Wahaya na Fasihi ya Majigambo au Ebyebugo

Idd Ninga

JF-Expert Member
Nov 18, 2012
5,209
4,406
Hakuna kitu nachokichukia na kinachonikera kama kusikia kuna watu wana amini kuwa eti Ushairi umeendelea kwa sababu ya waarabu na wengine kwenda mbali zaidi na kusema Kiswahili ni kiarabu na wengine kupitiliza mipaka ya kufikiria hovyo kabisa na kuona kwamba ukichanganya maneno ya kiarabu hata kama hayapo Katika Kiswahili lakini ukiyaweka Katika ushairi wa Kiswahili utakuwa umeandika tungo sahihi ya Kiswahili lakini ukiweka neno la Kiingereza Katika Kiswahili utakuwa umeharibu Shairi lako,hapa nakereka sana hadi najiuliza hivi hawa wanao amini hivi walilogwa au ndo kusema sasa wanawafuata Kina Kamange na rafiki yake Sarahani, wanawajua kweli,tuyaache hayo.
Turudi kwenye ambacho nilipanga kukuongelea leo, fasihi ina mambo mengi sana, ina utamu wake na uchungu wake, ina Faida yake na hasara yake,fasihi ni moja ya taaluma zenye uwezo wa kutoa wasomi wengi na wakubwa, Katika hali ya kawaida, wengi hatufahamu kuwa mbali na Kiswahili, kiingereza na lugha nyingine, hata makabila yetu nchi Tanzania yalokuwa na fasihi zao kulingana na mila na tamaduni zao, ingawa fasihi ya zamani kwa asilimia kubwa ilikuwa ni fasihi simulizi kwa sababu wanafasihi wenyewe wengi wao hawakujua kusoma na kuandika lakini walikuwa hodari wa kutunga na kuhifadhi kichwani, wanafasihi wa leo, Mungu anawaona.
Unakuta mtunzi mfano wa mashairi, anaandika shairi lake na halikai kichwani, sijui ni hivi vyakula tunavyokula ama nini, yani mshairi anakwenda kusoma shairi jukwaani huku ameshikilia makaratasi mkononi, kuna tatizo mahali tujitafakari sana.
Ebyebugo ni nene la Kihaya lenye kumaanisha Majigambo , wahaya bhana walikuwa na sanaa yao na fasihi yao ya kujigamba na kuonyesha majivuno mbele ya wengine, kwa kutumia mtindo wa kama ushairi lakini uliokuwa Katika lugha ya kihaya.
Fasihi hii ilikuwa ikifanyika sana mbele ya umati wa watu na mbele ya mtemi huku mjigambi akionyesha uwezo wake wa kujigamba kuelezea sifa za ukoo wake, nguvu alizonazo, afya yake na kila ambacho aliweza kukisema mbele ya mtemi na watu wengine,unajua hadi sasa wahaya bado wanasifa, ukikutana na muhaya ukamwambia umependeza, atakwambia ‘’Hukuniona Jana’’, natania jamani si unajua watanzania utani ni jadi yetu.
Nakiri kusema kwamba sanaa hii ya majigambo japokuwa imepotea sana lakini ukiitazama utajua kumbe watanzania tulianza kuwa wasanii tangu siku nyingi sana kabla hata ya ujio wa wegeni.
Ebyebugo ilikuwa ni fasihi ya kujigamba lakini majigambo ambayo yalitakiwa kufuatana na ukweli, hakuna mjigambi alieruhusiwa kutoa habari za uongo wakati wa kujigamba na kama wakati wa kujigamba mtu angetoa majigambi ya uongo basi lingemkuta la kumkuta, tutaona hapo mbele kidogo.
Sanaa ya Majigambo kwa wahaya ilikuwa na shabaha moja kubwa ya kuonyesha matendo ya kishujaa yaliyotendwa na wana Jamii Katika Jamii ya Kihaya.
Mjigambi kabla ya kwenda kujigamba alitakiwa kuvaa mavazi Maalumu huku akiwa ameshika mkuki, panga au silaha yeyote ya kijadii ambayo itamfanya kuwa Katika muonekano wa kishujaa ili hata saa akijigamba watu wajue huyu shujaa kweli, huyu mwamba, vijana wa sasa wanasema, Jembe.
Majigambo yalikuwa yakifanyika Katika eneo Maalumu lilioandaliwa kwa ajili ya Tukio la kujigamba na wakati wa kujigamba mtu alikuwa akisindikizwa na ngoma Maalumu ilokuwa ikiitwa Omutoro, sasa hapa vijana tujiulize tu, hizi ala za kwenye muziki zinzotumika leo tofauti yake ni kubwa ni mifumo ya kisasa, lakini tangu zamani, hata kabla ya ya wakoloni kuikanyaga Tanganyika tayari wazee walikuwa wamebuni ala zao na wakizitumia, duh kumbe sisi tumebuni tu, wazee walishavumbua tangu zamani.
Hapo awali kabisa, Majigambo yalikuwa yakitolewa kabla ya mashujaa kwenda vitani na baada ya mashujaa kurudi Kutoka vitani . mashujaa walitumia Majigambo kama njia ya kupandisha mori na kujipa moyo ili wakashinde vita, na yote haya yalifanyika mbele ya Mtemi.
Wakati wa Kutoka vitani, Mashujaa walikutana tena kwa ajili ya kujigamba mbele ya mtemi na umati wa watu, hapa sasa palihitaji kuongea ukweli tu, mjigambi mara baada ya kumaliza kujigamba namna alivyokuwa hodari vitani,namna alivyoaangamiza madui zake na namna alivyoteka mifugo Pamoja na vitendo vyote vya kishujaa, mtemi aliwaauliza wananchi kama ambacho kimesemwa ni cha kweli ama kuna uongo ndani yake,kama mjigambi atakuwa kasema kweli, basi Mtemi alikuwa akimkabidhi zawadi ya pombe Pamoja na sehemu ya mifugo aloiteka wakati wa vita na shujaa huyo aliwekwa upande wa kulia wa mtemi.
Lakini, kama mjigambi akigundulika kuwa alisema taarifa ya uongo, kwa kujigamba kwa sifa za uongo, basi mtu huyo aliishiwa kuzomewa, alipewa maji badala ya pombe, na aliwekwa upande wa kushoto wa Mtemi na isitoshe mke wa mjigambi aliesema uongo na kuonekana siye shujaa , alijihisi hana Mume, na wakati mwingine Wanawake wa Kihaya ili kuficha aibu ya kuonekana wameolewa na Wanaume wasiokuwa mashujaa na majasiri, basi wao waliwataliki waume zao na hapo mazoe ya mume na mke yaliisha, duh, hawa Wanawake walikuwa jasiri kweli.
Mbali na vita, Ebyebugo ilitumika pia wakati wa kijana kuoa baada ya kuwa tayari amekabidhiwa mke na kumuingiza ndani, basi kijana alikuwa akitoka nje ya nyumba yake akiwa na mkuki na kwenda mbele ya baba yake Pamoja na watu wengine na kujigamba ili kuonyesha umwamba alio nao na ujasiri wake na baada ya hapo kijana alimkabidhi baba yake mkuki kama ishara ya kuionyesha heshima .
Fasihi hii ilikua ikitumika sehemu nyingi sana, hata Katika nyakati za uwindaji na kadhalika, lakini siyo kila sehemu mjigambi alitakiwa kujigamba akiwa na silaha.
Sanaa hii ya Majigambo ilianza kupotea zaidi mwaka 1962 wakati ambapo rasmi tawala za kitemi zilivunjwa wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere wa Uhuru Bingwa na Mwafasihi mkubwa.
Mabadiliko ya kielimu, kitamaduni, kiutandawazi yalichangia sana kupotea kwa sanaa hii ya fasihi lakini baada ya Kiswahili kuwa ndio lugha inayowaunganisha watanzania wote, hata fasihi ya Majigambo ilianza kubadilika na kuwa Katika lugha ya Kiswahili licha ya kuwa fasihi hii sasa hivi imepotea kwa kiasi kikubwa na itahitaji muda na uwezo mwingine kuweza kuirudisha sanaa hii.​

Idd Ninga
Arusha
+255624010160
iddyallyninga@gmail.com
 
Back
Top Bottom