Vyama vya siasa nchini, vilivyohusika katika harakati za uchaguzi mkuu 2015, vyatakiwa kurejesha ripoti ya gharama zilizotumika kuanzia kampeni hadi siku ya mwisho ya uchaguzi.
Sheria ya gharama za uchaguzi Namba 6/2010, inawataka wagombea wa vyama vyote kwa ngazi za Udiwani, Ubunge na Urais, kuwasilisha ripoti ya gharama walizotumia kwa vyama vyao ndani ya siku tisini (90) baada ya siku ya kupiga kura, hii ni bila kujali kama ameshinda au kushindwa katika nafasi aliyokuwa anawania.
Pia, kila chama cha siasa ambacho kimedhamini mgombea, kinatakiwa kuwasilisha ripoti kwa msajili iliyotoka kwa mgombea/wagombea ikiwa na marejesho sahihi katika fomu maalum ambayo inaonesha stakabadhi zote na risiti za gharama zilizotumika.
Haya yameelezwa leo na Msajili msaidizi gharama za uchaguzi na Elimu kwa umma, Bi. Piencia Kiure kwa waandishi wa habari waliofika ofisini kwake, ambapo amebainisha kuwa, vyama viwili pekee ndivyo vimerejesha ambavyo ni ACT na CCM kilichorejesha leo.
Pia, ametoa wito kwa vyama vingine kuwasilisha marejesho hayo kabla ya tarehe 25 mwezi huu, na kutahadharisha kuwa, faini itatolewa pamoja na adhabu kwa vyama vitakavyokiuka kutekeleza agizo hilo kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi inavyoeleza.
Faini hiyo ni kulipa shilingi milioni tatu (3) pamoja na kujipotezea sifa za kushiriki uchaguzi wowote ule, ikiwemo uchaguzi mkuu utakaofuata, isipokuwa tu kama chama kitawasilisha ripoti ya fedha na ukaguzi kwa namna itakayomridhisha Msajili kabla ya siku ya uteuzi itakayopangwa.