Usafiri wa daladala Dar waelekea ukingoni.
MABASI ya abiria yanayotoa huduma ya usafiri jijini Dar es Salaam maarufu kwa jina la daladala yatasitisha huduma hiyo kupisha mabasi ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) yanayoanza kutoa huduma hiyo rasmi leo hii.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya UDA Rapid Transit (UDART), David Mgwasa katika mahojiano kwenye kipindi cha Asubuhi Hii kinachorushwa na Redio ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ya TBC Taifa wakati akitathmini majaribio ya huduma ya usafiri wa mabasi ya BRT yaliyotolewa bure kwa wananchi juzi na jana.
Mgwasa alisema utaratibu wa kusitisha huduma za daladala umeshawekwa na tayari wahusika wa daladala wamenunua hisa BRT na wameshalipwa fidia ili kupisha mfumo huo mpya wa usafiri jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo alisema daladala hizo haziwezi kuondolewa ghafla, bali zitaondolewa taratibu kulingana na jinsi mfumo wa BRT utakavyofanya kazi kwa asilimia 100 na kutosheleza mahitaji ya huduma ya usafiri Dar es Salaam.
"Kwa misingi ya BRT daladala zote zinaondoka na utaratibu huo umeshawekwa. Utaona kuwa watu wengi wa daladala ambao walikuwa na daladala za Kimara kwenda Kivukoni wamenunua hisa kwenye mfumo wa BRT na wamelipwa fidia pia," alisema Mgwasa na kuongeza kuwa:
"Tutawaondoa taratibu kwa sababu sisi wenyewe tuko kwenye wakati mzuri wa kujifunza na wakati tunatoa amri ya kuwatoa ni lazima tuwe na uhakika kwa asilimia 100 na mfumo ambao unatosheleza mahitaji ya usafiri."
Alisema kwa sasa mabasi yaliyopo kwa ajili ya kutoa huduma hiyo yapo ya kutosha kukidhi mahitaji ya huduma hiyo kwa awamu ya kwanza na muda ukifika atazungumzia awamu ya pili ya mradi huo.
Akizungumzia changamoto zilizojitokeza wakati wa kufanya majaribio ya huduma hiyo, Mgwasa alisema wananchi wameipokea huduma hiyo vizuri sana ingawa tatizo kubwa aliloligundua ni ukosefu wa elimu juu ya huduma hiyo ya usafiri kwa wananchi.
"Changamoto ni nyingi lakini nyingi sana ni za elimu kwa kweli na lazima tuseme ukweli kuwa kitu cha msingi ambacho kimetokea ni kuwa upokeaji wa watu kwa huduma umekuwa mzuri sana," alisitiza Mgwasa.
Alisema hali ya mwitikio mkubwa inaashiria mategemeo ya wananchi katika huduma hiyo ni makubwa sana kutokana na tatizo la foleni kuwasumbua sana wananchi.
Hata hivyo, alisikitishwa na siku ya kwanza ya majaribio ambapo aligundua kuwa vibaka wengi walijigeuza kuwa viti vya mabasi hayo kwani walizunguka nayo kutoka Kimara hadi Kivukoni wakageuza nayo kutokana na kuwa yalikuwa yanatoa huduma hiyo bure.
"Changamoto kubwa ambayo ilikuja kujitokeza ni kuwa kwa sababu jana (juzi) ilikuwa ni bure vibaka wakawa wamekuwa viti vya magari wamejaa kwenye mabasi wanakwenda Kimara wanarudi Kivukoni wanakwenda Kimara wanarudi Kivukoni," alisema Mgwasa na kuongeza.
Chanzo: Gazeti la Majira