Uchaguzi 2025 Wanawake viongozi wanavyoipa migongo mitandao ya kijamii, wapewe elimu upande huu ili wajikomboe

Mijadala ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2025 (Kabla, wakati na baada)

Mdashi

New Member
Oct 8, 2024
2
0
Na -Nishan Khamis

Zanzibar: Mitandao ya kijamii imeleta mapinduzi makubwa katika mawasiliano ya kisasa, ikitoa fursa za kipekee kwa viongozi, wakiwemo wanawake, kujitangaza, kujenga majukwaa ya kuwasiliana na jamii, na kushawishi sera za kisiasa. Hata hivyo, changamoto nyingi zinawakabili wanawake viongozi katika matumizi ya mitandao hiyo.

Siti Ali Makame, mwenye umri wa miaka 55 na Diwani wa Wadi ya Bandakuu Nungwi, Wilaya ya Kaskazini A Unguja, alianza rasmi siasa mwaka 2024. Ameeleza kuwa, licha ya maendeleo ya kidijitali, hutumia mitandao kwa kiwango kidogo, hasa WhatsApp, ingawa anatamani kujifunza zaidi. "Mara moja moja sana natumia WhatsApp katika magroup nyumbani.

Kupata habari za mikoa yote kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa soma hapa: LGE2024 - Special Thread: Orodha ya Nyuzi za Mikoa yote Tanzania Bara inayoshiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024

Najua ni fursa nzuri ya kujitangaza juu ya harakati zangu, ila sipati watu wa kunipa elimu ya mitandao. Watuone na sisi watu wa vijijini kujua juu ya kutumia fursa hizi," alisema Siti.

Ripoti ya Women at Web Tanzania ya Januari 17, 2022, ilieleza kuwa asilimia 77 ya wanawake wanasiasa nchini Tanzania wamesimamisha matumizi ya mitandao kwa muda kutokana na unyanyasaji wa kijinsia. Aina kuu ya unyanyasaji ni uchokozi wa mtandaoni kwa asilimia 77, kukera kwa makusudi asilimia 61, kuvunjia heshima asilimia 47, na udhalilishaji wa kimwili asilimia 43.

Utafiti huo pia ulionyesha kuwa asilimia 73.1 ya wanawake hawajapata mafunzo ya kujikinga dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia mtandaoni, huku asilimia 76.9 wakionyesha utayari wa kupata mafunzo hayo.

Tunu Juma Kondo, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Zanzibar, alisema kuwa sera ya UWT ni kumuinua mwanamke kisiasa, kiuchumi, na kijamii, na mitandao ya kijamii ni sehemu sahihi ya kufanikisha malengo hayo. "Mimi binafsi natumia mitandao kuhamasisha wanawake kujiingiza katika uongozi, kwani sasa watu wengi wanafuatilia mitandao kuliko TV na redio," alisema Tunu.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), wanawake hukumbana zaidi na unyanyasaji wa kimtandao kuliko wanaume. Takwimu za Marekani zinaonyesha watu 30 huripotiwa kufa kila siku kutokana na udhalilishaji wa kimtandao. Tanzania ilipitisha Sheria ya Makosa ya Kimtandao mwaka 2015 ili kudhibiti vitendo hivyo.

Nasra Nassor Omar, Naibu Katibu wa Idara ya Mambo ya Nje wa ACT-Wazalendo, alisema kuwa licha ya changamoto hizo, mitandao ni fursa sahihi kwa wanawake kujinufaisha kiuchumi na kijamii. "Mimi pia ni mfanyabiashara, natumia mitandao kupata wateja. Chama chetu kinahamasisha matumizi ya mitandao kwa ushawishi katika harakati za kisiasa, kijamii, na kiuchumi," alisema Nasra.

Suleiman Abdulla, Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar (ZBC), alisema kuelekea uchaguzi wa 2025, mitandao ni nyenzo muhimu kwa wanawake kujijenga kisiasa na kujitangaza kwa njia sahihi.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Tanzania, Prof. Kitila Mkumbo, hadi Disemba 2023, Watanzania milioni 34.4 wanatumia intaneti, na milioni 16.7 wanatumia mitandao ya kijamii.

Dkt. Mzuri Issa, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA-Zanzibar, alisisitiza kuwa matumizi sahihi ya mitandao yataepusha wanawake na watoto dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia mtandaoni na kusaidia kukuza mijadala ya maendeleo. "Watu washindane kwa hoja na sio kudhalilishana," alisema Dkt. Mzuri.
 
Back
Top Bottom