Mwenyekiti wa Kamati ya bunge ya viwanda na biashara Mhe.Dr.Dalaly Peter Kafumu (CCM) ametoa rai ya kujiuzulu uongozi wa kamati hiyo, kufuatia kuandamwa na baadhi ya viongozi wa serikali kufuatia nia yake ya kumtembelea Mbunge wa Arusha mjini Mhe.Godbless Lema alipokuwa gerezani.
Dr.Kafumu ametoa rai hiyo kwenye kikao cha kwanza cha kamati ya viwanda na biashara kilichoanza leo. Kafumu na Makamu mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe.Vicky Kamata walipanga kumtembelea Mhe.Godbless Lema gerezani kwa kuwa ni mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo.
Baada ya taarifa hiyo, viongozi mbalimbali walisikika kukosoa utaratibu huo na kuwaita wasaliti. Kafumu amesema haoni sababu ya wao kuitwa wasaliti kwa kuonesha nia ya kumtembelea mjumbe mwenzao wa kamati. "Mhe.Lema ni mjumbe mwenzetu wa kamati hii, kwanini ionekane ni dhambi kumtembelea alipopata matatizo?" Dr.Kafumu amewahoji wajumbe wa kamati hiyo?
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe.Vicky Kamata amesema kuwa ikiwa Dr.Kafumu atajiuzulu uenyekiti, naye atajiuzulu nafasi yake ya makamu mwenyekiti.