Ushindi wa chama cha Imran Khan na kufufuka matumaini yake ya kurudi tena madarakani Pakistan

kimsboy

JF-Expert Member
Oct 17, 2016
9,839
20,285
Ushindi wa chama cha Imran Khan na kufufuka matumaini yake ya kurudi tena madarakani Pakistan

Oct 20, 2022 00:44 UTC

Ushindi wa Tehreek-e-Insaf ambacho ndicho chama kikuu cha upinzani nchini Pakistan katika awamu ya pili ya uchaguzi wa kabla ya muhula wa uchaguzi mkuu umempa matumaini makubwa Imran Khan na chama chake hicho ya kurudi tena madarakani.

Takriban miezi sita iliyopita, Imran Khan aliondolewa kwenye wadhifa wa uwaziri mkuu wa Pakistan baada ya wabunge kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye. Imran Khan, ambaye anataka ufanyike uchaguzi wa mapema, bila shaka atashikilia zaidi takwa lake hilo kutokana na ushindi huo aliopata. Awamu ya pili ya uchaguzi wa katikati ya muhula kabla ya uchaguzi mkuu wa Pakistan imefanyika ili kutafuta wawakilishi wa viti 11 vya bunge la taifa na vya majimbo katika miji tofauti ikiwemo Peshawar, Karachi na Multan, ambapo wagombea wa chama cha Tehreek-e-Insaf kinachoongozwa na Imran Khan walifanikiwa kushinda viti vinane, vikiwemo sita vya bunge la taifa na kukiweka chama hicho katika nafasi ya juu zaidi kuliko muungano wa vyama viwili vya Wananchi and Muslim League Nawaz.

Vyama hivi viwili, ambavyo vinajulikana kuwa ni vyama vya jadi na vyenye ushawishi mkubwa nchini Pakistan, vilipata viti vitatu tu vya Bunge la taifa katika uchaguzi huo wa hivi majuzi, ambalo linachukuliwa kuwa ni pigo kubwa kwao. Sababu ni kuwa chama cha Wananchi na cha Muslim League Nawaz kwa pamoja viliungana kumwondoa madarakani Imran Khan kwenye wadhifa wa uwaziri mkuu na kudai pia kwamba vina uungaji mkono wa wananchi, lakini matokeo ya uchaguzi wa katikati ya muhula yamethibitisha kuwa uhalisia wa mambo unapingana na dai lao hilo.

Imran Khan (aliyekunja ngumi) akihutubia mkutano wa wafuasi wake

Abdulhayi Varshan, mtaalamu wa masuala ya kisiasa, analizungumzia hilo kama ifuatavyo:

"Chama cha Tehreek-e-Insaf kina uungaji mkono wa wananchi nchini Pakistan na kinaweza kuvishinda vyama muhimu endapo utafanyika uchaguzi huru na wa haki. Lakini hii sio hadithi yote ya yanayojiri katika uwanja wa siasa za Pakistan; kwani mchezo wa uwaniaji madaraka katika nchi hii uko tata mno."

Kutokana na mfumo wa uchaguzi wa Pakistan, uwezekano wa kufanyika udanganyifu ni mdogo sana; na ndiyo maana vyama huwa vinaingia kwenye uchaguzi kwa imani kamili; na kura vinazopata huakisi umaarufu na uungwaji mkono halisi vilionao kwa wananchi.

Lakini kuhusu yale yanayojiri katika uwanja wa ushikaji na upokezanaji wa madaraka nchini Pakistan si lazima yaendane na nafasi na ushawishi tu wa vyama bungeni, bali ni miamala inayojiri nyuma ya pazia la utwaaji madaraka, hasa na jeshi, ambalo ndilo lenye sauti ya juu kuhusu chama kitakachoshika madaraka na kuunda serikali.

Wakati wa uwaziri mkuu wa Nawaz Sharif, chama cha Muslim League-Nawaz kilinasa kweye mtego huo mara kadhaa na yeye mwenyewe akaenguliwa madarakani kwa ushirikiano wa jeshi na mahakama. Imran Khan pia alinaswa kwenye mtego huo miezi sita iliyopita na akauzuliwa wadhifa wa uwaziri mkuu. Kwa hiyo, pamoja na kwamba kufanyika maandamano ya upinzani na migomo ya kuketi kunadhihirisha nguvu za vyama vya upinzani mbele ya serikali, lakini ikiwa vyama hivyo vya siasa havitafikia maridhiano na jeshi, hata kama chama chochote kile kitafanikiwa kuunda serikali, umri wa serikali yake hautakuwa mrefu.

Kwa hiyo kwa Imran Khan, ambaye ameweza kutamba na kuwaonyesha wapinzani wake uungaji mkono wa umma alionao kwa kushinda chaguzi mbili za kabla ya muhula wa uchaguzi mkuu, kutegemea viti vya bunge tu hakutoshi kumrejesha madarakani, bali ni lazima akubali kutafuta maelewano ndani ya duru za wenye satua katika muundo wa madaraka nchini Pakistan.

Shehbaz Sharif

Abdulatif Nazari, mtaalamu wa masuala ya kisiasa amelizungumzia hilo kwa kusema:

"Jeshi la Pakistan lina sauti ya juu katika uga wa siasa za nchi hii. Kwa hivyo, chama chochote kinachotaka kuingia madarakani lazima kishirikiane na jeshi. Hivi sasa inaonekana kuwa, Imran Khan atajitosa kwenye ulingo wa siasa za Pakistan akiwa na tajiriba nzuri zaidi".

Alaa kulli hal, kwa ushindi kilichopata katika uchaguzi wa hivi majuzi, chama cha Tehreek-e-Insaf kimeonyesha ustahiki kilionao wa kurudi madarakani. Ni kwa sababu hiyo, Imran Khan, ambaye anaichukulia serikali ya Waziri Mkuu Shehbaz Sharif kuwa imetokana na mashinikizo ya nje, hayuko tayari kwa namna yoyote ile kuitambua serikali hiyo. Hata hivyo, serikali ya Shahbaz Sharif, ambayo ingali inategemea uungaji mkono wa jeshi, haijaingiwa na hofu kwa kushindwa katika uchaguzi wa karibuni wa katikati ya muhula na haijatoa kauli ya kuonyesha kuguswa na matokeo hayo.

Lakini suala muhimu pia ni kwamba Jeshi la Pakistan linavipa uzito vyama kulingana na uungwaji mkono vilionao. Hii ina maana kwamba, kuna uwezekano wa Imran Khan kuubadilisha mkondo wa siasa nchini Pakistan kwa manufaa ya chama chake cha Tehreek-e-Insaf kutokana na tajiriba ya huko nyuma na kwa namna anavyoungwa mkono na wananchi.../
 
Mbona kuna sehemu nimesoma tume ya uchaguzi ya hiyo nchi imemuengua kwenye list ya wagombea?,au mimi ndio najichanganya?,,na kama ni kweli hilo ni shinikizo la US
 
Back
Top Bottom