Watuhumiwa wa Uhalifu pamoja na Dawa za Kulevya zakamatwa Arusha

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
3,713
13,463
Jeshi la Polisi Mkoani Arusha limesema hali ya ulinzi na usalama mkoani humo kwa mwezi Februari hadi sasa ni shwari huku likiwakamata watuhumiwa wa uhalifu, dawa za kulevya pamoja pikipiki zinazotumika katika uhalifu.

Akitoa taarifa hiyo leo Machi 18, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amesema mafanikio hayo yametokana na operesheni mbalimbali zilizofanywa na jeshi hilo dhidi ya uhalifu na wahalifu.

SACP Masejo amebainisha kupitia misako dhidi ya dawa za kulevya walifanikiwa kukamata Watuhumiwa 21 wakiwa na Mirungi Kilogramu 549.8 pamoja na watuhumiwa 14 wakiwa na Bhangi kilogramu 157.5.

Aidha, walifanikiwa kukamata watuhumiwa 02 wakiwa na vipande 02 vya Pembe za ndovu ambapo watuhumiwa wote wamefikishwa Mahakamani na kuhukumiwa Kwenda Jela kifungo cha miaka 20 kila mmoja.

Sambamba na hilo, Jeshi hilo lilikamata jumla ya pikipiki 07 ambazo zilikua zinatumiwa na wahalifu katika matukio mbalimbali ya uhalifu mkoani humo.

Halikadhalika Kamanda Masejo amesema kuwa walifanikiwa kukamata Watuhumiwa 25 wakiwa na pombe ya Moshi lita 143 na watuhumiwa wote wamefikishwa Mahakamani kwa taratibu za kisheria.

Vilevile Jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani Watuhumiwa 19 wa makosa ya Ulawiti na Ubakaji ambapo mtuhumiwa mmoja kati ya hao amehukumiwa kifungo cha Maisha Jela kwa kosa la Ulawiti.

Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha limetoa wito kwa madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani na wale wenye namba ambazo sio rasmi (3D), kuwa litawakamata na kuwafikisha mahakamani kwani imebainika kuwa madereva wengi wanaamini wakivunja sheria watalipa faini pekee.
WhatsApp Image 2024-03-18 at 13.51.24_e5591285.jpg

WhatsApp Image 2024-03-18 at 13.51.24_8c9c023e.jpg
 
Back
Top Bottom