi yetu kwani binadamu ni kiumbe mwenye akili na sio anayepelekeshwa na kuyumbishwa huku na huko.
Asanteni.