Uswahiba mpaka jino kwa jino

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536

Msemo huo unasadifu na hali iliyojitokeza katika siasa za Tanzania kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka jana. Baadhi ya wanasiasa waliokuwa wakionekana marafiki wa kufa na kuzikana, waligeukana na sasa wanadaiwa hawapikiki chungu kimoja.

Makovu hayo ya uchaguzi yanaelezwa na baadhi ya wasomi wa siasa kwamba hayawezi kusaidia nchi na badala yake kuwa na athari zaidi kwa walioko madarakani.

Wanasema, laiti wanasiasa hao ambao ni maadui, wangeungana tena baada ya kutoka kwenye uchaguzi, manufaa yangekuwapo kwa kuwapa changamoto walioko madarakani ili watekeleza vyema wajibu wao kwa wananchi.

Lowassa na Kikwete

Baadhi ya mifano ya wanasiasa hao ambao iko dhahiri kwa wananchi kutokana na matamshi yao wenyewe au wapambe wao, ni pamoja na aliyekuwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, dhidi ya Edward Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu kwenye awamu yake ya kwanza ya urais, kabla ya kujiuzulu mwaka 2008 na hatimaye mwaka jana kuhama CCM CCM na Chadema.

Kuzorota kwa uhusiano wa wanasiasa hawa wanaoelezwa kuwa marafiki wa miaka mingi waliopanga mengi pamoja ikiwa ni pamoja na kuwania urais wa nchi mwaka 2005 na 2015.

Hata hivyo, katika miaka ya karibuni, kulikuwapo ishara za kuzorota uhusiano baina yao, ingawa wenyewe walizikanusha taarifa hizo.

Wakati fulani Lowassa aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari akisema: "Huyu bwana mkubwa (Rais Kikwete) hatukukutana barabarani na watu hawawezi kutuvuruga barabarani."

Wakati Lowassa akianza mbio za urais ndani ya CCM, alionekana ni mtu mwenye kuzungumza kwa tahadhari ili kulinda uhusiano wake mwenyekiti wake wa chama, hali iliyobadilika kuanzia Julai 11, baada ya Kamati Kuu ya CCM kukata jina lake.

Licha ya kwamba aliendelea kuzungumza kwa tahadhari na Julai 28, alijiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kuchukua kadi ya Chadema, kwa mara ya kwanza alizungumzia sakata la zabuni ya kufua umeme ya Richmond, aliposema ilitekelezwa kwa agizo kutoka ngazi za juu (Rais Kikwete).

Hatua hiyo ilifungua ukurasa mpya wa kurushiana maneno, ikianzia kwa Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, ambaye kwa nyakati tofauti alinukuliwa na vyombo vya habari akimtaka Rais Kikwete asema Richmond ni ya nani.

Akiwa kwenye moja ya mikutano ya kampeni, mkoani Kigoma, Kikwete naye alimtaka Lissu kumtaja mwenye Richmond kwa madai kwamba anatembea naye kwenye kampeni kila siku. Hatua hiyo ilisababisha mwanasiasa huyo naye kumjibu Kikwete kwa kusema Richmond ilikuwa ya mwenyekiti huyo wa CCM.

Baada ya kauli hiyo, Kikwete alitumia mkutano wa mwisho wa kampeni wa CCM, Oktoba 24 kwa kusema Richmond ilikuwa ya Lowassa na kuwa yeye akiwa mkuu wa nchi aliruhusu mitambo hiyo kuagizwa lakini akataka sheria ya ununuzi ifuatwe, jambo ambalo Lowassa na kamati ya makatibu wakuu iliyoteuliwa na Waziri Mkuu hawakulizingatia.

Hali hiyo ilionekana kuwa mwisho mbaya wa marafiki hao wa miaka mingi walioanza pamoja mbio za kuingia Ikulu mwaka 1995 na pia walioanza utumishi wa TANU na baadaye CCM baada ya kuhitimu shahada zao chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katikati ya miaka ya 1970.

Inajulikana wazi kuwa Lowassa na Kikwete walikuwa marafiki wa siku nyingi, ndiyo maana waliunda `ushirika’ wakati wakiwania urais kupitia CCM mwaka 1995.

Watu hao walifikia hatua ya kukodi ndege moja kwa ajili ya kwenda Dodoma kuchukua fomu ya kuwania urais kupitia CCM, mwaka 1995 kwa makubaliano kuwa mmoja angekosa nafasi angemuunga mkono mwenzake.

Kipindi hicho walikuwa ndio wanasiasa maarufu vijana, walipachikwa jina la `Boys II Men’, ambalo lilikuwa kundi maarufu la muziki la Marekani miaka ya 1990.

Kundi la Boyz II Men lilikuwa linaundwa na vijana watatu, watanashati na ndio likawa chimbuko la kina Lowassa na Kikwete kupewa jina hilo akiongezwa na Rais wa zamani wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, ambaye naye alikuwa karibu na watu hao wawili.

Lowassa na Kikwete walipigana kufa na kupona kuhakikisha Karume anashinda urais wa Zanzibar mwaka 2000. Jina hili lilishika kasi na kufifia mwaka 2005, walipounda kundi la `mtandao’, ambalo lilimsaidia Kikwete kushinda urais mwaka huo.

`Mtandao’ huo uliundwa na wanachama na vigogo wa ndani ya serikali ya Rais wa awamu ya tatu ya Benjamin Mkapa na kumsaidia Kikwete kufanikisha ndoto yake ya urais.

Hata hivyo, `mtandao’ huo ulisambaratika baada ya miaka mitatu ya urais wa Kikwete, kutokana na Lowassa kujiuzulu Uwaziri Mkuu.

Nchimbi na Kikwete

Marafiki wengine walioonekana kufarakanishwa na uchaguzi huo ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dk Emanuel Nchimbi, na mwenyekiti wa chama chake, Kikwete.

Nchimbi, aliyekuwa Mbunge wa wa Songea Mjini kupitia CCM, anaelezwa kwamba alikuwa mtu wa karibu na Kikwete, kabla ya Julai 11, mwaka jana.

Usiku wa Julai 11 unaelezwa ulikuwa mwisho wa urafiki wa Dk Nchimbi na Kikwete, baada ya mwanasiasa huyo kijana, kutoka kwenye kikao cha Kamati Kuu akiwa na wenzake Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM, Sophia Simba na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa, na kuzungumza na vyombo vya habari akisema hawakubaliani na matokeo kwa sababu mwenyekiti (Kikwete), aliingia kwenye kikao na majina yake mfukoni.

Licha ya kwamba wanasiasa hawa, baada ya tukio hilo hawajaonekana kurushiana maneno, inadaiwa uhusiano wao umepungua kwa kiasi kikubwa na hata kutishia mustakabali wa kisiasa wa Nchimbi.

Ukweli ni kwamba Nchimbi ni kati ya hazina ya wanasiasa ndani ya CCM kutokana na nyadhifa nyeti alizowahi kushika. Amekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM kwa zaidi ya miaka 15 na pia kuongoza wizara nzito kwenye serikali ya Kikwete kama ile ya Mambo ya Ndani na ile ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

Wafuatialiaji wa masuala ya kisiasa walikuwa wanampa nafasi kubwa Nchimbi kuwania urais kupitia CCM na hata kumrithi Kikwete. Hiyo ni kutokana na uzoefu wake kwenye masuala ya chama na kiasi cha kuwa na uungwaji mkono mkubwa.

Hata hivyo, kuhusishwa kwake na Lowassa kunaonekana kumgharimu mwanasiasa huyo kijana, kwani bado jina lake lilikatwa alipowania kugombea nafasi ya Spika wa Bunge wa Jamhuri ya Muungano kupitia chama hicho.

Mkapa na Sumaye

Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye, aliyefanya kazi kwa miaka 10 na Rais Benjamin Mkapa, mpaka sasa ndiye anayeshika historia kwa kuwa waziri mkuu aliyeshika wadhifa huo kwa muda mrefu Zaidi tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.

Kitendo cha watu hao wawili kufanya kazi kwa miaka 10, kuanzia mwaka 1995 hadi 2005, ni ishara tosha ya kuaminiana baina yao. Katika uongozi wao, walisifika kwa kujenga uchumi imara. Lakini urafiki wao uliingia dosari Agosti 22, mwaka jana, baada ya Sumaye kujivua uanachana wa CCM na kujiunga na Ukawa.

Sumaye alinukuliwa akisema wakati huo, "kulizuia wimbi la mageuzi ninaloliona ni ngumu kweli kweli" na kuwahimiza waliobaki CCM na walio kwenye madaraka, wajiunge na upinzani ili kuharakisha mabadiliko hayo.

Kwa kile kilichotafsiriwa kuwa ni kumjibu Sumaye na wenzake waliokuwa Ukawa, Mkapa alirusha bomu wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM, Agosti 23, mwaka jana.

Mkapa alitumia mkutano huo uliofanyika jangwani, Dar es Salaam kwa kudai: “Kuna vyama vinajifanya vinataka kuleta ukombozi, ukombozi uliletwa na ASP na TANU. Hao wanaojiita vyama vya ukombozi ni wapumbavu, ni malofa.”

Matamshi hayo yalizua mjadala mzito na kuwapo kwa malalamiko kuwa alikuwa amevunja sheria za uchaguzi, ambazo zinazuia matumizi ya lugha zisizofaa wakati wa kampeni.

Dk Slaa na Mbowe

Kwa upande mwingine, Dk. Willibrod Slaa aliyefanya kazi kubwa ya kuimarisha Chadema kwa muda aliokuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, alikuwa mtu wa karibu wa mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.

Ukaribu wa watu hao wawili ulianza kulegalega miezi michache kabla ya uchaguzi. Septemba Mosi, mwaka jana, mambo yaliharibika baada ya Dk. Slaa kutangaza kuhama chama hicho huku akikituhumu kupoteza misingi yake kwa kumpokea Lowassa.

Alipinga kitendo cha Chadema kumpokea Lowassa na kukifananisha na kusaliti ajenda yao ya ufisadi. Alidai kwa kuwa Lowassa alihusishwa na kashfa ya Richmond, hivyo haikuwa sawa kumpokea.

Dk. Slaa ambaye kwa sasa anadaiwa kuishi nchini Canada, wakati wa kampeni alikuwa akiendelea kurusha tuhuma dhidi ya Chadema na wagombea wake.

Hatua hiyo ilimfanya Mbowe kumjibu Dk. Slaa kwa kusema yeye ndiye aliyemleta Lowassa Chadema lakini sasa amegeuka. Maneno hayo yaliendelea mpaka ikafika hatua ya kutoleana siri na namna alivyosaidiwa kujenga nyumba na mambo mengine.

Kafulila na Zitto

Kwa upande mwingine, uhusiano wa aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila na yule wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, unadaiwa kuzorota kutokana na Kafulila kumtuhumu Zitto kwamba alisababisha akose ubunge.

Chanzo cha ugomvi wao, kinaelezwa ni mkutano wa Ukawa uliofanyika Kigoma. Kafulila alihutubia na kudaiwa kusema Ukawa ndiyo mpango mzima na si utitiri wa vyama, huku akisema vingine vinaweza kuonekana ni vya `wakulima wa mawese’.

Inadaiwa kuwa, viongozi wa ACT Wazalendo walitumia kauli hiyo dhidi ya Kafulila na upinzani huo unadaiwa kuchangia Kafulila kupoteza jimbo lake.Zitto na Kafulila walikuwa marafiki wa muda mrefu tangu wakiwa Chadema.

Inaaminika kuwa Kafulila alipata misukosuko mingi alipokuwa Chadema kutokana na kuwa kundi moja na Zitto, ambaye wakati huo alikuwa mwiba ndani ya chama hicho kutokana na harakati zake za kuwania uenyekiti wa Chadema.

Kafulila alipoondoka Chadema na kujiunga na NCCR-Mageuzi bado walikuwa pamoja. Zitto alipotimuliwa Chadema na kujiunga na ACT-Wazalendo, watu wengi waliamini Kafulila angejiunga na chama hicho.

Wafuatiliaji wa mambo ya kisiasa wanaamini kuwa kitendo cha Kafulila kugoma kujiunga na ACT-Wazalendo ndicho chanzo cha kuhitilafiana.

Bashe, Lowassa na Serukamba

Waathirika wengine ni wanasiasa vijana, Hussein Bashe ambaye sasa ni Mbunge wa Nzega Mjini na yule wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba. Bashe na Serukamba walikuwa viungo muhimu kwenye mikakati ya kampeni za Lowassa kuwania urais kupitia CCM.

Bashe kuna wakati alikuwa anajitambulisha kuwa msemaji wa familia ya Lowassa na kuhusika kujibu makombora yaliyokuwa yakielekezwa kwa mwanasiasa huyo na wapinzani wake wa kisiasa, hasa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.

Wakati wa mchakato wa kutafuta kuteuliwa kugombea urais kupitia CCM, Nape alimtuhumu Lowassa kwa kuita watu nyumbani kwake ili wamshawishi. Bashe alijibu: “umefika wakati Nape atangaze hadharani mgombea urais wake, ambaye mimi Bashe namjua, badala ya kuwatisha wana-CCM wengine kwa kutumia Ukatibu Mwenezi wa chama.

“Kwa hiyo, mimi kama Bashe, ambaye ni mwana-CCM nataka tu nimhakikishie Nape na wenzake kuwa hawana hatimiliki ya CCM. Wote wana CCM tuna kadi moja ya rangi moja na tunalipia ada sawa. Hakuna mwanachama wa daraja la kwanza wala wa daraja la pili.”

Bashe alijipambanua kama `askari’ mwaminifu wa Lowassa, sawa na Serukamba ambaye kwenye Bunge lililopita alikuwa anatoa hoja nyingi zilizoonekana kumtetea Lowassa.

Baada ya Lowassa kukatwa CCM, inadaiwa waliachana na Lowassa kimyakimya. Wakati Lowassa akihamia upinzani, watu wengi waliamini Bashe na Serukamba wangehama naye lakini ikawa kinyume chake. Hivi sasa wamejitenga na kundi la Lowassa.

Namelok Sokoine na Lowassa

Namelok Sokoine ni kati ya wanasiasa waliotengana na Lowassa ambaye alikuwa mtu wake wa karibu kisiasa kutokana na siasa za uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Binti huyo wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Sokoine, alikuwa karibu na Lowassa kiasi cha kuwa na nafasi kubwa kurithi kiti cha ubunge jimbo la Monduli.

Kabla hata ya uchaguzi mkuu, Namelok alikuwa akitajwa kuwa ndiye mridhi wa Lowassa, lakini baada ya kuhama chama kwa mwanasiasa huyo kila kitu kilibadilika. Lowassa alipoihama CCM, Namelok aligoma kuhama na kujiunga na Chadema lakini aliendelea kupambana kumshawishi Namelok ahamie Chadema.

Akiwa katika moja ya mikutano ya kampeni jimbo la Monduli, Lowassa alisema: “Nimekuwa mbunge kwa miaka 20 hivyo natakiwa nimjue mbunge atakayefuata, nitakubaliana na Namelok akikataa kupanda basi hili, basi.”

Baada ya mazungumzo ya wawili hao kutofikia muafaka, Lowassa alifanya mkutano mwingine Monduli mjini na kumkana rasmi Namelock. Badala yake alitangaza kumuunga mkono Julius Kalanga kuwa mgombea ambaye hatimaye alishinda uchaguzi.

Wasomi waonya

Mhadhiri Mwandamizi wa UDSM, Dk. Donath Olomi, akitoa maoni yake kuhusu uadui na makovu yaliyoachwa na viongozi wa vyama baada ya uchaguzi, alisema mategemeo ya wananchi ni kuona watu hao wanakuwa kitu kimoja na ili kuipeleka nchi mbele.

“Kinyume na hapo uwezekano wa kupigana vita kichini chini lazima uchukue nafasi. Unakuta aliyeko madarakani anapigwa vita na wakati mwingine wanaweza kucheza na mitandao ili kumharibia aonekane hajafanya lolote,” alisema.

Alisema ni vizuri uchaguzi unapoisha wanasiasa warudi kwenye mstari mmoja kwa sababu lengo ni moja la kuitoa nchi ilipo na kuipelekea kwenye maendeleo. Alisema kuendeleza mvutano hakutaleta tija kwa taifa.

Mchambuzi wa masuala kisiasa na kijamii, Bashiru Ally, alisema uhasama wa kiasiasa haupo bali mapambano ya kimaslahi.
Alisema uhasama wa kisiasa ambao ni hatari ni ule unaohusisha wanasiasa kwa kuwatumia wananchi lakini kama ni wa watu wawili, hayo ni mambo yao binafsi.

“Lowassa asilazimishe mambo. Yeye alipambana na Kikwete ambaye sasa ni mstaafu. Kama wanaendeleza huo ni uadui nje ya siasa, lakini nani alijua kama Mbowe na Zitto wangegombana.

Tulishuhudia Dk. Shein na Maalim Seif wakikaa meza moja, wanasiasa wasiwahadae wananchi kwa sababu hakuna uadui wa kisiasa, hawa wanagombania maslahi tu,” alisema.Aidha, alisema viongozi wa siasa wa Afrika wakiwemo Tanzania ni vigeugeu.

“Mfano Lowassa alisema hatahama CCM lakini mwaka jana tulishuhudia akihamia Chadema, tatizo hawajajenga misingi na kanuni ya kusimamia vyama vyao,” alisema.

Mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu, alisema kovu kubwa lililopo sasa ni uchaguzi wa marudio wa Zanzibar na ule wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam.

“Wananchi wanachosubiri ni kuona nchi ikiwa imetulia, haya yaliyotokea kwenye uchaguzi wa marudio wa Zanzibar na ule wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam unaweza kusababisha matatizo makubwa,” alisema.

Chanzo Nipashe

Maoni yangu

Jk alikuwa sahihi kwa kuwa alikuwa Rais wa nchi, pia alishaona rafiki yake hakuwa na nia njema na watanzania maskini kwa kuutaka urais kwa gharama yeyote huku kukiwa na kundi la watu miongoni mwao walikuwa wanashutumiwa kwa ufisadi mbalimbali pamoja na matajiri ambao walikuwepo nyuma yake waliokuwa wakimchangia mapesa ili aupate urais wakati hatukujua atawalipaje hao waliokuwa wakimchangia zaidi ya kusema anauchukia umasikini.

Pia hakuweza kufanua pesa anazozoitumia kuusaka urais na kuchangisha makanisani na misikitini na sehemu mbalimbali alikuwa amezitoa wapi ikiwa ni za kwake mwenyewe.

Mungu ambariki JK kwa kutuacha katika mikono salama.
 
Nilikuwa napita tu...nikakutana na huu Uzi...Mungu mbariki jk kwa kutuacha ktk mikono salama....sijui kama jk ndivo anavoona sasa hv???hv yeye kama yeye yupo ktk mikono salama kweli???....hv ule usingizi aliosema atalala analala kweli???..sidhani...
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…