Kufuatia kuwepo kwa taarifa katika mitandao ya kijamii hususani JForums, juu ya kupandishwa kizimbani kwa aliyekuwa mkurugenzi wa NSSF Dr. Dau, waandishi wa habari na wapiga picha waliweka kambi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu jijini Dar es Salaam juzi kumsuburi.
Kutokana na kuenea kwa taarifa hizo, Ijumaa waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari na wapiga picha walionekana kwa muda mrefu wakizunguka zunguka katika mahakama hiyo wamkisubiri kufikishwa mahakamani.
Waandishi hao baada ya kusubiri Kisutu kwa muda mrefu bila kupata walichokuwa wakisubiri walielezwa na vyanzo mbalimbali vya habari kwamba huenda Dk. Dau atafikishwa mahakamani hapo kesho.
“Tumeambiwa na chanzo kimoja kwamba kama hataletwa Jumatatu basi ndani ya wiki ijayo lazima atafikishwa Kisutu,” alisema mwandishi mmoja wa habari aliyekuwa mahakamani hapo.
Februari 15, mwaka huu, Rais John Magufuli alimteua Dk. Dau kuwa balozi sanjari na Mathias Chikawe na Asha-Rose Migiro.
Kuondolewa kwake kwenye nafasi hiyo nyeti na kuteuliwa kuwa balozi kulisababisha mijadala kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, baadhi wakisema amepanda na wengine wakisema kuwa ameporomoshwa. Zimepita siku 56 tangu Dk. Dau ateuliwe bila kupangiwa kituo cha kazi. Machi 19, Rais Magufuli alimteua Profesa Godius Kahyarara kuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF.
Muda mfupi tangu alipoteuliwa Mkurugenzi huyo mpya ambaye alikuwa Mkuu wa Shule Kuu ya Sayansi ya Jamii (COSS) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kashfa za mfuko huo zilianza kuwa habari ya mjini kwenye vyombo mbalimbali vya habari na katika mitandao ya kijamii.
Kashfa hizo zinahusu mikataba mibovu ambayo NSSF iliingia wakati wa uongozi wa miaka 15 wa Dk. Dau na makampuni mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa miradi yake, hasa majengo na hoteli za kisasa.
Akihojiwa na Nipashe Msemaji wa Takukuru, Tunu Mleli alisema masuala ya uchunguzi hayawekwi hadharani kutokana na unyeti wake hivyo alishauri wananchi wawe na subira kuhusu suala la NSSF. Alisema hawawezi kuweka hadharani uchunguzi kama sheria inavyowataka kufanya hivyo.
“Watuhumiwa wa Egma na Stanbic si mmeona wamefikishwa mahakani, sasa msiwe na papara kutaka kufichua mambo ambayo hayajakamilika," alisema Mleli. "Kwani kama NSSF kuna ufisadi si uchunguzi utafanyika na hatua zitachukuliwa kama zingine ambazo zimeshachukuliwa kwa wengine?”
Wiki iliyopita Takukuru ilimfikisha Kamishna Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake wawili mahakamani kwa tuhuma za utakatishaji wa Dola za Kimarekani Milioni 6 (sawa na Sh. trilioni 1.3) mali ya serikali. Kesi hiyo inahusu kashfa ya Enigma na Stanbic aliyokuwa akizungumzia msemaji wa Takukuru, Mleli jana.
Source: Nipashe