Ushiriki Huru wa Wananchi Katika Shughuli za Kisiasa Ndiyo Msingi Thabiti wa Utawala Bora

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
746
2,095
Ushiriki Huru wa Wananchi Katika Shughuli za Kisiasa na Kidemokrasia.jpg


Ushiriki wa umma katika masuala ya kisiasa na kidemokrasia hauishii kwenye kufahamu tu yanayoendelea, bali wanaoathiriwa na maamuzi wana haki ya kushirikishwa kisawasawa katika mchakato wa kufanya maamuzi hayo. Ushiriki huu ni sehemu muhimu ya utawala wa kidemokrasia.

Lengo kuu la ushirikishwaji wa umma ni kuhakikisha kuwa wananchi wanatoa michango yenye maana katika mchakato wa kufanya maamuzi ambayo wanayategemea katika maisha yao. Ushirikishwaji huu pia unatoa fursa ya mawasiliano kati ya taasisi zinazoyofanya maamuzi na umma. Watu hukubali au kuunga mkono maamuzi ambayo wanasaidia kufanya. Lakini pia, ushirikishwaji mzuri wa umma unahimiza uwajibikaji.

Unaweza kujiuliza, ushiriki katika masuala ya kidemokrasia ni nini? Upigaji kura ulio huru na wa haki ni njia mojawapo ya kushiriki katika demokrasia yetu. Haiishi tu hapo, inaweza pia kuwa ni ushiriki katika kuunga mkono au kubadilisha sheria, kutoa maoni ili kufanya mabadiliko ya masuala mbalimbali yanayowahusu wananchi n.k.

Ushiriki huu unaweza kufanyika kwa namna mbalimbali ikiwamo kidigitali na kwa mikusanyiko ya ana kwa ana, lakini pia utategemea sana mazingira mazuri katika maeneo mengine kama vile uhuru wa kujieleza, uhuru wa vyombo vya habari, haki za kibinadamu lakini pia na uraia hai (active citizenship). Uraia hai unamaanisha wananchi kujitolea kwa moyo mmoja katika masuala ya demokrasia katika ngazi zote, vijijini na mjini.

Kuna dhana mbaya ya kuziona taasisi na watu binafsi wakijihusisha kwa karibu na masuala ya kidemokrasia kama maadui wa nchi wanaotumika na “mabeberu”. Si kweli, wenye mtazamo wa “bora liende” ndiyo maadui wakubwa wa nchi. Wenye mapenzi ya dhati na nchi ni wale wanaotambua panapovuja na kutoa taarifa kuepusha madhara makubwa.

Demokrasia duniani yadorora

Kwa sasa ni dhahiri kuwa matumizi ya “mabavu” yanazidi kuimarika katika serikali zisizo za kidemokrasia. Ripoti ya International Institute for Democracy and Electoral Assistance (IDEA), shirika la kiserikali linaloundwa na zaidi ya nchi wanachama 30 zinazofanya kazi kutetea demokrasia duniani kote, imeutaja mwaka 2020 kuwa mbaya zaidi katika rekodi, kwa upande wa idadi ya nchi zilizoathiriwa na kuongezeka tawala zisizo za kidemokrasia.

Ripoti hiyo inasema kuwa demokrasia duniani imedorora maradufu katika muongo mmoja uliopita. Hii inajumuisha nchi zenye demokrasia imara kama vile Marekani, lakini pia nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kama vile Hungary, Poland na Slovenia. Zaidi ya theluthi mbili ya idadi ya watu duniani sasa wanaishi katika demokrasia iliyodorora au tawala za kiimla (autocratic governments).

Idadi ya nchi zilizorudi nyuma kidemokrasia haijawahi kuwa juu kama katika muongo uliopita. Asilimia 70 ya idadi ya watu duniani sasa wanaishi katika tawala zisizo za kidemokrasia au ndani ya nchi zilizorudi nyuma kidemokrasia. Asilimia ya idadi ya watu duniani wanaoishi katika demokrasia nzuri ni asilimia 9 pekee.

Hali ilivyo Tanzania

Tanzania kama sehemu ya mikataba kadhaa ya kikanda na kimataifa, ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, ina wajibu wa kisheria kuheshimu na kulinda haki za kimsingi, hasa haki ya uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari, kukusanyika kwa amani, kuunda na kujiunga na vyama, na kushiriki katika masuala ya umma, ambayo ni haki za msingi kwa ajili ya uchaguzi huru na wa haki katika jamii ya kidemokrasia.

Kama mwanachama wa Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Tanzania imejitolea kudumisha na kukuza kanuni za kidemokrasia, ushiriki wa wananchi na utawala bora.

Hata hivyo, kwa miaka kadhaa Tanzania imetekeleza mipango ya kuwanyanyasa Watetezi wa Haki za Binadamu, kunyamazisha uandishi wa habari huru na kuzuia uhuru wa kujieleza, kukusanyika kwa amani na kujumuika ili kujiletea manufaa ya kidemokrasia.

Ingawa Watanzania wana haki ya kujiunga katika vyama vya siasa na kushiriki kwa uhuru shughuli za kisiasa, chama tawala kimelaumiwa “ku-enjoy” zaidi upendeleo wa kiutawala ambao unaokwamisha ushindani.

Upinzani wa kisiasa pia umeshambuliwa, huku kukiwa na vikwazo kama vile kupigwa marufuku kabisa kwa mikutano ya kisiasa ulioathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wa vyama pinzani kufanya kazi kwa ufanisi na kuweka ukuta dhidi ya Wananchi kushiriki katika haki yao ya msingi ili kufanya maamuzi sahihi (informed decisions).

Suala hili limezungumzwa na kujadiliwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Taasisi nyingi duniani kwa umoja wake zimewahi kuandika barua za pamoja kukemea unyang’anyaji wa Haki na uhuru wa wananchi nchini Tanzania. Moja ya barua hizo ni pamoja ambayo iliandikwa na taasisi ya Robert F. Kennedy Human Rights ambayo ilisainiwa na taasisi nyingine 66. Mfano mwingine ni hii iliyoandikwa na Frontline Defenders ambayo ilisainiwa na taasisi 64 duniani kote.

Ripoti ya taasisi ya Freedom House inayoitwa Freedom in the World imerekodi mdororo wa Uhuru wa haki za kisiasa na uhuru wa kiraia nchini Tanzania. Mdororo huo umeifanya Tanzania kuwekwa katika kundi la Huru Kiasi (partly free). Katika kuangazia hali ilivyo nchini mwaka Tanzania 2021, kwa mfano, katika suala la Haki za Kisiasa ilipata alama 12/40 huku ikipata alama 22/60 katika Uhuru wa Raia na hivyo kunyakua jumla ya alama 34/100.

Hali ya Uhuru Tanzania (4).png

Kielelezo 1: Hali ya Uhuru wa Kiraia na Kisiasa Tanzania kuanzia mwaka 2017-2021. Ripoti ya Freedom House inakadiria ufikiaji wa watu kwa haki za kisiasa na uhuru wa kiraia katika nchi 210 kupitia ripoti yake ya kila mwaka ya "Freedom in the World".

Ni vema kama taifa tukajitafakari na kuchukua hatua sahihi ambayo itakuwa na manufaa kwa kila mmoja katika ardhi hii ya Mama Tanzania.

Ushiriki wa wananchi katika michakato hii unahakikisha kwamba ni viongozi waliochaguliwa tu walio na nia ya kufanya kilicho sahihi wanaweza kuingia madarakani. Hii ina maana kwamba ni lazima watekeleze kazi zao vyema na kutimiza wajibu wao vizuri ili waweze kuchaguliwa tena.

Wahusika wa mchakato wa kusikiliza, kuhoji, kutafakari na kisha kufanya maamuzi yoyote katika nchi fulani ni wananchi wenyewe. Hawahitaji kusubiri mtu mwingine ajitokeze na kufanya mabadiliko. Ikiwa wanaamua kubadilisha kitu, wanaweza kuchukua jukumu la kujihusisha na kufanya kile kinachowapendeza. Hivyo, kila hatua ya kukuza demokrasia inategemea sana ushiriki ulio huru na wa haki wa kila mwananchi. Vikwazo vya kisheria na kimabavu havina nafasi katika ustawi wa demokrasia imara na utawala bora.
 
MISINGI YA UTAWALA BORA

Uwazi
Ushirikishwaji

Ni kuwahusisha wananchi wa jinsia zote na makundi yote katika kupanga na kufanya maamuzi ya mambo yanayowahusu. Ushirikishwaji unaweza ukawa wa moja kwa moja au kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi.
 
Back
Top Bottom