armmando
Member
- Jan 18, 2016
- 21
- 11
USHIRIKA KAMA NYENZO KUU YA MAENDELEO.
Vyama vya ushirika ni msamiati unaokaribia kufutika kabisa kwa kizazi cha sasa. Vyama kama SHIRECU, KCU na KNCU viliweza, kwa wakati wao, kuleta mapinduzi kwenye sekta za kilimo cha mazao ya kibiashara kama pamba na kahawa. Kupuuzwa kwa dhana ya ushirika kumepelekea leo viwanda vyetu kama Mutex, Urafiki na Ginneries zilizokua maeneo mbali mbali nchini kubaki magofu. Pia matatizo ya uhaba wa mbolea na mafuta ya kula, licha ya sababu zingine, ni matokeo ya kutokusimamiwa vizuri kwa sekta ya ushirika nchini.
Mara nyingi dhana ya ushirika umekua ikihusishwa moja kwa moja na sera za ujamaa, hivyo, kuanguka kwa ushirika huenda kukaonekana kama hatua ya lazima kufuatia kupotea kwa ujamaa. Hata hivyo, kwa kuwa ushirika ni muungano wa hiyari wa wanachama wenye lengo moja, kwenye andiko hili nitazungumzia ushirika kama “Limited Liability Corporations” ambazo zinamilikiwa na wanajamii wenyewe, wenye malengo sawia kwenye sekta moja.
Kwa kuwa na ushirika imara, tutaweza kuunganisha mitaji, kulima na kuchakata mazao yetu wenyewe, kuwa bidhaa nyingi za kwetu katika soko la ndani na kuacha kutegemea bidhaa kutoka ng’ambo. Kwa mfano, sote tunafahamu kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye mifugo mingi Afrika. Wafugaji 2000 wakiunda ushirika, wakitoa mifugo michache kila mmoja, tunaweza kuanzisha kiwanda bora kabisa cha viatu na bidhaa za ngozi au kiwanda cha kusindika nyama. Vivyo hivyo kwa wakulima na makundi mengine. Mfano: kila mfugaji akitoa ng’ombe sita, wenye thamani ya shilingi laki tano, kwa wafugaji elfu mbili, itakusanywa Bilioni 6. Haitoshi kuanzisha kiwanda kizuri kuchakata ngozi? Haitoshi kuanzisha kiwanda cha kuchakata nyama tukaacha kununua kutoka nje? Haitoshi kuanzisha kiwanda kitakacholeta ushindani kwa NIDO au Lactogen? Ni aibu, kwa idadi ya mifugo tuliyonayo, kuendelea kuvaa viatu vya mitumba ‘vilivyotupwa’ na wenzetu walionunua ngozi kutoka kwetu, au kuendelea kuagiza maziwa kutoka nje.
Vivyo hivyo katika kilimo, wakulima wakiungana wataweza kuzalisha mbolea wenyewe, kuchakata na kuongezea thamani mazao yao na kuuza bidhaa zilizosindikwa. Wataweza kujenga skimu za umwagiliaji, kufanya kilimo cha kisasa na kuwa na uhakika wa bei sokoni. Hivyo, tutapunguza au kumaliza kabisa tatizo la mafuta ya kupikia, mbolea na soko, na bidhaa zetu zitakua na ubora wa kuuzwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na mabara mengine. Hii si kwa sekta ya kilimo na mifugo tu, bali hata kwa sekta zingine. Graduates 1000 wenye shilingi laki moja kila mmoja, hawawezi kufanya chochote kwa pamoja kwa mtaji wa milioni mia moja? Kwani ni lazima wote waende kuwa machinga?
Maendeleo kwa jamii yoyote ile, hutokana na uwezo wa jamii hiyo kumiliki nyenzo za uchumi, usimamizi mzuri wa rasilimali kwa manufaa ya wote pamoja na utawala bora. Kupitia ushirika, jamii itawezeshwa kwa pamoja, kumiliki rasilimali, kuzalisha na kuwa na sauti ya pamoja katika soko. Ushirika ni mali ya wanaushirika, kama ukisimamiwa vizuri na kutekeleza matakwa ya wanaushirika na malengo ya kuanzishwa kwake, utasaidia kuiinua jamii kiuchumi, kuiwezesha jamii kumiliki nyenzo za uzalishaji na kuondoa umasikini. Tukiwa na ushirika imara, tutamiliki uchumi wetu.
Kwa kuwa na ushirka imara, tutaweza kusimamia vizuri rasilimali zetu. Fedha inayokwenda mfano, kwenye Kamari na kunufaisha wachache, ikiwekwa kwenye uzalishaji itabaki kwenye jamii na kunufaisha wanajamii. Jamii inapaswa sasa kufikiri zaidi kuhusu ushirika na kuunda ‘Limited Liability Corporations’ badala ya kufanya uwekezaji wa mtu mmoja mmoja. Kwa kuunganisha mitaji, tutajenga mashirika mengi makubwa yanayomilikiwa na jamii yenyewe na yanotoa huduma kwa jamii husika. Ushirika imara katika kilimo utamaliza tatizo la mafuta ya kupikia, ngano na shayiri na mbolea nchini.
Nini kifanyike?
Kwa jamii, tunapaswa kubadili mtazamo kutoka kufanya uwekezaji wa kibinafsi na kwenda kwenye Ushirika. Mara nyingi uwekezaji/biashara ya kibinafsi (sole proprietorship) ni uchuuzi (wholesale and retail) ulio kwenye hatari ya kufikia ukomo mmiliki anapofariki ama kuacha biashara. Mtu anaweza, mathalani, kuweka mtaji mkubwa kuuza nguo (kuwa mchuuzi wa bidhaa za viwanda vya nchi zingine), lakini hayuko tayari kuunganisha mtaji na wengine mia moja au elfu, kuzalisha bidhaa kama hizo hapa nchini. Jamii ikibadilika katika hili, itawesha kukusanya mitaji na kufanya uwekezaji mkubwa.
Vilevile jamii inapaswa kufikiri zaidi katika uwekezaji wenye faida kuliko anasa. Leo hii, vituo vingi vya habari (redio na televisheni) na mitandao karibu yote ya simu inaendesha michezo ya kubahatisha. Biko, moja spesho, buruza ndinga n.k. Fedha inayowekwa huku ingaliweza kuunda mitaji mikubwa ikawekezwa na kuinua jamii kiuchumi. Ongezeko la Kamari linatokana na mtazamo tulionao kama jamii. Tunapewa tunachokitaka. Tukibadilika kutoka kuwaza anasa, na kuwaza uwekezaji, tutapiga hatua.
Serikali pia, inapaswa kuhamasisha jamii kuunda ushirika na Limited Liability Corporations, kutoa ruzuku au nafuu ya kodi, kuweka mazingira bora ya uwekezaji, kuandaa sera nzuri zinazoendana na wakati ili kujenga mazingira bora ya uwekezaji nchini na kuviacha huru vyama vya ushirika. Kama jamii ikiwezeshwa kukua kiuchumi itapunguza mzigo kwa serikali na kuongeza mapato yatakayotokana na kodi na uuzwaji wa bidhaa nje ya nchi na kupungua kwa gharama zinazotumika kuagiza bidhaa tunazoweza kuzizalisha wenyewe. Jamii inayomiliki uchumi wake itaweza kutoa huduma za jamii kwa watu wake na kuboresha maisha.