Wabunge wekeni tofauti zenu pembeni mdai fedha za michango ya waathirika wa tetemeko-Kagera

magode

JF-Expert Member
Oct 2, 2014
2,204
3,337
Wanabodi
Salaam;

Anaandika Luqman maloto.

Mfiwa hufarijiwa kwa maneno na vitendo. Ukimsimanga mfiwa unamtonesha kidonda chake ambacho pengine huwa kimeanza kupona na kugeuka kovu.

Mtu ambaye hukumbwa na janga hupozwa kwa maneno mazuri na msaada mbalimbali. Maneno matamu na misaada huwa havifuti maumivu na hasara, isipokuwa hupunguza machungu.

Angalau mfiwa au mwathirika wa janga hujiona kuna watu wanaungana naye kwenye kipindi kigumu anachokuwa nacho. Kipindi cha ufiwa au uathirika wa jambo fulani, hakuna mtu ambaye angependa kuambiwa maneno mabaya.

Wanaharakati wa mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi, wamefanikiwa kupunguza unyanyapaa kwa kiasi kikubwa. Mtu anaumwa halafu unamwongezea mzigo wa masimango, si unamfanya atamani kufa?

Hata yule ambaye anamshambulia mwathirika wa dawa za kulevya (teja), naye ana upungufu wa utu. Mtu yupo kwenye maumivu makali, wewe unamwongezea mzigo wa mashambulizi. Unamfanya azidi kukata tamaa.

Ukikutana na mwathirika wa dawa za kulevya akikulilia kuwa anatamani kuacha uteja, wewe mtie moyo kuwa anaweza kuacha, pengine kwa maneno yako akapata nguvu na kujiona kweli anaweza kushinda vita hiyo.

Binafsi hata ule utani wa makabila huwa siukubali nyakati za matatizo. Nimefiwa uje unitanie hatuwezi kuelewana. Msiba usikie kwa mwenzako, ukikufika unaweza kunena lugha za mataifa yote.

MWANGWI KUTOKA KAGERA

Waathirika wa tetemeko wameshaambiwa kuwa hawatejengewa nyumba wala kufidiwa kwa chochote na Serikali. Kwamba kila mmoja ajue namna ya kujenga nyumba yake.

Serikali haikusababisha tetemeko, hivyo huwezi kuilaumu. Tetemeko la ardhi kama lililotokea Bukoba, Kagera, Septemba 10, mwaka jana, ni tukio ambalo huwa halina matazamio kisayansi. Hutokea tu.

Uwezo wa Serikali ya Tanzania ni mdogo kujenga nyumba za waathirika wote na kuzifanya ziwe mpya tena. Hilo pia linafahamika na katika hilo, huwezi kuilaumu Serikali kwamba inakataa kuwajengea nyumba waathirika pamoja na kuwapa fidia nyingine.

Hata hivyo, michango ya waathirika wa tetemeko kwa namna ilivyotolewa na jinsi harakati za ukusanyaji wa michango zilivyofanywa, ndiyo inatoa sauti yenye mwangwi kuonesha kuwa lipo jambo halipo sawa na lazima lisemwe.

Michango ilikusanywa na ikapatikana, hata kama haiwezi kujenga nyumba ya kila mmoja, si vibaya hesabu ikapigwa, angalau kuwe na kiasi fulani cha fidia, kisha kila mwenye nyumba ajiongeze na zake aweze kuinua ‘mjengo’ wake.

Tangazo la michango lilisema “changia waathirika wa tetemeko”, kwa hiyo walengwa ni waathirika. Kwa mantiki hiyo lazima wapewe walichochangiwa.

Kwamba michango itatumika kujenga miundombinu iliyoharibiwa na tetemeko. Ni sawa, miundombinu ni muhimu mno, lakini ingekuwa vizuri kama tangu awali, wachangiaji wangeambiwa kuwa michango yao ni kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu.

Matangazo kuwa waliokuwa wanachangiwa ni waathirika kisha fedha zikawa zinatangazwa kadiri wachangiaji walivyokuwa wanachangia, iliwapa matumaini kuwa michango hiyo inawahusu lakini inapitia kwenye mkono wa kamati ya maafa.

Kinachozungumzwa kwa sasa ni kuwa kama mtu alitaka kumchangia ndugu yake Bukoba ili ajenge nyumba yake, alipaswa kufunga safari moja kwa moja akaonane naye na kumpa huo mchango.

YAPO MAMBO TUKUMBUSHANE

Kipindi cha ukusanyaji wa michango zilikuwepo tamthiliya nyingi. Kwanza watu wengi waliokwenda kuchangia, waliambiwa hawawezi kwenda moja kwa moja mpaka michango yao ipitishwe kwenye kamati.

Ni kamati moja tu ya maafa iliyokuwa chini Waziri Mkuu, ndiyo iliyokuwa na mamlaka ya kukusanya michango. Hatauwezi kuacha kukumbusha kuwa ‘figisufigisu’ za michango zilikuwa nyingi.

Ikiwa tu waliokwenda na viroba vya mchele iliamriwa michango yao isipokelewe mpaka kwanza ipitishwe kwenye kamati maalum, je, nani mwingine mwenye fedha angeweza kukubalika kuonana na waathirika moja kwa moja?

Tukumbuke kuwa wakati wa ukusanyaji wa michango, ipo akaunti ‘batili’ ilifunguliwa kwa ajili ya ukusanyaji wa fedha za waathirika. Wahusika walitumbuliwa na kufikishwa mahakamani.

Aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Amantus Msole, Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Kelvin Makonda, Mhasibu wa Mkoa wa Kagera, Simbaufoo Swai na Meneja wa CRDB tawi la Bukoba, Carlo Sendwa, waliburuzwa mahakamani.

Hii maana yake ni kuwa hakuna mtu ambaye alikuwa anaruhusiwa kukusanya michango zaidi ya kamati iliyoundwa. Tunapokumbushana huwa na maana mbili, kurejeshana kwenye mstari kama kuna usahaulifu, vilevile kusemezana kuwa hatujasahau.

Matangazo yangetolewa kuwa wenye kutaka kuwachangia waathirika moja kwa moja wawafuate Kagera, pengine wengine wangekwenda au wangetokea wengine wenye kukusanya michango ya moja kwa moja kwa waathirika.

Wahusika wanapaswa kutambua kuwa ukakasi mkubwa unatokana na aina ya ukusanyaji wa michango na matangazo yake. Uamuzi wa sasa unaonekana kama kuwageuka waliochangia na waliodhaniwa kuwa wanachangiwa.

Jambo rahisi kwa Serikali, ingeomba radhi kuwa kamati yake chini ya Waziri Mkuu, haikuwa na madhumini ya michango ya waatirika moja kwa moja, bali kilichotokea ni makosa ya lugha. Labda hapo kwa mbali, watu wanaweza kuelewa.

Nasisitiza: Kwa mbali watu wanaweza kuelewa. Ni kutokana na ukweli kuwa maelezo ya mwanzo na uamuzi wa baadaye kuna mpishano mkubwa. Kwa nia njema, Serikali iseme kuwa ilikosea lugha ya “changia waathirika”, bali ilikusudia kutamka “changia athari za miundombinu ya tetemeko.”

Hata kauli ya Waziri Mkuu alipokuwa anahimiza watu kuchangia, alieleza nyumba za waathirika zilizoharibiwa ni nyingi. Kauli yake hiyo, ilikuwa inazidi kujenga picha kuwa walengwa wa michango ni waathirika na mali zao zilizoharibiwa na tetemeko. Tunakumbushana tu, tena tunakumbushana kwa nia njema.

BUNGE LINAPASWA KUHOJI

Sauti za wananchi kwa wingi wao hazijatosha kuifanya Serikali ione kuwa michango iliyokusanywa siyo fedha za ukarabati wa miundombinu bali ni msaada wa moja kwa moja kwa waathirika wa tetemeko Kagera.

Serikali kupitia kamati ya maafa iliyoongozwa na Waziri Mkuu, yenyewe ilijikasimisha jukumu la kukusanya michango na imani ikawepo kuwa baada ya makusanyo, waathirika wangegawiwa kile walichochangiwa.

Ujenzi wa miundombinu ni shughuli ya Serikali. Ingeweza kurejea bungeni kwa hati ya dharura kuomba fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundominu iliyoharibiwa na tetemeko Kagera. Hakuna mbunge ambaye angepinga wakati ni janga lililoishtua dunia nzima.

Hivyo basi, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kakao chake cha Januari hii, linapaswa kumbana Waziri Mkuu katika maswali papo kwa papo. Aeleze ni kwa nini msingi wa kuchangia waathirika umekiukwa na imekuwa kama vile michango ililenga Serikali?

Nimeshaeleza ujenzi wa miundombinu ni jukumu la Serikali. Ukisema fedha zinakarabati miundombinu maana yake Serikali ndiyo ilichangiwa. Utaona kuwa Serikali imesababisha mgongano wa maslahi, kati yake na waathirika wa tetemeko. Kumbe wote walikuwa wanahitaji kuchangiwa.

Mkanganyiko unakuja kwa sababu wakati Serikali na waathirika kila upande ukihitaji kuchangiwa, Serikali ndiyo ikawa mkusanya michango. Mwisho kabisa Serikali ikatamka, “fedha ni za Serikali” kwa ajili ya kukarabati miundombinu.

Bunge linatakiwa lifanye kazi yake ya kuibana Serikali kwa ajili ya waathirika wa tetemeko. Likionesha uimara wake kama nchi na kwa hisia juu walioumizwa na janga la tetemeko Kagera, wataweza kuizuia Serikali kutumia fedha za waathirika, kisha zitaelekezwa kwa walengwa.

SERIKALI IPENDE KUJIFUNZA

Mataifa mengine yote, athari za majanga kama tetemeko la ardhi, mafuriko, kimbunga na kadhalika kwa kutambua kuwa huacha hasara kubwa kwa wananchi, Serikali hujitahidi kuwapa waathirika nafuu mbalimbali.

Hapa Tanzania waathirika wa tetemeko Kagera, wameambiwa ili wapate unafuu wa vifaa vya ujenzi inabidi watafute wawekezaji, waanzishe viwanda vya vifaa vya ujenzi Kagera kisha ndiyo wauziwe kwa bei nafuu.

Kipindi hiki ambacho mwananchi nyumba yake ilibomolewa, anaishi nje kwa kukosa makazi, ushauri anaopewa ni kutafuta wawekezaji wa viwanda vya vifaa vya ujenzi, halafu bei za vifaa ikipungua ndiyo aweze kujenga na kuondokana na shida ya kulala nje.

Mataifa mengi duniani kama siyo kuwajengea waathirika wa majanga, basi huwapa vifaa vya ujenzi ama bure au kwa bei nafuu ili waweze kumudu kununua. Hufanya hivyo kwa sababu majanga hutokea bila matazamio ya kisayansi, hivyo wananchi wanakuwa hawajajiandaa.

Agosti 24, mwaka jana, tetemeko la ardhi lilitokea kwenye miji ya Lazio, Umbria na Marche, Italia. Likarejea tena Marche Oktoba 26, mwaka jana na Oktoba 30, mwaka jana lilitikisa Umbria na Marche, Italia.

Oktoba mwaka jana, Waziri Mkuu wa Italia, Matteo Renzi, aliahidi kuwa Serikali itawajengea waathirika wote nyumba za muda mfupi ili waweze kuishi wakati Serikali na wananchi wakijipanga kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za kudumu.

Oktoba 27, mwaka jana, Kamishna Mkuu wa Ujenzi wa Italia, Vasco Errani, aliwaahidi Waitaliano wote kuwa jukumu la ujenzi wa kila nyumba ya mwathirika ni la Serikali kwa asilimia 100.

“Tutajenga kila kitu, kwa asilimia 100, hilo ni jukumu la Serikali,” alisema Errani kama alivyonukuliwa vyombo vya habari vya Italia na vile vya kimataifa.

Ukienda Marekani, Serikali hutoa mafao ya unafuu wa majanga (Disaster Relief Benefits). Eneo ambalo litatangazwa kukumbwa na janga, waathirika ambao athari zao huwa haziwezi kufidiwa na bima, hupewa unafuu wa kimaisha baada ya majanga.

Ukibomokewa na nyumba, taasisi ya Small Business Administration (ABA) ambayo ni tawi la mafao ya Serikali, hukopesha mpaka dola 200,000 (Sh417 milioni) kwa mwathirika kujenga nyumba yake au kuikarabati. Fedha hizo mwathirika hulipa kidogokidogo kwa miaka 30.

Ukiharibikiwa na biashara kwa sababu ya janga au ulikuwa na mkopo, kwa hiyo unashindwa kulipa kutokana na athari uliyopata baada ya janga, SBA pia hushughulikia changamoto hiyo kwa kumwezesha mwathirika kufufua upya biashara yake na kulipa mkopo.

Ikiwa janga limesababisha kifo cha mkuu wa kaya, kwa hiyo waliobaki hawana ajira ya kuwawezesha kuindeleza kaya, mpango wa kuwasaidia waathirika wa janga wasio na ajira (Disaster Unemployment Assistance) hutumika kuwasaidia makazi na kuwawezesha kimaisha.

Ipo mipango ya kila namna, ikiwa shamba limeharibika au mazao yameharibiwa, kama ulikuwa na kesi kabla ya janga, ulikuwa unadaiwa kodi na Serikali na mambo mengine, yote yana vitengo vyake vya kushughuikia.

Tanzania haina uchumi mkubwa kama Marekani na Italia lakini suala la utu wa Mtanzania linapaswa kuwa kipaumbele cha Serikali. Isijenge nyumba za Waathirika kama ambavyo Italia wanafanya, wala wasitoe mafao kama Marekani lakini mawili yanawezekana.

Mosi, kuwapa msamaha wa kodi ya vifaa vya ujenzi waathirika wa Kagera ili wapate unafuu wa kujenga na kurejesha makazi yao, pili kuwapa fedha zao walizochangiwa na watu mbalimbali duniani.
 
Back
Top Bottom