Mindyou
JF-Expert Member
- Sep 2, 2024
- 983
- 2,586
Wakuu,
Siku ya leo Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu atakuwa ananguruma wakati anazungumza na vyombo vya habari
Fuatilia uzi huu kujua nini kinaendelea kwenye mkutano huo.
Akiongea na Waandishi wa Habari, Makamu wa Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, Tundu Lissu, amesema anaaamini na Wanachama wengine wanaamini kuwa ana sifa zote za Kugombea nafasi ya juu kabisa ya Uongozi wa Chama hicho kwa ngazi ya Taifa, kama zilivyoanishwa katika Katiba ya Chama.
Lissu amesema amewasilisha taarifa rasmi kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA ya kuondoa kusudio lake la kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti (Tanganyika) na badala yake amewasilisha kusudio la Kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama taifa katika Uchaguzi Mkuu wa Chama ujao.
KAULI YA MHESHIMIWA TUNDU ANTIPHAS LISSU, MAKAMU MWENYEKITI WA CHADEMA (TANGANYIKA), KUHUSU KUSUDIO LA KUGOMBEA NAFASI YA MWENYEKITI WA CHAMA TAIFA, KATIKA UCHAGUZI WA CHAMA 2024
UTANGULIZI
Ndugu zangu na wanachama wenzangu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo,
Tangu mwaka jana, chama chetu kimekuwa katika Uchaguzi Mkuu kichama. Katika Uchaguzi Mkuu huu, sisi wanachama wa CHADEMA tumekwishafanya uchaguzi wa viongozi wetu katika ngazi mbali mbali za chama, kuanzia ngazi ya Msingi hadi Mikoa na sasa tunaelekea kukamilisha uchaguzi katika ngazi ya Kanda. Mara baada ya kukamilisha uchaguzi wa Kanda, tutaingia kwenye uchaguzi wa ngazi za kitaifa za chama chetu.
MISINGI YA KIKATIBA
Kama inavyofafanua Katiba ya chama chetu, Uchaguzi Mkuu wa chama ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa falsafa yetu ya ‘Nguvu na Mamlaka ya Umma’, inayolenga kutengeneza uongozi “unaoweza kumilikiwa, kuhojiwa na kuwajibishwa na umma kwa kutumia vyombo vilivyopatikana kwa utashi wa wengi kwa kupitia chaguzi huru na za haki.”1 Aidha, kwa Uchaguzi Mkuu, sisi wanachama tunapata fursa ya kuonyesha na kuthibitisha kile ambacho Katiba yetu inakiita madaraka yetu ‘ya mwanzo na ya mwisho’ katika kuamua hatima ya chama chetu “... pasipo kuingiliwa, kudanganywa au kughilibiwa na viongozi, watawala au wageni.”2
Ndugu zangu na wanachama wenzangu,
Mojawapo ya madhumuni ya kisiasa ya chama chetu - kwa mujibu wa Katiba yetu - ni kuendeleza na kudumisha demokrasia na “... kujenga utamaduni wa demokrasia katika jamii kwa kutambua haki za wengi katika maamuzi na pia kutambua haki za wachache zinasikilizwa, kuheshimiwa na kulindwa, sambamba na kukubali ushindani huru, wa haki na wa wazi katika uchaguzi.”3
Ili kutekeleza madhumuni haya, Katiba yetu imetoa haki kwa kila mwanachama “... kuchagua viongozi wa Chama wa ngazi inayohusika kwa mujibu wa Katiba.”4 Aidha, kila mwanachama ana haki ya “... kuchaguliwa kuongoza na kuwakilisha Chama katika ngazi yoyote kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa ya sifa za uongozi.”5
WASIFU WANGU
Ndugu zangu na wanachama wenzangu,
Mimi ni mwanachama na nimekitumikia chama chetu katika ngazi mbali mbali muhimu na zenye dhamana kubwa kwa zaidi ya miaka ishirini. Nilianza utumishi wangu wa chama kama Mkurugenzi wa Katiba, Sheria na Haki za Binadamu, na baadae nikawa Mwanasheria Mkuu wa Chama. Aidha, kwa kipindi kifupi, nimewahi kuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Kati; na, tangu Disemba 2019, nimekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama kwa upande wa Tanganyika.
Zaidi ya hayo, kwa kupitia udhamini wa chama chetu, nimewahi kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa vipindi viwili, hadi utumishi wangu bungeni ulipokatishwa katika mazingira ya kikatili kufuatia jaribio la mauaji dhidi yangu la tarehe 7 Septemba, 2017. Na, kama mnavyofahamu, mwaka 2020 mlinipa heshima ya kuongoza mapambano ya chama chetu kama mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo. Ninapenda kuamini kwamba, katika nafasi zote hizi, utumishi wangu kwa chama chetu na kwa nchi yetu, uliwapa ninyi wanachama na wananchi sababu kubwa ya kujivunia.
Nje ya utumishi wa chama chetu, kama mnavyokumbuka, nimewahi kushikilia nafasi ya Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), kufuatia uchaguzi wa kihistoria wa Machi 2017, katika kilele cha utawala wa kidikteta wa Rais John Pombe Magufuli. Aidha, katika miaka ya ujana wangu, nilikuwa mwanasheria na mwanaharakati jasiri katika masuala ya ulinzi wa mazingira na utetezi wa haki za binadamu, nikiwa sehemu ya Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira (LEAT). Nimewahi pia kuwa mtafiti katika masuala ya rasilimali za asilia katika Taasisi ya Rasilimali za Dunia (WRI) yenye makao makuu yake Washington DC nchini Marekani.
Kwa sababu zote hizi, ninaamini, na ninapenda kuamini kwamba ninyi wanachama wenzangu mnaamini, kuwa nina sifa za kutosha za kugombea
nafasi ya juu kabisa ya uongozi katika chama chetu, yaani nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa, kama zilivyoainishwa katika ibara ya 10.2 ya Katiba ya chama chetu. Aidha, ninapenda kuwajulisheni rasmi kwamba, nimeshawasilisha taarifa rasmi kwa Katibu Mkuu wa chama chetu ya kuondoa kusudio langu la kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti kwa upande wa Tanganyika nililoliwasilisha tarehe 6 Agosti 2024. Badala yake, sasa nimewasilisha kwa Katibu Mkuu kusudio rasmi la kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa katika uchaguzi ujao wa ngazi hiyo ya juu.
URITHI WETU
Ndugu zangu na wanachama wenzangu,
Tangu mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kumekuwa na majaribio mengi, kutoka kwa baadhi ya wanachama na viongozi wa chama chetu, ya kunishawishi kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama chetu. Mara zote nimechukulia ushawishi huo kuwa ulikuwa na nia njema ya kuhakikisha kwamba tunaendeleza na kuimarisha utamaduni wa kubadilisha uongozi na madaraka ya uongozi ndani ya chama chetu uliowekwa na viongozi wakuu waanzilishi wa chama chetu, yaani Mzee Edwin Isaac Mbiliewi Mtei na marehemu Mzee Bob Nyanga Makani.
Wazee wetu hawa walikuwa wasomi waliosomeshwa katika mila na desturi za kisiasa za Kiingereza. Bila shaka walikuwa wanafahamu, na walizingatia, funzo la kutong’ang’ania madaraka lililotolewa na Oliver Cromwell kwa wabunge wa Uingereza mwaka 1653 wakati wa vita kati ya wafuasi wa Bunge na wa Mfalme Charles I: “Mmekaa hapa kwa muda mrefu sana kwa mazuri yoyote ambayo mmekuwa mkiyafanya. Ondokeni, nasema, ili tumalizane nanyi. Kwa jina la Mungu, nendeni zenu.” Kwa sababu ya ufahamu wao wa historia hii, Mzee Mtei na Mzee Makani hawakutaka kukaa madarakani mpaka watakapolazimishwa kuondoka kwa aibu. Waliandaa utaratibu wa kuondoka madarakani kwa hiari yao na kwa kutumia taratibu za kikatiba.
Kwa msiokuwa na kumbu kumbu za urithi wa wazee wetu hawa, Mzee Mtei alitumikia wadhifa wake wa Mwenyekiti wa Chama Taifa kwa kipindi kimoja tu cha miaka mitano, na alistaafu uongozi mwaka 1998 akiwa na umri wa miaka sitini na sita. Kama ambavyo ameeleza katika kitabu cha historia ya maisha yake, Kutoka Mchunga Mbuzi Hadi Gavana, mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 huku akiwa na umri wa miaka 63, Mzee Mtei alitambua haja ya ‘damu changa’ na mpya, yaani Wabunge wa CHADEMA ambao hawakuwa wajumbe wa Kamati Kuu, kuchukua dhamana ya uongozi wa chama.6 Hivyo alianzisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya chama ili kuwezesha ‘damu changa’ hiyo kuwa wajumbe wa Kamati Kuu wa moja kwa moja.7
Hivyo ndivyo ilivyotokea kwamba Mzee Bob Makani, aliyekuwa Katibu Mkuu mwanzilishi wa CHADEMA, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama, huku Makamu Mwenyekiti akiwa Dr. Willibrod Slaa badala ya Mzee Brown Ngwilulupi, na Katibu Mkuu akiwa Dr. Amani Walid Kabourou kuchukua nafasi ya Mzee Makani.8 Kwa upande wake, Mzee Bob Makani alishikilia madaraka ya Mwenyekiti wa chama kwa kipindi kimoja hadi mwaka 2003 alipostaafu na nafasi yake kuchukuliwa na Mwenyekiti wetu wa sasa, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe. Nafasi ya Katibu Mkuu ilichukuliwa na Dr. Slaa, huku Dr. Kabourou ‘akipandishwa cheo’ na kuwa Makamu Mwenyekiti.9
Ndugu zangu na wanachama wenzangu,
Ni muhimu kusisitiza kwamba mabadiliko yote haya ya uongozi wa juu wa chama yalifanyika kwa njia ya uchaguzi kwa mujibu wa Katiba ya chama. Haijatokea katika historia yote ya chama chetu kwamba uongozi wa juu wa chama chetu umetolewa kwa mwanachama yeyote kama zawadi au fadhila kutoka kwa kiongozi au viongozi walioko madarakani. Huu ndio urithi wa wazee wetu na waanzilishi wa chama chetu tunaopaswa kuuenzi na kuuendeleza.
Kwa sababu hiyo, mwanachama wa CHADEMA au mtu mwingine yeyote anayeona ajabu, au anayechukizwa na uamuzi wangu wa kutangaza nia ya kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa chama chetu, atakuwa ama hajui, au amesahau au hataki kuenzi na kuendeleza urithi tulioachiwa na wazee wetu Edwin Mtei na Bob Makani wa kuachiana madaraka ya uongozi ndani ya chama kwa njia ya uchaguzi huru na wa haki. Mtu wa aina hiyo anatakiwa kuelimishwa au kukumbushwa juu ya urithi huu, na kwa vyovyote vile asiruhusiwe kutuletea utamaduni tofauti katika kubadilishana madaraka na uongozi katika chama chetu.
UAMUZI MGUMU
Ndugu zangu na wanachama wenzangu,
Haikuwa rahisi kwangu kufikia uamuzi wa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa chama chetu. Tangu mwaka 2015 vishawishi vya kunitaka kugombea nafasi hiyo vilipoanza hadi miezi michache iliyopita, nimesema mara kwa mara, hadharani na faraghani, kwamba siko tayari kugombea nafasi hiyo. Ili kuondoa mashaka yoyote juu ya msimamo wangu huo, tarehe 6 Agosti ya mwaka huu niliwasilisha rasmi kusudio langu la kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti ambayo nimeitumikia tangu Uchaguzi Mkuu wa chama uliopita wa mwaka 2019. Kwa vyovyote vile, kubadili msimamo wangu unaojulikana wazi na kwa muda mrefu kunadai majibu ya swali la kwa nini? Swali hili ni halali na halina budi kujibiwa kwa ukweli na kwa ufasaha. Nitajaribu kufanya hivyo kwa kadri ya uwezo wangu.
MAZINGIRA MAPYA
Ndugu zangu na wanachama wenzangu,
Tangu mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, nchi yetu imeingia katika kipindi cha kipekee kabisa katika historia yake. Hiki ni kipindi ambacho wataalamu na wasomi wa siasa za Tanzania wamekiita ‘utawala wa kiimla usiokubali ushindani wa kiuchaguzi.’10 Hiki ni kipindi ambacho kimetawaliwa na siasa za kidhalimu za matumizi ya vyombo vya mabavu vya dola, mauaji, utekaji na upotezaji wa wapinzani wa kisiasa wa chama tawala. Ni kipindi ambacho vyombo vyote vya dola - majeshi, utawala, mahakama na vyombo vya propaganda - vinatumika wakati wa uchaguzi kuhakikisha kwamba hakuna ushindani wowote wa maana kwa Chama cha Mapinduzi.
‘Utawala wa kiimla usiokubali ushindani wa kiuchaguzi’ ulijidhihirisha kwa mara ya kwanza kwenye Uchaguzi wa Vijiji na Mitaa wa mwaka 2019.
Kama inavyofahamika, katika uchaguzi huo, utawala wa Rais John Pombe Magufuli, kwa kutumia udhibiti wake wa mfumo mzima wa uchaguzi, ulihakikisha kwamba karibu wagombea wote wa vyama vya upinzani wanafutwa kwa madai ya kukosa sifa za kuwa wagombea. Matokeo yake, wagombea wote wa CCM walihesabika kuwa wamechaguliwa bila kupingwa, na hivyo kuifanya nchi yetu kutawaliwa na viongozi wasiochaguliwa kabisa na wananchi kwa mara ya kwanza katika historia yetu kama nchi huru.
Ndugu zangu na wanachama wenzangu,
‘Mafanikio’ hayo ya kuiba uchaguzi wote wa vijiji na mitaa yaliufanya utawala wa Rais Magufuli kufanya maovu makubwa na mabaya zaidi katika Uchaguzi 10 Dan Paget, ‘Tanzania: The Authoritarian Landslide’, Journal of Democracy, July 2021.
Mkuu wa mwaka 2020. Magufuli alipofariki dunia mwezi Machi ya 2021 na nafasi yake kuchukuliwa na Samia Suluh Hassan, watu wengi walidanganyika na ahadi zake za kufanya mabadiliko ya kiutawala ili kuondokana na maovu ya utawala wa Magufuli. Lugha ya maridhiano ikatawala mjadala wa kisiasa.
Hata hivyo, licha ya ahadi zake, hakuna mabadiliko yoyote ya maana yaliyofanyika. Katiba ya nchi yetu imebaki vile vile ya miaka yote. Sheria za uchaguzi na mfumo mzima wa uchaguzi umebaki vile vile wa miaka yote. Watendaji wa serikali waliosimamia chaguzi zote za nyuma na kuzivuruga ni wale wale. Vyombo vya ulinzi na usalama vilivyotumika kuumiza vyama vya upinzani na viongozi na wanachama wao, kukandamiza raia na kuhujumu chaguzi za nyuma havijabadilika kwa namna yoyote ile. Mauaji ya kisiasa, utekaji nyara na upotezaji watu na matumizi mabaya ya mfumo wa kimahakama yamerudi kama ilivyokuwa wakati wa Rais Magufuli.
Na kama ambavyo Uchaguzi wa Vijiji na Mitaa wa mwezi uliopita umethibitisha, utawala wa Samia nao ni ‘utawala wa kiimla usiokubali ushindani wa kiuchaguzi.’ Kwa kifupi, kama kauli mbiu yake mwenyewe inavyoashiria, Samia Suluh Hassan ameendeleza kazi ya John Pombe Magufuli. Kama ambavyo nimesema kwingineko, tofauti pekee ya utawala wa Samia na ule wa mtangulizi wake inaelekea kuwa ni jinsia zao tu.
Ndugu zangu na wanachama wenzangu,
Utawala wa aina hii unahitaji mbinu tofauti kukabiliana nao na kuushinda. Maridhiano yameshindikana. Sasa tunahitaji kurudi kwenye hoja za msingi: Katiba Mpya ya Kidemokrasia, Mfumo Mpya wa Uchaguzi wenye Tume Huru na Sheria Bora ya Uchaguzi, Haki kwa Watu Wote. Kama ambavyo Kamati Kuu yetu imeelekeza, kauli mbiu yetu kuanzia sasa inatakiwa kuwa: ‘No Reform, No Election’, ‘Bila Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi’! Ili kutekeleza msimamo huu mpya kwa ufanisi, ni lazima tuinue ari ya mapambano ya wanachama, viongozi na wafuasi wetu na ya wananchi kwa ujumla wao. Hili litakuwa jukumu la kwanza la uongozi mpya wa chama chetu.
UONGOZI MPYA, MBINU MPYA
Ndugu zangu na wanachama wenzangu,
Mahali ambapo Samia Suluh Hassan ameifikisha nchi yetu na jukumu la kupigania Hoja za Msingi nilizozitaja kunahitaji aina mpya ya uongozi na mbinu mpya. Kwa bahati nzuri, Katiba yetu ya chama imetupatia mwongozo wa aina
ya uongozi unaohitajika katika hatua hii ya sasa ya mapambano ya kidemokrasia. Kwa mujibu wa Katiba yetu, hatua hii ya sasa inahitaji kiongozi mwenye “... historia ya uadilifu na kukubalika na jamii.”11 Ninapenda kuamini kwamba historia ya uadilifu wangu na kukubali kwangu na jamii ya Watanzania inajulikana wazi na Watanzania walio wengi.
Aidha, hatua hii ya mapambano inahitaji kiongozi aliyeonyesha “kwa tabia na mwenendo uzalendo wa kupenda … na kutetea nchi yake”12, na aliyethibitisha kuwa na “msimamo wa kuaminika.”13 Hapa pia ninaamini kwamba uzalendo wangu na msimamo wangu umepimwa na kuthibitishwa katika mapito na majaribu mengi ambayo nimepitishwa katika takriban miongo mitatu ya maisha yangu ya utetezi wa haki za wananchi wetu, na rasilimali za nchi yetu.
Kwa sababu hizo, ninapenda kuamini kwamba, baada ya zaidi ya miaka ishirini katika utumishi wa chama na wa nchi yetu katika dhamana kubwa za uongozi, mimi nina sifa hizo mahsusi na nyingine zilizotajwa katika Katiba yetu ya chama. Ninapenda kuamini kwamba, kwa sifa na sababu hizi, nina nafasi nzuri zaidi ya kuongoza mapambano ya kidemokrasia kwa ufanisi mkubwa endapo ninyi wanachama wenzangu mtanipatia dhamana ya kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama chetu.
UKOMO WA MADARAKA
Ndugu zangu na wanachama wenzangu,
Ili kuweza kutekeleza majukumu yanayodaiwa na mazingira ya sasa ya mapambano ya kidemokrasia, tunahitaji kuimarisha chama chetu katika maeneo mbali mbali muhimu. Kwanza, tunahitaji kufanya maboresho katika Katiba yetu ya chama.
Chama chetu kimekuwa kikubwa sana. Hakuna tena hofu ya kukosa viongozi katika ngazi mbali mbali za uongozi wa chama. Michuano mikali ambayo tumeishuhudia katika chaguzi za chama zinazoendelea ni ushahidi tosha kwamba chama kimekua. Katika mazingira haya, hatuna budi kurudisha tena utaratibu wa kikatiba wa ukomo wa madaraka katika chama tuliokuwa nao katika miaka ya mwanzo ya chama chetu.
Kuweka ukomo wa madaraka katika uongozi wa chama sio tu utaondoa uwezekano wa viongozi wa chama kung’ang’ania madaraka, bali pia utawezesha kujengeka kwa utamaduni wa kuandaa viongozi wapya wa chama wa kila kizazi.
Utaratibu huu utawezesha pia kupatikana kwa mawazo mapya na mbinu mpya katika uongozi na uendeshaji wa chama kwa vizazi vijavyo ili kuhakikisha chama kinaendelea kukua na kuimarika. Hii ndio ilikuwa ndoto ya Mzee Mtei wakati anajiandaa kung’atuka kwenye madaraka yake ya Mwenyekiti mwanzilishi wa CHADEMA.
Ukomo wa madaraka utapunguza sana, kama sio kuondoa kabisa, upambe na uchawa unaoshamiri pale viongozi wanapong’ang’ania madaraka katika mazingira yasiyokuwa na ukomo wa madaraka. Katika hili ni muhimu tukumbuke tahadhari aliyowahi kuitoa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere: “Kila nilipokuwa nikitaka kung’atuka walikuwa wakiniambia: ‘Mwalimu endelea tu, hii nchi ni changa na umeitoa mbali. Nchi hii haitaendelea bila wewe.’ Nami niliendelea hadi pale nilipokuja kugundua kumbe nchi changa waliyoiongelea ni familia zao, na hazitaendelea bila mimi kuwepo madarakani, maana walikuwa hawana uhakika kama Rais ajaye atawaacha katika nafasi walizokuwa nazo.”
UKOMO KATIKA VITI MAALUM
Ndugu zangu na wanachama wenzangu,
Ukomo wa madaraka unahitajika pia katika suala nyeti la ubunge na udiwani wa viti maalum. Wote tu mashahidi wa jinsi ambavyo suala la mgawanyo na namna ya kuwapata wabunge na madiwani wa viti maalum limeleta mgawanyiko mkubwa na kutishia umoja ndani ya chama chetu.
Mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2020, ilibidi chama chetu kiwafukuze uanachama karibu viongozi waandamizi wote wa BAWACHA kwa sababu ya kukubali kwao kurubuniwa na Serikali ya Magufuli ili wafanywe wabunge wa viti maalum. Hadi hivi leo wabunge hao feki wanajulikana kama COVID-19 kuashiria ubaya wa kitendo walichokifanya dhidi ya chama chetu.
Utaratibu wa wabunge na madiwani wa viti maalum uliwekwa katika Katiba ya nchi yetu ili kuwawezesha wanawake kupata uzoefu na uwezo wa kisiasa na kiuchumi katika shughuli za bunge na halmashauri za serikali za mitaa. Kwa sababu ya ubovu wa Katiba ya nchi yetu, utaratibu huu haukuwekewa masharti ya ukomo wa utumishi wa wabunge na madiwani hao, ili kuwezesha wanawake wengi zaidi kupata fursa za kujijengea uzoefu na uwezo wa kuwa wabunge na madiwani.
Matokeo yake ni kwamba tumejikuta tukikabiliwa na uwezekano wa kuwa na wabunge na madiwani wa kudumu wa viti maalum katika nchi yetu na katika
chama chetu. Ukomo wa madaraka kwa wabunge na madiwani wa viti maalum wanaotokana na chama chetu, utapanua fursa kwa wanachama wengi zaidi wa BAWACHA kuwa wabunge na madiwani wa viti maalum na hivyo na wao kujengewa uzoefu na uwezo katika shughuli za kibunge na halmashauri za serikali za mitaa. Utaratibu huu utawezesha utekelezaji kivitendo wa lengo la mwanzo la kuwa na wabunge na madiwani wa viti maalum katika vyombo vya uwakilishi wa wananchi.
MFUMO WA UCHAGUZI WA CHAMA
Ndugu zangu na wanachama wenzangu,
Eneo lingine linalohitaji maboresho ya Katiba ya chama ni suala la uchaguzi wa ngazi mbali mbali ndani ya chama. Kama nilivyosema mwanzoni, bado tuko katika mchakato wa chaguzi za chama ulioanza mapema mwaka jana. Pamoja na ukweli kwamba chaguzi hizi bado hazijakamilika hadi sasa, itakuwa kosa kubwa kusema kwamba bado ni mapema sana kujifunza masomo muhimu ya chaguzi ambazo tayari zimekwishafanyika. Mimi nimejifunza masomo mawili muhimu.
La kwanza ni umuhimu mkuu wa kuzingatia na kuheshimu Katiba ya chama katika taratibu zote za uchaguzi. Kuacha kuzingatia na kuheshimu Katiba ya chama ni kukaribisha kila aina ya uhuni, rushwa, uonevu na mambo ya hovyo katika uendeshaji wa chaguzi za chama chetu. Matokeo yake ni kupatikana kwa viongozi wa chama wasiokidhi mahitaji ya chama katika nyakati hizi ngumu za ‘utawala wa kiimla usiokubali ushindani wa kiuchaguzi.’
Aidha, matokeo ya kuachana na taratibu za kikatiba za kuendesha chaguzi za ndani ya chama kunazaa migogoro na mipasuko katika chama ambayo inakidhoofisha chama katika nyakati hizi ngumu na za hatari. Kwa vyovyote vile, ni lazima turudi katika kuendesha chaguzi na shughuli nyingine za chama kwa kuzingatia na kuheshimu Katiba yetu. Kufanya hivyo kutatuweka salama. Utaratibu mwingine wowote utatupeleka mahali ambako ni maadui zetu pekee ndio wanaotuombea twende huko. Tusiwasaidie maadui zetu katika maombi yao hayo.
Ndugu zangu na wanachama wenzangu,
Somo la pili ambalo nimejifunza kutokana na chaguzi zinazoendelea ndani ya chama chetu ni haja kubwa ya kuwa na mfumo huru wa kusimamia na kuendesha chaguzi zetu za chama. Kama ambavyo tunahitaji Tume Huru ya
Uchaguzi na mfumo huru wa uchaguzi katika chaguzi zetu za umma, ndivyo tunavyohitaji chombo huru cha kusimamia chaguzi zetu za ndani ya chama. Wanachama wetu wanaotaka kugombea nafasi mbali mbali za uongozi katika chama lazima wawe na uhakika kwamba watatendewa haki na wasimamizi wa uchaguzi katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi.
Wale wasioridhika na matokeo au na mchakato wa uchaguzi lazima wawe na uhakika kwamba rufaa zao zitasikilizwa katika wakati muafaka na chombo cha rufaa kilicho huru. Haya yote yanawezekana endapo tutarekebisha Katiba yetu ya chama ili kuweka mfumo huru wa kusimamia chaguzi za chama. Kama chama tunaweza kuchukua mfumo wa uchaguzi kama ule unaotumiwa kwenye chaguzi za Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) na kuuboresha ili kukidhi mahitaji na mazingira ya chama cha siasa cha upinzani kama CHADEMA.
FEDHA NA RASILIMALI ZA CHAMA
Ndugu zangu na wanachama wenzangu,
Chama chetu pia kinahitaji utaratibu mpya na bora wa kutafuta, kusimamia na kutumia fedha na rasilimali nyingine za chama. Kwanza, tunahitaji kuunda idara au kitengo ambacho kitakuwa na jukumu moja kuu: kutafuta fedha na rasilimali kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za chama. Utaratibu wa kutegemea mtu mmoja kuwa mtafutaji mkuu wa fedha na rasilimali za kuendeshea shughuli za chama ni wa hatari na unatengeneza utegemezi usiokuwa na afya au manufaa yoyote kwa chama. Aidha, utaratibu huo unaibua maswali mengi yasiyopendeza kuhusu umiliki wa fedha na rasilimali hizo na uwazi na uwajibikaji katika matumizi yake.
Pili, tunahitaji kutengeneza utaratibu bora zaidi wa mgawanyo wa fedha na rasilimali za chama kwa kuzingatia mazingira na mahitaji halisi ya chama. Kwa kuangalia muundo wa kikatiba wa chama chetu, shughuli nyingi na kubwa za chama zinafanyika katika ngazi za Kanda, Mikoa, Wilaya na majimbo na ngazi za chini zaidi. Aidha, ngazi hizi za chama zina viongozi, watendaji na hata wataalamu wenye uwezo wa kutekeleza majukumu mengi ya chama katika maeneo yao.
Katika mazingira haya, ni muhimu sehemu kubwa ya fedha na rasilimali za chama zielekezwe katika ngazi hizo ili kuwezesha ufanisi katika utendaji wa shughuli za chama na matumizi bora ya fedha na rasilimali hizo. Aidha, shughuli zote za chama zinazotakiwa kufanyika katika Kanda, Mikoa, Wilaya, n.k., zinatakiwa kufanyika katika ngazi hizo kwa kuzingatia hali yao halisi. Ni jambo
lisiloeleweka kisiasa na hata kiutendaji kwa shughuli za kawaida za chama kwenye Kanda, Mikoa, Wilaya na Majimbo kutekelezwa na maafisa wa chama kutoka Makao Makuu wakati kuna utaalamu wa kutosha katika Kanda, Mikoa, au Wilaya husika.
Ili kuhakikisha fedha na rasilimali hizo zinafika katika ngazi husika ya chama na kwa muda muafaka, kunatakiwa kuwa na utaratibu ambapo fedha hizo zitapelekwa moja kwa moja kwenye akaunti za ngazi husika, badala ya kupelekwa kwanza Makao Makuu ya chama halafu ndio zirudishwe kwenye ngazi za chini. Utaratibu huu utapunguza urasimu na usumbufu usiokuwa na lazima.
SEKRETARIETI MPYA NA IMARA
Ndugu zangu na wanachama wenzangu,
Sambamba na maboresho ya Katiba ya chama niliyoyaelezea hapo juu, chama kinahitaji kuunda upya sekretarieti za chama katika Makao Makuu na katika Kanda, Wilaya na Majimbo. Jukumu hili ni muhimu. Hatua hii ya mapambano ya kidemokrasia katika mazingira ya ‘utawala wa kiimla usiokubali ushindani wa kiuchaguzi’ yanatudai tuwe na sekretarieti ya Makao Makuu na sekretarieti za Kanda, mikoa, wilaya na majimbo zenye weledi mkubwa wa masuala mbali mbali yatakayokikabili chama chetu katika kipindi hiki. Kwa sababu hiyo, chama kitahitaji kuongeza nguvu ya idadi na utaalamu katika sekretarieti zake za Makao Makuu na katika ngazi zote za chini yake ili kuongeza ufanisi katika shughuli za chama.
HITIMISHO
Ndugu zangu na wanachama wenzangu,
Masuala yote haya ninayopendekeza kuboreshwa yanahitaji aina mpya ya uongozi wenye mawazo na firka mpya. Katiba yetu ya chama inataka kiongozi awe na sifa mahsusi ya kuwa na “... uzoefu katika masuala ya uongozi wa jumuiya katika nyanja za kisiasa au kwenye utumishi wa umma au taasisi mbalimbali.”14 Vile vile, kiongozi anatakiwa kuwa na “kipaji cha ubunifu, uwajibikaji na uadilifu kwani vyote hivi ni muhimu kwa kiongozi bora na mahiri.”15
Ninapenda kuamini kwamba, kwa uzoefu wangu wa kitaaluma na kisiasa; kwa historia yangu ya utumishi katika chama, bungeni na kwingineko, na kwa msimamo wangu thabiti na usiotetereka, ninazo sifa na uwezo wa kusimamia maboresho yote yanayohitajika katika uendeshaji bora wa shughuli za chama chetu katika kipindi hiki kigumu. Nitaendelea kuyafafanua masuala haya na mengineyo katika siku na wiki za kuelekea uchaguzi wa chama katika ngazi hii muhimu ya chama chetu. Aidha, ninawakaribisheni katika kuyajadili na kuyaboresha mapendekezo yangu haya kwa kadri mtakavyoona inafaa.
Nawashukuruni wote kwa kuitikia wito wangu wa kuwa pamoja nami katika siku hii ya leo.
Tundu A.M. Lissu MTIA NIA
12 Disemba 2024

- Katika mkutano huo uliofanyika Mlimani City, Tundu Lissu amedokeza kuwa anagombea nafasi ya Uenyekiti wa CHADEMA ambayo kwa sasa inashikiliwa na Freeman Mobwe
- Lissu amesema kuwa tayari ameshawasilisha maombi yake ya kugombea nafasi ya Uenyekiti kwa viongozi wa juu wa CHADEMA