Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,807
- 13,575
Saa chache tangu taarifa ya kufukuzwa shule kwa wanafunzi 14 wa Shule ya Msingi Izinga kwa madai ya wazazi wao kukiunga mkono Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nkasi, Afraha Hassan amesema waliokumbwa na kadhia hiyo walikuwa tisa na tayari wamewarudisha.
Taarifa hiyo ya Mkurugenzi imetolewa leo Alhamisi Desemba 5, 2024, imesema wamebaini mwalimu mkuu aliwasimamisha shule wanafunzi hao na kuwataka wazazi watafute shule nyingine na siyo kufukuzwa shule kama ilivyoripotiwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
“Uamuzi wa kuwasimamisha wanafunzi hao haukufuata utaratibu wa miongozo ya wizara. Aidha wanafunzi waliosimamishwa shule hawakuwa na kosa lolote la kinidhamu,” amesema.
Akitaja hatua walizochukua Hassan amesema: “Wanafunzi wote tisa (9) waliosimamishwa shule wamerejeshwa shuleni bila masharti yoyote. Hatua za kiutawala na uongozi dhidi ya mwalimu mkuu wa shule hiyo zitachukuliwa pindi uchunguzi unaoendelea utapokamilika.”
Mapema leo asubuhi, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda aliagiza timu ya wataalamu udhibiti ubora kwenda kuchunguza taarifa ya wanafunzi 14 wa Shule ya Msingi Izinga, iliyopo Nkasi Kusini kufukuzwa shule kwa madai ya wazazi wao kuiunga mkono Chadema kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika hivi karibuni.