Waumini wa kanisa Anglikana nusura kupigana ngumi ibadani sakata la Askofu Mokiwa.

Bilionea Asigwa

JF-Expert Member
Sep 21, 2011
16,515
28,487
BAADHI ya waumini wa makanisa ya Anglikana Dar es Salaam, nusura wazichape jana.
Hiyo ni baada ya mapadri wao kutaka kusoma waraka wa Halmashauri ya Kudumu ya Dayosisi ya Dar es Salaam unaomtetea Askofu wa Dayosisi hiyo, Dk. Valentino Mokiwa, ambaye ametakiwa kujiuzulu kwa sababu ya kashfa mbalimbali.

Waraka huo uliokuwa unasomwa jana ulilenga kujibu ule uliotolewa na Askofu Mkuu wa Kanisa hilo nchini, Dk. Jacob Chimeledya, ambao uliorodhesha tuhuma zilizokuwa zikimkabili Dk. Mokiwa ukisema kwa sasa dayosisi hiyo itakuwa chini ya Askofu Mkuu.

Baadhi ya makanisa ya Dar es Salaam, Januari 8, mwaka huu yalisomewa waraka huo wa Askofu Mkuu, Dk. Chimeledya huku mengine yakiwa hayajasomewa licha ya kutakiwa kufanya hivyo na ngazi ya taifa.

Jinsi ilivyokuwa

Katika baadhi ya makanisa, jana vurugu zilizuka mapadri walipoanza kusoma waraka wa Halmashauri ya Kudumu ya Dayosisi ya Dar es Salaam.

Hapo ndipo baadhi ya waumini walipogoma wakisema wanataka kwanza kusomewa ule wa Askofu Mkuu wajue tuhuma zinazomkabili Dk. Mokiwa.

Katika Kanisa la Mtakatifu Batholomayo Ubungo, hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya baadhi ya waumini kupiga kelele na kwenda kumzimia kipaza sauti Padri wa Kanisa hilo, James Hiza, huku wengine wakinyanyuka kwenye viti wakimtaka kutokuusoma waraka huo wa Mokiwa.

Kutokana na kelele hizo ndani ya kanisa, mmoja wa waumini hao alikwenda kuzima mfumo wa umeme na kusababisha vipaza sauti kutofanya kazi.

Hata hivyo, hatua hiyo haikusaidia kwa kuwa Padri huyo alikuwa akiendelea kusoma waraka huo.

Kuona hivyo, baadhi ya waumini walisikika wakisema ‘kama unasoma huo hakikisha unasoma waraka zote mbili’.

Hapo Katibu wa Kamati Tendaji ya Kanisa, John Mapunda, alisimama akiwa ameshikilia waraka wa Askofu Mkuu nao kumtaka ausome mbele ya waumini na kuuacha aliokuwa akiusoma.

Hata hivyo, Padri huyo aliendelea kusoma waraka aliokuwa nao na kutowajali waliokuwa wakimtaka kuacha kusoma waraka huo.

Mbali na katibu huyo wa kanisa, pia mzee wa makamo alikwenda kumsihi Padri huyo kutosoma waraka huo.

Lakini juhudi zao hazikuzaa matunda kwani alisoma waraka huo mpaka mwisho ingawa waumini waliendelea kupiga kelele muda wote bila kumsikiliza.

Baada ya kumaliza kusoma waraka huo Padri, Hiza alirudi na kukaa katika nafasi yake huku akiwataka waumini kutulia.

Waondoka na sadaka

Baada ya kumaliza kusoma waraka huo na vurugu kutulia, baadhi ya waumini ambao hawakuridhika na yaliyotokea walionekana kususa shughuli nyingine ikiwa ni pamoja na kutoa sadaka.

Waumini hao licha ya kuwa na bahasha maalumu ambazo hutumika kutolea sadaka, muda wa matoleo ulipofika, waliendela kukaa kwenye viti vyao wakiwa na bahasha zao.

Pia wengine walisusa kushiriki Meza ya Bwana ingawa wahudumu waliwasihi wasifanye hivyo.

“Tusimfanyie hasira Mungu, hata kama mmekasirika vumilieni tuendelee na ibada yaani hata kupokea mwili hamtaki?” aliwauliza mhudumu wa kanisani humo.

Baada ya ibada, Katibu wa Kamati Tendaji, Mapunda aliwaambia waandishi wa habari kuwa walikuwa wamefanya kikao na kukubaliana kutosoma waraka wowote kwa sababu Jumapili iliyopita hawakuusoma ule uliotolewa na Askofu Mkuu. Dk. Chimeledya.

“Waraka wa Baba Askofu Chimeledya hakuusoma wiki iliyopita, alisema hajaupata kumbe ulikuwapo.

“Siku chache badaye na Askofu Mokiwa ambaye ameshafukuzwa katoa waraka wake.

“Huo ndiyo alitaka kuusoma tukamwambia kwa kuwa ule wa kwanza haukusomwa kanisani na huu usiusome au usome zote ili tusiingie katika mgogoro huu. Alikubali lakini kafika madhabahuni akatugeuka,” alisema Mapunda.

Padri Hiza alipofuatwa na waandishi kuzungumzia suala hilo alisema, “Hili suala limefikia ngazi ya juu ya dayosisi, mimi siwezi kuliongelea kwa kuwa si msemaji wa dayosisi.”

Polisi watanda

Wakati hayo yakiendelea, polisi walikuwa wametanda nje ya kanisa hilo.

Baada ya vurugu kutulia kanisani, polisi hao walionekena wakizungumza na Katibu wa Kamati ya Utendaji ya Kanisa, Mapunda na baadaye wakaondoka kwenye eneo hilo.

Makanisa mengine

Hali ya sintofahamu ilitokea pia katika Kanisa la Hollyghost Kimara Mbezi ambako mgogoro wa kutaka kusoma waraka wa Dk. Mokiwa au usisomwe, uliibuka na mwisho Padri akaamua kuacha kuusoma.

Kabla ya Padri kuacha kuusoma, zilizuka vurugu za hapa na pale kiasi cha watu kufikia hatua ya kutaka kupigana.

Katika Kanisa la Mtakatifu Mariam lililopo Padre wa kanisa hilo alitaka kuusoma waraka wa Mokiwa lakini waumini walikuja juu na kuusoma wa Askofu Mkuu Dk. Chimeledya.

Katika Kanisa la Kinondoni la Kristo Mfalme, Padri Aidan Mbulinyingi aligoma kusoma waraka wa Askofu Mkuu na akausoma wa Dk. Mokiwa lakini hali ilikuwa ya utulivu.

Kanisa la Yombo Mtakatifu Thomas ulisomwa waraka wa Askofu Mkuu na kuacha wa Dk. Mokiwa huku ibada ikiisha bila vurugu.

Kanisa la Anglikana Kawe nako Padri wake aliusoma wa Askofu Mkuu na kuacha kusoma waraka wa Dk.Mokiwa.

Katika Kanisa la Mtakatifu Nikolao lililopo Ilala, Katibu wa kanisa hilo, alipoanza kusoma waraka wa Halmashauri ya Kudumu ya Dayosisi ya Dar es Salaam, waumini walipaza sauti wakimtaka ausome pia wa askofu mkuu.

Magomeni wasoma waraka wa Askofu Mkuu

Katika Kanisa la Magomeni la Mtakatifu Andrea, Kiongozi wa Walei Mkoa Dar es Salaam, Sylivester Haule aliwasomea waumini wake waraka wa Askofu Mkuu huku wakitoa msimamo wao kuhusu kuvuliwa uaskofu, Dk. Mokiwa.

Akisoma waraka huo, alisema si vema kupingana na tamko la kuvuliwa uaskofu kwa Dk. Mokiwa huku akiwasihi makasisi na mashemasi wakiwamo wainjilisti ambao wamekuwa wakitumika pasipo kujifahamu na kupoteza utii kwa Askofu Mkuu.

Haule alisema wote wanaopoteza utii kwa Askofu Mkuu kuna haja ya kujitafakari kwa sababu bado ni wachungaji.

Kiini cha mgogoro

Alisema chimbuko la tatizo ni mashtaka dhidi ya Dk. Mokiwa ambayo yaliandaliwa na Walei 32 baada ya kujiridhisha kuwa kama tatizo lingeachwa kuendelea lingelitafuna kanisa hilo kwa kiwango kikubwa.

Haule alisema mashtaka hayo yalikuwa 10 na yaliandaliwa kwa mujibu wa Kifunbgu cha 21 cha Katiba ya Dayosisi ya Dar es Salaam.

“Hivyo Halmashauri ya Kudumu ya Dayosisi ilikutana Mei 2 na 16 mwaka juzi chini ya Kasisi Kiongozi (Vicar General) na kutoa ushuri kuhusu mashtaka hayo.

“Baada ya kupitia mashtaka hayo, Halmashauri ya Kudumu ya Dayosisi ilikiri kuwapo hoja ya msingi katika shtaka lililolohusu ubadhirifu wa mali za kanisa na kuwapo mikataba mibovu ndani ya dayosisi yetu,” alisema.

Alisisitiza kuwa mikataba hiyo mibovu ilibaininka katika uwekezaji kwenye shamba ya Kanisa la Mtoni Buza, Jengo la Kanisa la Buguruni Malapa, ubia kati ya Kanisa la Mt. Andrea Magomeni, Uwekezaji katika Kanisa la Mt. Mariam Kurasini.

Mingine ni kutelekezwa kwa nyumba ya Askofu Oyesterbay, Jengo la Kanisa la Silver Oak Muhimbili na maeneo mengine ya kanisa yakiwamo makao makuu ya Dayosisi ya Mt. Nicholas Ilala.

“Tunawasihi sana maaskofu wetu na wahudumu, tusome katiba zote mbili, yaani ya Dayosisi Dar es Salaam na ya Kanisa Angalikana Tanzania ya 1970 iliyorekebishwa mwaka 2004 ili tusiwapotoshe zaidi wakristo kwenye kauli zetu na pasipo kuchukua upande wowote wa mgogoro huu.

“Tunaomba tuelewe kuwa Kanuni za Kanisa zinasimamiwa na msingi wa Mungu ambao ni Biblia. Ukanuni wa Askofu ni Miongozo ya Vitabu vya Mungu, na hivyo tujielekeze kwenye Biblia kujua kama huo ‘ukanuni’ tunaoutamka ni wa Mungu au wa Dunia,” alisema.

Habari hii imeandaliwa na Tunu Nassor, Faraja Masinde, Asha Bani, Koku David na Jonas Mushi

Source: Mtanzania
 
Dah!, hadi dini zimeshaingiliwa na shetan kama siasa naona kila padri anaunga mkono upande wake bila kujali maslahi mapana ya kanisa/dhehebu husika pamoja na miongozo yao kwa ujumla inachowataka wasimamie.
 
Waumini wa ondokeni humo kuna chukizo haribifu limesimama mahali patakatifu.
 
Back
Top Bottom