Uongozi wa bunge umepwaya, ujitathimini

mwankuga

JF-Expert Member
Aug 30, 2010
334
120
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lipo kwa mujibu wa katiba ibara ya 62.Bunge ni mojawapo ya mhimili wa dola,mihimili mingine ni serikali na mahakama.Katika dhana ya mgawanyo wa madaraka , mihimili yote ina nguvu sawa na majukumu yake hayaingiliani japo hutegemeana.

Bunge lina uongozi wake kama ilivyo mihimili mingine.Bunge huongozwa na Spika akisaidiwa na Naibu Spika, wenyeviti wa bunge na kamati mbalimbali.

Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaongozwa na Spika Job Ndugai na Naibu Spika Dr.Tulia Ackson Mwansasu.Ni miezi mitano sasa tangu uongozi wa bunge la 11 uingie madarakani.Ni muda huu ambao mambo mengi yametokea ambayo yanatia shaka utendaji wa viongozi wa bunge na bunge lenyewe.

Imekuwa kawaida sana kwa uongozi wa bunge kwa kushirikiana na wabunge wa CCM ambao ndio wengi bungeni kufanya kila liwezekanalo kuitetea serikali na kuikumbatia.Moja ya matukio ya hovyo na ya kujipendekeza kwa serikali, ni hatua ya bunge kuhariri hotuba ya Kambi ya Upinzani iliyokuwa iwasilishwe na waziri kivuli wa mambo ya ndani, Mhe.Godbless Lema.

Ni jambo la fedheha kuona bunge linaacha kutekeleza majukumu yake ya kuisimamia na kuishauri serikali, na badala yake bunge kuwa tawi la serikali. Kwa maoni yangu, hotuba ya Lema haikuwa na shida, bali kulikuwa na hoja za msingi ambazo zilitakiwa kujibiwa na serikali.Kibaya zaidi ni pale uongozi wa bunge usipotaka Rais Mtukufu kutokukosolewa.Kama bunge linataka kumsaidia rais basi ni vema uongozi wa bunge ukaruhusu hoja na mijadala ambayo itaifanya serikali kutimiza wajibu wake.

Suala lingine la fedheha , ni hili la bunge kutoonyeshwa live.Hoja ya kutoonyesha bunge live ilianzia serikali, na hatimaye kushushwa bungeni.Hoja za kutoonyesha bunge live ni dhaifu sana na zinabadilika kila kukicha.Hata suala hilo lilipofika bungeni, uongozi wa bunge ulifanya kila liwezekanavyo kuzima hoja za wabunge wa upinzani.Mwisho ukatolewa uamuzi wa wengi wape, ambao walibariki bunge kuwa mafichoni.Uongozi wa bunge unatakiwa kujua kuwa bunge ni chombo cha wananchi , hivyo mambo yote yanayojadiliwa na kuamuliwa bungeni sharti wananchi wajue, vinginevyo bunge linakosa uhalali wa kuwa chombo cha wananchi.

NAIBU SPIKA AJITATHIMI.

Jina la Dr Tulia Ackson Mwansasu limefahamika na kuvuma sana mwishoni mwa mwaka 2015 baada ya kujitokeza kugombea nafasi ya Uspika wakati huo akiwa Naibu Mwanasheria Mkuu.Tarehe 16/11/2015 ,Rais John Pombe Magufuli alitengua uteuzi wa Naibu Mwanasheria Mkuu, na kumteua kuwa mbunge.Harakaharaka Dr.Tulia akaondoa jina lake kugombea nafasi ya Uspika na kuchukua fomu ya kugombea unaibu spika.

Siku moja baada ya kuteuliwa na rais kuwa mbunge, Dr.Tulia Ackson akapitishwa na wabunge wa CCM kwa kauli moja kugombea nafasi ya Unaibu Spika baada wa wagombea wengine kujitoa.Kuibuka ghafla na mseleleko wa matukio ulitiliwa mashaka na baadhi ya watu, kwamba huenda Dr.Tulia alikuwa anaandaliwa kufanya kazi maalumu.Lakini kwa upande wa pili, wasifu wake ulikuwa unambeba na kwamba angeweza kuitendea haki nafasi ya Naibu Spika.

Maswali aliyoulizwa na Esther Matiko na David Silinde wakati wa kuomba kura ndani ya bunge, yalikuwa mtihani wa kwanza kwa Dr Tulia na yangemwongoza Naibu Spika kutenda haki.Matiko aliuliza hivi : "Tunatambua alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu na hakupaswa kuwa mwanachama wa chama chochote, leo unaomba nafasi ya naibu spika ukiwa mtendaji lakini tayari unachukua upande wa CCM.Unatuaminisha vipi hutaegemea upande?".

Ndani ya miezi mitano aliyohudumu nafasi hiyo, uwezo wake umeonekana wazi.Moja ya sifa muhimu ambayo ilitegemewa ingembeba ni ubobozi wake katika mambo ya sheria.Lakini Mwanasheria huyu amekuwa akisigina kanuni za bunge bila woga na kulifanya bunge kuwa shemu ya serikali. Amekuwa akiminya mijadala yenye masilahi kwa nchi tofauti na hata kiapo chake.Kama sakata la wanafunzi zaidi ya 7000 kuondolewa chuoni UDOM kama wahaini, na naibu spika akaona si japo la maana, kipi cha maana kwa mama huyu?.Ni wakati muafaka kwa mama huyu kujitathimini na kuona kàma anatosha kuvaa viatu vya Naibu Spika, ama abadilike au ajiondoe kulinda heshima yake.

YUKO WÀPI JOB NDUGAI?

JOB NDUGAI ,Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana uzoefu wa kutosha kuendesha bunge kwani alikuwepo kwenye bunge la 10 akiwa kama naibu spika chini ya uongozi wa Anne Makinda.Bunge la 9 chini ya Uongozi wa Samwel Sitta lilionyesha uhai na kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa katiba.

Pamoja na udhaifu wa Sitta lakini alijitahidi sana kuruhusu hoja na mijadala ambayo ilikuwa na lengo la kuisimamia serikali.Anne Makinda alipopata nàfàsi ya uspika alifanya juhudi kulirudisha bunge kwenye kwapa za serikali.Pamoja na hilo, Job Ndugai alionekana yuko tofauti na mkuu wake.Ndio baada ya kupata nafasi ya Uspika baadhi ya watu walikuwa nà imani naye.

Lakini ndani ya miezi 5 mambo yamekuwa kinyume chake.Binge limeoneka kuwa vipande vipande.Bunge la Job Ndugai na binge la Dr Tulia Ackson.Bahati mbaya zaidi kila inapotokea hoja za msingi Spika Job Ndugai anakuwa mafichoni.Mategemeo yangu ni kwamba kwa kuwa Naibu Spika ni mgeni katika uongozi wa bunge hivyo alihitaji kupata nafasi ya kujifunza kutoka kwa mzoefu Job Ndugai.

Uongozi wa bunge unatakiwa kujitathimini kama unaenda sawa.Nafasi ya kurudi kwenye mstari bado ipo.Ili bunge liweze kuisaidia serikali, sio kufunika na kuzuia hoja na mijadala yenye masilahi kwa taifa, bali kuacha bunge kutimiza majukumu yake .Ibara ya 63 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema "bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambacho kitakuwa na madaraka kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa katiba hii".

EM.
 
Mungu wasaidie wanyonge Wa Tanzania, ambao hawana pa kusemea, hata wakisema sauti zao haziwezi kusikika, walinde, wape ujasiri na moyo mkuu Wa kusimama kila moja kwa nafasi yake, amen
 

Absolutely true
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…