Waziri Mkuu azuia uvunaji wa miti

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesitisha utoaji wa vibali vya uvunaji wa mbao kutoka katika mashamba manane ya miti ya kupandwa, yanayosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Agizo hilo lilitolewa jana, ambapo taarifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ilifafanua kuwa, usitishaji huo unalenga kutathmini taratibu, kanuni na vigezo sahihi vinavyotakiwa kutumika katika kugawa malighafi kutoka kwenye mashamba hayo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii inamiliki mashamba ya miti ya kupandwa 18.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, kati ya mashamba hayo uvunaji umekuwa ukifanyika katika mashamba manane ambayo ni Sao Hill (Mufindi), Buhindi (Sengerema), Meru/Usa (Arumeru), West Kilimanjaro (Hai), Shume (Lushoto), North Kilimanjaro (Rombo), Kiwira (Rungwe) na Kawetire (Mbeya Vijijini).

Kutokana na hatua hiyo, Waziri Mkuu kupitia taarifa hiyo amewataka wadau wote wa viwanda vinavyojikita katika malighafi ya misitu na hususani wamiliki wa viwanda vya kupasua mbao, kuwa watulivu wakati utaratibu huu ukifanyiwa mapitio na umma utatangaziwa rasmi pindi uboreshaji huo utakapokamilika.

Kabla ya hatua hiyo ya Waziri Mkuu nchi nzima, Aprili mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Steven, alizuia kwa muda vibali vilivyotolewa kwa wafanyabiashara wa uvunaji miti katika mkoa huo.

Dk Kebwe yeye alisema lengo lilikuwa kutoa fursa kwa serikali za vijiji na kata kupata miti ya kutosha kwa ajili ya kutengeneza madawati ya shule za msingi na sekondari.

Kabla ya Mkuu huyo wa Mkoa kufikia hapo, alibaini kuwepo kwa urasimu wa mamlaka za Maliasili katika wilaya zilizomo mkoani humo, katika kutoa vibali kwa serikali za vijiji na kata, ili kupata miti ya mbao za kutengeneza madawati.

Wakati mamlaka hizo zikiwa na urasimu wa kutoa vibali kwa ajili ya serikali za mitaa kufanya kazi ya kutengeneza madawati, Dk Kebwe alibaini urasimu huo haupo kwa vibali vilivyokuwa vikitolewa kwa watu binafsi. Alisema ni aibu kwa watoto kukaa chini, wakati mkoa wa Morogoro una rasilimali nyingi za misitu, ambazo zinavunwa na wafanyabiashara.


Chanzo: Habarileo
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…