Upatanishi wa Afrika Ukraine

Hamid Rubawa

Member
May 23, 2018
72
208
Upatanishi wa Afrika Ukraine

Picha: Baadhi ya viongozi wa nchi za Afrika wanaoshiriki katika juhudi za upatanishi wa amani katika Vita ya Ukraine, wakiwa na Rais wa taifa hilo, Volodymyr Zelensky jijini Kiev wiki iliyopita. Viongozi wanaoonekana pichani ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Azali Assoumane, kulia kwa rais huyo. Wengine kutoka kushoto ni marais Macky Sall wa Senegal, Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini na Hakainde Hichilema wa Zambia. Picha kwa Hisani ya Al Jazeera

Na Ahmed Rajab

KUNA walioishangilia na kuna walioikebehi taarifa ya kwamba nchi za Kiafrika zinapeleka ujumbe Ukraine na Urussi kujaribu kuzipatanisha nchi hizo. Hisia zote hizo mbili — za furaha na kejeli — zina chimbuko moja: mazoea.

Ulimwengu umezoea kuyaona mataifa ya nje, hasa ya Magharibi, yakitumia diplomasia na kuingilia kati kila pazukapo migogoro Afrika. Yayo ndiyo yenye kuonekana kuwa na uwezo wa kuitanzua migogoro na kuleta suluhu katika nchi zinazohasimiana au zilizokwishaingia vitani. Mataifa hayo yamejipa nguvu za kutunga ajenda za utanzuaji wa migogoro pamoja na kupendekeza mikakati na mbinu za usuluhishi.

Hata dhana na misamiati inayotumika katika mijadala ihusuyo migogoro nayo hufumwa na wataalamu wa Magharibi wenye kujitwaza kuwa ndio mastadi wa upatanishi. Wanajiona kuwa ndio wenye mizungu yote ya usuluhishi na kuwa wao ni majogoo wa suluhu.

Inashangaza kwamba nchi za Magharibi pamoja na taasisi zao hushindwa kuingilia kati panapokuwa na ishara za kuzuka migogoro Afrika.

Nchi za Kiafrika nazo zinaonekana kuwa hazina lao jambo katika kuleta suluhu Afrika seuze nje ya Afrika. Ndio maana wengi walishangaa waliposikia kwamba Waafrika wanapeleka ujumbe wa amani Ukraine na Urussi.

Juhudi ya mwanzo ya Afrika ya kuleta usuluhishi wa kimataifa, nje ya bara hilo, ilifanywa mwaka 1966 na Kwame Nkrumah, aliyekuwa Rais wa Ghana. Tarehe 21 Februari ya mwaka huo alifunga safari kutoka Accra akielekea Hanoi kujaribu kuleta suluhu kati ya iliyokuwa Vietnam ya Kaskazini na Marekani. Bahati mbaya juhudi hiyo ilikufa kabla ya kusimama kwa sababu Nkrumah akiwa hewani kuelekea Hanoi huku nyuma wanajeshi wake walimpindua.

Hata huko Ukraine, Waafrika walikwishajaribu kuleta suluhu. Rais Macky Sall wa Senegal alijaribu akashindwa. Rais wa Guinea-Bissau, Umaro Mokhtar Sissoco Embaló, alijaribu kwa niaba ya Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (Ecowas). Naye pia alishindwa.

Mikono ya mtu wa nje ilihusika na juhudi zote hizo mbili. Naye ndiye mkunga wa juhudi hii ya sasa. Jumatano iliyopita nilipohojiwa na BBC Dira TV kuhusu ujumbe huo nilimtaja mtu huyo kuwa ni mfanyabiashara wa Kifaransa aitwaye Jean-Yves Ollivier. Bwana huyu aliyezaliwa Algeria miaka 78 iliyopita, na ambaye masahibu zake wanamwita JYO, si mgeni katika medani za upatanishi wa kimataifa.

Siku hizi biashara yake kubwa ni ya kuuza nafaka, hasa ngano. Pia anashughulika na chumi za nchi zinazoendelea na zenye fungamano na masoko makuu ya fedha ya dunia.

Ollivier alianza biashara zake miaka ya 1960. Akichuuza bidhaa baina ya Ulaya na Afrika. Baada ya kufanya biashara Afrika kwa takriban miaka 20, Ollivier alijipatia uelewa mkubwa wa bara hilo na mambo yake. Aliweza pia kupanga usuhuba na marais kadhaa wa Kiafrika.

Ollivier ni mwanafunzi wa siasa wa Félix Houphouët Boigny, aliyekuwa Rais wa Côte d’Ivoire. Boigny ndiye aliyemsomesha Ollivier siasa, hasa za kanda ya Afrika ya Magharibi. Boigny alikuwa na watu wake katika haya mambo ya nafaka, mafuta na siasa za siri. Ollivier alikuwa miongoni mwao na alipata baraka zake Boigny. Somo muhimu alilolipata kutoka kwa Boigny ni kutafautisha baina ya diplomasia ya kujenga na ile ya kujidanganya.

Boigny pia alimfahamisha kwamba ikiwa mgeni anaingia kwenye kijiji cha Afrika ni sharti atafute mtu wa kijiji hicho afuatane naye. Mafunzo hayo mawili yamemsaidia pakubwa Ollivier.

Sall wa Senegal ni rafiki yake mkubwa na anamuunga mkono aongezewe muda wake wa utawala. Kuna wasemao kuwa Ollivier ndiye mwenye kumuendesha Sall pamoja na Faure Gnassingbé, Rais wa Togo.

Baadhi ya marafiki zake wengine ni Embaló, Rais Paul Kagame wa Rwanda, Olusegun Obasanjo, Rais wa zamani wa Nigeria, Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Rais Denis Sassou-Nguesso wa Congo-Brazzaville. Alikuwa rafiki mkubwa wa Winnie Mandela, mke wa kwanza wa Nelson Mandela. Ollivier akimuona kama ni dada yake. Nelson Mandela naye alitambua kwamba mtu kama Ollivier anaweza kufanya mambo ambayo viongozi wa Kiafrika hawawezi kuyafanya.

Nje ya Afrika, Ollivier ana usuhuba na Xi Jinping wa China na Vladimir Putin wa Urussi.

Usuhuba wake na viongozi umeifanya nyota yake ing’are katika mitandao ya kidiplomasia, ingawa hujaribu kukiweka kichwa chake chini asionekane. Amejipatia umaarufu mkubwa katika duru za wachezaji wa ile iitwayo “parallel diplomacy au para diplomacy” yaani diplomasia isiyo rasmi iendayo sambamba na ile ya kiserikali. Aghalabu duru za diplomasia isiyo rasmi huwa ni za watu au taasisi zisizo za kiserikali lakini zenye kuyashughulikia masuala nyeti ya kimataifa.

Kufikia mwongo wa 1980, Ollivier aliteuliwa na Jacques Chirac, meya wa siku hizo wa Paris, awe mshauri wake wa Afrika. Tayari Chirac alishawahi kuwa waziri mkuu wa Ufaransa na baadaye akawa Rais.

Ollivier kwanza aliuona mlango wa diplomasia isiyo rasmi ukifunguka wakati huo. Chirac alimtaka afunge safari ya siri kwenda Lebanon kuwaokoa Wafaransa wanne waliokuwa wameshikwa mateka. Ulikuwa ni wakati mgumu kwani vita vya wenyewe kwa wenyewe vilikuwa vimepamba moto nchini humo.

Kufikia 1987, Ollivier alipata fanikio jingine. Alianzisha mazungumzo baina ya jeshi la Angola na lile la Chama cha Ukombozi cha Swapo cha Namibia, kwa upande mmoja, na serikali ya Afrika Kusini kwa upande wa pili. Mazungumzo yalimhusu kapteni wa Vikosi Maalum vya Afrika Kusini, Waynand Du Toit. Majeshi ya Angola yalimteka Du Toit 1985 na serikali ya Afrika Kusini ilifanya juu chini aachiwe huru.

Kwa juhudi za Ollivier serikali ya Angola ilimuachia huru Du Toit na serikali ya makaburu ikawaachia huru wanajeshi 133 wa Angola na wapiganaji 50 wa Jeshi la Ukombozi la Namibia (PLAN).

Katika miaka ya kati ya 1980, askari wa kukodiwa wa Kifaransa na Kibelgiji, wakiongozwa na Bob Denard, walivigeuza visiwa vya Comoro kuwa uwanja wa fujo. Aliyewakodi mamluki hao, Rais Ahmed Abdallah, hakuweza kufurukuta kwa vitimbi vyao.

Mwanzoni, Abdallah akikanusha kwamba hapakuwa na mamluki nchini mwake. Nakumbuka mwaka 1979 nilipokuwa nazungumza naye kwenye Ikulu ya Beit-Salam, mjini Moroni, alikanusha kuwa kuna mamluki Comoro. Nikamuuliza mbona nawaona mitaani? Akanijibu kwamba hao walikuwa ‘askari wawili watatu niliowakodi.’

Hatimaye, Abdallah hakuwa na hila ila kupanga mkakati wa kuwaondoa. Kazi hiyo ikamwangukia Said Hilali, mwananchi wa Comoro, mwenye uzoefu mkubwa kama Ollivier wa mikakati ya diplomasia isiyo rasmi.

Bahati mbaya mkakati huo ulivuja. Kina Denard walipopata habari kwamba watatimuliwa, walimuua Abdallah katika Ikulu yake.

Hilali akamtaka Ollivier amsaidie. Alikuwa mtu muwafaka kwani alikuwa na maingiliano mazuri na vigogo wa utawala wa kikaburu wa Afrika Kusini, hasa waziri wa mambo ya nje Pik Botha na wakuu wa idara ya ujasusi wa kijeshi. Uhusiano wake na aliyekuwa Rais wa Ufaransa, François Mitterrand, pia ulikuwa mzuri. Ndo wakafanikiwa kuwatoa mamluki kutoka Comoro.

Baada ya mamluki hao kufurushwa, Ollivier alisaidia wachaguliwe marais wawili waliomfuatia Abdallah — Sayyid Mohamed Djohar na Mohamed Taki.

Mwezi Agosti, 2014, Ollivier akishirikiana na Bibi Ilmas Futehally wa India walianzisha taasisi ya kiraia, jijini London, iitwayo Brazzaville Foundation. Kazi zake zinahusika na maeneo matatu — amani, mazingira na afya.

Kuhusu amani, taasisi hiyo inajishughulisha na michakato kuachiwa huru mateka na jitihada za kuleta suluhu Libya. Jambo ambalo tunalifichua hapa kwa mara ya kwanza ni kwamba taasisi yake Ollivier ndiyo iliyotoa wazo la kupeana mikono aliyekuwa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na waziri mkuu wa zamani Raila Odinga Machi 9, 2018 na hivyo kuleta suluhu baina yao.

Na sasa kuna hii jitihada ya kuzipatanisha Ukraine na Urussi.

Kwa zaidi ya miezi sita, Ollivier amekuwa akiuchonga ujumbe wake wa Ukraine uwe na maana. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken, alimsaidia awe na mawasiliano na Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine. Ollivier aliiarifu pia serikali ya Uingereza kuhusu azma yake na aliandamana na Obasanjo kwenye mazungumzo na Waingereza.

Ollivier alizichagua nchi zenye misimamo tafauti kuhusu mgogoro huo. Ujumbe uliokwenda Ukraine Ijumaa na Urussi Jumamosi ulikuwa na viongozi saba — marais wa Afrika Kusini (Cyril Ramaphosa), Comoro (Azali Assoumane), Senegal (Sall) na Zambia (Hakainde Hichilema) pamoja na waziri mkuu wa Misri (Mostafa Madbouly) na wawakilishi wa marais Sassou-Nguesso wa Congo-Brazzaville na Museveni wa Uganda.

Comoro imeingizwa kwa sababu ndiyo mwenyekiti wa sasa wa AU; Afrika Kusini na Uganda zinaelemea upande wa Urussi. Zambia iko upande wa Ukraine; na Senegal, Misri na Congo-Brazzaville zinasema haziko upande wowote.

Jitihada hii ni ya kutia moyo lakini kufanikiwa kwake kuna mashaka. Kutategemea iwapo Marekani itafanya uungwana wa kuiachia diplomasia ifanye kazi.

Ollivier aliyeiasisi jitihada hiyo ana maadui wengi Washington na Paris. Wakubwa katika miji hiyo wanamuona kuwa ni mkorofi kwa sababu anakataa kufuata amri zao.

Naye anajihisi kwamba anaijua Afrika, nje ndani. Na anazidi kumuudhi Rais Emmanuel Macron kwa kusema kuwa Macron halifahamu vilivyo bara hilo licha ya kwamba alifanya kazi kwa miezi sita katika ubalozi wa Ufaransa, Nigeria, mnamo 2002 alipokuwa na miaka 23.

Ollivier hakuingia Afrika bure bure. Amejitahidi kuifuma jitihada ya kuzipatanisha Ukraine na Urussi kwa kuipa sura ya Kiafrika. Lakini Ramaphosa si Mandela wala si Thabo Mbeki. Uwezo wa Assoumane haulingani na ukubwa wa kichwa chake. Kwa hivyo, kazi kubwa itamuangukia Ollivier.

Ubaya wa mambo ni kwamba Ollivier, kwa mujibu wa waliofanya naye kazi, anapata shida kuwa na nidhamu. Haielekei kwamba huu ujumbe wake utakuwa na mustakbali mwema. Wala sidhani kama ni busara kuwaachia wachuuzi wa ngano wasimamie diplomasia ya kiwango cha juu kama hicho.

Na panazuka swali: jee, jitihada hii itaendelea au itakufa? Hatari iliyopo ni kwamba ujumbe huo usipofanikiwa basi ulimwengu hautolitia maanani bara la Afrika kwa muda mrefu ujao.

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab

Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.
Screenshot_20230620-174745_Chrome.jpg
 
Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.View attachment 2663399
Napenda jinsi unaandika makala zako
mpaka sasa msafara wa hao viongozi toka Africa umeshindwa
Ulishindwa siku ya kwanza tu ya safari yenyewe hasa baada ya msafara wa rais wa afrika kusini kuyumbishwa
 
Back
Top Bottom