Upigaji vituo vya mabasi, Kituo cha Magufuli chawalipia wapangaji bili ya umeme na maji Tsh. Milioni 563.02

BigTall

JF-Expert Member
Mar 9, 2022
496
1,196
Upigaji.jpg

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, amebaini upigaji na madudu yanayofanywa katika vituo mbalimbali vya mabasi hapa nchini.

Kupitia Ripoti Kuu ya Ukaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 iliyotoka hivi karibuni, pia amesema kuna uendeshaji duni katika vituo hivyo.

Kituo cha Magufuli
Kwa mujibu wa Kichere, Kituo cha Mabasi cha Magufuli kilichopo Mbezi, Dar es Salaam kinachoendeshwa na Manispaa ya Ubungo kina mapato yasiyofichuliwa yaliyokusanywa katika hoteli zilizomo kituoni humo.

Wakati wa ukaguzi wake, amebaini kiasi cha Sh milioni 45.64 ambazo ni mapato kutoka huduma za hoteli katika kituo hicho kwa Desemba, mwaka juzi hadi Januari, mwaka jana yaliyokusanywa na Kampuni ya Rahabu Logistics Ltd kama wakala wa ukusanyaji, hayakuwekwa katika akaunti za benki za halmashauri kama ilivyo kwa mujibu wa Agizo la 50 (5) la Memorandamu ya Fedha za Serikali za Mitaa ya mwaka 2009.

Pia amesema aliomba ripoti za ukusanyaji mapato kwa huduma za hoteli kuanzia Februari hadi Juni, mwaka jana lakini hazikutolewa kwa ajili ya ukaguzi na hakukuwa na ushahidi wa kuthibitisha kama mapato yaliyokusanywa wakati huo yalikuwa yameingizwa katika akaunti za halmashauri.

Mbali na hayo, amesema alibaini kuanzia Februari hadi Juni, mwaka jana wakala wa ukusanyaji mapato alifanya kazi bila mkataba uliosainiwa na halmashauri unaozua wasiwasi kuhusu masharti na hali za uendeshaji wa hoteli wakati huu.

“Kushindwa kuwasilisha taarifa za ukusanyaji mapato zilizoombwa kwa madhumuni ya ukaguzi kunapunguza wigo wa ukaguzi kwa ukamilifu wa kutathmini uwazi na usimamizi wa kifedha,” amesema.

Pia amesema Kituo cha Taifa cha Takwimu za Mtandao (NIDC) kinafanya kazi bila mkataba.

“Nilibaini kwamba makubaliano ya awali kati ya halmashauri na NIDC yalikuwa kwa ajili ya kuweka mageti katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli. Halmashauri ilikuwa na jukumu la kuweka mfumo wa ukusanyaji mapato.

“Hata hivyo, kutokana na kucheleweshwa kwa utekelezaji wa mfumo mpya wa mapato wa TAUSI, halmashauri iliruhusu NIDC kukusanya mapato kwa kutumia programu yao kwa muda wakati wakisubiri mfumo mpya,” amesema.

Tangu Februari 20, mwaka jana amesema NIDC inafanya kazi na mashine za N-Card kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato katika kituo hicho bila mkataba rasmi na halmashauri.

“Baadaye, NIDC iliomba halmashauri kulipa asilimia 7.2 ya jumla ya mapato yaliyokusanywa kwa kutumia mfumo wa N-Card kama ilivyobainishwa katika barua yenye kumbukumbu namba 23/NIDC/MNG.06/15 iliyotolewa Juni 28, 2023, lakini halmashauri bado haijaitikia ombi hilo,” amesema.

Mikakati duni ya usimamizi wa halmashauri wa mikataba na ukusanyaji wa mapato na wakala katika kituo hicho, amesema kunaweza kusababisha ubadhirifu wa mapato.

Katika hatua nyingine, amesema manispaa hiyo ilitumia jumla ya Sh milioni 563.02 kwa malipo ya ankara za maji na umeme.

“Halmashauri ililipa Sh milioni 333 kama gharama za umeme, na maji ililipa Sh milioni 229.54. Matumizi haya yangepunguzwa kama kila mpangaji angelipia matumizi yake ya maji na umeme, kama ilivyoelekezwa katika mikataba yao,” amesema.

Amependekeza uchunguzi ufanyike na hatua zichukuliwe dhidi ya maofisa waliozuia kutoa taarifa kuhusu mapato yaliyokusanywa kutoka biashara ya hoteli wakati huu.

Pia amependekeza uchunguzi ufanyike na hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya maofisa wa manispaa walioruhusu mawakala kufanya kazi bila mkataba, kisha waeleze kwa uwazi katika mikataba ya upangaji kiasi anachotakiwa kulipa kila mpangaji kwenye gharama za umeme na maji.

“Au vinginevyo kufanya usakinishaji wa mita za umeme za kujitegemea kwa ajili ya wapangaji kwa ajili ya kupima matumizi kwa usahihi,” amesema.

Kodi zashindwa kukusanywa
Katika ukaguzi uliofanywa kuhusu utendaji wa uendeshaji wa vituo vya mabasi, amesema amebaini katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 kodi ya Sh milioni 742.75 haikukusanywa kutoka kwa maduka na vibanda vilivyokamilika vilivyopo katika vituo vya mabasi vya Magufuli, Bweri, Geita Mji, Nyamhongolo Investment Property, Mizengo, Chogo, Makambako, Mbinga, Magugu, Lushoto, Kigamboni (stendi ya zamani), Mpanda, Ikwiriri na Karatu.

“Kifungu Na. 6(1) (m) cha Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura ya 290 kinasema kuwa mapato ya mamlaka za serikali za mitaa yatajumuisha fedha zinazotokana na ada zilizolipwa kutokana na kodi za maduka.

“Machinjio, vibanda vya masoko, ada za watumiaji, ada za huduma na kodi za burudani kwa matangazo ya biashara kwenye mabango, michoro au taarifa,” amesema.

Kukosekana kwa udhibiti wa kutosha katika michakato ya ukusanyaji wa mapato, kama vile kutokuhuisha mikataba ya umiliki na ufuatiliaji wa malipo ya kodi, amesema kumesababisha mapato ya vituo hivyo kupungua.

“Napendekeza mamlaka za serikali za mitaa ziweke mifumo thabiti ya udhibiti wa ndani. Hii ni pamoja na kuhuisha mifumo ya taarifa ya wapangaji, kusimamia mikataba yenye viwango vilivyoidhinishwa na kuwa na usimamizi makini.

“Kuweka kipaumbele katika ukusanyaji wa kiasi kinachodaiwa kutoka kwa wapangaji ni muhimu kwa kuboresha usimamizi wa mapato na kuwa na uhakika wa fedha,” amesema.

DED Ubungo ajibu
Akizungumza na JAMHURI mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ubungo, Aron Kagurumjuli, amesema yeye bado ni mgeni katika kituo chake cha kazi hivyo hawezi kuwa na taarifa zaidi.

“Hiyo ripoti ya CAG sijaisoma na bado haijafika kwetu. Kwa hiyo hadi niipate hiyo ripoti niangalie hoja zilizoibuliwa ndipo nitakuwa na nafasi ya kuzungumza zaidi.

“Maana kuna mambo mengi mno katika ripoti hizi za CAG, kwa hiyo lazima nijiridhishe ndiyo naweza kuwa na la kusema,” amesema.

Kuhusu wapangaji kulipiwa bili za maji na umeme na manispaa amesema: “Lakini kituo kilivyojengwa hakina muundo wa kila mpangaji awe na mita yake ya umeme na maji. Haikutengenezwa hivyo, nafikiri hayo ndiyo mambo yanayopaswa kurekebishwa baadaye. Hawalipi kwa sababu mita ya umeme na maji ni moja kwa kituo kizima. Ili walipe mmoja mmoja ni lazima kuwe na utaratibu wa kuwawekea wapangaji kila mtu na mita yake.”

Kwa upande wake, mmoja wa madiwani wa Manispaa ya Ubungo (hakutaka jina lake liandikwe gazetini) ameiambia JAMHURI hivi karibuni kuwa suala la uvujaji wa mapato katika kituo hicho cha mabasi wameshalijadili mara kadhaa katika vikao vyao.

“Hilo linajulikana na sisi tumeshalipigia kelele, kwa sababu pamoja na kuweka mashine za ku-scan kadi lakini bado kuna mageti mengine katika Kituo cha Magufuli na watu wanaweza kuingia na wasilipe fedha,” amesema.

Uwekezaji katika masoko
Katika hatua nyingine, Kichere, amesema kuna upotevu wa mapato ya Sh bilioni 1.72 katika uwekezaji kutokana na matumizi ya viwango visivyoidhinishwa.

“Usimamizi makini wa viwango vya kodi ya pango ni muhimu kwa mamlaka za serikali za mitaa ili kuongeza mapato na kuwa na fedha toshelevu ili kukidhi mahitaji ya jamii zao,” amesema na kuongeza:

“Viwango vya kodi ya pango mara nyingi hupangwa kwa kufuata taratibu za kisheria na kupitishwa na mamlaka husika ili kuhakikisha haki na uwiano.

“Katika tathmini za hivi karibuni, nimebaini matukio mengi na viwango visivyoidhinishwa vya kodi ya pango vilitumika na kusababisha hasara hiyo.”

Amesema halmashauri zinapoteza kiasi hicho cha fedha kila mwaka kutokana na kutozingatia vifungu vya sheria ndogo.

“Nashauri TAMISEMI, sekretarieti za mikoa, na halmashauri kuhakikisha kuna usimamizi bora wa ukusanyaji wa mapato ili kuhakikisha viwango vilivyobainishwa kwenye sheria vinafuatwa na kuchukua hatua muhimu dhidi ya wale wanaohusika na kutumia viwango visivyoidhinishwa,” amesema.

Pia amesema kuna uendeshaji usio na ufanisi katika masoko ya halmashauri wenye thamani ya Sh bilioni 1.02.

Baada ya kupitia uendeshaji wa masoko ya Hanang', amebaini licha ya uwekezaji mkubwa wa kifedha katika masoko ya Measkron, Gendabi, Masakta na Bassotu yenye thamani ya Sh milioni 140 lakini hayafanyi kazi kwa muda mrefu.

Aidha, Soko la Kimataifa la Mazao la Endagawa lenye thamani ya Sh bilioni 1.02 halifanyi kazi kama ilivyotarajiwa kwa muda mrefu.

“Wakati wa ukaguzi Oktoba 4, mwaka jana nililitembelea na nilibaini kuwapo kwa mazao lakini sikupata kufahamu mapato yaliyopatikana kutokana na kutokuwapo kwa mikataba rasmi kutoka kwa wakulima walioweka mazao yao.

“Kutokufanya kazi kwa muda mrefu kwa miundombinu ya soko na kukosekana kwa mikataba rasmi na wakulima kumesababisha upotevu wa mapato, hususan kutokana na ushuru wa mazao.

“Napendekeza uongozi wa halmashauri kufanya tathmini kamili ya uwezekaji katika masoko yaliyoanzishwa, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika miundombinu muhimu kama mizani na ujenzi wa mifumo ya majitaka ili kuongeza ufanisi wa masoko,” amesema.

CHANZO: JAMHURI
 
Hii uzi haiwezi pata wachangiaji wengi wabongo wanaza mapenzi na soka...waache watu wenye akili wajipigie pesa taratibu
 
Back
Top Bottom