Februari 10 hadi 11, Mkutano wa Kilele wa Hatua za Akili Bandia (AI) ulifanyika mjini Paris, Ufaransa, huku program ya akili bandia ya China DeepSeek toleo la bure inayovutia macho ya dunia nzima ikipelekea nchi mbalimbali kutambua tena uwezo wa uvumbuzi wa China na kuitumia China kuendelea kuchukua jukumu muhimu katika usimamizi wa akili bandia duniani.
Programu ya DeepSeek toleo la bure sio tu imevunja hadhi ya ukiritimba ya nchi za kimagharibi katika sekta ya akili bandia, bali pia inaleta suluhisho la kimapinduzi kwa kupunguza pengo la kidijitali duniani. Hivi karibuni, Rais Donald Trump wa Marekani alisema, "DeepSeek ni teknolojia inayoibuka......nadhani tutafaidika wote...ni ya gharama nafuu sana." Wakati huohuo, kampuni ya OpenAI ya Marekani nayo ilitangaza kuwa itawaruhusu wateja wote kutumia bure huduma yake ya akili bandia, inayojulikana kama ChatGPT. Mabadiliko haya, uwe kwa mtazamo au hatua halisi yanaonyesha kuwa mapinduzi makubwa ya akili bandia yanaletwa na DeepSeek ambayo inachochea demokrasia katika teknolojia ya akili bandia duniani, na kupunguza vizingiti kwa nchi na kampuni mbalimbali kutumia teknolojia hiyo, vilevile kusaidia kupeana maarifa. Hasa katika msukumo wa mkakati wa "Akili Bandia+" ambao unasisitiza matumizi ya teknolojia ya akili bandia katika sekta mbalimbali, kuna ukuaji wa uchumi unaotarajiwa kupatikana katika maeneo mapya.
Hivi sasa, Afrika inatafuta maendeleo katika tasnia ya akili bandia, na DeepSeek toleo la bure itawezesha nchi na kampuni za Afrika kupata teknolojia ya akili bandia na uwezo wa kutumia kwa gharama nafuu, na kuchangia mabadiliko ya kidijitali barani Afrika. Katika sekta ya afya, DeepSeek itasaidia kushughulikia tatizo la uhaba wa rasilimali za matibabu barani Afrika, na kutoa huduma za ushauri wa kiafya kwa watu waishio katika maeneo ya pembezoni. Hasa katika udhibiti wa magonjwa ya kuambukizwa, DeepSeek inaweza kuchambua kwa haraka data za milipuko, na kutoa msaada kwa watu wanaofanya maamuzi, jambo ambalo ni muhimu kwa nchi za Afrika.
Katika sekta ya kilimo, DeepSeek itasaidia kuchambua data za hali ya hewa na taarifa za udongo, ili kuwapa wakulima ushauri wa kilimo bora, na kuongeza tija ya uzalishaji. Aidha, mfumo wa viwango vya bei za mazao unaotumia akili bandia utaweza kuwasaidia wakulima kufahamu vizuri mwelekeo wa soko, na kuongeza mapato yao. Katika sekta ya elimu, DeepSeek inaweza kushughulikia tatizo la upungufu wa walimu, na pia kutoa vifaa vya kufundishia kwa mujibu wa tamaduni za kiafrika. Na katika uchumi wa kidigitali, DeepSeek pia itatoa fursa kwa nchi za Afrika na kukuza sekta mpya kama vile fedha za kidijitali, biashara ya mtandaoni, na kutengeneza fursa mpya za ajira…
Hali halisi ni kwamba uzinduzi wa DeepSeek toleo la bure unaendana na wazo la "Njia ya Hariri ya Kidigitali" lililotolewa na serikali ya China. Kama mpango wa ushirikiano wa kidijitali unaoendeshwa chini ya pendekezo la "Ukanda Mmoja, Njia Moja", "Njia ya Hariri ya Kidigitali" inazingatia kanuni ya kufaidika pamoja, na DeepSeek toleo la bure ndio mfano hai wa jinsi China inavyohimiza maendeleo jumuishi ya teknolojia na manufaa ya digitali kwa wote.
Katika enzi hii ambapo akili bandia inabadilisha muundo wa dunia, mafanikio ya DeepSeek duniani sio tu ni mafanikio ya China katika sekta ya uvumbuzi, bali pia yameonyesha mabadiliko katika mfumo wa usimamizi wa teknolojia duniani. Inadhihirisha kuwa, ni kwa kushikilia kanuni za uwazi na uvumbuzi, ushirikiano wa kunufaishana, maendeleo ya teknolojia ya akili bandia yanaweza kupatikana kihalisia, na kunufaisha binadamu wote. Huu sio tu ni mwelekeo usiozuiliwa wa maendeleo ya teknolojia, bali pia ni maana halisi ya kujenga jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja.