Habari za J3 wapendwa
Nilikuwa msibani hivyo, nipeni pole, nilifiwa na shost.
Shost huyu anaitwa Jane, nilifanya nae mafundisho ya communion miaka ile, baba yake alikua capernter. Alitengeneza vitu kama milango na madirisha yaliyoharibika kanisani. Baba Jane alifanya kazi pia za kusafisha mazingira ya kanisa, kufyeka na kumwagilia maji maua. Ujira aliopewa ulisaidia familia.
Kijana Dan alipata kazi kwenye shirika la kigeni linalojishughulisha na utafiti, utafiti aliopewa Dan ulikuwa katika wilaya anayoishi Jane. Jumapili Dan alihudhuria ibada kanisani na baada ya misa alikwenda kujitambulisha kwa baba paroko kama mwana parokia mgeni. Wakati huo Dan alikuwa bado anaishi hotelini, katika maongezi ya hapa na pale, baba paroko alimfahamisha Dan maeneo mazuri ya kuishi katika mji ule.
Baada ya Dan kupata nyumba, alihitaji mtu wa kumsaidia kazi za ndani, alimwendea tena baba paroko, ambae alimfahamisha Dan kwa baba Jane. Wakati huo Jane alikuwa amehitimu darasa la saba na wazazi wake hawakua na uwezo wa kumwendeleza. Kupata ajira kwa Jane ilikuwa msaada mkubwa kwa familia. Jane alikwenda kazini asubuhi saa mbili na kumaliza kazi saa kumi jioni.
Baada ya kufanya kazi kwa muda mfupi, hisia za mapenzi zilianza kati ya Jane na Dan. Dan aligundua kuwa Jane bado ni mwana mwali (bikra), alijiona ni mwanaume mwenye bahati sana. Alianza mipango ya harusi, baada ya wazazi kuridhia, ndoa ilifungwa kanisani.
Mafanikio ya kazi ya Dan yalimfanya apate kazi sehemu nyingi katika Afrika, mkataba wake uliofuatia baada ya pale alikwenda Malawi, Zimbabwe, Afrika Kusini na sehemu nyingi nyingine. Alimjengea baba Jane nyumba, alimnunulia shamba na kumpa mtaji uliomwezesha kulea familia.
Ndoa ya Dan na Jane ilibarikiwa kupata watoto wanne wote wa kiume. Baada ya miaka 20 ya ndoa ndipo Jane alipata matatizo ya cancer ya kwenye kizazi. Jitihada za matibabu hazikuleta suluhisho jema, Jane aliaga dunia.
Tukiwa msibani siku ya tatu, baba Jane alimfahamisha Dan kuwa, kufiwa na mke kusimvunje moyo, Jane ana wadogo zake pale na wakimaliza msiba aondoke na mmoja anaempenda. Maneno haya yalimpa hasira sana Dan ambae kwake Jane alikuwa faraja ya moyo wake, leo hii unataka kuniambia nichukue binti yeyote Jane hakuwa TV au radio kuwa unaweza kubadilisha.
Baba Jane aliyafanya yote haya akiwa na lengo kuwa Dan asioe mbali, mke mpya anaweza kuja kutesa wajukuu wake. Pia kwa fadhila alizofanyiwa na Dan, baba Jane aliamua kuwa mkarimu lakini ukarimu wake haukuwa katika nafasi nzuri.