Waziri Biteko: Tanzania imejipanga vema kuhakikisha inatumia fursa ya uwepo wa soko la pamoja la EAPP la mauziano ya umeme

Kadodo1

Member
Apr 18, 2024
25
23
TANZANIA IPO TAYARI KUTUMIA FURSA YA SOKO LA PAMOJA KUUZIANA UMEME - DKT. BITEKO

📌Ni kufuatia uwepo wa fursa hiyo kwa nchi 13 wanachama wa EAPP

📌Mawaziri waridhia uwepo wa kitengo huru cha masoko cha kuuziana umeme

📌Wanachama EAPP watachangia Megawati Elfu 90 kwenye soko la pamoja la kuuziana umeme

Kampala, Uganda

Tanzania imejipanga vema kuhakikisha inatumia fursa ya uwepo wa soko la pamoja la mauziano ya umeme kwa nchi wanachama wa soko la pamoja la nchi za Mashariki mwa Afrika (East African Power Pool)- EAPP kwa kuhakikisha inaunganisha miundombinu yake ya kusafirisha umeme na nchi wanachama wa EAPP.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati wa mkutano wa 19 wa nchi wanachama wa umoja wa mauziano ya umeme EAPP uliowakutanisha Mawaziri wa Nishati na Makatibu Wakuu nchini Uganda.

Mkutano huo umezungumzia masuala mbalimbali ikiwemo kupitisha mabadiliko ya muundo wa kiuongozi wa EAPP, kuridhia kanuni na taratibu za kiuendeshaji za EAPP sambamba na kuridhia uwepo wa kitengo huru cha masoko kinachojitegemea kusimamia soko la pamoja la mauziano ya Umeme kwa nchi wanachama.

‘"Nafurahi kuona kuwa tumefikia muafaka kwenye masuala ya msingi kwenye kikao cha Mawaziri wa Nishati hususani uwepo wa kitengo huru cha Masoko kinachojitegemea kwa ajili ya kusimamia mauziano ya umeme na kwakuwa Tanzania tutakuwa na umeme kutoka mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere -JNHPP, tutatumia vema fursa hiyo kuwauzia umeme nchi wanachama pale tutakapokuwa na ziada na sisi kununua tutakapokuwa na upungufu’’ amesema Dkt. Biteko.

Katika kufanikisha hilo Dkt. Biteko amesema tayari miundombinu wezeshi inaendelea kuwekwa kupitia Shirika la Umeme Tanzania TANESCO ili kujiandaa kuingia kwenye soko la pamoja ambapo laini kubwa ya kuunganisha Tanzania na Kenya kupitia Namanga imeshajengwa na imekamilika na ile ya kuunganisha Tanzania na Zambia- TAZA imeshaanza kujengwa na itakamilika ifikapo 2026.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa sasa wa soko la pamoja la kuuziana umeme la nchi za kaskazini Mashariki EAPP na Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini nchini Uganda Mhe. Dkt. Ruth Ssentamu amesema EAPP imeridhia ushiriki wa Makatibu Wakuu wa Nishati kutoka nchi wanachama kushirikishwa katika muundo wa kiutawala wa EAPP kwa ajili ya kusaidia kuchakata na kupitia taarifa kutoka kwa watendaji wa kisekta kabla ya kupelekwa katika kikao cha baraza la Mawaziri la nchi wanachama ili kutolewa maamuzi.

Aidha, Mhe Ssentamu amesema maadhimio hayo yamefikiwa kufuatia makubaliano ya mkutano wa 18 wa baraza la mawaziri ulioanyika nchini Kenya kuhusu umuhimu wa kupitia mapendekezo ya uendeshaji wa shughuli za EAPP.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mha. Felchesmi Mramba amesema pindi uuzaji wa umeme kwenye soko la pamoja utakapoanza utatoa nafasi za ajira kwa nchi wanachama wa EAPP pamoja na kubadilishana wataalamu hususan kwenye miradi ya kusafirisha umeme na hivyo kuiongezea TANESCO mapato na hatimae kutoa nafasi ya ukuaji wa pato la Taifa.

Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo wa Baraza la Mawaziri wa Nishati uliongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo, Katibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mha. Felchesmi Mramba, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mha. Gissima Nyamo-Hanga, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mipango, Utafiti na Uwekezaji TANESCO CPA Renata Ndege, viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
IMG-20240816-WA0011.jpg
IMG-20240816-WA0007.jpg
IMG-20240816-WA0010.jpg
IMG-20240816-WA0008.jpg
IMG-20240816-WA0009.jpg
IMG-20240815-WA0032(2).jpg
IMG-20240815-WA0029(1).jpg
IMG-20240815-WA0028(1).jpg
IMG-20240815-WA0027(1).jpg
IMG-20240815-WA0026(1).jpg
 
Back
Top Bottom