Bilionea Asigwa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2011
- 16,515
- 28,487
WAKAZI wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, wamejikuta wakizilaumu nafsi zao na kujutia kumchagua Mbunge wa jimbo hilo, Angelina Mabula kutokana na kile walichodai ameshindwa kutatua kero mbalimbali ikiwemo za migogoro ya ardhi.
Wananachi hao wamesema kitendo cha mbunge huyo kushindwa kutatua migogoro ya ardhi katika kata za jimbo hilo, kimesababisha kujutia kumchagua na kwamba maamuzi waliyoyafanya mwaka 2015, hawawezi kuyarudia tena katika uchaguzi ujao wa mwaka 2020.
Hatua ya wananchi hao inakuja kufuatia kuwepo kwa migogoro ya ardhi ya mara kwa mara ambayo inaonekana imeshindwa kupatia ufumbuzi na viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya wilaya hadi Taifa.
Wananchi hao wametoa kilio chao siku chache zilizopita mbele ya mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella, ambaye alitembelea katika maeneo ya Shibula kwa lengo la kuzungumza na wananchi hao kuhusu mgogoro wa ardhi uliopo.
Mmoja wa wananchi hao, Maduhu Daud amesema kuwa tangu mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, aingie madarakani hajawahi kutatua mgogoro wa ardhi katika wilaya hiyo.
Amesema kuwa wilaya hiyo, kila kona kumeshamiri migogoro ya ardhi lakini viongozi wenye dhamana, wameshindwa kuchukua hatua na kusababisha wananchi hao kuzurumiwa ardhi zao na watu wenye fedha na baadhi ya viongozi wa serikali.
Daud ameyataja baadhi ya maeneo yenye migogoro kwa muda mrefu ni Kitangiri katika maeneo ya jiwe kuu, mhonze, Busweru, maeneo yote yanayozunguka uwanja wa ndege wa mwanza, Kahama na Igombe.
“Mimi binafsi najuta sana kumchagua Mabula (Angelina Mabula) kwa sababu nilitarajia baada ya kuteuliwa kuwa waziri atasaidia kutatua migogoro ya ardhi kumbe ndio kabisa migogoro inazidi kushamili.
“Hawa wananchi wote unaowaona hapa, wanakabiliwa na migogoro ya ardhi kwa muda mrefu na chanzo cha migogoro hii inachangiwa na watumishi wa idara ya ardhi na baadhi ya viongozi (anawataja majina) na sasa hatuji hatima yetu,” amesema Daud.
Hata hivyo, Daud amesema wamekuwa wakifikisha malalamiko yao kwa mbunge huyo na wakati mwingine kuyafikisha kwa mkuu wa mkoa wa Mwanza lakini hakuna ufumbuzi wowote unaopatikana.
Neema Elias ni mkazi wa Kahama yeye kwa upande wake amesema kuwa pamoja na kuwepo kwa migogoro ya ardhi kwa muda mrefu katika wilaya hiyo, pia kuna kero ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Amesema nusu ya wakazi wa wilaya hiyo wanatumia maji ambayo sio safi na salama na kwamba walio wengi maji wanayotumia ni ya visima na ziwa Victoria ambayo ni hatari kwa afya zao.
Elias amesema pamoja na ukosefu huo wa maji kwa muda mrefu lakini mbunge huyo hajawahi kuwaeleza ni lini wananchi hao watapata huduma ya maji safi na salama.
“Sisi ambao hatupati maji safi na salama tulishazoea hali hiyo na kuna tatizo lingine kwenye wilaya hii kuna tatizo la mgao wa maji watu wanakaa wiki hadi wiki mbili bila maji lakini tatizo hili hatufahamu litaisha lini,” amesema Elias.
Kutokana na hali hiyo, Elias ameiomba serikali kuangalia suala hilo na kuchukua hatua za haraka kwa kuwa migogoro ya ardhi na ukosefu wa maji safi na salama katika wilaya hiyo ni vya muda mrefu.
Mtandao huu, ulipomtafuta mbunge huyo ili kuzungumzia suala hilo, amesema amejitahidi kutatua migogoro katika jimbo lake kadri alivyoweza na kwamba hawezi kuchukua hatua za kutatua mgogoro kinyume cha sheria.
“Wananchi walio wengi wanataka nivunje sheria na mimi kuwa mbunge sio mpaka nivunje sheria nafanya kazi kulingana na sheria za nchi, tayari nimetatua migogoro kwa asilimia 90 kwa migogoro yote iliyonifikia kwenye jimbo langu,” amesema Mabula.
Source: Mwanahalisi