figganigga
JF-Expert Member
- Oct 17, 2010
- 25,689
- 55,662
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitaka maelezo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo na Mizani Magdalena Chuwa(kulia)kuhusu sababu zilizomfanya azuie matumizi ya flow Meter katika kuhakiki kiwango cha mafuta yanayoingia nchini kupitia bandari ya Dar es salaam wakati alipofanya ziara kwenye badari hiyo Leo. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymound Mushi.
Inaonekana bandarini mambo bado hayajakaa sawa. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof.Makame Mbarawa, wameenda Baandarini tena.
Safari hii lazima kieleweke.
Baada ya kutoka TPA, sasa Waziri Mkuu Kaelekea Kitengo cha upakuaji mafuta cha Kurasini Oil Jet(KOJ)
========
UPDATE
Aibukia kitengo cha mita za kupimia mafuta Kurasini
*Akuta mafundi wakizitengeneza, akuta zimejaa kutu
*Ataka barua ya maelezo ifikapo saa 11 leo jioni
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefanya ziara ya ghafla kwenye kitengo cha upimaji mafuta bandarini (Oil Flow Metres) na kukuta zimejaa kutu baada ya kutelekezwa kwa miaka zaidi ya mitano. Pia alitembelea mita za kupimia mafuta zinazoendelea kujengwa Kigamboni. Aidha, Waziri Mkuu amempa saa nne tu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA), Bi. Magdalena Chuwa aandike barua ya kujieleza ni kwa nini aliamua kufunga mita hizo zisitumike kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita na amletee barua hiyo ofisini kwake ifikapo saa 11 leo jioni.
“Nataka unieleze ni kwa nini ulitoa maelekezo ya kufunga mita hizo, na kwa nini jana uliamua kubadili uamuzi huo? Ni kwa nini umeamua kuchukua maamuzi haya baada ya kupokea ujumbe wa simu ya mkononi (sms) wakati mita zimekaa bila kufanya kazi kwa miaka mitano? Ni kwa nini umeamua kufanyia kazi ujumbe wa sms wakati unajua Serikali inafanya kazi kwa maandishi rasmi?” alisema Waziri Mkuu. “Umesema mlikuwa mnatumia utaratibu wa kupima kwa kijiti. Huu hauna uhakika na huwezi kutegemea taarifa ya mtu mwingine au kuingia kwenye meli ya mtu na kuanza kuchukua vipimo hadi ujiridhishe. Nataka kujua ni kwa nini mlikuwa na utaratibu wa ku-bypass mafuta ili yasipite kwenye mita za kupimia mafuta? Ni kwa nini umetoa amri zianze kutengenezwa jana na siyo mwaka 2012 au 2013?” alihoji Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu alisema mita hizo za Kurasini zilinunuliwa na Serikali kwa gharama za dola za marekani milioni 1.2 (wakati huo) na haiwezekani kuacha kuzitumia wakati watu wanachezea mifumo na kuongeza mianya ya kupoteza mapato kwa Serikali. Ameagiza mita hizo zianze kufanya kazi mara moja. Wazir Mkuu alisema matumizi ya mita hizo yaliafikiwa na Serikali baada ya kubaini upotevu mkubwa wa kodi kwenye mafuta yanayoingizwa nchini na baada ya kuona hakuna tija ya kuendelea na ukadiriaji au kupokea taarifa za waagizaji peke yao. Waziri Mkuu ambaye aliwasili Kurasini leo saaa 4: 30 asubuhi (Alhamisi, Februari 11, 2016) kwenye kitengo hicho kilichopo Kurasini (Kurasini Oil Jetty), alikagua mita hizo na kisha kwenda kukagua meli iliyokuwa ikishusha mafuta bila kutumia mita hiyo ya kupima mafuta yanayopokelewa kwa sababu mafundi walikuwa bado wanaendelea na ukarabati.
Akiwa Kurasini, Waziri Mkuu alielezwa na Bibi Chuwa kwamba mita hizo zilianza kufanyiwa ukarabati jana na leo asubuhi moja imekamilika ambayo ni ya kupokelea mafuta ya petroli. Ya dizeli ilikuwa inafunguliwa na mafundi na kukutwa imejaa kutu sababu ya kutotumika kwa muda mrefu. “Hii ya dizeli imefunguliwa leo na ile ya mafuta ya kula, haijawahi kufanya kazi tangu ilipofungwa mwaka 2011,” alielezwa Waziri Mkuu na Kaimu Mkurugenzi wa Bandari, Eng. Aloyce Matei. Alipoulizwa ni kwa nini aliamua kuzifungia mita hizo ziisifanye kazi, Bi. Chuwa alijibu kuwa alifikia uamuzi huo baada ya kupokea malalamiko kwamba zinawapunja wateja. Hata hivyo, hakufafanua ni wateja gani au wa aina gani.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa, ametembelea na kukagua mita mpya za kupimia mafuta ambazo zinajengwa Kigamboni. Mita hizo zimegharimu dola za marekani milioni 6 (sawa na sh. bilioni 12.96/- za sasa). Akiwa hapo, Waziri Mkuu alielezwa kwamba ujenzi huo ambao ulianza miezi nane iliyopita, unatarajiwa kukamilika ifikapo katikati ya mwezi Machi, 2016. “Tunajitahidi kazi hii ikamilike ifikapo katikati ya mwezi ujao,” alisema Eng. John Bura, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya BQ Contractors Ltd ambayo inasimamia ujenzi wa mita hizo.
Vilevile, Waziri Mkuu alitembelea sehemu ya kuchukulia mafuta yanayotoka bandarini (TPA Manfold) iliyoko Kigamboni na kukagua mitambo ya kusambazia mafuta kwenye matenki ya mafuta ya kampuni ya TIPER yaliyoko Kigamboni yanayomilikiwa kwa ubia bainaya Serikali na kampuni ya Oryx Energies. Katika ziara hiyo ilibainika kuwa Kampuni ya TIPER imejiunganishia bomba la moja kwa moja kutoka kwenye bomba kubwa la mafuta linalotoka bandarini hali iliyomlazimu Waziri Mkuu kuagiza kwamba bomba hilo litolewe kwenye maungio hayo ndani ya mwezi mmoja.
“Natoa mwezi mmoja hili bomba liondolewe kwenye mfumo huu na kama yapo mabomba mengine pia yaondolewe,” alisema huku akionyesha karatasi iliyokuwa mfukoni kwake yenye mchoro unaobainisha kuwa kuna bomba jingine la inchi 10 limeungwa kinyemela kwenye bomba kuu. “Kila mmoja anapaswa aje kuchukua pale kwenye manfold ili tujue nani kachukua nini. Msajili wa Hazina hili ni eneo lako na wewe unamiliki TIPER kwa asilimia 50, hebu simamia hili. Ninyi TPA leteni mapendekezo yenu Serikalini ili tuone tunaweza kudhibiti vipi vitendo kama hivi,” alisema Waziri Mkuu. Pia alimtaka Msajili wa Hazina, Bw. Lawrence Mafuru awasiliane na Mwanasheria Mkuu ili waangalie upya mkataba na umiliki wa matenki hayo uwe chini ya Serikali kwa asilimia 100 ili mafuta yanayoagizwa na Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (Petroleum Bulk Procurement Agency) yaweze kuhifadhiwa huko.
Mapema, Waziri Mkuu ambaye alifuatana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, alikagua eneo la manfold ya Mamlaka ya Bandari iliyopo Kigamboni na kukuta ni kampuni nne tu zenye matenki Kigamboni ambazo zinachukua mafuta yao hapo. Kampuni hizo ni HASS, WORLD OIL, LAKE OIL na MOIL. TIPER haikutaka kufuata mfumo huo licha ya kuwa nafasi ya kufanya hivyo ipo.