Watatu jela maisha kwa kukutwa na kemikali za kutengeneza ‘Smart Gin’, ‘Double Kick’

Uzalendo wa Kitanzania

JF-Expert Member
Mar 8, 2020
3,378
7,718
Dar es Salaam.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni imewahukumu adhabu ya kifungo cha maisha jela vijana watatu waliokuwa wanajishughulisha na uzalishaji na usambazaji wa pombe kali bandia.

Ni baada ya kuwatia hatiani kwa kosa na kukutwa na kemikali hatarishi aina ya ‘ethanol’ isivyo halali.

Vijana hao waliohujumiwa adhabu hiyo, ambao walitumia kemikali hiyo kutengeneza vileo vikali aina ya K-Vant, Double Kick na Smart Gin kisha kuandika stika za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na nembo bandia za kampuni zinazozalishwa vileo hivyo, ni Frank Donatus Mrema, Faham Salim Ngoda na Issa Juma Hassan.

Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatatu, Mei 27, 2024 na Hakimu Mkazi Veneranda Kaseko baada ya kuridhika na ushahidi wa upande wa mashtaka, kuwa umethibitisha kesi katika mashtaka yote matatu yaliyokuwa yakiwakabili.

Hakimu Kaseko amesema kamikali hiyo ya ethanol washtakiwa walikuwa nayo wakitengenezea bidhaa hizo ambazo ni hatari kwa maisha ya watumiaji bila kuzingatia maelekezo ya wataalamu na kwamba kwa kosa kama hilo adhabu yake ni kifungo cha maisha jela.

"Mahakama hii imezingatia kifungu cha Sheria namba 15(1), (2) na 3) cha Sheria ya Udhibiti Dawa za Kulevya ambapo shtaka la kupatikana na kujihusisha na kemikali hatarishi kwa afya za binadamu ya ethanol, adhabu pekee ni kifungo cha maisha jela," amesema Hakimu Kaseko.

"Kwa kuwa adhabu pekee kwa kifungu hicho ni kifungo cha gerezani maisha yote, Mahakama hii inafungwa mikono haiwezi kuamua tofauti na hivyo, na kutokana na kifungu hicho katika shtaka la kwanza washtakiwa wote mahakama inawahukumu kutumikia kifungo cha maisha gerezani."

Mbali na shtaka hilo, mashtaka mengine yaliyokuwa yakiwakabili ni kukutwa na stika bandia za TRA na kutumia isivyo halali nembo za biashara za kampuni zinazozalisha vileo hivyo.

Vijana hao walitiwa mbaroni Septemba 17, 2022, katika eneo la Uwanja wa Panda, Tegeta, wilayani Kinondoni, baada ya kukutwa na askari wa doria wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Kituo cha Polisi Kawe, wilayani Kinondoni, wakimiliki lita 531.2 za kemikali hiyo katika kiwanda walichokuwa wakitengenezea vileo hivyo.

Katika kuthibitisha mashtaka hayo upande wa mashtaka uliwaita jumla ya mashahidi 12 na kuwasilisha vielelezo 25, zikiwemo nyaraka na bidhaa bandia zilizokuwa zinatengenezwa na vijana hao.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo washtakiwa hawakuwa na huduma ya uwakili walijiwakilisha wenyewe.
 
Back
Top Bottom