JUMUIYA ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) jana ilipata Mwenyekiti mpya huku wajumbe kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wakisusia uchaguzi huo na kutoka nje.
Wajumbe walimchagua Gulam Mukadam ambaye ni Meya wa Manispaa ya Shinyanga (CCM) kuwa Mwenyekiti wa ALAT Taifa kwa kupata kura 179 kati ya kura 281 zilizopigwa. Mgombea mwingine Murshid Ngeze kutoka Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, alipata kura 97 huku kura tano zikiharibika.
Jumla ya kura zilizopigwa zilikuwa 276. Huo ni mkutano wa kwanza wa jumuiya hiyo katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, ambao kabla ya kuanza, Mwanasheria wa ALAT, Cleofasi Manyangu alisema nafasi zilizokuwa zikigombewa kuwa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wa Kamati Tendaji.
Steven Muhapa alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti kwa kupata kura 152 kati ya kura 280 zilizopigwa.
Manyangu alisema waliochukua na kurejesha fomu za kugombea uenyekiti wa ALAT Taifa kuwa ni Mukadam (Meya wa Shinyanga), Murshid Ngeze (Meya wa Bukoba Vijijini), Chiefu Kalumuna (Meya wa Bukoba Mjini) Isaya Mwita Charles (Meya wa Jiji la Dar es Salaam).
Mwanasheria huyo alisema waliokidhi vigezo kwa mujibu wa Katiba ya ALAT, Kanuni za Kudumu na Mwongozo vilivyozingatiwa katika kuendesha uchaguzi huo ni watia nia wawili tu, Mukadam na Ngeze wakati Kalumuna na Mwita hawakukidhi kwa vigezo vya kuwa wagombea ambavyo ni kurejesha fomu katika muda usiozidi saa sita ya siku moja kabla ya uchaguzi na kwamba hawakupata wadhamini 10 kama taratibu zinavyoelekeza.
Meya ya Dodoma, Jafari Mwanyemba alitangaza rasmi kuwa watakaogombea nafasi ya Uenyekiti ni wawili tu, Gulamu na Ngeze, kauli iliyoibua kutoelewana na kusababisha viongozi wa Halmashauri wanaounda Ukawa kususia shughuli zote za mkutano huo.
Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro aliomba meza kuu iruhusu wote waliochukua na kurudisha fomu za kugombea uenyekiti wapigiwe kura kutokana na kuwa maandalizi ya uchaguzi huo yalikiuka mwongozo hali iliyosababisha baadhi ya watia nia kushindwa kukidhi haja ya vigezo.
Hoja yake pamoja na nyingine zilipingwa kwa ufafanuzi. Katibu Mkuu wa ALAT, Abraham Shamumoyo alisema mkutano huo mkuu wa uchaguzi unahusisha wenyeviti wa Halmashauri na mameya wa halmashauri zote 181 nchini.
Pia wakurugenzi wa halmashauri zote na mbunge mmoja kwa kila mkoa na kufanya kuwe na idadi ya wabunge 26. Naye Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT-Wazalendo) alisema haoni sababu za Ukawa kususia mkutano huo wa uchaguzi.
“Kuna vikao vya kambi mbalimbali kwenye mambo kama haya lakini sioni sababu ya mameya kutoka kwenye uchaguzi huu,” alisema Zitto ambaye chama chake kinaongoza Halmashauri ya Kigoma Ujiji. Alisema si sahihi kujitoa ALAT kwani ni mkusanyiko wa halmashauri zote nchini na ambazo zina jukumu la kuhakikisha zinakwenda vizuri kwenye Serikali za Mitaa.
“Siamini kama ALAT itapoteza wanachama kwa sababu ya haya yaliyotokea,” alisema Zitto ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa ACTWazalendo.
Akitoa shukrani baada ya kuchaguliwa, Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Mukadam alisema wanataka kuijenga ALAT katika Awamu ya Tano kwa kwenda na mwendo kasi wa kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu na watajitahidi kuleta mabadiliko kwa mbinu mbalimbali ili makali ya halmashauri kutafuta vyanzo vya mapato vipungue.