Utekaji: naiweka kama nilivyoipata toka gazeti la jumatano la mwanchi

Father of All

JF-Expert Member
Feb 26, 2012
6,922
7,871
Tutateka, kutekwa, na kutekana hadi lini
Na Nkwazi Mhango Fyatu Mfyatuzi
Japo kadhi hii inaonekana kuzoeleka kama siyo kukubalika, fyatu sikubaliani na jinai hii. Siku hizi, katika kaya yetu, utekaji umegeuka dili. Unaweza kutekwa, kuteka, hata kujiteka. Hamkusikia ndata wakisema kuwa kuna mafyatu walijiteka wakadai walitekwa? Msinikumbushe kisa cha fyatu aliyelala kwa mchepuko akarejea home akamwambia bi mkubwa kuwa alikuwa amemezwa na fish. Tuache utani. Kaya yetu sasa ina sifa mbaya ya utekaji, upotezaji, na unyotoaji roho. Je tatizo ni nini na nani tumwajibishe? Je tujiwajibishe wote kama kaya kwa vile tumeshindwa kweli au tumeamua kushindwa?

Kwanza, hii kadhia na jinai ya utekaji inaharibu jina zuri la kaya yetu na kuifanya demokrasia kuonekana kuwa ghasia na mtego tulioingizwa bila kujiandaa ili tufyatuane na kuangamizana. Je nani ana au wanafaidika ana utekaji huu? Kweli, kama kaya, tumetekwa hivi? Siachi kushangaa na kujiuliza. Inakuwaje kaya yenye kila zana za udukuzi, ushushu, na undavandava inashindwa na genge dogo la wahalifu kama kweli ni wahalifu wanaoshindikana na kuifanya sirkal ionekane cha mtoto? Kweli wameshindikana au tumeshindwa sie katika ujumla wetu? Niliwahi kushauri tubinafsishe geshi la polishi ili tuwalete akina Rambo watulinde kama tumeshindwa kuwalinda. Wapo walioniona chizi wasijue najua mengi na naona mbali. Sasa si imeshakuwa mafyatu wanatekwa, wanateka, kutekana, na kuteketezana.

Pili, hivi kweli watekaji wasiojulikana hawajulikani au wanajulikana sema hatutaki wajulikane kwa vile wakijulikana kila kitu kitajulikana? Kwanini hawajulikani? Ina maana hata nao hawajijui ili wasijulikane? Je wana mbinu kali za kimandoo kuliko ndata? Kunani hapa mbona kila kitu hakijulikani hata kama kinajulikana? Kama tunashindwa na genge dogo la wahalifu, tukivamia na kaya adui tutafua dafu au kufuliwa kinomi?

Tatu, tunapaswa kuuliza na kujibu kwa usahihi. Kwanini wanatekaji wanateka watekwaji wa aina fulani? Je hii kiakili na kiusalama inashiria nini? Nani anawawezesha hawa wahalifu na ili iweje au apate faida gani? Kwanini mauaji ya kikatili na kishenzi ya mwendazake Ali Kibao hayakutumbua macho tukafyatuka na kufyatua hawa mafyatu wasiendelee kutisha kaya na kuwafyatua mafyatu wetu ambao huwa tunaaminisha kuwa kaya yetu ni kisiwa cha amani? Iko wapi hii amani katika utekaji?

Nasikia wanaendesha ndinga nzito hasa mashangingi meupe. Je wanapata wapi njuluku ya kutanua hivi? Nani anawalipa huyu fidhuli tumjue na kumfyatua? Namba za mashangingi zimenukuliwa mfano kwenye kisa cha utekaji wa majuzi namba ilitajwa waziwazi kuwa ni T 249 CMV. Je tunashindwa kumjua mwenye namba hii? Kama ni namba feki, je zipo kama hizi ngapi kayani, kwanini, toka lini, na zishasababisha madhara kiasi gani kwa mafyatu? Je wanawapitaje matrafiki wetu mabingwa wa kugundua hata michubuko kwenye ndinga hata mkokoteni? Je mamlaka ya usajili magari inashindwa kujua wenye namba hizi?

Je tumeishiwa kiasi hiki kiasi cha kutumia jinai kama njia ya kuendesha mashindano yetu ya kiulaji? Inawezekanaje mafyatu wachache na wakumbaff, watembeze undavandava mchana kweupe kana kwamba kaya haina geshi au geshi la polishi. Kama ndata wameshindwa, tuamuru mageshi yetu yaliyomchakaza na kumfyatua nduli yawachakaze na kuwafyatua wanahizaya hawa.
Nne, nitoe angalizo. Baada ya kadhia hii kuzidi, mbeba maono alitoa faraja akiwasihi mafyatu wasihangaike wala kugwaya. Kwani, kunyotolewa kwa mafyatu wawili wa tatu ni jambo la kawaida hata majuu kwa akina Joji Kichaka ambao aliwakaripia akitaka waache ngebe kana kwamba wao ni wasafi. Hivyo, tunapojadili inshu hii, tuepuke lawama na mihemko. Tutulie na kutuliza akili na kulisaka jawabu mujarabu kiutu uzima au siyo?

Kwa vile tuliambwa kuwa wahusika walikuwa wakijichunguza ili kuwabaini wasiojulikana wanaojulikana ili wajulikane na kuwashikisha adabu,tuepuke lawama, haraka, na mihemko. Ngojeni ‘uchunguzi’ ukamilike halafu mzoze. Kama mnadhani hawawezi kujichunguza, basi wachunguzeni nyinyi wenyewe. Kuna mafyatu wakisema eti iletwe Scotland Yard! Loh! Huu siyo ukoloni jamani? Mnataka watasha waje wavue mafyatu tena wanene nguo kama walivyomfanyia mzee Moyi kule Kenya? Mmenoa tena sana tu. Haji Scotland Yard, Scotland Parking Lot wala Scotland Driveway. Thubutu! Sisi ni kaya huru yenye uhuru hata wa kutekana na kutojulikana. Kwani hamjui? kwani hamjui kuwa si kazi nyepesi kuwasaka wasiojulikana? Wangejulikana wangefyatuliwa hata wao kutekwa hata kupotezwa kama wanaoteka na kuwafyatua. Hakuna kazi ngumu kama kushughulika na vitu visivyojulikana.

Kwa wasiojua mambo ya usalama, kitu chochote kinachohatarisha usalama hutegemea kinahatarisha maisha au usalama wa nani. Mfano, kama mwizi akiiba kuku, si jambo la kuhangaisha kaya kwa vile wote siyo wafuga kuku. Ikiibiwa silaha kituo cha polisi, hapa lazima tuchacharike kumsaka mwizi na kumtia adabu ili asiitumie kututia adabu. Kadhalika, wakiuawa makapuku, si jambo la kutukosesha usingizi kwa vile hawaendeshi kaya. Tumalizie. Je tumegeuka kaya ya kuteka, kutekwa, na kutekana? Tutateka, kutekwa na kutekana hadi lini na iwe nini?
 
Mkuu, kwa kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejaa watu mafyatu, basi kadhia hii tutegemee kuzidi kushika kasi katika siku za mbeleni.
 
Back
Top Bottom