KURA ya maoni iliyopigwa Uingereza Alhamisi Juni 23 ni somo kubwa kwetu sisi na watawala wetu. Kura hiyo ilipigwa kuwataka wakazi wa Uingereza waamue iwapo waendelee kuwamo ndani ya Umoja wa Ulaya (EU) baada ya miaka 43 au wajitoe.
Wapigakura milioni 17 waliamua kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya. Walioamua kujitoa walijenga hoja zao juu ya misingi ya hofu na chuki za kibaguzi.
Chuki hizo zilisababisha kuuliwa kwa kupigwa risasi na kuchomwa kisu mbunge mmoja wa chama cha upinzani cha Leba, Jo Cox, aliyekuwa akiwasaidia wahamiaji wanaoingia Uingereza.
Mwingereza mmoja alikamatwa na polisi kwa kuhusika na mauaji hayo. Alipofikishwa mahakamani na jaji alipomuuliza jina lake nani, alijibu kwa kusema: “Kifo kwa wasaliti. Uhuru kwa Uingereza.”
Ulimi wake ulikuwa fimbo. Fimbo ya chuki dhidi ya wageni waishio Uingereza. Hiyo ndiyo fimbo kubwa iliyokuwa ikitumiwa na waliotaka Uingereza ijitoe kutoka EU.
Nionavyo, kwa uamuzi wao, wameitumbukiza Uingereza gizani. Taifa limejikuta ndani ya maji makubwa ya bahari mpya isiyolijua. Wala haijulikani Uingereza itakutana na midude ya aina gani ndani ya bahari hiyo.
Waliokuwa wakitetea Uingereza ibakie ndani ya EU wamekuwa wakihoji kwamba Uingereza imepata faida kubwa za kiuchumi na nyinginezo kwa kuwa mwanachama wa EU.
Wenye kupinga wanasema kuwa muda wote wa miaka 43, na kila siku zikizidi, Uingereza imekuwa ikipunjika kwa kuwemo ndani ya EU. Baadhi ya huja zao zinafanana na zile zinazotolewa na Wazanzibari wasemao kwamba wamechoka na Muungano wa Tanzania.
Ndiyo maana Visiwani humo kuna wengi waliofurahishwa na matokeo ya kura ya maoni ya Uingereza.
Kama wanavyohoji baadhi ya Wazanzibari kuwa Muungano wa Tanzania si wa kidemokrasi, baadhi ya Waingereza nao wamekuwa wakihoji kwamba Umoja wa Ulaya si wa kidemokrasi.
Aidha, kama wanavyohoji baadhi ya Wazanzibari kwamba Muungano umeyapora mamlaka na uhuru wa kujiamulia mambo yao, baadhi ya Waingereza wamekuwa wakihoji vivyo hivyo kuhusu Umoja wa Ulaya na uhuru wao.
Kaulimbiu yao kuu imekuwa: “Tunataka turejeshewe nchi yetu” kwa sababu wanaamini ya kwamba madaraka yake mengi yamehaulishwa kutoka Bunge la Uingereza na kupelekwa Brussels, Ubelgiji, kwenye makao makuu ya EU.
Binafsi nimekuwa na mitizamo tofauti kuhusu Miungano hiyo miwili, miungano ambayo ina tofauti za kimsingi. Alhamisi iliyopita nilihakikisha kuwa niko Uingereza ili niipige kura yangu kutaka Uingereza iendelee kuwemo ndani ya EU. Kadhalika niliwahimiza wengine wapige kura kama mimi ya kukataa kujitoa.
Kusema kweli sikuwa na haja ya kushawishiwa maoni yangu yaelemee upande gani. Mwenye macho haambiwi tazama.
Kwa Muungano huu kura yangu ilikuwa ikisubiri tu. Tayari ilikwishaamua itakuwa upande gani kwa namna ninavyouenzi Muungano (Umoja) wa Ulaya licha ya taksiri zake.
Lakini lau pangekuwa na fursa ya kupigwa kura iwapo Wazanzibari wanataka waendelee kuwemo ndani ya Muungano wa Tanzania au la basi kura yangu niingeipiga vingine.
Ningefanya hivyo kwa sababu ninaamini kwamba Muungano huo hauipunji tu Zanzibar lakini umeimeza kabisa na haiwezi kufurukuta, kinyume na ulivyo uhusiano wa Uingereza na EU.