Utafiti kuhusu Wananchi na Haki ya Kupata Habari

Sauti za Wananchi

Senior Member
Sep 2, 2014
113
138

1. Utangulizi


“Taarifa ni moja kati ya njia muhimu zinazomuwezesha mwananchi kushiriki katika uongozi wa jamii yake.” - Justice A. P. Shah, former Chief Justice, Delhi and Madras High Courts, 2010.

Katika mfumo tulionao wa kidemokrasia, wananchi wanapata ari zaidi ya kushiriki katika masuala yanayohusu uongozi iwapo watapata taarifa kwa urahisi na kwa wakati. Hii huwawezesha kuelewa vyema majukumu ya taasisi za umma pamoja na kuelewa maamuzi yanayofanywa kwa niaba yao. Upatikanaji wa taarifa sahihi pia husaidia katika maamuzi sahihi ya uchaguzi wa mwakilishi wao, na katika kuiwajibisha serikali kupitia sera na utendaji wake

Serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa kuziweka wazi taarifa za umma. Ndiyo maana serikali huwasilisha taarifa za fedha na bajeti yake bungeni ili ziweze kujadiliwa na wabunge wanaowakilisha wananchi. Serikali ilikuwa ikirusha vikao hivi moja kwa moja kupitia runinga na redio, zikiwemo ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Vilevile Tanzania ni mwanachama wa Mpango wa Uendeshaji Shughuli za Serikali kwa Uwazi (OGP), ambayo ni mfumo wa kimataifa unaolenga kuhimiza ushiriki wa wananchi kuongeza upatikanaji wa taarifa za shughuli zinazofanywa na serikali, na kwa kuzingatia viwango vya juu vya taaluma.

Hata hivyo, matukio ya hivi karibuni yameonyesha kufifia kwa ari ya wananchi kutaka kupata taarifa. Mwanzoni mwa mwaka 2015, miswada minne iliyofikishwa bungeni (huku miwili ikipitishwa na kuwa sheria) ilitia shaka kuhusu msimamo wa awali wa serikali wa kujikita kwenye uwazi. Miswada hiyo inaonekana kwenda kinyume na haki ya uhuru wa mawazo kama ilivyoelezwa kwenye ibara ya 18 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sheria ya Takwimu (Statistics Act), kwa mfano, imeweka vizuizi vingi katika kuchapisha au kusambaza taarifa za kitakwimu. Sheria ya Makosa ya Mtandao (Cybercrimes Act) inawapa mamlaka makubwa askari polisi kutaifisha, pasipo kibali cha mahakama, takwimu ama kifaa chochote kinachoonekana kuwa na umuhimu kwenye upelelezi wa makosa ya jinai.

Vilevile sheria hiyo imeanisha adhabu za vifungo na faini kwa makosa yaliyoorodheshwa. Kwa mfano, uchapishaji wa taarifa zenye ‘upotoshaji’ adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka mitatu na/au faini ya shilingi milioni tano. Sheria hizi zinamnyima mwananchi uhuru wa kuikosoa serikali, zinapunguza uwazi, pamoja na kuzuia mijadala inayohusu maslahi ya umma.

Je wananchi wanafikiria nini? Je wananchi wanapata wapi habari? Je ni kwa kiwango gani wanaviamini vyombo vya habari na serikali? Na je wanadhani vyombo vya habari vinapaswa kuwa na uhuru wa kiasi gani? Je ni kwa kiasi gani wanazifahamu sheria mpya ambazo zinaweza kuwazuia kupata habari ama uhuru wa kutoa mawazo yao?

Takwimu za muhtasari huu zimeandaliwa na Sauti za Wananchi iliyoko Twaweza. Sauti za Wananchi ni utafiti wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi. Takwimu hizi zina uwakilishi wa Tanzania Bara.

Maelezo zaidi ya mbinu za utafiti huu yanapatikana kupitia www.twaweza.org/sauti Takwimu zilizotumika kwenye muhtasari huu zilikusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,811 wa kundi la pili la Sauti za Wananchi. Hii ikiwa ni awamu ya saba ya kupiga simu kwa kundi hili jipya, na simu zilipigwa kati ya tarehe 10 na 25 Februari 2016.

Mambo ya msingi yaliyogunduliwa:

• Asilimia 74 ya wananchi hutembelea taasisi za umma na asilimia 14 hupiga simu wakati wa kutafuta taarifa.

• Wananchi 8 kati ya 10 hawajawahi kutembelea taasisi za umma (kama vile shule, vituo vya afya, au ofisi za mamlaka za maji) kupata taarifa.

• Asilimia 70 ya wananchi wanategemea redio kama chanzo chao kikuu cha kupata taarifa. Redio (asilimia 80) na runinga (asilimia 73) ni vyombo vinavyoaminika zaidi katika utoaji wa taarifa kwa wananchi.

• Asilimia 2 ya wananchi wanaifahamu sheria ya Makosa ya Mtandao vizuri.

• Asilimia 91 ya wananchi wanapendekeza kwamba iwapo serikali ikitaka kulifungia gazeti, basi lazima kwanza ipeleke suala hilo mahakamani.

2. Mambo sita kuhusu upatikanaji wa habari nchini Tanzania.

Jambo la 1: Asilimia 74 hupata taarifa kwa kutembelea taasisi za umma
Katika kutekeleza maazimio yake chini ya Mpango wa Uendeshaji Shughuli za Serikali kwa Uwazi (OGP), serikali ya Tanzania imeanzisha tovuti, ikiwemo ya “upimaji wa vituo vya maji” (water point mapping) na “ninawezaje” (how do I) inayotoa taarifa mbalimbali. Serikali imefanya haya ikiamini kuwa tovuti hizi zitatumika kama nyenzo muhimu za wananchi kupata habari.

Hata hivyo, wananchi walipoulizwa njia wanazotumia kupata habari kutoka taasisi zinazotoa huduma kwa umma, asilimia 74 ya wananchi walisema hutembelea taasisi hizo. Ni asilimia 1 pekee waliosema wanatumia mtandao.



Jambo la 2: Wananchi zaidi ya 8 kati ya 10 hawajawahi kuulizia taarifa kutoka taasisi za umma
Wananchi wengi hawafuatilii kuhusu huduma za umma au jinsi taasisi za umma zinavyoendeshwa. Walipoulizwa ni lini mara ya mwisho walitembelea taasisi mbalimbali kwa ajili ya kupata habari; wananchi 8 kati ya 10 walisema hawajawahi kuulizia taarifa zozote kutoka kwenye taasisi zilizotajwa.


Jambo la 3: Wananchi hawana imani na upatikanaji wa habari kutoka vituo vya afya (asilimia 35) na shule (asilimia 39)
Imani ya wananchi juu ya upatikanaji wa taarifa kutoka kwenye taasisi mbalimbali inatofautiana; kwa mfano, wana uhakika zaidi wa kupata taarifa kuhusu kumsajili mtoto aliyezaliwa (asilimia 71), au kuwasilisha malalamiko yao kwa mamlaka ya maji (asilimia 63), lakini hawana uhakika wakupata taarifa kuhusu upungufu wa dawa (asalimia 35), upatikanaji wa ruzuku katika shule za umma (asilimia 39) au hata mipango ya maendeleo na bajeti za wilaya (asilimia 42).


Jambo la 4: Vyombo vya habari vya zamani (redio asilimia 80 na runinga asilimia 73) vinaaminika zaidi kama vyanzo vya habari
Wananchi wengi hutegemea redio (asilimia 70) na kwa kiwango kidogo runinga (asilimia 21) kama vyanzo vya kupata habari. Hata hivyo, wananchi walipoulizwa ni chombo gani cha habari wanachokiamini zaidi, redio (ambayo inaaminika na asilimia 80 ya wananchi) na runinga (ambayo inaaminika na asilimia 73 ya wananchi) vilitajwa zaidi, huku magazeti yakiaminika kwa aslimia 27 tu na wananchi.

Pamoja na kwamba mitandao ya kijamii inaaminika kwa kiwango kidogo, takwimu za Sauti za Wananchi zinaonyesha kuwa asilimia 47 ya wananchi hutumia mitandao ya kijamii kwa kiwango fulani mara kwa mara.


Jambo la 5: Asilimia 2 tu ya wananchi ndio wanaoelewa vizuri Sheria ya Makosa ya Mtandao.
Sheria ya Makosa ya Mtandao (Cybercrimes Act 2015) ilipitishwa Aprili 2015 na kuanza kutumika rasmi mwezi Septemba 2015. Mashirika ya kijamii na waandishi wa habari waliona uwezekano wa sheria hii kuzuia mawazo yanayokinzana na yale ya serikali huku ikiwafanya wadau wa vyombo vya habari na wananchi kujidhibiti wenyewe. Hata hivyo ni asilimia 2 tu ya wananchi wanaoifahamu kwa kina Sheria ya Makosa ya Mtandao huku asilimia 31 wakiwa wameisikia tu. Kwa upande wa sheria ya Takwimu (Statistics Act 2015) ni asilimia 1 tu ya wananchi wanaoifahamu kwa kina.


Jambo la 6: Asilimia 91 ya wananchi wangependa serikali ipate kibali cha mahakama kabla ya kulifungia gazeti lolote lile

Wananchi wanaunga mkono uhuru wa habari. Kusisitiza hilo, asilimia 91 yao wametoa pendekezo kwamba kabla serikali haijatoa maamuzi ya kufungia gazeti lolote, basi vielelezo vya maamuzi hayo vitolewe mahakamani ili mahakama iwaruhusu. Wananchi wanadai serikali iruhusiwe kuweka vizuizi pale tu itakapoona kutolewa kwa taarifa ambazo ni muhimu kwa usalama wa taifa (asilimia 60).

Hata hivyo, asilimia 78 wanaamini uhuru wa kupata habari ungesaidia kupunguza rushwa na maovu mengine nchini. Haya ni mabadiliko madogo tu ukilinganisha na Mwaka 2015 ambapo asilimia 80 ya wananchi waliamini hivyo pia.


3. Hitimisho

Ili mfumo wa kidemokrasia ukue na kustawi, na ili wananchi waweze kushiriki vema katika mfumo wa uongozi, ni muhimu kuwa na uhuru na haki ya kupata taarifa hasa hasa juu ya mambo mbalimbali ikiwemo sera na utendaji wa serikali yao. Cha kushangaza ni kwamba wananchi wana imani zaidi na redio na runinga kama vyanzo vyao vikuu vya kujipatia habari kuliko taasisi za umma. Je serikali ielekeze zaidi rasilimali zake kwenye vyombo hivyo vya habari badala ya kuweka taarifa zake kwenye mtandao? Au pengine ihakikishe tovuti za serikali zinapatikana kwa urahisi, zikiwa na habari za kutosha na zenye kuvutia wananchi kusoma na kujua zaidi? Suala la matumizi duni ya tovuti za serikali, ilihali watu wengi wanatumia mitandao ya kijamii, linafaa kuchunguzwa zaidi.

Tukiangalia sheria zinazotawala upatikanaji wa taarifa, Sheria ya Makosa ya Mtandao (Cybercrimes Act) na Sheria ya Takwimu (Statistics Act) za mwaka 2015 zinatia hofu kwa vyombo vya habari kutokana na adhabu kali zilizowekwa iwapo sheria hizo zitakiukwa, 7pamoja na kuwapa mamlaka makubwa askari polisi. Wananchi wamesikia kuhusu Sheria ya Makosa ya Mitandao (asilimia 31) na Sheria ya Takwimu (asilimia 20), lakini ni wachache wanaojua yaliyomo ndani ya sheria hizo.

Kwa ujumla wananchi wanaamini kuwa kuna umuhimu wa kupata habari, ikiwa wananchi 8 kati ya 10 wakiamini kuwa uhuru wa kupata habari utasaidia kupunguza rushwa na vitendo vingine viovu. Mtazamo wa serikali ya awamu ya tano kuhusu haki ya wananchi ya kupata habari bado haupo wazi japokuwa suala la uwajibikaji wa wafanyakazi wa umma kwa wananchi limepewa kipaumbele.

Hata hivyo, kumekuwa na maamuzi kadhaa ambayo yanaashiria kutia dorasi uwazi wa kupata habari. Kwa mfano, kwanza, mapema mwaka huu, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo alitangaza kufulingia gazeti la Mawio huku matangazo ya moja kwa moja ya vipindi vya bunge yakiwa yamepunguzwa kutokana na sababu zilizotajwa kuwa za kifedha.

Pili, miswada ya Haki ya Kupata Habari na Huduma za Vyombo vya Habari– ambayo imekuwa ikipingwa vikali na wanaharakati na waandishi wa habari mwaka 2015 imeendelea kuwekwa kwenye ajenda za bunge bila kuwa na utaratibu unaoelekeza namna ya kujadili masuala muhimu yaliyoibuliwa. Katika harakati za kuhakikisha nchi inaongozwa vizuri na huduma bora zinapatikana kwa wananchi, serikali ya awamu ya tano itafanya vizuri iwapo itapitisha sheria ya Haki ya Kupata Habari (Access to Information).

Kama taarifa za umma zitakuwepo kwa wingi na kupatikana kwa urahisi, wananchi watakuwa na uelewa wa maamuzi yanayofanywa kwa niaba yao, wataweza kushirikiana na serikali hata pale inapotekeleza sera mpya na pia watasaidia katika kufichua vitendo viovu. Uwazi siyo hakikisho la uwajibikaji, lakini bila uwepo wake, wananchi hawataweza kuwawajibisha viongozi wao.

Haki ya kupata habari inaweza isionekane kuwa na umuhimu kwa wananchi kama chakula, kipato, elimu au huduma za afya. Pamoja na hayo, wananchi wanafahamu umuhimu wa uwazi na kwa ujumla wanaunga mkono haki ya kupata habari. Bila ushirikiano kutoka kwa wananchi wenye taarifa za kutosha, juhudi za serikali ya awamu ya tano kuleta maendeleo na mabadiliko zitakwama.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…