Visa na Mikasa: NIRUDISHIENI MWILI WANGU by Gilbert Evarist Mushi

gilbert35

JF-Expert Member
Nov 20, 2021
253
475
Riwaya: NIRUDISHIENI MWILI WANGU
Mwandishi: GILBERT EVARIST MUSHI
Phone: +255765824715

UTANGULIZI
Nilikuwa nikijitahidi kuchochea pedali katika baiskeli yangu ili baiskeli ikimbie zaidi ya ikimbiavyo, japokuwa ulikuwa ni mteremko mkali mbele yangu na baiskeli ilikuwa katika mwendo mkali lakini hata sikujali. Siku hiyo ya Jumatatu ilikuwa ni siku muhimu sana kuwahi sokoni ili nikafungue biashara yangu mapema sana.
Wateja wengi hupendelea kuja siku ya Ijumaa na Jumatatu kufungasha mizigo katika soko letu. Na hii ndiyo sababu ya mimi kutaka kuwahi nikafungue biashara. Soko letu ni soko kuu la Samaki wabichi kanda ya Kaskazini, kwa jumla na rejareja. Soko hili lipo mkoa wa Kilimanjaro, katika wilaya ya Hai.
Niliridhika na kasi ya baiskeli, nikaacha kupiga pedali. Na hapo nikataka kuhakikisha kama fundi wangu wa baiskeli aliyenisaidia hapo jana kukaza mskanio wa baiskeli amefanya vema. Ni kweli baiskeli haikuyumba nilipojaribu kuachia mikono yote miwili. Hapo ndipo niliponogewa na kitendo kile. Mara ghafla kutahamaki mbele yangu nikakutana na jiwe kubwa katikati ya barabara, haraka sana nikazikamata breki zote mbili za baiskeli, ya nyuma na mbele kwa pamoja. Nikakata kona kali yenye mchepuo wa njia nyembamba kushoto kwangu. Na hapo ndipo lilipotokea kosa kubwa lililonigharimu, likanipelekea mimi kuwaandikieni kisa hichi leo.

Sehemu ya 01
Kwa majina niite Kinje. Ni kijana mwenye umri wa miaka 26. Sina mtoto wala sijaoa, ila nina mpenzi. Kila siku panapopambazuka huwa najiandaa na kuanza safari nikiwa na baiskeli yangu inayonisaidia kunipeleka hadi sokoni kufanya biashara. Naishi na mama yangu na mdogo wangu wa mwisho aitwaye Happy. Mdogo wangu mwingine ni wa kike yeye ameshaolewa, huku wa kiume yeye akiwa na baba Dar es Salaam wakifanya biashara pamoja. Kiufupi sisi sote katika familia yetu ni watafutaji, wapambanaji.
Nikiwa naendesha baiskeli yangu kuwahi sokoni nililiona jiwe kubwa mbeke yangu. Kwa vile sikuwa nimeliona mapema ikanibidi nikunje kushoto kwa uharaka huku nikizikandamiza breki za matairi yote mawili ili kupunguza mwendo.
Nilipokunja kushoto, ndipo nilipokutana na bodaboda iliyokuwa ikija kwa kasi. Nikavaana nayo uso kwa uso, hii ikanipelekea kurushwa juu na kisha kutua chini. Nilianguka kibaya sana, kwani wakati naanguka ni kichwa kilitangulia. Nikiwa pale chini nilifanikiwa kumwona dereva wa pikipiki ile akikimbia baada ya kuniona nimelala pale chini. Nikajitahidi kujinyanyua, nikanyanyuka bila kuhisi maumivu yoyote yale, nikaokota begi langu la mgongoni na kulivaa, nikaitazama baiskeli yangu, ilikuwa haitamaniki, iliharibika vibaya mno. Nikaachana na baiskeli yangu na kuiokota simu yangu iliyokuwa chini, ilikuwa ni simu ndogo aina ya Vodafone. Japokuwa sikuweza kuupata mfuniko wake lakini niliridhika kuitia katika mfuko wa suruali yangu. Miguu ilikuwa peku, nikafanikiwa kukiona kiatu kimoja tu, nikakivaa hivyohivyo huku mguu mwingine nisipate kiatu chake.

"Nyumbani ni karibu" Nilijiambia. Nilihitaji kurejea nyumbani kwanza nikabadilishe mavazi kwani haya tayari yamechafuka na kuchanika pia.

"Lakini sokoni ni karibu zaidi." nilijiambia huku nikikumbuka jirani na biashara yangu kuna kijana mfanyabiashara anayeishi palepale na anaweza kunisaidia mavazi ya kujisitiri hadi jioni.
Mkuku mkuku nikakimbia kuelekea sokoni kuwahi kwani ni siku nzuri ya kuuza bidhaa zangu. Nikaviacha baiskeli, pikipiki na vingine ambavyo sikupata kuviona wakati navitafuta.
Dakika 15 mbele nilifika. Soko lilikuwa limefurika watu tayari. Wamama wengi na wanaume wachache wachache walikuwa wamebeba ndoo mikononi mwao kwa ajili ya kubebea samaki wabichi. Magari yalikuwa tisa, na yote yalikuwa na samaki wapya kabisa, manne yalikuwa na samaki kutoka bwawa la Nyumba ya Mungu na mengine kutoka Ziwa Eyasi. Hii ikanifanya nitabasamu kwani niliamini siku ya leo nitauza sana mafuta, ukwaju, magazeti na malimao.
Nikiwa naelekea mahali kilipo kibanda changu nikafungue biashara yangu nilikuwa nikipishana na watu ninaofahamiana nao na wengine sura ngeni. Japokuwa niliwasalimia lakini hawakuitikia wala kuonesha kwamba wana muda nami, wala sikujali.

"Ni ubize wa kutafuta maokoto. Kwanza ni hela, salamu baadae" nikajisemea.

"Mama B' shkamoo..." nilimsalimu jirani yangu, yeyealishaifungua biashara yake kitambo. Ni mimi tu ndio sijafungua ila wengi wao tayari. Hakuitikia salamu yangu, alionekana ni mtu mwenye majonzi sana. Kwa vile ni mmoja kati ya watu wangu wa karibu hapa sokoni sikuona tabu kumfwata.
Kwake nilijali utu kwanza halafu biashara baadae.
"Mama B' vipi kwema?" nikamsabahi baada ya kumkaribia.

"Acha tu Mama Malick, yule kijana wa watu maskini ndio kwanza alikuwa anaanza kujitafuta kupitia kabiashara kake maskini. Mungu ameamua kumchukua mapema. Ndiyo nataka nimwachie Aloyce ofisi hapa mi niende mochwari ya Mawenzi Hospital kumtazama Kinje" Mama B' alikuwa akimweleza mwanamke mmoja aliyesimama naye pembeni.
Maneno yake yalinishtua sana. Eti mimi nimechukuliwa mapema sana, na nimepelekwa mochwari. Kivipi wakati mimi nipo pembeni yake?

"Ngoja na mimi nitafute wa kumwachia mihogo yangu tuende wote. Kinje alikuwa anaongea na kila mtu vizuri sana jamani. Yaani najiuliza imekuwaje hadi agongwe na pikipiki sehemu kama ile ambayo haipitishi hata magari. Ni ajabu" Mama Malick alizungumza.
Nikamgusa mama B, akanigeukia kunitazama, lakini ni kama alikuwa anatafuta kitu kilichomgusa.

"Inamaana sionekani?" niliwaza. Ghafla simu yangu ilianza kuita, wote wakanigeukia kunitazama.

"Huu mlio wa simu ni kama ule wa simu ya Kinje jamani, itakuwa ni mpita njia anapita huko. Yaani nilijua ni Kinje simu yake inaita, kumbe hata hatunaye tena jamani"
mama B' alisema.
Niliuona upendo wa dhati machoni pake, machozi yake ya uchungu yakanifanya nisahau kama simu yangu inaita. Nami machozi yalianza kunitoka.

Simu ilishakata, ikabidi nitazame ni nani alipiga.
Mama yangu jamani, bila shaka anataka kunijulia hali kama nimefika salama sokoni.

"Haloo mama," Nikasema simuni.

"Mungu wangu! Ni Kinje jamani anaongea. Kinje upo hai? Upo hai mwanangu?" mama alikuwa anaongea kama amechanganyikiwa vile. Sauti yake ilionesha ni kama ametoka kulia sana.

"Mama mbona sikuelewi? Nimekufa kwani unavyosema nipo hai? Hebu acha kuzungumza ujinga bhana, au unataka nife?" nilihoji kwa ukali kidogo.

"Nimepewa taarifa mwanangu umepata ajali ya baiskeli baada ya pikipiki kukugonga ukafa. Hivi navyozungumza na wewe najiandaa nilikuwa najiandaa kuelekea mochwari ulipopelekwa mwili wako Kinje. Sasa nashangaa naongea na wewe ambaye nimejuzwa umefariki. Na eneo la tukio simu yako haijaonekana, bali mfuniko tu wa simu yako pamoja na kiatu kimoja ndivyo vilivyoonekana."

Maneno yake yalizidisha kasi ya mapigo ya moyo wangu. Nilihisi kuchanganyikiwa. Kiukweli baada ya ajali kutokea niliondoka huku nikiwa na simu isiyokuwa na mfuniko. Pia mguuni nilivaa kiatu kimoja ambacho ndicho nilichokiona.

"Mama" niliita

"Abee mwanangu" Mama aliitikia kwa upole.

"Ni kweli wakati nakuja sokoni nilipata ajali, lakini wala sijaumia, ila baiskeli yangu ndiyo imeharibika nikaiacha palepale na kuja sokoni. Nilichukua begi langu, na pia kiatu kimoja ninacho maana nilipotafuta kiatu cha pili nilikosa ikanibidi nikivae hikihiki niwahi sokoni. Hapa ninapozungumza nawe nipo sokoni mama, lakini pia huku nashangaa kila nikijaribu kuwaongelesha watu wala hawa..."

"Toka pepo mkubwa wewe. Wewe si Kinje. Nakuambia utashindwa tu mpumbavu wewe ushindwe pepo tokaa" mama alipiga kelele ghafla na simu ikakatwa. Ni kama hakuamini kile nilichokuwa nikimweleza.

"Nini kimenipata?" Nilijiuliza. Kwa mbali nilisikia kelele za mtu akipiga mayowe. Mara zikaongezeka kelele zile.

"Ngoja nielekee kule, labda nitapata kujua kitu." Niliwaza.
Mkuku mkuu nikawahi huko kelele zinapotokea. Ni upande wa pili wa sokoni, barabara ambayo inapitisha wanaoingia na kutoka sokoni.
Ni Bite jamani analia, yeye na marafiki zake. Bite yeye amalala chini analia huku akiliita jina langu. Kiufupi Bite ni mpenzi wangu. Ni mwanamke ambaye mimi na yeye tunatarajia kuoana.

"Bite mpenzi wangu. Unalia nini mama?" nilimsogelea pale chini na kumuuliza. Ghafla aliacha kupiga kelele, akaanza kuniita huku akipepesa macho kila kona.

"Kinje... Kinje upo wapi? Nimekusikia ukiniita Kinje jamani." alinyanyuka na kuanza kuita. Kila mtu alikuwa akimtazama.

"Huyu ameshachizika. Mshikeni asije akaleta maafa. Iweje amskie marehemu ambaye yupo mochwari tayari? Uchizi huo jamani." Mama mmoja alisema..

"Lakini wapendanao huwa na hisia. Yamkini nafsi ya Kinje inajaribu kumuaga mpenzi wake na sisi tunachukulia kama ni kichaa kimempanda bite." Mzee mmoja wa makamo alichangia.

"Hizo ni dhana tu. Tusiamini vitu kama hivyo. Oneni anachofanya jamani huyu binti. Jamani mshikeni huyooo..." mama yule alisema. Nikamwona Bite akishikwa na vijana wenye nguvu kwani alishaanza kufanya fujo. Wakamfunga na kitenge mikononi na miguuni ili asiweze kufurukuta.
Mara simu yangu ikaita tena. Awamu hii ni Baba yangu mzazi anapiga. Nikasogea pembeni niweze kupokea.

"Haloo baba, shkamoo". Nilisalimu.

"Marahaba mwanangu, hujambo? Nilijua tu hii taarifa ni ya kipuuzi nimepewa. Wewe ni jembe langu huwezi kuniacha kirahisi hivi. Ishi sana mwanangu maisha marefu. Nimeambiwa umepata ajali ya baiskeli umefariki eti." Baba alisema nami. Yeye yupo jijini Dar es Salaam katika biashara zake. Maneno yake yalinipa nguvu kiasi, lakini pia yakaniachia maswali mengi mazito. Wakati huo Bite alikuwa akipakizwa kwenye gari kupelekwa hospitalini kwani alionekana kupoteza fahamu.

Usikose sehemu ijayo hapahapa. Hii ni sehemu ya kwanza. Hii ni kalamu ya Gilbert Evarist Mushi iitwayo NIRUDISHIENI MWILI WANGU.
WhatsApp 0765824715
ITAENDELEA
CapaEbook_a5f7fb20-8777-44e0-a2d2-01c2367cca4d.jpg
 
Riwaya: NIRUDISHIENI MWILI WANGU
Imeandikwa na GILBERT EVARIST MUSHI
Phone: +255765824715

Tulipoishia...
"Marahaba mwanangu, hujambo? Nilijua tu hii taarifa ni ya kipuuzi nimepewa. Wewe ni jembe langu huwezi kuniacha kirahisi hivi. Ishi sana mwanangu maisha marefu. Nimeambiwa umepata ajali ya baiskeli umefariki eti." Baba alisema nami. Yeye yupo jijini Dar es Salaam katika biashara zake. Maneno yake yalinipa nguvu kiasi, lakini pia yakaniachia maswali mengi mazito. Wakati huo Bite alikuwa akipakizwa kwenye gari kupelekwa hospitalini kwani alionekana kupoteza fahamu.

Sehemu ya 02
Kwa ninayoyaona na yanayozidi kuendelea ukijumlisha na mazingira tata kunihusu, nilimwonea baba yangu huruma. Machozi yalikuwa yakinichuruzika kwa wingi, mashavu yangu yalikuwa yakiwaka kutokana na kulowanishwa machozi.

"Baba kuna kitu sikielewi mimi. Ni kweli nilipata ajali wakati nakuja sokoni, lakini hata huku sokoni kila mtu ana taarifa kuwa mimi nimefariki na nipo mochwari. Hata mama nimempigia analia tu na hajaamini kama ni mimi. Anadai mimi ni pepo nimetumwa. Ni kitu gani kimenipata baba? Mbona nikiongea na watu hata hawanitazami wala kunijibu? Ni kama vile hawanioni baba" Nilieleza kwa huruma. Mpenzi wangu ndiye huyo amepelekwa hospitali, mama yangu ndiye huyo anaimboleza juu ya kifo changu. Baba naye ndio huyo taarifa za kifo changu zimemfikia lakini baada ya kunisikia simuni ameanza kuwa na matumaini.

"Kwakweli hapo kuna kitu hakipo sawa. Nimezungumza na ba mdogo wako yule wa kule Bonite amesema ni kweli mwili wako umehifadhiwa katika hospitali ya mawenzi kwani ilimbidi aende kuhakikisha kwa macho. Basi kuna mchezo umefanyika kuhusiana na mwili wako. Hivi si majuzi tu uliniambia umekuta damu mbichi zimenyunyuzwa eneo la biashara yako?"
Maneno yake baba yaliifungua akili yangu. Nikakumbuka siku nne zilizopita.
Siku hiyo kama kawaida yangu niliwahi sana sokoni, nikausogelea mlango wa banda langu niweze kufungua. Lakini wakati nautekenya ufunguo kwenye kofuli nilihisi mshiko usio wa kawaida katika mikono yangu. Kumbe katika kofuli lile kulikuwa na damu. Hii ikanifanya mwili wangu kusisimka sana. Nilipojaribu kuangaza kwa tochi nikapata kuona michirizi mingi ya damu pande zote kulizunguka banda langu. Mbele kabisa wasimamapo wateja kulikuwa na alama ya msalaba iliyochorwa kwa damu huku katikati ya msalaba huo kukiwa na herufi 'K' iliyochorwa pia kwa damu. Nadhani herufi hiyo ilimaanisha Kinje ambalo ni jina langu. Nakumbuka siku hiyo nilimwelezea mama B' ambaye ni jirani yangu ambaye kibanda chake kipo upande wa nyuma wa kibanda changu. Upande wa juu na wa chini ni vibanda vya wadada wawili ambao hatuna maelewano mazuri kutokana na sababu fulani ambazo naweza kuziita ni sababu za kijinga.
Baada ya kumweleza mama B' siku hiyo akanielekeza nikojoe mkojo kisha niuchanganye na chumvi ya mawe na magadi soda kisha ninyunyuze sehemu zote zenye michirizi ya damu. Nakumbuka nilifanya hivyo na baada ya kufanya hivyo damu ilichemka kiasi cha kutoa moshi. Niliyafanya hayo kwa usiri mkubwa ili majirani wale wawili wenye chuki nami wasiweze kuona. Nakumbuka siku hiyo ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuuza sana. Siku hiyo nilipata fedha nyingi mno kwani kila mteja anayepita alikuja kwangu. Wateja wakawa wanasongamana kweli lakini nikawa najitahidi kuwamudu niwahudumie wote. Majirani zangu walikuwa wananitazama kwa macho mabaya sana, nikawa nawajibu tu kwa kutabasamu. Ndivyo navyopenda. Kutabasamu kwa kila mtu. Hata wateja wao siku hiyo walikuwa ni wateja wangu. Kiufupi mauzo yao siku hiyo yalikuwa ni sifuri.

"Unaona sasa? Ile dawa inafanya kazi. Ni wao wamefanya hivyo. Tena wameshirikiana. Utaona leo wanafunga mapema kutokana na aibu kuwashika"
Mama B' aliniambia hivyo. Na kweli siku hiyo hawakukaa sokoni hadi jioni kama ilivyo desturi yao. Ilipofika saa saba mchana walifunga na kuondoka zao.
Kuachilia hilo nikakumbuka pia kuna siku nilikuwa napima mafuta ya kupikia ghafla utumbo wa kuku ukiwa na damu mbichi ulitua pembeni ya ndoo. Haraka nikatoka nje kutazama mrushaji ni nani lakini kila mtu alikuwa bize. Nilipojaribu kumuuliza jirani wa upande wa chini alijibu labda ni kunguru amepita akaangusha bahati mbaya. Jibu lake lilinichekesha maana juu ya kibanda changu kuna paa lenye bati, hivyo kama kunguru angeangusha utumbo huo ungedondokea batini na si kunifwata hadi kibandani. Hilo pia nililipotezea hata sikumwambia mama yangu.
Nilikumbuka yote haya na mengine mengi wakati simu yangu ipo hewani nikizungumza na baba yangu.

"Ni kweli baba. Sasa tunafanyaje?" Nilihoji

"Ngoja nifanye maandalizi ya kuja Moshi, nitamwachia mdogo wako biashara huku azisimamie. Ni lazima nihakikishe mwili wako unarudi, kuna mahali upo kwa sababu. Hiyo ni nafsi tu inatangatanga mwanangu. Tutajuzana kila hatua" Baba aliniambia.
Nikaagana nae.

Gari moja aina ya toyota ilikuwa imemaliza samaki. Gari hii ilikuwa imepakiza watu sita na safari ilikuwa ni kwenda hospitali ya Mawenzi kuutazama mwili wangu. Sikukubali kupitwa. Haraka nikaelekea kibandani kwangu na kufungua mlango kisha nikalivua begi langu na kulitundika juu. Kwa nje nilisikia wateja wangu wakilalamika kunikosa kwani walishazoea kununua vitu kwangu. Sikujali sana, nilifunga mlango kwani funguo sikupata shida kuiona kwakuwa ilikuwa ndani ya begi langu. Nikautia katika mfuko wa suruali niliyoivaa baada ya kuacha begi ndani.

"Jamani oneni tena maajabu. Mlango unajifunga sasa wenyewe. Hapa si bure kuna kitu" Nilisikia mtu akisema, sikujali, akili yangu ilikuwa inawaza kuwahi ile gari nami niongozane nao hadi mochwari.

Bila kujua kama nimepanda na kuchangamana nao ndani ya gari, tulifika salama hospitali ya Mawenzi. Nikawafwata nyuma hadi tulipofika sehemu ya kuhifadhia maiti. Watu walikuwa ni wengi sana waliofika. Wengi niliwajua, wengine sikuwahi kuwaona hapo kabla.
Mama yangu na mdogo wangu wa kike nao walishafika muda, walikuwa wanalia sana huku wakinilaumu kwanini nimewaacha. Punde tukaitwa tuweze kwenda kuutazama mwili wangu.
Tukaingia ndani, lakini nyuma yangu kuna mama mmoja alikuwa ananitazama kwa macho makali sana, alikuwa amevakia gauni jeusi na baibui jeusi. Nyusi zake zilikuwa nyeusi sana na zimekolezwa na wanja mweusi. Mama huyu bila shaka alikuwa ananiona, nikashangaa sana amewezaje kuniona wakati sionekani tangu nipate ile ajali.
Ajabu nilipomgusa nilisisimka sana mwili kama vile nimegusa kitu chenye umeme kikanipa shoti. Kitendo kile kikamfanya mama huyo afure kwa hasira nyingi mno huku akinitazama. Sikutilia maanani sana lile, akili yangu ilikuwa inawaza kuuona mwili wangu.

Jokofu lilifunguliwa na mhudumu wa mochwari.
Mwili wangu ukiwa umetulia tuli umelala ndani ya jokofu ukiwa hauna nguo tena wala hauwezi kufanya kitu. Nililia sana, taratibu nikaanza kuusogelea mwili ule, na kadiri nisogeavyo ni kama akili yangu ilikuwa inapotea huku hisia za msukumo zikizidi kunishika. Zikabaki hatua kama nne hivi niweze kuusogelea mwili kwa karibu. Nikageuka nyuma kutazama waombolezaji. Wote hawakuwa na nyuso za furaha, wote hawakuwa na habari nami kwani hawakuwa wakiniona. Isipokuwa mtu mmoja tuu...
Yule mama mweusi mwenye mavazi meusi.
Alipiga hatua kunifwata kwa jazba kubwa sana. Ni kama alidhamiria kunipiga ama kunishika. Haraka nikazidisha kasi kuusogelea mwili wangu ulio ndani ya jokofu, nilipoufikia nikanyoosha mkono wangu wa kuume niweze kuushika nihakikishe ule ni mwili wangu.

"Achaaaaaaaaaaaaaaaaaa"
Mama yule alilua kwa sauti kubwa iliyopelekea jumba lile la kuhifadhia maiti liweze kutikisika.

Kabla sijaugusa mwili wangu nikapigwa kibao cha mkono kisha mwili ule ukarudishwa ndani. Aliyefanya hivyo alikuwa ni yule mhudumu wa mochwari.
Wakati huo Mama mwenye mavazi meusi alinifikia na kugusa paji langu la uso, nikajihisi kuvutiwa mahali kwa nguvu.

Pakawa kimya.

***
Hewa ilikuwa ni nzito sana ndani ya chumba. Chumba hakikuwa na dirisha wala mlango. Hakikuwa na kiti wala meza. Kilikuwa na umbo la duara, kuta zake zilikuwa za plastiki ngumu. Lakini mbali na hewa kuwa nzito sikupata shida kwani nilikuwa siwezi kupumua. Kuvuta pumzi na kutoa ilikuwa ni ngumu kwangu. Ni kama pua zangu zilikuwa zimeziba na koo langu la hewa pia.

"Lakini mbona nahisi harufu ya soda aina ya Fanta pashen" nilijiuliza. Harufu nahisi vizuri tu lakini kuvuta pumzi siwezi na wala sipati shida yoyote. Nilijikuta nalia kama mtoto. Kitendo cha kutokuweza kuvuta pumzi kilinikosesha matumaini ya kuishi tena.
Nikakata tamaa, nikajilaza chini sakafuni nikisubiri hatima ya mambo yote.

Nilikuja kushtuka giza limetanda ndani ya chumba. Kama kawaida bado sikuwa naweza kupumua. Taratibu nikaanza kuzoea. Nikakumbuka kuitoa simu yangu mfukoni. Nilikuta orodha ya simu ishirini zimenipigia.

"Mmmmh" niliguna huku nazitazama kwenye orodha. Baba yangu alinipigia mara kumi na nne. Mara sita zilipigwa na watu wengine tofauti tofauti. Haraka nikabofya kitufe cha kupiga niweze kumpata baba yangu.

"Namba unayoipigia inatumika kwa sasa, tafadhali subiri au jaribu baadae" Muhudumu wa kike kutoka mtandao husika alitoa maelekezo. Nikaamua kusubiri mpaka pale baba atakapomaliza kuongea na simu nyingine.

"Achaa ni languu, ni languu"

"Mimi ni wa kwanza kuliona samweli. Ni languu"
Nilisikia kwa mbali sauti za watoto zikigombea kitu fulani. Ghafla chumbani nilipokuwepo kukatokea mtikisiko. Nikawa najigonga na kurushwa, mara nibiringike yaani tabu tupu. Lakini sikuhisi maumivu hata kidogo.

"Haloo Kinje, upo wapi mbona nasikia kelele kelele?" Simu yangu iliongamishwa na baba, nikamsikia huku nikizidi kujigonga. Ni kama kile chumba kilikuwa kikigeuzwa juu chini.

"Hata haufunguki, basi tufanye uwe mpira bwana. Mi naanza kupiga....., mimiii....." mmoja kati ya watoto wale nilimsikia kwa mbali.
Ghafla nikaanza kudunda kama mpira ndani ya kile chumba. Nyumba yote ilikuwa ni kama inabomolewa ama kugeuzwa juu chini.

"Naam baba, sijui nimefungiwa wapi nasikia tu makelele huko nje" Nilijaribu kusema.
Kumbe simu yangu ilishazima muda. Ni kutokana na zile purukushani za ndani ya chumba.
Betri la simu lilikuwa limetoka kabisa, ni kutokana na simu kutokuwa na mfuniko kwani ulibaki pale nilipopatia ajali.
Chumba kilikuwa kunachezacheza, hakikuwa kinageukageuka tena kama awali, awamu hii kilikuwa kinachezacheza kama vile kinanyanyuka juu na kushuka chini. Hali hii ikaendelea bila kukoma. Wakati huo zile kelele za watoto hazikuwa zikisikika tena.
Nikachukua betri la simu lililokuwa pembeni na kurudishia kwenye simu, nimaiwasha simu ikawaka.

"No Sim Card"
maandishi haya yalisomeka baada ya kujaribu kumpigia baba yangu.
Nikalitoa betri kwa hasira baada ya kuhisi laini ya simu ilikaa vibaya kiasi kwamba ikashindwa kusoma kwenye simu.
Cha ajabu laini haikuwepo, hata nilipojaribu kuangaza mle chumbani hakukuwa na laini ya simu. Chumba kilikuwa hakina kitu chochote kile zaidi ya mimi niliyevaa kiatu mguu mmoja.
Nikajilaza kwenye kuta ya chumba.
Hakika nilichoka.

ITAENDELEA
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom