Mwaka 2022, watu bilioni 2.7 bado hawakuwa na upatikanaji wa intaneti. Tofauti hii inatishia kuongeza kutokuwiana baina na ndani ya nchi. Kutofikia teknolojia na taarifa kunakoendelea kutaendelea kuyatenga makundi ambayo tayari yako nyuma, ikiwa ni pamoja na wanawake na wasichana wa vijijini na kutoka katika jamii zilizotengwa.
Takwimu za hivi karibuni za kimataifa zinaendelea kuthibitisha changamoto zinazoendelea kuzuia wanawake kushiriki kwa usawa katika sekta za kiuchumi zinazojumuisha
ubunifu na teknolojia.
Mwaka 2020, wanawake walishikilia nafasi moja tu kati ya tatu za utafiti duniani na moja tu kati ya tano katika nyanja za sayansi, teknolojia, uhandisi, na hesabu – yaani
Science, Technology, Engineering and Mathematics (STEM). Kutokuwepo kwao katika sekta ya Akili Bandia (
AI) inayoibuka kwa kasi tayari pia kunaathiri jinsi teknolojia hii inavyoweza kuwasaidia wanawake na kutoa majibu kwa mahitaji yao.
Kwa mujibu wa UN Women, mtafiti mmoja kati ya watatu ni mwanamke. Wanawake wanashikilia chini ya 25% ya nafasi za kazi katika Sayansi, Uhandisi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (THEHAMA) kwa kiwango cha kimataifa, na 17% ya wabunifu katika hati za umiliki wa kimataifa ni wanawake, ikilinganishwa na 83% ya wanaume. Na wanawake wana uwezekano mdogo mara mbili zaidi kuliko wanaume kujua jinsi ya kuandika programu ya kompyuta.
Ripoti hiyo inaeleza pia kuwa mifumo ya kutambua uso na sauti (
facial and voice recognition systems), kwa mfano, kwa kawaida huundwa na wanaume na ina ufanisi zaidi katika kutambua sauti za wanaume na nyuso za wanaume wenye ngozi nyeupe; wanawake wenye ngozi nyeusi ndio kundi lililowekwa pembeni zaidi.
Kuongeza ushiriki wa wanawake katika elimu na teknolojia ni muhimu sana ili kubadilisha taarifa na teknolojia ili zifanye kazi kwa usawa wa kijinsia. Kwa kusaidia mabadiliko ya msingi,
kikao cha 66 cha Tume ya Hali ya Wanawake mwaka 2022 kilitoa wito wa hatua za kuchukua kushughulikia pengo la digitali linaloongezeka, ikiwa ni pamoja na sera zinazosaidia elimu na ustadi wa digitali kwa wote na sera zinazosaidia ushiriki sawa wa wanawake katika nafasi za uongozi wa juu.
Ni muhimu kwa jamii kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa mapinduzi ya teknolojia yanakuwa na manufaa sawa kwa wanawake na wanaume, na hii inaweza kufikiwa kupitia sera na sheria zinazosimamia usawa wa kijinsia katika matumizi ya teknolojia na katika sekta za STEM. Kwa kufanya hivyo, tutaweza kujenga jamii yenye usawa na maendeleo endelevu.