Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,850
- 34,294
Maelezo ya picha,Baadhi ya watu walipotea katika mfululizo wa matukio ya utekaji nchini Tanzania
Maelezo kuhusu taarifa
- Author,Sammy Awami
- Nafasi,BBC Swahili
- Akiripoti kutokaTanzania
- Saa 3 zilizopita
“Madereva wenzake wa bodaboda wanasema wakiwa wamekaa kijiweni, ilikuja gari aina ya Noah, wakashuka watu wakamkamata kwa nguvu wakamuingiza kwenye gari. Walipowauliza nyie ni kina nani na mnaelekea wapi, walisema wao ni polisi,” alisema Consolata, dada wa Benson Ishungisha aliyepotea tangu Novemba 2023 na mpaka sasa hajapatikana.
Hizi ni baadhi ya shuhuda kutoka kwa ndugu kumi ambao BBC imezungumza nao wakielezea kupotea kwa ndugu zao katika mazingira ya kutatanisha nchini Tanzania.
Tukio la kutekwa kwa kijana Edgar Mwakabela maarufu kama Sativa mnamo tarehe 23 Juni 2024 na kupatikana siku nne baadae akiwa amejeruhiwa liliibua mjadala mkubwa katika mazungumzo ya ana kwa ana, mitandao ya kijamii na hata katika vyombo vya habari.
Wakati hali yake ya kiafya ilichochea mshikamano wa kuchangia fedha kuanzia kwa mtumiaji wa kawaida wa mtandao wa kijamii hadi Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alichangia kiasi cha shilingi 35 milioni.
Tukio hilo pia liliibua maswali juu ya waliomteka Sativa na watu wengine kadhaa ambao ndugu zao walijitokeza kwa namna moja au nyingine kuripoti kupotelewa kwa wapendwa wao katika mazingira ya kutatanisha.
Katika maelezo yake, Sativa aligusia kupitishwa katika kituo cha polisi cha Oysterbay jijini Dar es Salaam lakini akapelekwa katika jengo la karakana iliyopo eneo la kituo hicho.
Hata hivyo, mamlaka si tu zimekanusha kuhusika kwa namna yoyote na matukio haya ya utekaji, lakini zimeendelea kusisitiza kwamba raia wako salama. Viongozi wa ngazi za juu wamekwenda mbali hata kudai kwamba matukio haya ni ya kufikirika tu na hayana ukweli wowote.
Katikati ya mwezi Julai, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania (IGP) Camilius Wambura alikanusha taarifa zinazowahusisha polisi na matukio ya utekaji.
“Kwanza ifahamike, hatuhusiki na shughuli kama hizo za utekaji wa watu. Sisi ni jeshi ambalo linalinda usalama wa watu na mali zao. Kwahiyo wanaoleta tuhuma za namna hiyo ni vitendo vya kutukosea adabu. Jambo hilo halifanyiki,” alisema IGP Wambura.
IGP Wambura aliongeza kwamba kuna kasumba ya watu kujipoteza na kudai wametekwa, huku akitoa mfano wa tukio lililotokea mkoani Mwanza ambapo alisema mtoto mdogo wa miaka 12 alijiteka yeye na mdogo wake na kudai fedha kutoka kwa mama yake.
Tarehe 20 Julai, Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na machifu jijini Dodoma aliwaasa kuyakemea matukio ya utekwaji katika maeneo yao huku akilaani lawama ambayo serikali hutupiwa juu ya vitendo vya utekaji.
“Tukizungumza haya ya kutekwa haya, utasema ‘katekwa nani?’ unasikia mtoto alijiteka mwenyewe anapiga simu kwao zitoke pesa. Huku mama kamtekesha mwanawe, ili baba atoe pesa. Mwingine, sijui katekwa na nani. Yaani vidude vya drama drama tu hivi. Lakini vinavyoandikwa kwenye vyombo vya habari na magazeti ni kama serikali imelala, watu wanatekwa hovyo tu huko,” alisema Rais Samia.
Mapema mwezi huu, taarifa nyengine za utekaji zilizua gumzo nchini Tanzania. Inaripotiwa kuwa mnamo tarehe 2 Agosti, kijana Shadrack Chaula (24) alitekwa na watu wasiojulikana na mpaka sasa hajapatikana. Chaula alipata umaarufu baada ya kufungwa miaka miwili jela mnamo Julai 4 mwaka huu kwa kosa la kuchoma moto picha ya Rais Samia. Siku nne baadae, Chaula aliachiwa huru baada ya watumiaji wa mitandao ya kijamii kumchangia faini ya milioni tano.
Tarehe 9 mwezi huu (Agosti) Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kililiaani ongezeko la matukio ya utekaji na watu kupotea na kikatoa orodha ya watu 83 waliofikwa na kadhia hiyo kati ya mwaka 2016 na mwaka huu. Zifuatazo ni simulizi za familia tano ambazo zimepoteza ndugu zao katika mazingira ya kutatanisha. Jitihada zetu za kuzungumza na polisi juu ya matukio haya matano hazikuzaa matunda.
Maelezo ya picha,Benson Erasto Arbogast Ishungisa
Benson Erasto Arbogast Ishungisa, Dar es Salaam (Novemba 2023)
Imetimu miezi tisa tangu Benson apotee. Benson alikuwa na miaka 26, na alikuwa dereva wa bodaboda. Familia yake ilipata taarifa kupitia madereva bodaboda wenzake katika eneo la Buza Makangarawe ambao walisema lilikuja gari aina ya Noah, madereva wenzake walipowauliza wale watu kwenye Noah kwamba wanampeleka wapi mwenzao, wale watu walijibu kwamba wao ni polisi lakini hawakusema walikuwa wanampeleka wapi.Ndugu hao walitembelea kituo cha polisi cha Makangarawe, Chang’ombe, Maturubai, pamoja na vituo vyote vya polisi wilaya ya Temeke. Polisi waliwaambia hawalijui hilo gari kwa sababu bodaboda wenzie hawakuchukua namba zake za usajili hivyo hawakuwa na namna ya kuwasaidia.
Dada yake Benson, Consolata Ishungisa anamuelezea mdogo wake kama mtu ambaye hakuwa mkorofi. Anasema starehe yake ilikuwa kufurahia maisha na rafiki zake. Lakini kamwe hakuwa mtu wa kujihusisha na vitendo vya kihalifu au kisiasa na wala hakuwahi kusema ikiwa alikuwa na ugomvi na mtu yeyote.
“Kwa kweli hatuna matumaini tena ya kumpata. Hadi tumefika hatua hii, yaani miezi tisa sasa imeshafika. Sisi kwa kweli imefika hatua tumeamua kusema tu ‘sawa, asante Mungu. Utakavyoamua wewe, maana wewe ndio unajua kule alipo’, maana tumeshahangaika kwenye mahospitali na mochwari zote hayupo. Kwa hiyo tumebaki tu kumshukuru Mungu na kusema kwamba labda ipo siku atarudi,” anasema Consolata.
Maelezo ya picha,Yonzo Shimbi Dutu
Yonzo Shimbi Dutu, Kishapu Shinyanga (Machi 2024)
Kwa maelezo ya ndugu zake, bahati mbaya ya Yonzo ni kwamba alikuwa sehemu isiyo sahihi katika wakati usio sahihi.Yonzo, mwenye umri wa miaka 82, alikuwa anaishi wilaya ya Maswa, lakini alikuja kishapu kwa ajili ya kupata huduma kwa mganga wa jadi. Ijumaa moja ya katikati ya mwezi Machi, Yonzo alikwenda kwa mganga huyo na kupata huduma.
Inasemekana alipofika pale alimkuta kijana ambaye alikuwa ni mdogo wa mke wa mganga. Kijana huyu alikuwa anaishi mji wa Ngudu, wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza. Umbali kutoka sehemu hizi mbili, Maswa na Ngudu ni kama kilomita 80.
Ndugu wa mganga waliwaambia ndugu wa Yonzo kwamba walifahamu kwamba kijana yule alikuwa anatuhumiwa kwa mauwaji kule alikotoka ambapo mtu aliyekuwa anavutana nae kuhusu ardhi alikutwa amekufa na kutupwa.
Siku moja baada ya Yonzo kuwasili kwa mganga, magari mawili yalivamia nyumba hiyo. Inadaiwa gari moja lilikuwa limeandikwa polisi, hili lilikuwa kubwa, lakini lingine dogo halikuwa na alama yoyote. Watu walioshuka kwenye magari hayo walijitambulisha kuwa ni polisi kutoka Mwanza.
Inasemekana kwamba wale waliojitambulisha kama polisi walimchukua Yonzo na yule kijana mwingine na kuwaweka katika gari dogo lisilo na alama. Halafu wakawachukua mganga na mke wake, na majirani wengine wapatao sita wote wakawaweka katika gari kubwa iliyokuwa imeandikwa polisi.
Baadhi yao walipelekwa katika kituo cha Hungumarwa huku wengine wakipelekwa kituo cha Ngudu. Hata hivyo, hawakujua Yonzo na yule mtuhumiwa mwingine walipelekwa wapi kwasababu hawakuona gari walilokuwa wamepandishwa limeelekea wapi.
Seni Shimbi, ambaye ni mdogo wake Yonzo hakuwa na shaka maana alijulishwa kuwa watu waliokwenda kuwakamata walijitambulisha kama askari polisi
Zilipopita takribani wiki mbili, ndipo ndugu wa Yonzo walipoanza kupata wasiwasi na kuanza kuzunguka katika vituo vyote vya polisi ndani ya eneo hilo. Hata hivyo aliambiwa polisi hawakuwa wanamshikilia kaka yake. Lakini polisi walisisitiza pia kwamba gari iliyokwenda kuwachukua wahalifu lilikuwa ni moja tu na kwamba Yonzo na yule mtuhumiwa mwingine haijulikani wamekwenda wapi.
“Nilipoambiwa mwanzoni kwamba Yonzo amechukuliwa na polisi, nilisema hilo ni jambo la kawaida tu, wacha tusubiri, wao watatoka tu. Siku hadi siku nikaona hii kazi kumbe, nikaamua kwenda Hungumarwa kituo cha polisi wakasema hawajawakamata, nikaenda Ngudu hawajawakamata nikaongea na mkuu wa polisi wa wilaya na kwenyewe hivyo hivyo. Nilipokwenda Ngudu waliniambia gari lilikuwa moja, hayakwenda magari mawili. Sasa hapo ramani inaanza kupotea kuniambia gari lilikuwa moja tu,” anasema Seni.
Kaka wa Yonzo anasema wamejaribu kufanya kila wawezalo lakini wamekwama. Sasa hawajui tena nini cha kufanya.
Yonzo ameacha mke na watoto watano.
Maelezo ya picha,Lilenga Isaya Lilenga
Lilenga Isaya Lilenga, Mwandiga, Kigoma (11 Mei 2024)
Lilenga Lilenga (50) ni mfanyabiashara wa usafiri na uvuvi katika Ziwa Tanganyika. Siku ya Jumamosi ya Mei 1, alitoka nyumbani kwake akiaga kwamba anakwenda kukutana na wavuvi wake. Mke wake anasema anaamini alikamatwa wakati akirudi kutoka huko.“Saa sita na dakika 43 niliongea nae. Lakini ilipofika majira ya saa saba alikuwa hapatikani tena kwenye simu,” mke wake Johari Rajabu Kabwe anasema.
Bi Johari anasema siku chache kabla hajapotea, mtu aliyejitambulisha kwa jina la Elisha na kwamba ni afisa usalama wa taifa alikwenda eneo linaonitwa Mwamgongo ambapo chombo cha bwana Lilenga kilikuwa kikitengenezwa. Siku tatu baadae ndipo Lilenga alipotea.
“Huko nyuma aliwahi kukamatwa na polisi na walikuwa wanapeleleza vyombo vyake. Leo inajirudia tena wanaulizia kilekile chombo, lazima nipate shaka (kwamba ni polisi)? Ilikuwa tarehe 29 Mei 2022 mume wangu alikamatwa Dar es Salaam na walikuwa wakiulizia vyombo hivyo hivyo anavyovimiliki. Leo anakuja mtu kuviulizia vyombo vyake na anajitambulisha kwamba ni usalama halafu baada ya siku tatu mtu anapotea, mtu anasemaje hapo?”
Alipokamatwa Dar es Salaam miaka miwili iliyopita, Lilenga aliwekwa kituo cha Buguruni kwa wiki mbili. Lakini siku moja ndugu zake walipokuwa wakipeleka chakula waliambiwa hayupo hapo. Walipouliza yuko wapi askari walisema wao hawajui. Baada ya wiki moja ndugu wa Lilenga walimpata mkuu wa kituo na kumuuliza hata kwenda mbali na kumtaka awaambie ikiwa ndugu yao ameuwawa wajue. Mkuu wa kituo pale aliwaambia amepelekwa Kigoma kwa upelelezi zaidi kwa kuwa huko ndiko nyumbani na ndiko ambako anafanyia biashara zake. Upelelezi ulioendelea Kigoma ulihusu vyombo vyake anavyotumia kufanyia biashara za uvuvi na usafirishaji.
“Baadhi ya maswali aliyoniambia kuwa walikuwa wanamuuliza ilikuwa namna alivyovipata vile vyombo. Lakini yeye aliwaeleza wazi kwamba alivipata kupitia biashara zake tu.”
“Mume wangu ni mtu wa kujishusha, ndio kitu ninachompendea. Hata ukikosana nae yeye atajishusha na kutaka yaishe tu. Hana mgogoro na mtu, yeye ni mtu wa watu. Njoo hata nyumbani hapa umuulize mtu yeyote yule atakwambia. Kitendo chake cha kupotea kinawasikitisha watu wengi sana hadi dakika hii.”
Mke wa Lilenga anaamini chanzo kabisa cha msukosuko kati ya mume wake na mamlaka ilikuwa mwaka 2016 wakati mume wake alipokwenda Makka. Mamlaka ilitilia shaka safari hii hata kumkamata na kumuhoji mkewe wakati bwana Lilenga akiwa Makka. Anadai walimuhoji kuhusu alikozipata pesa mume wake za kwenda Makka.
Kwa mujibu wa Bi Johari, mumewe aliporudi na kwenda kujisalimisha kituoni alihojiwa kutwa nzima huku akitakiwa kutoa vielelezo vyote ikiwa ni pamoja na pasipoti iliyogongwa muhuri wa uhamiaji Makka
"Alipokamatwa kwa mara ya kwanza, polisi walimwambia wana mashaka na watu fulani anaowasiliana nao. Lilenga alikuwa tayari kushirikiana nao kuwapatia mawasiliano ya hao watu," mkewe anasema.
“Hatuna jinsi tena, maana tunafuatilia huko ambako hakuna hata majibu,” anasema Bi Johari.
Maelezo ya picha,Johnham Shayo
Johnham Shayo, Mabwepande Dar es Salaam (Mei 4, 2024)
Kaka wa Johnham na ndugu wengine wamekwenda vituo vingi vya polisi, hospitali na hata nyumba za kuhifadhia maiti lakini hawajampata ndugu yao. Waliandika hadi barua kwenda kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi na Waziri wa Mambo ya Ndani, lakini huko nako hawajafanikiwa.Ilikuwa ni mida ya mchana, Johnham alikuwa nyumbani anapata chakula na watoto ambapo alipata simu kutoka kwa mtu anayemfahamu. Mtu huyo alimwambia atoke aende barabarani ambapo ni karibu na nyumbani kwao Johnham kwenda kukutana nae.
“Akawaambia watoto samahani kuna mtu ameniita hapo njiani, naomba mfunike chakula hiki, nitarudi kuja kula” anasema Steve Omary, kaka wa Johnham.
Lakini Johnham hakurudi tena. Mke wake alidhani kwamba alipata safari ya ghafla, lakini simu yake haikuwa inapatikana. Ilipofika tarehe 9 mke wake ikabidi aende polisi kuripoti. Polisi waliwaambia kuwa watamtafuta. Hata hivyo ndugu wa Johnham wamekuwa wakisubiri majibu hadi sasa bila mafanikio.
Johnham (48) ana mke na watoto watatu, alikuwa ni dereva katika karakana iliyopo Tegeta. Miaka ya nyuma, kaka yake anasema Johnham aliwahi kushutumiwa kuhusika na upotevu wa magari. Hatahivyo, baada ya kukalishwa vikao kadhaa na familia, alionekana kuachana na shughuli zake hizo za kihalifu na kwamba kwa zaidi ya miaka minne sasa ndugu zake hawakuwahi kusikia tena kesi yoyote dhidi yake.
“Ukimuona Johnahm utafikiri ni padri. Ni mtaratibu, mnyenyekevu, ni mtu mkimya mkimya sana” Ni mpole mno, mcheshi, mkarimu” anasema binamu yake.
Maelezo ya picha,William Herman
William Herman, Kanganye, Mwanza ( Januari 2 2024)
Mara ya mwisho William - au Wile kama mama yake anavyomuita - alizungumza na mama yake Azerada Paulo siku ya Jumanne majira ya saa saba mchana, akimuuliza amepika nini mchana huo. Baada ya mama yake kumjulisha kuwa alikuwa amepika ugali, Wile akamwambia kuwa atarudi baada ya muda mfupi mara tu baada ya kuzungumza na afande Edward, ambaye alikuwa amemuita katika kilabu cha pombe maeneo ya Nyakato.Ilipofika majira ya saa tisa alasiri, mama yake alianza kupiga simu ya Wile, lakini haikuwa inapatikana tena. Kesho yake alianza kumuulizia kwa ndugu ikiwa alikuwa huko, lakini wote walisema hakuwepo. Baadae alipata simu kutoka kwa mmoja wa rafiki zake watano ambao miaka miwili iliyopita walituhumiwa kwa unyang'anyi wa kutumia silaha. Baada ya kukaa mahabusu kwa mwaka mmoja na miezi mitatu, waliachiwa huru baada ya mahakama kuwakuta hawana hatia.
Rafiki yake huyu alimwambia Mama Wile kwamba mwenzao mmoja alivamiwa usiku wa manane akiwa amelala nyumbani kwao na watu waliokuwa wameficha sura zao. Mama Wile na ndugu wengine walipozunguka vituo vya polisi waliambiwa hakuwepo. Inadaiwa kwamba kijana mwingine ambaye alikuwa anashikiliwa na polisi na kuachiwa alikuja kumwambia Mama Wile kwamba alimuona Wile kituo cha Bondeni akiwa amewekwa chumba cha peke yake. Hata hivyo baadae alitolewa kituoni hapo na haijulikani alipelekwa wapi.
Mama Wile alipokwenda kituo hicho cha Bondeni kuulizia aliambiwa hawana taarifa za Wile.
“Na huyo afande (Edward) siku wanawaachia aliwaambia wazi kabisa ‘nyinyi tunawaachia, mwende mkajirekebishe huko mtaani vinginevyo tutawakamata halafu tutawapoteza. Si mnaona kuna vijana wengine wa Meko hapo wamepotea, wazazi wao wamewatafuta hadi wamechoka, mnajua walipo? Basi na nyinyi mtakuwa hivyo hivyo. Tukishawakamata hatuwaleti tena polisi, tutawapoteza.’ Yaani walikuwa wanawaambia hivi wote tunasikia, na sio askari mmoja, askari kama watatu hivi wote wanasema hivyo ‘tutawapiga kabisa risasi, tutawapoteza hata ndugu zenu hawatajua tumewapeleka wapi’,” anasema Mama Wile.
Wile alikuwa ni kijana mwenye umri wa miaka 22 tu, na alikuwa akijihusisha na biashara za umachinga.
Baada ya kutoka mahabusu Butimba, familia yake Wile ilimkalisha kitako kumuonya juu ya vitendo vyake vinavyomuingiza matatani. Mama anasema baada ya kikao hicho Wile alionekana kubadilika kabisa hata akaanza kusaidia shughuli za nyumbani kwa bidii.
“Sisi tumeshazunguka kwenye vituo vyote vya polisi na wanatuambia hawajui. Basi, sisi tumeamua kumuachia Mungu tu, ni Mungu mwenyewe ndio anayejua. Sijui serikali yetu ina shida gani, maana unaweza kuamua kwenda hata ngazi za juu lakini hata haisaidii. Hata ukienda huko juu, hauwezi kusikilizwa”. chanzo.BBC