Umuhimu wa elimu yetu kuzingatia ubunifu

c_alphonce

New Member
Apr 27, 2024
1
0
Ripoti ya George Land wa NASA 1960 Inawezekana ndio ikawa muarobaini wa matatizo yetu yote kama nchi ambayo msingi wake ni aina ya elimu. Katika utafiti huo George Land aligundua mfumo wa elimu ndio unaua ubunifu kutoka 98% hadi 2%. Ni utafiti ambao waziri wa elimu hapaswi kulala bila kuuwaza, wakuu wa VETA nq kila mzazi. Imagine going to school to learn uncreative thinking.

==========

KUTOKA KITABU CHA “MALEZI DONDOO 24” KILICHOANDIKWA NA MWANDISHI ALPHONCE COSMAS LUHAMBA

NAMNA YA KUKUZA UBUNIFU KWA WATOTO NA VIJANA


Hivi karibuni, nimezindua kitabu changu, "Malezi, Dondoo 24", ambacho kimejaa dondoo muhimu kwa walimu, wazazi, na walezi. Dondoo hizi zinahusu masuala kama usalama wa watoto, vyanzo vya tabia, mfumo wa motisha, athari za vifaa vyenye mwanga kwa watoto, ufahamu kuhusu ubongo wa mtoto, ukuaji wa watoto, ubunifu, na umuhimu wa baba na mama kushiriki pamoja katika malezi.

Kitabu hiki, "Malezi, Dondoo 24", kimeandikwa kwa lugha rahisi ambayo kila mzazi anaweza kuelewa. Moja ya mada muhimu zilizowekwa wazi ni kuhusu mfumo wa elimu na mazingira yanayosaidia kukuza ubunifu wa mtoto. Katika makala hii, nitatilia mkazo Dondoo ya 17 kati ya zile 24 zilizopo ndani ya kitabu, ambayo inahusu ubunifu wa watoto.

Watoto hutumia sana upande wa kulia wa ubongo, ambao unafanya kazi vizuri zaidi katika mazingira yasiyo na makatazo mengi, sheria, au kanuni nyingi. Sehemu hii ya ubongo hufanya kazi kwa ufanisi zaidi pale mtoto anapopewa uhuru. Makatazo kama “acha hiki, acha kile” hupunguza uwezo wa mtoto wa kuwa mbunifu.

Tukirudi kwenye utafiti wa NASA (Shirika la Usimamizi wa Anga za Mbali la Marekani), mwaka 1960 walifanya utafiti wa kipekee kuhusu ubunifu wa binadamu badala ya kuzingatia anga za mbali pekee. Walihitaji kuwabaini watu wenye akili za kipekee kwa ajili ya miradi yao ya anga za mbali. Zoezi hili lilisimamiwa na George Land pamoja na timu yake.

Katika utafiti huo, walichukua kundi la watoto watano wenye umri wa miaka mitatu hadi mitano, kabla ya kuanza shule. Walibaini kwamba, kiwango cha ubunifu na ujiniazi ndani ya watoto hawa kilikuwa asilimia 98%. Utafiti ulihusisha uwezo wao wa ubunifu, kutatua matatizo, na kuona mbali.

Cha kusikitisha ni kwamba, baada ya uchunguzi zaidi, waligundua kuwa mfumo wa elimu ulikuwa chanzo kikubwa cha kuporomoka kwa ubunifu. George Land alithibitisha kuwa ubunifu hupungua sana kutoka asilimia 98% utotoni hadi asilimia 30% wanapofikisha miaka 10, na kushuka hadi asilimia 12% katika miaka 15, kisha kubaki asilimia 2% wanapokuwa watu wazima.

Utafiti huu unatuonyesha umuhimu wa kuzingatia mfumo wa elimu na malezi ambayo yanatoa fursa kwa watoto kuwa wabunifu, badala ya kuwazuia na kuwawekea mipaka mingi ambayo inapunguza uwezo wao wa kufikiri kwa ubunifu.

Utafiti wa George Land ulibaini kuwa kushuka kwa ubunifu miongoni mwa watoto kunatokana na mfumo wa elimu. Watoto wengi wanapopoteza ubunifu wao ni katika hatua za mwanzo za kuanza shule, ambapo mfumo wa elimu haukuzingatii mbinu za kukuza ubunifu na uwezo wa kutatua matatizo. Kwa masikitiko makubwa, George Land anaeleza kuwa watoto wanakwenda shule “kujifunza namna ya kutokuwa wabunifu” (going to school to learn uncreative behavior and thinking).

Watoto wanapoanza shule, sehemu kubwa ya ubunifu wao hupungua kwa kasi. Utafiti wa NASA unaonesha kuwa ubunifu wa watoto, ambao ulikuwa asilimia 98% kabla ya shule, unashuka hadi asilimia 2% kutokana na mifumo ya elimu inayowadidimiza. Sheria, mitaala, na utaratibu wa baadhi ya shule zinaua ubunifu na kuwafanya watoto kukosa uhuru wa kuonesha vipaji vyao na ujasiri ambao wamejaliwa.

Katika umri wa miaka 1-5, mtoto anastawi zaidi katika mazingira huru yasiyo na makatazo mengi. Mtoto anaweza kupiga kelele, kuchana karatasi, au kuvunja vitu, na kazi ya walimu ni kumlinda na kumsaidia kuendeleza ubunifu wake badala ya kumwekea makatazo au kumpiga viboko. Mtoto ni kama sanduku la zawadi; jukumu la walimu na walezi ni kulifungua taratibu na kuonesha kilichomo ndani, badala ya kujaribu kupandikiza au kuumba kile ambacho tayari kipo ndani yake.

Elimu inapaswa kuwa mchakato wa kumwezesha mtu kujifunza namna ya kukabiliana na mazingira yake. Wale wanaotoa elimu wanabaki kuwa wawezeshaji muhimu wa kumsaidia mtoto kuwa vile alivyo. Hata hivyo, utafiti wa George Land unatia huzuni kuona ubunifu wa mtoto, aliyezaliwa na IQ ya asilimia 98%, unashuka hadi asilimia 30% anapofika miaka 10 kwa sababu ya mifumo ya elimu isiyokuza ubunifu na utofauti.

Mojawapo ya mambo yanayozuia watu wabunifu kufikia kilele cha uwezo wao ni hali ya kulazimishwa kufanana na wengine au kuendana na mfumo uliopo. Kama nilivyoeleza awali, watoto hutumia sana ubongo wa kulia, ambao haufurahii sana mazingira yenye sheria na kanuni nyingi. Ustawi wa mtoto unategemea uhuru wake, si kufuata sheria zisizo na sababu. Katika enzi za zamani, watoto waliruhusiwa kucheza kwa uhuru, na mara tu walipoitwa, walijua kwamba chakula kimeiva, na si kwa sababu nyingine.

Shule ya IBM (IBM Creativity School) inapendekeza njia zifuatazo ili kukuza ubunifu:

I. Kuruhusiwa Kukosea na Kushindwa (Permission to fail): Ubunifu unakuzwa kwa kuunda mazingira yanayoruhusu majaribio na makosa. Watoto wanapaswa kuruhusiwa kukosea ili wajifunze kutokana na majaribio yasiyofanikiwa, kwani kuna somo muhimu linalopatikana katika kushindwa.

II. Kuhusiana na Taasisi/Marafiki Wenye Akili na Ubunifu wa Hali ya Juu: Mazingira ya watu wenye ubunifu yanasaidia kukuza ubunifu wa mtoto. Mzazi anapaswa kuhakikisha mtoto anazungukwa na watu wenye fikra bunifu, huku akiwaepusha na watu wa wastani au wale wasiokuwa na fikra za kujenga.

III. Kufuata Mchakato wa Kuondoa Maarifa ya Zamani Kichwani (Unlearning Process): Fikra zisizobunifu zinafundishwa shuleni, hali inayopunguza ubunifu wa mtoto. Ili kuwa mbunifu, ni muhimu mtoto aachane na maarifa ya kizamani yanayotolewa kwenye mfumo wa elimu wa sasa.

IV. Kuachana na Mitindo Iliyopitwa na Wakati Inayopendekezwa na Elimu ya Sasa: Elimu ya kukariri na kufanya mitihani ya kufanana inachangia kuua ubunifu. George Land anashauri tuwe na mitaala inayokuza ubunifu badala ya kuiga mitindo iliyopitwa na wakati.

V. Kujitambua: Watoto wanapaswa kujengwa ili waamini katika ndoto kubwa na zisizo na mipaka. Ni muhimu kupambana na mipaka iliyowekwa na mila, desturi, na jamii kwa ujumla. Kujitambua ni hatua muhimu ya kuvunja vikwazo vya kijamii vilivyowekwa kama pingu za kuzuia mafanikio. Mzazi anapaswa kuhakikisha kuwa watoto wake wanapewa nafasi ya kujadili mambo muhimu na kufikiri kwa uhuru bila kulazimishwa kufuata mkondo wa fikra za wengine.

Kwa hivyo, kukuza ubunifu kunahitaji uhuru wa kufikiri, ujasiri wa kujaribu bila hofu ya kushindwa, na mazingira yanayochochea fikra huru.

Moja ya sababu kuu ya kutokutazama picha za ngono ni kwamba akili ni sehemu takatifu ya mwili – "sacred place of reasoning" – ambayo inapaswa kulindwa. Ni kupitia akili ambapo ubunifu na mawazo chanya huzaliwa; watu wamebuni chanjo na kuleta kinga dhidi ya magonjwa, wameunda sera ambazo zimekuza uchumi na kutoa majawabu kwa changamoto mbalimbali, na wamefanya tafiti ambazo zimeongeza uzalishaji. Kwa hivyo, akili inapaswa kulindwa dhidi ya mawazo na picha zisizofaa, kwani ni chanzo cha maendeleo makubwa katika jamii.

Uchambuzi huu unaletwa kwenu na: Alphonce Cosmas Luhamba
 

Attachments

  • ubunifu_091444.pdf
    360.9 KB · Views: 2
Back
Top Bottom