Miss Zomboko
JF-Expert Member
- May 18, 2014
- 4,569
- 9,430
WATOTO watano wamekufa maji kutokana na mafuriko wilayani Korogwe mkoani Tanga na kufikisha idadi ya waliofariki kufikia 12 mkoani hapa kutokana na mvua.
Aidha, kaya zaidi ya 300 zimekosa makazi kutokana na mvua hizo zinazoendelea kunyesha kwa takribani wiki mbili sasa katika maeneo mbalimbali ya mkoani Tanga.
Pia daraja la Mto Mandera lililopo Kata ya Segera mpakani mwa Wilaya za Handeni na Korogwe mkoani Tanga limekata mawasiliano ya barabara kati ya mitano ya Tanga, Dar e Salaam, Arusha, Pwani na Manyara na kusababisha magari zaidi ya 200 kukwama kwa zaidi ya saa 36, huku abiria takribani 800 wakilala nje.
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kissa Gwakisa, alisema mafuriko hayo yametokea katika Kitongoji cha Magunga - Mzia Kata ya Foroforo baada ya nyumba iliyokuwa na watu wanane wa familia moja nyumba yao kuanguka nawatoto watano kati yao kusombwa na maji ambapo kati yao miili yote mitano imepatikana.
Kufuatia hali hiyo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Korogwe ilifika katika kijiji hicho pamoja na Jeshi la Zimamoto na Uokoajiambapo kwa kushirikiana na wananchi wamefanikiwa kufukua miili ya watoto hao iliyofunikwa na mchanga usiku wa kuamkia jana.
Gwakisa alisema watu 120 ambao makazi yao yamezingirwa na maji wamehifadhiwa katika kambi maalum kijijini hapo, na ametoa tamko la watu kutokurudi katika makazi yao hadi tamko la serikali hata kama hali itarejea kuwa ya kawaida.
Naye Mbunge wa Korogwe Vijijini, Timotheo Mnzava, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Charles Mweta na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Kwame Andrew Daftari walifanya ziara ya kutembelea jimbo hilo na kujionea uharibifu wa miundombinu ya barabara.
Barabara zilizoathirika ni ya Kwashemshi-Dindila-Bungu kutokea Jimbo la Bumbuli wilayani Lushoto, ambapo kulianguka mawe makubwa yaliyoziba njia katika bonde la Kwang'andu ambapo mbunge huyo alifika hapo Ijumaa kuanzia majira ya asubuhi hadi mchana kusimamia shughuli ya kuondoa mawe na tingatinga.
Barabara nyingine zilizoharibika ni za Lewa -Lutindi, Makuyuni-Bungu, Dindila -Mpale na Mswaha. Eneo jingine lililoharibika ni daraja la Kwashemshi -Dindila eneo la Kwakibili limesombwa na maji.
Mvua hiyo imeanza kuleta madhara katika kijiji cha Dindira kilichopo wilayani Korogwe ambapo watu saba walikufa kwa kusombwa na maji na kuziacha bila makazi zaidi ya kaya 300.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Kwame Daftari, alisema kutokana na hali hiyo, magari yaliyokuwa yanasafiri kati ya Arusha na Dar es Salaam yanatakiwa yapitie njia ya Handeni kupitia Mkata wakati magari yanayofanya safari zake kati ya Tanga -Arusha, Tanga - Korogwe, Tanga - Lushoto yalisimama safari.