Mpango huu, uliotekelezwa kuanzia Aprili 18 hadi 21, 2025, unalenga kusaidia jamii zisizopata huduma za afya ya macho kwa urahisi kutokana na changamoto mbalimbali.
Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika katika hafla maalum iliyohudhuriwa na viongozi wa serikali, wadau wa sekta ya afya, wawakilishi wa sekta binafsi, wananchi pamoja na wageni waalikwa.
“Kupitia ushirikiano wetu na KSI Charitable Eye Centre, tunatoa huduma hizi bure kwa siku tatu mfululizo kwa wote wanaohitaji matibabu ya macho. Tunaamini kwa dhati kuwa afya bora ya macho ni kichocheo cha maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla. Kampeni hii itanufaisha watu wanaosumbuliwa na matatizo kama mtoto wa jicho, pamoja na wale wanaofanya kazi hatarishi kama wachomeleaji vyuma na waendesha bodaboda ambao mara nyingi hupuuza matumizi ya vifaa kinga,” alisema Meneja wa Masoko ya Biashara wa YAS, Eric Charles.
Huduma zinazotolewa ni pamoja na uchunguzi wa kina wa macho, matibabu ya magonjwa mbalimbali ya macho, ushauri wa kitaalamu kutoka kwa madaktari bingwa wa macho, pamoja na upasuaji kwa wagonjwa watakaohitaji huduma hiyo. Pia, washiriki walipata elimu kuhusu namna ya kujikinga dhidi ya maradhi ya macho kwa kutumia vifaa kinga na kuhakikisha mazingira salama kazini.
Zoezi hili la Mbeya ni sehemu ya kampeni ya kitaifa inayoendelea inayotekelezwa na YAS na KSI Charitable Eye Centre kwa lengo la kufikisha huduma za macho kwa jamii mbalimbali nchini, baada ya mafanikio katika maeneo ya Zanzibar, Mtwara, Tanga na Mkuranga.
“YAS itaendelea kuwa karibu na jamii kuhakikisha upatikanaji jumuishi wa huduma bora za kijamii na mawasiliano. Huduma hizi za afya si msaada wa muda tu — ni sehemu ya dhamira yetu ya kizalendo ya kuboresha maisha ya Watanzania,” aliongeza Charles.
Wakazi wa Mbeya na maeneo ya jirani walihamasishwa kujitokeza kwa wingi katika vituo vilivyotengwa ili kunufaika na huduma hizi za bure za macho, na kuwahamasisha ndugu na marafiki kushiriki pia.