John McAfee, mwanzilishi wa kampuni mashuhuri ya kutengeneza programu za kuzuia na kupambana na programu za kompyuta, amesema anaweza kuifungua simu aina ya iPhone iliyotumiwa na Syed Farook aliyetekeleza mauaji San Bernardino, California mwaka jana.
Bw McAfee ametoa ahadi hiyo kwa shirika la uchunguzi wa jinai la Marekani FBI kwenye makala aliyoiandika kwenye Business Insider.
Kampuni ya Apple, inayotengeneza simu za iPhone, imekataa kutii agizo la mahakama la kuitaka ifungue simu hiyo.
Hatua hiyo imeibua hisia mseto kuhusu iwapo ni haki kampuni hiyo kushurutishwa kufanya hivyo.
Lakini Bw McAfee amesema yeye na kundi lake la wataalamu wafafanya kazi hiyo “bila malipo”.
Bw McAfee bado anaendelea na kampeni za kutaka kuchaguliwa kuwa rais wa Marekani kupitia chama cha Libertarian.
"Itatuchukua wiki tatu,” amesema kwenye makala yake.
Mtaalamu wa masuala ya usalama wa kompyuta Graham Cluley ameambia BBC kwamba ana shaka kuhusu iwapo Bw McAfee anaweza kufungua simu hiyo.
"Simu za iPhone huwa ngumu sana kudukua ukilinganisha na simu nyingine,” amesema.