Usiruhusu Kusemwa Kwako Vibaya Kukakuzuia Kufanya Mambo Ya Msingi

Samson Ernest

JF-Expert Member
Aug 28, 2014
625
971
Zab 69:12 SUV
[12] Waketio langoni hunisema, Na nyimbo za walevi hunidhihaki.

Kusemwa kupo, tena kama ulikuwa hujui ujue Leo, na nikuambie kwamba utasemwa sana, utasemwa na marafiki zako, utasemwa na wapendwa wenzako, utasemwa na walevi, utasemwa na majirani, utasemwa na operesheni wenzako, na wale wasiokufahamu, na usiowafahamu.

Unachopaswa kujiuliza unasemwa kwa ajili ya nini, kinachosemwa ni kweli? Kama ni kweli jirekebishe haraka Sana, kama sio kweli endelea kusimama kilele ambacho Mungu amekupa.

Wakati mwingine tunajitia moyo kuwa mti wenye matunda ndio unaopigwa mawe, napenda ufahamu kwamba, mti uliobeba nyoka na upo karibu na makazi ya watu lazima urushiwe mawe ili nyoka atoke.

Hatupaswi kuogopa kusimama imara, maana mwingine unasemwa sana kutokana na kitu kikubwa ulichobeba, Shetani hataki kabisa usonge mbele.

Kuna watu kupitia kusemwa wameacha kusudi la Mungu, wameacha kufanya kile Mungu aliwaagiza wafanye, maneno mabaya waliyosemwa nayo yamewaondoa kwenye mstari sahihi.

Unaweza kudhihakiwa kutokana na hali yako ya sasa unayopitia, inaweza kuwa hali ya uchumi, huduma, kazi, biashara, familia, lakini Mungu akawa anakuandalia kesho yako njema.

Usitishwe na dhihaka za watu wasiojua kile Mungu amesema na wewe, simama na Mungu, tunza maisha yako ya wokovu, watu wasione mambo mabaya uliyoyatenda kweli, wasione dhambi mbaya kusimama iliyo mbele yako.

Kwa kuwa Shetani anajua ulichobeba kitaharibu mambo yake mengi, anaweza kutumia watu wengine kukuvuruga ili usitumie muda wako mwingi kutumikia kusudi lako, bali uhangaika na wanaokusema.

Zab 69:14 SUV
[14] Uniponye kwa kunitoa matopeni, Wala usiniache nikazama. Na niponywe nao wanaonichukia, Na katika vilindi vya maji.
Mwambie Bwana akusaidie katika hali unazokutana, akupiganie katika vita vya maneno mabaya yanayoinuka juu yako, akulinde moyo wako usije ukachoka na kuacha kutumikia kusudi la Mungu.


Mwisho, nikukaribishe kwenye chaneli ya wasap kupata maarifa mbalimbali kama haya, bonyeza link hii kujiunga=>>Samson Ernest | WhatsApp Channel

Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia yako
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
 
Back
Top Bottom